Mithali 21

1 Moyo wa mfalme uko katika mkono waBwana;

huuongoza kama mkondo wa maji, po pote apendapo.

2 Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake,

baliBwanahuupima moyo.

3 Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika

zaidi kwaBwanakuliko dhabihu.

4 Macho ya kudharau na moyo wa kiburi,

ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!

5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,

kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.

6 Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo

ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.

7 Jeuri ya waovu itawaburuta mbali,

kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa.

8 Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu,

bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu.

9 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba

kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

10 Mtu mwovu hutamani sana ubaya,

jirani yake hapati huruma kutoka kwake.

11 Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa,

mjinga hupata hekima;

wakati mtu mwenye hekima afundishwapo,

hupata maarifa.

12 Mwenye haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu,

naye atawaangamiza waovu.

13 Kama mtu akizibia masikio kilio cha maskini,

yeye pia atalia wala hatajibiwa.

14 Zawadi itolewayo kwa siri hutuliza hasira

na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali.

15 Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki,

bali kitisho kwa watenda mabaya.

16 Mtu anayepotea kutoka katika mapito ya ufahamu,

hupumzika katika kundi la waliokufa.

17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini,

ye yote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.

18 Waovu huwa fidia kwa ajili ya wenye haki,

nao wasio waaminifu kwa ajili ya wanyofu.

19 Ni afadhali kuishi jangwani

kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi.

20 Katika nyumba ya mwenye hekima

kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta,

lakini mtu mpumbavu

hutafuna vyote alivyo navyo.

21 Yeye afuatiaye haki na upendo

hupata uzima, mafanikio na heshima.

22 Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu,

na kuangusha ngome wanazozitegemea.

23 Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake

hujilinda na maafa.

24 Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake;

hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.

25 Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake,

kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi.

26 Mchana kutwa hutamani zaidi,

lakini mnyofu hutoa pasipo kuzuia.

27 Dhabihu ya mtu mwovu ni chukizo,

si zaidi sana itolewapo kwa nia mbaya!

28 Shahidi wa uongo ataangamia,

bali maneno ya mwenye kusikia yatadumu.

29 Mtu mwovu ana uso wa ushupavu,

bali mtu mnyofu huzifikiria njia zake.

30 Hakuna hekima, wala akili, wala mpango

unaoweza kufaulu dhidi yaBwana.

31 Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita,

bali ushindi huwa kwaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/21-5fdc06d6f9d93f0c2ebc3a7a2601e682.mp3?version_id=1627—

Mithali 22

1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi,

kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.

2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:

Bwanani Muumba wao wote.

3 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

bali mjinga huendelea mbele kama kipofu nayo ikamtesa.

4 Unyenyekevu na kumchaBwana

huleta utajiri, heshima na uzima.

5 Katika mapito ya waovu kuna miiba na mitego,

bali yeye ailindaye nafsi yake hukaa mbali nayo.

6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

naye hataiacha hata akiwa mzee.

7 Matajiri huwatawala maskini

naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye.

8 Yeye aupandaye uovu huvuna taabu,

nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa.

9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa

kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.

10 Mfukuze mwenye dhihaka,

nayo mashindano yatatoweka;

ugomvi na matukano vitakoma.

11 Yeye apendaye moyo safi na yeye ambaye maneno yake ni ya neema,

mfalme atakuwa rafiki yake.

12 Macho yaBwanahulinda maarifa,

bali huyapinga maneno ya asiye mwaminifu.

13 Mvivu husema, “Kuna simba nje!”

au, “Nitauawa huko njiani!”

14 Kinywa cha mwanamke kahaba ni shimo refu;

yeye aliye chini ya ghadhabu yaBwana

atatumbukia ndani yake.

15 Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto,

bali fimbo ya adhabu itaufukuzilia mbali naye.

16 Yeye amuoneaye maskini ili kujiongezea mali,

naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini.

Misemo Ya Wenye Hekima

17 Tega sikio na usikie misemo ya wenye hekima,

elekeza moyo wako kwenye yale nifundishayo,

18 kwa maana inapendeza unapoyahifadhi moyoni mwako

na kuwa nayo yote tayari midomoni mwako.

19 Ili tumaini lako liwe katikaBwana,

hata wewe, ninakufundisha leo.

20 Je, sijakuandikia misemo thelathini,

misemo ya mashauri na maarifa,

21 kukufundisha maneno ya kweli na ya kuaminika,

ili uweze kutoa majibu sahihi

kwake yeye aliyekutuma?

22 Usiwadhulumu maskini kwa hila kwa sababu ni maskini,

wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,

23 kwa sababuBwanaatalichukua shauri lao

naye atawateka wao waliowateka.

24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka,

usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,

25 la sivyo utajifunza njia zake

na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.

26 Usiwe mwenye kupana mikono katika rehani,

au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni.

27 Kama ukikosa njia ya kulipa,

kitanda chako ukilaliacho

kitachukuliwa ukiwa umekilalia.

28 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani

lililowekwa na baba zako.

29 Je, unamwona mtu stadi katika kazi yake?

Atahudumu mbele ya wafalme;

hatahudumu mbele ya watu duni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/22-921199a38e30e30f2a58a145b3c75beb.mp3?version_id=1627—

Mithali 23

1 Uketipo kula chakula na mtawala,

angalia vyema kile kilicho mbele yako,

2 na utie kisu kooni mwako

kama ukiwa mlafi.

3 Usitamani vyakula vyake vitamu

kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.

4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri,

uwe na hekima kuonyesha kujizuia.

5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,

huwa kama umepata mabawa ghafula,

ukaruka na kutoweka angani kama tai.

6 Usile chakula cha mtu mchoyo,

usitamani vyakula vyake vitamu,

7 kwa maana yeye ni aina ya mtu

ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama.

Anakuambia, “Kula na kunywa,”

lakini moyo wake hauko pamoja nawe.

8 Utatapika kile kidogo ulichokula,

nawe utakuwa umepoteza bure

maneno yako ya kumsifu.

9 Usizungumze na mpumbavu,

kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.

10 Usiondoe jiwe la mpaka wa zamani

wala kujiingiza kwenye mashamba ya yatima,

11 kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu,

atalichukua shauri lao dhidi yako.

12 Elekeza moyo wako kwenye mafundisho

na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.

13 Usimnyime mtoto adhabu,

kwa maana ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.

14 Mwadhibu kwa fimbo

# na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini.

15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima,

basi moyo wangu utafurahi,

16 utu wangu wa ndani utafurahi,

wakati midomo yako

itakapozungumza lililo sawa.

17 Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi,

bali kila mara uwe na bidii katika kumchaBwana.

18 Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako,

nalo taraja lako halitakatiliwa mbali.

19 Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima,

weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.

20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,

au wale walao nyama kwa pupa,

21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini,

nako kusinzia huwavika matambara.

22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,

wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.

23 Nunua kweli wala usiiuze,

pata hekima, adabu na ufahamu.

24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,

naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.

25 Baba yako na mama yako na wafurahi,

mama aliyekuzaa na ashangilie!

26 Mwanangu, nipe moyo wako,

macho yako na yafuate njia zangu,

27 kwa maana kahaba ni shimo refu

na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.

28 Kama mnyang’anyi, hungojea akivizia,

naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.

29 Ni nani mwenye ole?

Ni nani mwenye huzuni?

Ni nani mwenye ugomvi?

Ni nani mwenye malalamiko?

Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?

Ni nani mwenye macho mekundu?

30 Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo,

hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.

31 Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu,

wakati unapometameta kwenye bilauri,

wakati ushukapo taratibu!

32 Mwisho huuma kama nyoka

na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.

33 Macho yako yataona mambo mageni

na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.

34 Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari,

alalaye juu ya kamba ya merikebu.

35 Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia!

Wamenichapa, lakini sisikii!

Nitaamka lini

ili nikanywe tena?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/23-0898d8042d66cab56ecc9751e2ae6a5b.mp3?version_id=1627—

Mithali 24

1 Usiwaonee wivu watu waovu,

usitamani ushirika nao;

2 kwa maana mioyo yao hupanga mambo ya jeuri,

nayo midomo yao husema juu ya kuleta taabu.

3 Kwa hekima nyumba hujengwa,

nayo kwa njia ya ufahamu huimarishwa,

4 kwa njia ya maarifa vyumba vyake hujazwa

vitu vya thamani na vya kupendeza.

5 Mtu mwenye hekima ana uwezo mkubwa,

naye mtu mwenye maarifa huongeza nguvu,

6 kwa kufanya vita unahitaji maongozi

na kwa ushindi washauri wengi.

7 Hekima i juu mno kwa mpumbavu,

katika kusanyiko langoni

hana lo lote la kusema.

8 Yeye apangaye mabaya

atajulikana kama mtu wa hila.

9 Mipango ya mpumbavu ni dhambi,

watu humchukia mwenye dhihaka.

10 Ukikata tamaa wakati wa taabu,

jinsi gani nguvu zako ni kidogo!

11 Okoa wale wanaoongozwa kwenye kifo;

wazuie wote wanaojikokota

kuelekea machinjoni.

12 Kama mkisema, “Lakini hatukujua lo lote kuhusu hili,”

je, yule apimaye mioyo halitambui hili?

Je, yule awalindaye maisha yenu halijui hili?

Je, hatamlipa kila mtu kulingana na aliyotenda?

13 Ule asali mwanangu, kwa kuwa ni nzuri;

asali kutoka kwenye sega ni tamu kwa kuonja.

14 Ujue pia kwamba hekima ni tamu kwa nafsi yako,

kama ukiipata, kuna matumaini kwako ya siku zijazo,

nalo tumaini lako halitakatiliwa mbali.

15 Usivizie kama haramia afanyavyo ili kuyashambulia

makao ya mwenye haki,

wala usiyavamie makazi yake,

16 Kwa maana ingawa mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena,

lakini waovu huangushwa chini na maafa.

17 Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo;

wakati ajikwaapo,

usiruhusu moyo wako ushangilie.

18 Bwanaasije akaona na kuchukia

akaiondoa ghadhabu yake mbali naye.

19 Usikasirike kwa sababu ya watu wabaya

wala usiwaonee wivu waovu,

20 kwa maana mtu mbaya hana tumaini la siku zijazo,

nayo taa ya mtu mwovu itazimwa.

21 Mwanangu, mcheBwanana mfalme,

wala usijiunge na waasi,

22 kwa maana hao wawili watatuma maangamizi ya ghafula juu yao,

naye ni nani ajuaye maafa wawezayo kuleta?

Misemo Zaidi Ya Wenye Hekima

23 Hii pia ni misemo ya wenye hekima:

Kuonyesha upendeleo katika hukumu si vyema:

24 Ye yote amwambiaye mwenye hatia,

“Wewe huna hatia,”

Watu watamlaani

na mataifa yatamkana.

25 Bali itakuwa vyema kwa wale watakaowatia hatiani wenye hatia,

nazo baraka tele zitawajilia juu yao.

26 Jawabu la uaminifu

ni kama busu la midomoni.

27 Maliza kazi zako za nje,

nawe uweke mashamba yako tayari,

baada ya hilo, jenga nyumba yako.

28 Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu,

au kutumia midomo yako kudanganya.

29 Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda mimi,

nitamlipiza mtu yule kwa kile alichonitendea.”

30 Nilipita karibu na shamba la mtu mvivu,

karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,

31 miiba ilikuwa imeota kila mahali,

ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na

ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.

32 Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona,

nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:

33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

bado kukunja mikono upate kupumzika,

34 Nao umaskini utakuja juu yako kama mnyang’anyi,

na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/24-7b0ff0260e60d66853c644eea57f340c.mp3?version_id=1627—

Mithali 25

Mithali Zaidi Za Solomoni

1 Hizi ni mithali zaidi za Solomoni, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda:

2 Ni Utukufu wa Mungu kuficha jambo,

bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.

3 Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini,

ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.

4 Ondoa takataka kwenye madini ya fedha,

nako ndani yake kutatokea kitu halisi

kwa ajili ya mfua fedha.

5 Ondoa waovu mbele ya mfalme,

nacho kiti chake cha enzi

kitaimarishwa kwa njia ya haki.

6 Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme,

wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu.

7 Ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,”

kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu.

Kile ulichokiona kwa macho yako

8 usiharakishe kukipeleka mahakamani,

maana utafanya nini mwishoni

kama jirani yako atakuaibisha?

9 Kama ukifanya shauri na jirani yako,

usisaliti siri ya mtu mwingine,

10 ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha

na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.

11 Neno lisemwalo kwa wakati ufaao

ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu

yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.

12 Kama vile kipuli cha dhahabu

au pambo la dhahabu safi,

ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima

kwa sikio lisikilizalo.

13 Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno

ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao,

huburudisha roho za bwana zake.

14 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua

ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.

15 Kwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa,

nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa.

16 Kama ukikuta asali, kula kiasi tu cha kukutosha,

ukila zaidi, utatapika.

17 Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache,

ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.

18 Kama vile rungu au upanga au mshale mkali

ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.

19 Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa,

ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.

20 Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi,

au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi,

ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.

21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale,

kama ana kiu, mpe maji anywe.

22 Kwa kufanya hivi, unampalia makaa ya moto kichwani pake,

nayeBwanaatakupa thawabu.

23 Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua,

ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.

24 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,

kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

25 Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka

ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.

26 Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au

kisima kilichotiwa taka

ndivyo alivyo mtu mwenye haki

anayeshindwa na uovu.

27 Si vyema kula asali nyingi sana,

wala si heshima

kujitafutia heshima yako mwenyewe.

28 Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka

ndivyo alivyo mtu

ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/25-8d43f51a751bb756c7c7ecb464c68b40.mp3?version_id=1627—

Mithali 26

1 Kama theluji wakati wa kiangazi au mvua wakati wa mavuno,

ndivyo asivyostahili heshima mpumbavu.

2 Kama shomoro apigapigavyo mbawa zake

au mbayuwayu katika kuruka kwake kasi,

ndivyo ilivyo laana isiyo na sababu haimpati mtu.

3 Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda,

nayo fimbo kwa migongo ya wapumbavu!

4 Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,

ama wewe mwenyewe utakuwa kama yeye.

5 Mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,

ama atakuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe.

6 Kama vile ilivyo kujikata miguu au kujitafutia shida,

ndivyo ilivyo kutuma ujumbe kwa mkono wa mpumbavu.

7 Kama miguu ya kiwete inavyoning’inia

ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha mpumbavu.

8 Kama kufunga jiwe kwenye kombeo,

ndivyo ilivyo kumpa mpumbavu heshima.

9 Kama mwiba kwenye mkono wa mlevi

ndivyo ilivyo mithali kinywani mwa mpumbavu.

10 Kama mpiga upinde ambaye hujeruhi ovyo,

ndivyo alivyo yeye aajiriye mpumbavu au ye yote apitaye njiani.

11 Kama mbwa ayarudiavyo matapishi yake,

ndivyo mpumbavu arudiavyo upumbavu wake.

12 Je, unamwona mtu ajionaye mwenye hekima

machoni pake mwenyewe?

Liko tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake.

13 Mvivu husema, “Yuko simba barabarani,

simba mkali anazunguka mitaa!”

14 Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake,

ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake.

15 Mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

naye hushindwa kuurudisha tena kinywani mwake.

16 Mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe,

kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.

17 Kama yeye amkamataye mbwa masikio,

ndivyo alivyo mtu apitaye njiani na kujiingiza kwenye ugomvi usiomhusu.

18 Kama mtu mwendawazimu

atupaye vijinga vya moto au mishale ya kufisha,

19 ndivyo alivyo mtu amdanganyaye jirani yake na kusema,

“Nilikuwa nikifanya mzaha tu!”

20 Bila kuni moto huzimika,

pasipo uchongezi ugomvi humalizika.

21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka na kama kuni kwenye moto,

ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi.

22 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu,

huingia sehemu za ndani sana za mtu.

23 Kama rangi ing’aayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo

ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.

24 Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake,

lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.

25 Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini,

kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.

26 Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu,

lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.

27 Kama mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake,

kama mtu akivingirisha jiwe, litamrudia.

28 Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza,

nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/26-7ddee7da96e3fbf1331eb895a9ff5efa.mp3?version_id=1627—

Mithali 27

1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,

kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.

2 Mwache mwingine akusifu,

wala si kinywa chako mwenyewe;

mtu mwingine afanye hivyo

na si midomo yako mwenyewe.

3 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,

lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito

zaidi kuliko hivyo vyote viwili.

4 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,

lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?

5 Afadhali karipio la wazi

kuliko upendo uliofichika.

6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,

bali busu la adui ni udanganyifu.

7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,

bali kwa mwenye njaa

hata kile kilicho kichungu

kwake ni kitamu.

8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,

ndivyo alivyo mtu atangatangaye

mbali na nyumbani mwake.

9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,

nao uzuri wa rafiki huchipuka

kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.

10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,

tena usiende nyumbani mwa ndugu yako

wakati umepatwa na maafa.

Bora jirani wa karibu

kuliko ndugu aliye mbali.

11 Mwanangu, uwe na hekima,

nawe ulete furaha moyoni mwangu,

ndipo nitakapoweza kumjibu ye yote

anitendaye kwa dharau.

12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

bali mjinga huendelea mbele nayo ikamtesa.

13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana

kwa ajili ya mgeni;

lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo

kwa ajili ya mwanamke mgeni.

14 Kama mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu

asubuhi na mapema,

itahesabiwa kama ni laana.

15 Mke mgomvi ni kama

matone yasiyokoma ya siku ya mvua.

16 Kumzuia yeye ni kama kuuzuia upepo

au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.

17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,

ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.

18 Yeye atunzaye mtini atakula tunda lake,

naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.

19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji,

ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonyesha alivyo.

20 Kuzimu na uharibifu havishibi

kadhalika macho ya mwanadamu.

21 Kalibu ni kwa ajili ya fedha

na tanuru kwa ajili ya dhahabu,

bali mtu hupimwa kwa sifa azipokeazo.

22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,

ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,

hutauondoa upumbavu wake.

23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako

ya kondoo na mbuzi,

angalia kwa bidii ng’ombe zako.

24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,

nayo taji haidumu vizazi vyote.

25 Wakati majani makavu yameondolewa

na mapya yamechipua,

nayo majani toka milimani yamekusanywa,

26 wana-kondoo watakupatia mavazi

na mbuzi thamani ya shamba.

27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi

kukulisha wewe na jamaa yako,

na kuwalisha watumishi wako wa kike.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/27-52269f3e7dd2363a0399a4e52e2375de.mp3?version_id=1627—

Mithali 28

1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna ye yote anayemfukuza,

bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2 Wakati nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi,

bali mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.

3 Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi

ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao.

4 Wale waiachao sheria huwasifu waovu,

bali wale waishikao sheria huwapinga.

5 Watu wabaya hawaelewi haki,

bali wale wamtafutaoBwanawanaielewa kikamilifu.

6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama

kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.

7 Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye hekima,

bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.

8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno

hukusanya kwa ajili ya mwingine,

ambaye atamhurumia maskini.

9 Kama mtu ye yote akikataa kusikia sheria,

hata maombi yake ni chukizo.

10 Yeye ambaye humwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya,

ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe,

bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.

11 Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe,

bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.

12 Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa,

bali mwovu atawalapo, watu hujificha.

13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

bali ye yote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humchaBwana,

bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu

huangukia kwenye taabu.

15 Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye,

divyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge.

16 Mtawala dhalimu hana akili,

bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu

atafurahia maisha marefu.

17 Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua

atakuwa mtoro mpaka kufa;

mtu ye yote na asimsaidie.

18 Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama

hulindwa salama,

bali yeye ambaye njia zake ni potovu

ataanguka ghafula.

19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

bali afuataye mambo ya upuzi

atakuwa na umaskini wa kumtosha.

20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,

bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka

hataacha kuadhibiwa.

21 Kuonyesha upendeleo si vizuri,

hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.

22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,

naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.

23 Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi,

kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.

24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye

na kusema, “Si kosa,”

yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.

25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina,

bali yule amtegemeayeBwanaatafanikiwa.

26 Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu,

bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.

27 Yeye ampaye maskini

hatapungukiwa na kitu cho chote,

bali yeye awafumbiaye maskini macho

hupata laana nyingi.

28 Wakati mwovu atawalapo,

watu huenda mafichoni,

bali mwovu anapoangamia,

wenye haki hufanikiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/28-c9b27f4f9e96255ef117c7d4b8b3ea4d.mp3?version_id=1627—

Mithali 29

1 Mtu anayeendelea kuwa na shingo ngumu baada ya maonyo mengi,

ataangamia ghafula, wala hapati dawa.

2 Wenye haki wanapostawi, watu hufurahi;

waovu watawalapo, watu hulia kwa huzuni.

3 Mtu apendaye hekima huleta furaha kwa baba yake,

bali aambatanaye na kahaba hutapanya mali yake.

4 Kwa haki mfalme huipa nchi uthabiti,

bali mfalme aliye na tamaa ya rushwa huiangamiza.

5 Ye yote amsifuye jirani yake isivyostahili,

anautandaza wavu kuitega miguu yake.

6 Mtu mbaya hutegwa na dhambi yake mwenyewe

bali mwenye haki huweza kuimba na kufurahi.

7 Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini,

bali mwovu hajishughulishi na hilo.

8 Wenye mzaha huuchochea mji,

bali watu wenye hekima hugeuzia mbali hasira.

9 Kama mwenye hekima akienda mahakamani na mpumbavu,

mpumbavu hukasirika na kudhihaki, wala hakuna amani.

10 Watu wamwagao damu humchukia mtu mwadilifu

na hutafuta kumwua mtu mnyofu.

11 Mpumbavu huonyesha hasira yake yote,

bali mwenye hekima hujizuia.

12 Kama mtawala akisikiliza uongo,

maafisa wake wote huwa waovu.

13 Mtu maskini na mtu anayeonea wanafanana kwa jambo hili:

Bwanahutia nuru macho yao wote wawili.

14 Kama mfalme akiwaamua maskini kwa haki,

kiti chake cha enzi kitakuwa thabiti siku zote.

15 Fimbo ya maonyo hutia hekima,

bali mtoto aliyeachiwa bila maonyo

humwaibisha mama yake.

16 Wakati waovu wanapostawi,

pia dhambi vivyo hivyo,

lakini wenye haki wataliona anguko lao.

17 Mrudi mwanao, naye atakupa amani,

atakufurahisha nafsi yako.

18 Mahali pasipo na maono, watu huangamia,

bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.

19 Mtumishi hawezi kuonywa kwa maneno matupu,

ajapoelewa, hataitikia.

20 Je, unamwona mtu azungumzaye kwa haraka?

Kuna matumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko yeye.

21 Kama mtu akimdekeza mtumishi wake tangu ujanani,

atamletea sikitiko mwishoni.

22 Mtu mwenye hasira huchochea ugomvi,

naye mtu mwenye hasira ya haraka

hutenda dhambi nyingi.

23 Kiburi cha mtu humshusha,

bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu

hupata heshima.

24 Anayekubaliana na mwizi ni adui wa nafsi yake mwenyewe;

huapishwa lakini hathubutu kushuhudia.

25 Kuwaogopa watu huwa ni mtego,

bali ye yote amtumainiayeBwanaatakuwa salama.

26 Watu wengi hutafuta kusikilizwa na mtawala,

bali mtu hupata haki kutoka kwaBwana.

27 Mwenye haki huwachukia sana wasio waaminifu;

waovu huwachukia sana wenye haki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/29-a0bd8a50165e60899aeb735a8ea5d0ed.mp3?version_id=1627—

Mithali 30

Mithali Za Aguri

1 Mithali za Aguri mwana wa Yake, mausia:

Huyu mtu alimwambia Ithieli,

naam, Ithieli na Ukali:

2 “Mimi ni mjinga kuliko wanadamu wote;

sina ufahamu wa kibinadamu.

3 Sijajifunza hekima,

wala sina maarifa ya kumjua yeye Aliye Mtakatifu.

4 Ni nani ameshapanda mbinguni na kushuka?

Ni nani ameshakusanya upepo

kwenye vitanga vya mikono yake?

Ni nani ameshafungia maji kwenye nguo yake?

Ni nani ameimarisha miisho yote ya dunia?

Jina lake ni nani na mwanawe anaitwa nani?

Niambie kama unajua!

5 “Kila neno la Mungu ni kamilifu;

yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia.

6 Usiongeze kwenye maneno yake,

ama atakukemea na kukuthibitisha kuwa mwongo.

7 “Ninakuomba vitu viwili, EeBwana;

usininyime kabla sijafa:

8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;

usinipe umaskini wala utajiri,

bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.

9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana

na kusema, ‘Bwanani nani?’

Au nisije nikawa maskini nikaiba,

nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.

10 “Usimchongee mtumishi kwa bwana wake,

asije akakulaani, ukapatilizwa kwalo.

11 “Wako watu wale ambao huwalaani baba zao

na wala hawawabariki mama zao;

12 wale ambao ni safi machoni pao wenyewe

kumbe hawakuoshwa uchafu wao;

13 wale ambao daima macho yao ni ya kiburi,

ambao kutazama kwao ni kwa dharau;

14 wale ambao meno yao ni panga

na ambao mataya yao yamewekwa visu

kuwaangamiza maskini katika nchi,

na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu.

15 “Mruba anao binti wawili waliao,

‘Nipe! Nipe!’

“Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe,

naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’:

16 Ni kaburi, tumbo lisilozaa,

nchi, isiyoshiba maji kamwe,

na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’

17 “Jicho lile limdhihakilo baba,

lile linalodharau kumtii mama,

litang’olewa na kunguru wa bondeni,

litaliwa na tai.

18 “Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana,

naam, vinne nisivyovielewa:

19 Ni mwendo wa tai katika anga,

mwendo wa nyoka juu ya mwamba,

mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari,

nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.

20 “Huu ndio mwendo wa mwanamke mzinzi,

hula akapangusa kinywa chake na kusema,

‘Sikufanya cho chote kibaya.’

21 “Kwa mambo matatu nchi hutetemeka,

naam, kwa mambo manne haiwezi kuvumilia:

22 Mtumwa awapo mfalme,

mpumbavu ashibapo chakula,

23 mwanamke asiyependwa aolewapo,

naye mtumishi wa kike achukuapo nafasi ya bibi yake.

24 “Vitu vinne duniani vilivyo vidogo,

lakini vina akili nyingi sana:

25 Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo,

hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi.

26 Pelele ni viumbe vyenye uwezo mdogo

hata hivyo hujitengenezea nyumba zao kwenye miamba.

27 Nzige hawana mfalme,

hata hivyo huenda pamoja vikosi vikosi.

28 Mjusi anaweza kushikwa kwa mkono,

hata hivyo huonekana katika majumba ya kifalme.

29 “Viko vitu vitatu ambavyo vinapendeza katika mwendo wao,

naam, vinne ambavyo hutembea kwa mwendo wa madaha:

30 simba, mwenye nguvu miongoni mwa wanyama,

asiyerudi nyuma kwa cho chote;

31 jogoo atembeaye kwa maringo, pia beberu,

naye mfalme pamoja na jeshi lake lililomzunguka.

32 “Ikiwa umefanya upumbavu na ukajitukuza mwenyewe,

au kama umepanga mabaya,

piga kinywa chako kofi.

33 Kwa maana kama vile kusukasuka maziwa hutoa siagi,

na pia kule kufinya pua hutoa damu,

kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/30-15e152ecb99384ffbe2c5150455bf405.mp3?version_id=1627—