Mithali 1

Utangulizi: Kusudi Na Kiini

1 Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:

2 Kwa kupata hekima na nidhamu,

kwa kufahamu maneno ya busara,

3 kwa kujipatia nidhamu na busara,

kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea,

4 huwapa busara wajinga,

maarifa na akili kwa vijana,

5 wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,

wenye kupambanua na wapate mwongozo,

6 kwa kufahamu mithali na mifano,

misemo na vitendawili vya wenye hekima.

7 KumchaBwanandiyo chanzo cha maarifa,

lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.

Onyo Dhidi Ya Ushawishi Wa Marafiki Waovu

8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

na mkufu wa kuipamba shingo yako.

10 Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi,

usikubaliane nao.

11 Kama wakisema, “Twende tufuatane,

tukamvizie mtu na kumwaga damu.

Njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia,

12 tuwameze wakiwa hai kama kaburi,

wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.

13 Tutapata aina zote za vitu vya thamani

na kujaza nyumba zetu kwa nyara.

14 Njoo ushirikiane nasi,

vitu vyote tutakavyopata tutagawana,”

15 mwanangu, usiandamane nao.

Usiweke mguu wako katika njia zao,

16 kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,

ni wepesi kumwaga damu.

17 Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu

wakati ndege wote wanakuona!

18 Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe,

hujivizia tu wenyewe!

19 Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila;

huuondoa uhai wa wale wenye mali.

Onyo Dhidi Ya Kukataa Hekima

20 Hekima huita kwa sauti kuu barabarani,

hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;

21 kwenye makutano ya barabara za mji

zenye makelele mengi hupaza sauti,

kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:

22 “Enyi wajinga, mtang’ang’ania ujinga wenu hadi lini?

Mpaka lini wenye mizaha watafurahia mizaha

na wapumbavu kuchukia maarifa?

23 Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu,

ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu

na kuwafahamisha maneno yangu.

24 Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita

na hakuna ye yote aliyekubali

niliponyosha mkono wangu,

25 kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote

na hamkukubali karipio langu,

26 mimi nami nitawacheka katika maafa yenu,

nitawadhihaki wakati janga litakapowapata,

27 wakati janga litakapowapata kama tufani,

wakati maafa yatakapowazoa kama upepo wa kisulisuli,

wakati dhiki na taabu zitakapowalemea.

28 “Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu,

watanitafuta lakini hawatanipata.

29 Kwa kuwa walichukia maarifa,

wala hawakuchagua kumchaBwana,

30 kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu,

na kukataa maonyo yangu,

31 watakula matunda ya njia zao,

na watashibishwa matunda ya hila zao.

32 Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua,

nako kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza,

33 lakini ye yote anisikilizaye ataishi kwa usalama,

atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/1-0b5742ff8c29a4403f401e70ecd2823c.mp3?version_id=1627—

Mithali 2

Faida Za Hekima

1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu

na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,

2 kutega sikio lako kwenye hekima

na kuweka moyo wako katika ufahamu,

3 na kama ukiita busara

na kuita kwa sauti ufahamu,

4 na kama utaitafuta kama fedha

na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,

5 ndipo utakapoelewa kumchaBwana

na kupata maarifa ya Mungu.

6 Kwa maanaBwanahutoa hekima,

na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.

7 Huifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,

yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,

8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki

na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.

9 Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki

na sawa, katika kila njia nzuri.

10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako,

nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.

11 Busara itakuhifadhi

na ufahamu utakulinda.

12 Hekima itakuokoa kutoka katika njia za waovu,

kutoka watu ambao maneno yao yamepotoka,

13 wale waachao mapito yaliyonyooka

wakatembea katika njia za giza,

14 wale wapendao kutenda mabaya

na kufurahia upotovu wa ubaya,

15 ambao mapito yao yamepotoka

na ambao ni wapotovu katika njia zao.

16 Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba,

kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno

ya kushawishi kutenda ubaya,

17 aliyemwacha mwenzi wa ujana wake

na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.

18 Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo

na mapito yake kwenye roho za waliokufa.

19 Hakuna ye yote aendaye kwake akarudi,

au kufikia mapito ya uzima.

20 Hivyo utatembea katika njia za watu wema

na kushikamana na mapito ya wenye haki.

21 Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi,

nao wasio na lawama watabakia ndani yake,

22 bali waovu watakatiliwa mbali kutoka katika nchi,

nao wasio waaminifu watang’olewa kutoka humo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/2-ea08cd3b924427c425c645de0f3f04e9.mp3?version_id=1627—

Mithali 3

Faida Nyingine Za Hekima

1 Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,

bali zitunze amri zangu moyoni mwako,

2 kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako

na kukuletea mafanikio.

3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;

vifunge shingoni mwako,

viandike katika ubao wa moyo wako.

4 Ndipo utapata kibali na jina zuri

mbele za Mungu na mwanadamu.

5 MtumainiBwanakwa moyo wako wote

wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

6 katika njia zako zote mkiri yeye,

naye atayanyosha mapito yako.

7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe,

mcheBwanaukajiepushe na uovu.

8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,

na mafuta kwenye mifupa yako.

9 MheshimuBwanakwa mali zako na

kwa malimbuko ya mazao yako yote;

10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,

viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.

11 Mwanangu, usidharau marudi yaBwana

na usichukie kukaripiwa naye,

12 kwa sababuBwanahuwarudi wale awapendao,

kama vile baba afanyavyo

kwa mwana apendezwaye naye.

13 Heri mtu yule aonaye hekima,

mtu yule apataye ufahamu,

14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha

na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.

15 Hekima ana thamani kuliko marijani,

hakuna cho chote unachokitamani

kinachoweza kulinganishwa naye.

16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume,

katika mkono wake wa kushoto

kuna utajiri na heshima.

17 Njia zake zinapendeza,

mapito yake yote ni amani.

18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;

wale wamshikao watabarikiwa.

19 Kwa hekimaBwanaaliiweka misingi ya dunia,

kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;

20 kwa maarifa yake vilindi viligawanywa,

nayo mawingu yanadondosha umande.

21 Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara,

usiache vitoke machoni pako;

22 ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako

na pambo la neema shingoni mwako.

23 Kisha utaenda katika njia yako salama,

wala mguu wako hautajikwaa;

24 ulalapo, hautaogopa;

ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.

25 Usiogope maafa ya ghafula

au maangamizi yanayowapata waovu,

26 kwa kuwaBwanaatakuwa tumaini lako

na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.

27 Usizuie wema kwa wale wanaostahili

ikiwa katika uwezo wako kutenda.

28 Usimwambie jirani yako,

“Njoo baadaye, nitakupa kesho,”

wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.

29 Usifanye hila ya kumdhuru jirani yako,

ambaye anaishi karibu na wewe akikuamini.

30 Usimshtaki mtu bila sababu,

wakati hajakutenda dhara lo lote.

31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri

wala kuchagua njia yake iwayo yote,

32 kwa kuwaBwanahumchukia mtu mpotovu,

lakini siri yake iko kwa mwenye haki.

33 Laana yaBwanai juu ya nyumba ya mwovu,

lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.

34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki kwa kiburi

lakini huwapa neema wanyenyekevu.

35 Wenye hekima hurithi heshima,

bali huwaaibisha wapumbavu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/3-0d7d31ecef474efe5f9e52c71d027fe1.mp3?version_id=1627—

Mithali 4

Hekima Ni Bora Kupita Vitu Vyote

1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu,

sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.

2 Ninawapa mafundisho ya maana,

kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.

3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,

ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,

4 baba alinifundisha akisema,

“Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote,

yashike maagizo yangu na wewe utaishi.

5 Pata hekima, pata ufahamu,

usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.

6 Usimwache hekima naye atakuweka salama,

mpende, naye atakulinda.

7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote, kwa hiyo jipatie hekima.

Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.

8 Mstahi, naye atakukweza,

mkumbatie, naye atakuheshimu.

9 Atakuvika shada la neema kichwani mwako

na kukupa taji ya utukufu.”

10 Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia,

nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi.

11 Ninakuongoza katika njia ya hekima

na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka.

12 Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa,

ukimbiapo, hutajikwaa.

13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake,

mshike maana yeye ni uzima wako.

14 Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu

wala usitembee katika njia ya watu wabaya.

15 Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo,

achana nayo na uelekee njia yako.

16 Kwa kuwa hawawezi kulala mpaka watende uovu,

wanashindwa hata kusinzia mpaka wamwangushe mtu.

17 Wanakula mkate wa uovu,

na kunywa mvinyo wa jeuri.

18 Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko,

ambayo hung’aa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu

19 Lakini njia ya waovu ni kama giza nene,

hawajui kinachowafanya wajikwae.

20 Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia,

sikiliza kwa makini maneno yangu.

21 Usiruhusu yaondoke machoni pako,

yahifadhi ndani ya moyo wako,

22 kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata

na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.

23 Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo,

maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

24 Epusha kinywa chako na ukaidi,

weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.

25 Macho yako na yatazame mbele,

kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.

26 Sawazisha mapito ya miguu yako

na njia zako zote ziwe zimethibitika.

27 Usigeuke kulia wala kushoto,

epusha mguu wako na ubaya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/4-b76a8a3d6bf6eda8ca51a36517ab8650.mp3?version_id=1627—

Mithali 5

Onyo Dhidi Ya Uzinzi

1 Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu,

sikiliza vizuri maneno yangu ya busara,

2 ili uweze kutunza busara

na midomo yako ihifadhi maarifa.

3 Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba

hudondoza asali,

na maneno ya kinywa chake

ni laini kuliko mafuta,

4 lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo,

mkali kama upanga ukatao kuwili.

5 Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo,

# hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini.

6 Yeye hafikiri juu ya njia ya uzima,

njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui.

7 Sasa basi wanangu, nisikilizeni,

msiache ninalowaambia.

8 Njia zenu ziwe mbali naye,

msiende karibu na mlango wa nyumba yake,

9 usije ukatoa nguvu zako nzuri kwa wengine

na miaka yako kwa aliye mkatili,

10 wageni wasije wakasherehekea utajiri wako

na jitihada yako ikatajirisha

nyumba ya mwanaume mwingine.

11 Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu,

wakati nyama na mwili wako vimechakaa.

12 Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia marudi!

Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo!

13 Sikuwatii walimu wangu

wala kuwasikiliza wakufunzi wangu.

14 Nimefika ukingoni mwa maangamizi kabisa

katikati ya kusanyiko lote.”

15 Kunywa maji kutoka kwenye kisima chako mwenyewe,

maji yanayotiririka kutoka kwenye kisima chako mwenyewe.

16 Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji

na vijito vyako vya maji viwanjani?

17 Na viwe vyako mwenyewe,

kamwe visishirikishwe wageni.

18 Chemchemi yako na ibarikiwe

na umfurahie mke wa ujana wako.

19 Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri,

matiti yake na yakutosheleze siku zote,

nawe utekwe daima na upendo wake.

20 Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba?

Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine?

21 Kwa maana njia za mtu ni wazi kabisa mbele zaBwana,

naye huyapima mapito yake yote.

22 Matendo mabaya ya mtu mwovu humnasa yeye mwenyewe;

kamba za dhambi yake humkamata kwa nguvu.

23 Atakufa kwa kukosa nidhamu,

akipotoshwa kwa upumbavu wake mwenyewe.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/5-ec7bece217996f84309c7493d7146286.mp3?version_id=1627—

Mithali 6

Maonyo Dhidi Ya Upumbavu

1 Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako,

ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi

kwa ajili ya mwingine,

2 kama umetegwa na ulichosema,

umenaswa kwa maneno ya kinywa chako,

3 basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru,

kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako:

Nenda ukajinyenyekeshe kwake,

msihi jirani yako!

4 Usiruhusu usingizi machoni pako,

usiruhusu kope zako zisinzie.

5 Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji,

kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji.

6 Ewe mvivu, mwendee mchwa,

zitafakari njia zake ukapate hekima!

7 Kwa maana yeye hana msimamizi,

wala mwangalizi, au mtawala,

8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi

na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.

9 Ewe mvivu, utalala hata lini?

Utaamka lini kutoka katika usingizi wako?

10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

bado kukunja mikono upate usingizi!

11 Hivyo umaskini wako huja kama mnyang’anyi

na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.

12 Mtu mbaya sana na mlaghai,

ambaye huzungukazunguka

na maneno ya upotovu,

13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake,

anayetoa ishara kwa miguu yake

na kuashiria kwa vidole vyake,

14 ambaye hupanga ubaya

kwa udanganyifu moyoni mwake:

daima huchochea fitina.

15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula;

ataangamizwa mara, pasipo msaada.

16 Kuna vitu sita anavyovichukiaBwana,

naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

17 macho ya kiburi,

ulimi udanganyao,

mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

18 moyo ule uwazao mipango miovu,

miguu ile iliyo myepesi kukimbilia uovu,

19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo

na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

Onyo Dhidi Ya Uasherati

20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,

wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

21 Yafunge katika moyo wako daima,

yakaze kuizunguka shingo yako.

22 Wakati utembeapo, yatakuongoza,

wakati ulalapo, yatakulinda,

wakati uamkapo, yatazungumza nawe.

23 Kwa maana amri hizi ni taa,

mafundisho haya ni mwanga

na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,

24 yakikulinda na mwanamke aliyepotoka,

kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka.

25 Moyo wako usitamani uzuri wake

wala macho yake yasikuteke,

26 kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini

hata ukose kipande cha mkate

naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa.

27 Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake

bila nguo zake kuungua?

28 Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto yanayowaka

bila miguu yake kuungua?

29 Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine;

hakuna ye yote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa.

30 Watu hawamdharau mwizi kama akiiba

kukidhi njaa yake wakati ana njaa.

31 Pamoja na hayo, kama akikamatwa,

lazima alipe mara saba,

ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake.

32 Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa;

ye yote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe.

33 Mapigo na aibu ni fungu lake

na aibu yake haitafutika kamwe;

34 kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume,

naye hataonyesha huruma alipizapo kisasi.

35 Hatakubali fidia yo yote;

atakataa malipo hata yakiwa makubwa kiasi gani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/6-a4b3c022120d52ef14e70a88c5e20644.mp3?version_id=1627—

Mithali 7

Onyo Dhidi Ya Mwanamke Mzinzi

1 Mwanangu, shika maneno yangu

na kuzihifadhi amri zangu ndani yako.

2 Shika amri zangu nawe utaishi;

linda mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako.

3 Yafunge katika vidole vyako,

yaandike katika kibao cha moyo wako.

4 Mwambie hekima, “Wewe ni dada yangu,”

uite ufahamu jamaa yako;

5 watakuepusha na mwanamke mzinzi,

kutokana na mwanamke mpotovu

na maneno yake ya kubembeleza.

6 Kwenye dirisha la nyumba yangu

nilitazama nje kupitia upenyo

kwenye mwimo wa dirisha.

7 Niliona miongoni mwa wajinga,

nikagundua miongoni mwa wanaume vijana,

kijana asiye na akili.

8 Alikuwa akishuka njiani mahali barabara inakopindia,

akitembea kuelekea kwenye nyumba

ya huyo mwanamke

9 wakati wa machweo, jua likipungua nuru yake,

giza la usiku lilipokuwa likiingia.

10 Ndipo huyo mwanamke akatoka kumlaki,

hali amevaa kama kahaba

akiwa na nia ya udanganyifu.

11 (Ni mwanamke mwenye makelele na mkaidi,

miguu yake haitulii nyumbani,

12 mara kwenye barabara za mji,

mara kwenye viwanja vikubwa,

kwenye kila pembe huvizia.)

13 Huyo mwanamke alimkumbatia kijana na kumbusu,

na kwa uso usio na haya akamwambia:

14 “Nina sadaka za amani nyumbani,

leo nimetimiza nadhiri zangu.

15 Kwa hiyo nimetoka nje kukulaki,

nimekutafuta na nimekupata!

16 Nimetandika kitanda changu

kwa kitani za rangi kutoka Misri.

17 Nimetia manukato kitanda changu

kwa manemane, udi na mdalasini.

18 Njoo, tuzame katika mapenzi mpaka asubuhi,

tujifurahishe wenyewe kwa mapenzi!

19 Mume wangu hayupo nyumbani,

amekwenda safari ya mbali.

20 Amechukua mkoba uliojazwa fedha

na hatakuwepo nyumbani karibuni.”

21 Kwa maneno laini yule mwanamke akampotosha,

alimshawishi kwa maneno yake laini.

22 Mara huyo kijana alimfuata yule mwanamke

kama fahali aendaye machinjoni,

kama kulungu aingiaye kwenye kitanzi,

23 mpaka mshale umchome ini lake,

kama ndege anayenaswa kwenye mtego,

bila kujua itamgharimu maisha yake.

24 Sasa basi wanangu, nisikilizeni;

sikilizeni kwa makini nisemalo.

25 Usiruhusu moyo wako ugeukie njia za huyo mwanamke

wala usitangetange katika mapito yake.

26 Aliowaangusha ni wengi;

aliowachinja ni kundi kubwa.

27 Nyumba yake ni njia kuu iendayo kaburini,

ielekeayo chini kwenye vyumba vya mauti.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/7-462699024114165a2f98ded840077133.mp3?version_id=1627—

Mithali 8

Wito Wa Hekima

1 Je, hekima haiti?

Je, ufahamu hapazi sauti?

2 Juu ya miinuko karibu na njia,

penye njia panda, ndipo asimamapo,

3 kando ya malango yaelekeayo mjini,

kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:

4 “Ni ninyi wanaume, ninaowaita,

ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.

5 Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili,

ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.

6 Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema,

ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.

7 Kinywa changu husema lililo kweli,

kwa maana midomo yangu huchukia uovu.

8 Maneno yote ya kinywa changu ni haki,

hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi.

9 Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi,

hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.

10 Chagua mafundisho yangu badala ya fedha,

maarifa badala ya dhahabu safi,

11 kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani

na hakuna cho chote unachohitaji kinacholingana naye.

12 “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara,

ninamiliki maarifa na busara.

13 KumchaBwanani kuchukia uovu,

ninachukia kiburi na majivuno,

tabia mbaya na mazungumzo potovu.

14 Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu,

nina ufahamu na nina nguvu.

15 Kwa msaada wangu wafalme hutawala

na watawala hutunga sheria zilizo za haki,

16 kwa msaada wangu wakuu hutawala,

na wenye vyeo wote watawalao dunia.

17 Nawapenda wale wanipendao,

na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

18 Utajiri na heshima viko kwangu,

utajiri udumuo na mafanikio.

19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi,

kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.

20 Natembea katika njia ya unyofu

katika mapito ya haki,

21 nawapa utajiri wale wanipendao

na kuzijaza hazina zao.

22 “Bwanaaliniumba mwanzoni mwa kazi yake,

kabla ya matendo yake ya zamani;

23 niliteuliwa tangu milele,

tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.

24 Wakati hazijakuwapo bahari, nilikwishazaliwa,

wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji,

25 kabla milima haijawekwa mahali pake,

kabla vilima havijakuwapo, nilikwishazaliwa,

26 kabla hajaumba dunia wala mashamba yake

au vumbi lo lote la dunia.

27 Nilikuwapo alipoziweka mbingu mahali pake,

wakati alipochora mstari wa upeo wa macho

juu ya uso wa kilindi,

28 wakati alipoweka mawingu juu

na kuziweka imara chemchemi za bahari,

29 wakati alipoiwekea bahari mpaka wake

ili maji yasivunje agizo lake,

na wakati alipoweka misingi ya dunia.

30 Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake.

Nilijazwa na furaha siku baada ya siku,

nikifurahi daima mbele zake,

31 nikifurahi katika dunia yake yote

nami nikiwafurahia wanadamu.

32 “Basi sasa wanangu, nisikilizeni;

heri wale wanaozishika njia zangu.

33 Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima;

msiyapuuze.

34 Heri mtu yule anisikilizae mimi,

akisubiri siku zote malangoni mwangu,

akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.

35 Kwa maana ye yote anipatae mimi amepata uzima

na kujipatia kibali kutoka kwaBwana.

36 Lakini ye yote ashindwaye kunipata

hujiumiza mwenyewe;

na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/8-d4c99cb9aea433eb7256382a216b2dca.mp3?version_id=1627—

Mithali 9

Makaribisho Ya Hekima Na Ya Upumbavu

1 Hekima amejenga nyumba yake,

amechonga nguzo zake saba.

2 Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake;

pia ameandaa meza yake.

3 Amewatuma watumishi wake wa kike, naye huita

kutoka mahali pa juu sana pa mji.

4 Anawaambia wale wasio na maamuzi,

“Wote ambao ni wajinga na waje hapa!

5 Njoni, mle chakula changu

na mnywe divai niliyoichanganya.

6 Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi;

tembeeni katika njia ya ufahamu.

7 “Ye yote anayemkosoa mwenye mzaha

hukaribisha matukano,

ye yote anayekemea mtu mwovu

hupatwa na matusi.

8 Usimkemee mwenye mzaha la sivyo atakuchukia;

mkemee mwenye hekima naye atakupenda.

9 Mfundishe mtu mwenye hekima

naye atakuwa na hekima zaidi,

mfundishe mtu mwadilifu

naye atazidi kufundishika.

10 “KumchaBwanani mwanzo wa hekima

na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.

11 Kwa maana kwa msaada wangu

siku zako zitakuwa nyingi,

na miaka itaongezwa katika maisha yako.

12 Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo;

kama wewe ni mtu wa mzaha,

wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”

13 Mwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele;

hana adabu na hana maarifa.

14 Huketi kwenye mlango wa nyumba yake,

juu ya kiti katika mahali pa juu sana pa mji,

15 akiita wale wapitao karibu,

waendao moja kwa moja kwenye njia yao.

16 Anawaambia wale wasio na maamuzi,

“Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani!”

17 “Maji yaliyoibiwa ni matamu,

chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”

18 Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo,

kwamba wageni wake huyo mwanamke

wako katika vilindi vya kuzimu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/9-c3a87b1a9f5e783705bc603cfc14739d.mp3?version_id=1627—

Mithali 10

Mithali Za Solomoni

1 Mithali za Solomoni:

Mwana mwenye hekima

huleta furaha kwa baba yake,

lakini mwana mpumbavu

huleta huzuni kwa mama yake.

2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,

lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.

3 Bwanahawaachi waadilifu kukaa njaa,

lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.

4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini

lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi

ni mwana mwenye hekima,

lakini yeye alalaye wakati wa mavuno

ni mwana mwenye kuaibisha.

6 Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,

lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

7 Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka,

lakini jina la mwovu litaoza.

8 Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo,

lakini mpumbavu apayukaye huangamia.

9 Mtu mwadilifu hutembea salama,

lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagundulika.

10 Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni,

naye mpumbavu apayukaye huangamia.

11 Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,

lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

12 Chuki huchochea faraka,

lakini upendo husitiri mabaya yote.

13 Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua,

lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.

14 Wenye hekima huhifadhi maarifa,

bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.

15 Mali ya tajiri ni mji wao wenye ngome,

bali ufukara ni maangamizi ya maskini.

16 Ujira wa wenye haki huwaletea uzima,

lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.

17 Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima,

lakini ye yote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.

18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,

na ye yote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.

19 Wakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani,

lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.

20 Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora,

bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.

21 Midomo ya mwenye haki hulisha wengi,

lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.

22 Baraka yaBwanahutajirisha,

wala haichanganyi huzuni.

23 Mpumbavu hufurahia tabia mbaya,

lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.

24 Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata,

kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.

25 Tufani inapopita, waovu hutoweka,

lakini wenye haki husimama imara milele.

26 Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,

ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.

27 KumchaBwanahuongeza urefu wa maisha,

lakini miaka ya mwovu inafupishwa.

28 Tarajio la mwenye haki ni furaha,

bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.

29 Njia yaBwanani kimbilio kwa wenye haki,

lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.

30 Kamwe wenye haki hawataondolewa,

bali waovu hawatasalia katika nchi.

31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima,

bali ulimi wa upotovu utakatwa.

32 Midomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa,

bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/10-5250544be7804d87ab7f98988d8167e9.mp3?version_id=1627—