Waebrania 8

Kuhani Mkuu Wa Agano Jipya

1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni,

2 yeye ahudumuye katika patakatifu, pa hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si mwanadamu.

3 Kila Kuhani Mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.

4 Kama angelikuwa duniani, hangelikuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.

5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Mose alionywa alipokaribia kujenga hema, akiambiwa: “Hakikisha kuwa unafanya kila kitu sawasawa na kile kielelezo ulichoonyeshwa kule mlimani.”

6 Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora zaidi kuliko yao kama vile lile Agano ambalo yeye ni mjumbe wake lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani, nalo limewekewa misingi juu ya ahadi zilizo bora zaidi.

7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile Agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.

8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema:

“Siku zinakuja, asema Bwana,

nitakapofanya Agano jipya

na nyumba ya Israeli

na nyumba ya Yuda.

9 Agano langu halitakuwa kama lile

nililofanya na baba zao

nilipowashika mkono

ili kuwatoa katika nchi ya Misri,

kwa kuwa hawakuendelea kuwa waaminifu katika Agano langu,

nami nikawaacha,

asema Bwana.

10 Baada ya siku zile, hili ndilo Agano nitakalofanya

na nyumba ya Israeli, asema Bwana.

Nitaweka sheria zangu katika nia zao

na kuziandika katika mioyo yao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

wala mtu hatamfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’

kwa sababu wote watanijua mimi,

tangu aliye mdogo wa wote hadi aliye mkuu sana.

12 Kwa kuwa nitasamehe uovu wao,

wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”

13 Kwa kuliita Agano hili “jipya” Mungu amefanya lile Agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/8-da391403df16dc980a95b56a1ce4abd0.mp3?version_id=1627—

Waebrania 9

Ibada Katika Hema La Kidunia

1 Basi Agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia.

2 Hema lilitengenezwa, katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu, hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu.

3 Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu,

4 ambako ndiko kulikokuwa na ile madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba na lile Sanduku la Agano lililofunikwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye ile mana, ile fimbo ya Aroni iliyochipuka na vile vibao vya mawe vya Agano.

5 Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.

6 Basi vitu hivi vilikuwa vimepangwa, kwamba makuhani wakiingia daima katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada,

7 lakini ni Kuhani Mkuu peke yake ndiye aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema, tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, lakini si bila kuchukua damu ambayo angetoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu waliotenda dhambi bila kukusudia.

8 Kwa njia hii, Roho Mtakatifu alikuwa anaonyesha kwamba maadamu ile hema ya kwanza ilikuwa bado imesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakafifu ilikuwa bado haijafunguliwa.

9 Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonyesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu.

10 Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.

Damu Ya Kristo

11 Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu.

12 Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama, lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele.

13 Damu ya mbuzi na ya mafahali na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa hata kuwaondolea uchafu wa nje.

14 Basi si zaidi sana damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa kutusafisha dhamiri zetu, kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

15 Kwa sababu hii Kristo ni mjumbe wa Agano Jipya, ili kwamba wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele, yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka katika dhambi walizozitenda chini ya Agano la kwanza.

16 Kwa habari ya wosia, ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa,

17 kwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu akishakufa, kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika akiwa bado yuko hai.

18 Hii ndiyo sababu hata lile Agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu.

19 Wakati Mose alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote.

20 Akisema, “Hii ndiyo damu ya Agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.”

21 Vivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye lile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada.

22 Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.

23 Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi.

24 Kwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu.

25 Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile Kuhani Mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe.

26 Ingelikuwa hivyo, ingelimpasa Kristo kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu.

27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu,

28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi, naye atakuja mara ya pili, si ili kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/9-f44d655b87c155325a0281f316f39de8.mp3?version_id=1627—

Waebrania 10

Dhabihu Ya Kristo Ni Mara Moja Tu

1 Kwa maana Torati ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka, kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu.

2 Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi.

3 Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka,

4 kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

5 Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema:

“Dhabihu na sadaka hukuzitaka,

bali mwili uliniandalia;

6 sadaka za kuteketezwa na za dhambi

hukupendezwa nazo.

7 Ndipo niliposema, ‘Tazama niko hapa,

kama nilivyoandikiwa katika kitabu,

Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ”

8 Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe).

9 Kisha akasema “Tazama niko hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili.

10 Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu.

11 Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi.

12 Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu.

13 Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake,

14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

15 Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:

16 “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao

baada ya siku hizo, asema Bwana.

Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,

na kuziandika katika nia zao.”

17 Kisha aongeza kusema:

“Dhambi zao na kutokutii kwao

sitakumbuka tena.”

18 Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yo yote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.

Wito Wa Kuvumilia

19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu,

20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake,

21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu,

22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi.

23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.

24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema.

25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi ya kukutana, tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi.

27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao utakaowaangamiza adui za Mungu.

28 Ye yote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu.

29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema?

30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Kulipiza kisasi ni juu yangu; mimi nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.”

31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

32 Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo mkiisha kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu.

33 Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani, wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliofanyiwa hivyo.

34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno.

36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi.

37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo tu,

“Yeye ajaye atakuja wala hatakawia.

38 Lakini mwenye haki wangu

ataishi kwa imani.

Naye kama akisitasita

sina furaha naye.”

39 Lakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/10-428accb1311af1d50bf6c5f3c6f650c1.mp3?version_id=1627—

Waebrania 11

Maana Ya Imani

1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni udhahiri wa mambo yasiyoonekana.

2 Naam, kwa imani baba zetu wa kale walishuhudiwa.

3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana viliumbwa kwa vitu visivyoonekana.

Mfano Wa Abeli, Enoki Na Noa

4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.

5 Kwa imani Enoki alitwaliwa kutoka katika maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu.

6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana ye yote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

7 Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

Imani Ya Abrahamu

8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda.

9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni, akaishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

11 Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angelitimiza ahadi yake.

12 Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.

13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani.

14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.

15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko.

16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.

17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu.

18 Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu, “Uzao wako utahesabiwa kwa njia ya Isaki,”

19 Abrahamu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaki kutoka kwa wafu na kwa kusema kwa mfano alimpata tena Isaki kutoka kwa wafu.

20 Kwa imani Isaki alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.

21 Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.

22 Kwa imani, Yosefu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.

Imani Ya Mose

23 Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.

25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu.

26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye.

27 Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme, alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho.

28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.

Imani Ya Mashujaa Wengine Wa Israeli

29 Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamukama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.

30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.

31 Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.

32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii,

33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, walipokea ahadi za Mungu, walifunga vinywa vya simba,

34 walizima makali ya miali ya moto, waliepuka kuuawa kwa upanga, udhaifu wao ukageuka kuwa nguvu, walikuwa hodari vitani wakayashinda majeshi ya wageni na kuyafukuza.

35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi.

36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani.

37 Walipigwa kwa mawe, walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno, waliuawa kwa upanga, walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, waliteswa na kutendwa mabaya,

38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.

39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa.

40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/11-933f13d092f3ced43e2c0ccf2de158f4.mp3?version_id=1627—

Waebrania 12

Mungu Huwaadibisha Wanawe

1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu.

2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa Mungu.

3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu.

5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema:

“Mwanangu, usidharau kuadibishwa na Bwana,

wala usikate tamaa akikukemea,

6 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,

na humwadhibu kila mmoja

anayemkubali kuwa mtoto wake.”

7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake?

8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali.

9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?

10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake.

11 Kuadibishwa wakati wo wote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.

12 Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea.

13 Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe.

Onyo Dhidi Ya Kuikataa Neema Ya Mungu

14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao, hakuna mtu atakayemwona Bwana.

15 Angalieni sana mtu ye yote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.

16 Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza.

17 Mnajua kwamba baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

18 Hamjaufikia mlima ule uwezao kuguswa na ambao unawaka moto, wala kwenye giza, utusitusi na dhoruba,

19 kwenye mlio wa tarumbeta, au kwenye sauti isemayo maneno ya kutisha kiasi ambacho wale walioisikia waliomba wasiambiwe neno jingine zaidi,

20 kwa sababu wasingeliweza kustahimili neno lile lililoamriwa: “Hata kama mnyama atagusa mlima huu, atapigwa mawe.”

21 Waliyoyaona yalikuwa ya kutisha kiasi kwamba Mose alisema, “Ninatetemeka kwa hofu.”

22 Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia,

23 kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa,

24 kwa Yesu mjumbe wa Agano Jipya na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Abeli.

25 Angalieni, msije mkamkataa yeye anenaye. Ikiwa wao hawakuepuka adhabu walipomkataa yeye aliyewaonya hapa duniani, sisi je, tutaokokaje tusipomsikiliza yeye anayetuonya kutoka mbinguni?

26 Wakati ule sauti yake ilitetemesha dunia, lakini sasa ameahidi, “Kwa mara moja tena nitatetemesha si nchi tu bali na mbingu pia.”

27 Maneno haya “kwa mara moja tena” yanaonyesha kuondoshwa kwa vile vitu vinavyoweza kuondoshwa, yaani vile vitu vilivyoumbwa, ili kusudi vibaki vile tu visivyoweza kutetemeshwa.

28 Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ule ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inavyompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji,

29 kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/12-9a2a685b842b5df7537837335146319f.mp3?version_id=1627—

Waebrania 13

Huduma Inayompendeza Mungu

1 Upendo wa kidugu na udumu.

2 Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua.

3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kama vile nanyi mmefungwa pamoja nao, pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kama vile ni ninyi wenyewe mnateswa.

4 Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote.

5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

“Kamwe sitakuacha,

wala sitakupungukia.”

6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

“Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

Mwanadamu atanitenda nini?”

7 Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao.

8 Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele.

9 Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria.

10 Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.

11 Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.

12 Vivyo hivyo Yesu naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe.

13 Kwa hiyo basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba.

14 Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.

15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani, matunda ya midomo inayolikiri Jina lake.

16 Msiache kutenda mema na kushirikiana vile mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

17 Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa hesabu. Watiini ili kwamba wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.

18 Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia.

19 Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.

Maombi Ya Kuwatakia Baraka

20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo,

21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, ili atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.

Maneno Ya Mwisho Na Salamu

22 Ndugu zangu, nawasihi mchukuliane na maneno yangu ya maonyo, kwa kuwa nimewaandikia waraka mfupi tu.

23 Nataka ninyi mjue kwamba ndugu yetu Timotheo amefunguliwa kutoka gerezani. Akifika mapema, nitakuja pamoja naye kuwaona.

24 Wasalimuni viongozi wenu wote na watakatifu wote. Wale wa kutoka Italia wanawasalimu.

25 Neema iwe nanyi nyote. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/13-7b9f81e9c84fd739294c0bb5b3412313.mp3?version_id=1627—

Filemoni 1

1 Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu:

Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi mwenzetu,

2 kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:

3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani Na Maombi

4 Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu,

5 kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote.

6 Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo.

7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

Maombi Ya Paulo Ya Kumtetea Onesmo

8 Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda,

9 lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu,

10 nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesmo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.

11 Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.

12 Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.

13 Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili.

14 Lakini sikutaka kufanya lo lote bila idhini yako, ili wema wo wote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari.

15 Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima.

16 Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.

17 Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe.

18 Kama amekukosea lo lote au kama unamdai cho chote, nidai mimi.

19 Mimi Paulo, ninaandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Si kwamba ninakudai hata nafsi yako mwenyewe.

20 Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo.

21 Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale nisemayo.

22 Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.

Salamu Za Mwisho Na Dua Ya Kuwatakia Heri

23 Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu.

24 Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watenda kazi wenzangu wanakusalimu.

25 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PHM/1-c02c81872025eb392b63e975d28ecde5.mp3?version_id=1627—

Tito 1

1 Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu na ujuzi wa kweli ile iletayo uchaji wa Mungu:

2 imani na ujuzi ulioko katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu,

3 naye kwa wakati wake aliouweka alilidhihirisha neno lake kwa njia ya mahubiri ambayo mimi nimewekewa amana kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu:

4 Kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tunayoshiriki sote:

Neema iwe kwako na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.

Kazi Ya Tito Huko Krete

5 Sababu ya mimi kukuacha huko Krete ni ili uweke kwenye utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwaweka wazee wa kanisa katika kila mji, kama nilivyokuagiza.

6 Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi.

7 Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali.

8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake.

9 Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwafundisha wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.

Walimu Wa Uongo

10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara.

11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu.

12 Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.”

13 Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani,

14 ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli.

15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna cho chote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka.

16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lo lote jema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/TIT/1-7befd35d637fee5a973428fe6b9ae05c.mp3?version_id=1627—

Tito 2

Fundisha Mafundisho Manyofu

1 Lakini kwa habari yako wewe, inakupasa kufundisha kulingana na mafundisho yenye uzima.

2 Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.

3 Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa unyenyekevu unaostahili utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema,

4 ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao,

5 wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu ye yote asije akalikufuru neno la Mungu.

6 Vivyo hivyo, sisitiza vijana wawe na kiasi.

7 Katika kila jambo wewe mwenyewe uwe kielelezo cha matendo mema na katika mafundisho yako uonyeshe unyofu, utaratibu, ukweli

8 na maneno yenye uzima, yale ambayo hayawezi kulaumiwa, hata wale wenye kukupinga watahayari, wakose neno lo lote baya la kusema juu yetu.

9 Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao,

10 wala wasiwaibie, bali watumwa waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwamba kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu kuwa ya kupendeza.

11 Kwa maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa.

12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya kumcha Mungu, katika ulimwengu huu wa sasa, huku

13 tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo,

14 yeye ndiye aliyejitoa nafsi yake kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na bidii katika kutenda mema.

15 Basi wewe fundisha mambo haya; onya na karipia kwa mamlaka yote. Mtu ye yote asikudharau.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/TIT/2-fe35cb1eed1fb802510fac447899d919.mp3?version_id=1627—

Tito 3

Kutenda Mema

1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema.

2 Wasimnenee mtu ye yote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.

3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi.

4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa,

5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu,

6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu,

7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele.

8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.

9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu haya hayana faida tena ni ubatili.

10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena.

11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.

Maneno Ya Mwisho Na Kumtamkia Baraka

12 Mara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.

13 Fanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao.

14 Watu wetu hawana budi kujifunza kujitoa kutenda mema, ili waweze kuwasaidia watu wenye mahitaji ya lazima ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.

15 Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale wanaotupenda katika imani.

Neema iwe nanyi nyote. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/TIT/3-80400f3cf64f758a550f4806e59753d1.mp3?version_id=1627—