Zaburi 50

Ibada Ya Kweli

(Zaburi Ya Asafu)

1 Mwenye Nguvu, Mungu,Bwana,

asema na kuiita dunia,

tangu maawio ya jua

hadi mahali pake liendapo kutua.

2 Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,

Mungu anaangaza.

3 Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,

moto uteketezao unamtangulia,

akiwa amezungukwa na tufani kali.

4 Anaziita mbingu zilizo juu

na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:

5 “Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,

waliofanya agano nami kwa dhabihu.”

6 Nazo mbingu zinatangaza haki yake,

kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.

7 “Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema,

Ee Israeli, nami nitawashuhudia dhidi yenu:

Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.

8 Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako,

au sadaka zako za kuteketezwa,

ambazo daima ziko mbele zangu.

9 Sina haja ya fahali wa banda lako,

au mbuzi wa zizi lako.

10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu,

nayo makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.

11 Ninamjua kila ndege mlimani,

nao viumbe wa kondeni ni wangu.

12 Kama ningekuwa na njaa nisingewaambia ninyi,

kwa maana ulimwengu ni wangu,

pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.

13 Je, mimi hula nyama ya mafahali

au kunywa damu ya mbuzi?

14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,

timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,

15 na uniite siku ya taabu;

nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”

16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema:

“Una haki gani kunena sheria zangu

au kuchukua Agano langu midomoni mwako?

17 Unachukia mafundisho yangu

na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

18 Unapomwona mwizi, unaungana naye,

unapiga kura yako pamoja na wazinzi.

19 Unakitumia kinywa chako kwa mabaya

na kuuongoza ulimi wako kwa hila.

20 Wanena daima dhidi ya ndugu yako

na kumsingizia mwana wa mama yako.

21 Mambo haya unayafanya nami nimekaa kimya,

ukafikiri Mimi nami ni kama wewe.

Lakini nitakukemea

na kuweka mashtaka mbele yako.

22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu,

ama sivyo nitawararua vipande vipande,

wala hapatakuwepo na ye yote wa kuwaokoa:

23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi,

naye aiandaa njia yake jinsi ipasavyo

nitamwonyesha wokovu wa Mungu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/50-ce8e48aa383d466ec190c7d8544492a7.mp3?version_id=1627—

Zaburi 51

Kuomba Msamaha

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Baada Ya Kukemewa Na Nabii Nathani Kwa Kuzini Na Bathsheba)

1 Ee Mungu, unihurumie,

kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,

kwa kadiri ya huruma yako kuu

uyafute makosa yangu.

2 Unioshe na uovu wangu wote

na unitakase dhambi yangu.

3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

ili uthibitike kuwa mkweli unenapo

na kuwa na haki utoapo hukumu.

5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,

mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba

kwa mama yangu.

6 Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,

ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.

7 Unioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,

unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.

8 Unipe kusikia furaha na shangwe,

mifupa uliyoiponda na ifurahi.

9 Uufiche uso wako usiitazame dhambi yangu

na uufute uovu wangu wote.

10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

11 Usinitupe kutoka mbele zako

wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.

12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,

unipe roho ya utii, ili initegemeze.

13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,

na wenye dhambi watakugeukia wewe.

14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye,

niokoe na hatia ya kumwaga damu,

ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.

15 EeBwana, fungua midomo yangu,

na kinywa changu kitatangaza sifa zako.

16 Wewe hupendezwi na dhabihu,

au ningaliileta,

hufurahii sadaka za kuteketezwa.

17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,

moyo uliovunjika wenye toba,

Ee Mungu, hutaudharau.

18 Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi,

ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.

19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki,

sadaka nzima za kuteketezwa

za kukupendeza sana,

pia mafahali watatolewa

madhabahuni mwako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/51-d7e86911e361376b39ce500423ad55e4.mp3?version_id=1627—

Zaburi 52

Hukumu Ya Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Utenzi Wa Daudi Baada Ya Doegi, Mwedomu, Kumwendea Sauli Na Kumjulisha Kuwa Daudi Amekwenda Nyumbani Kwa Abimeleki)

1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?

Kwa nini unajivuna mchana kutwa,

wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?

2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi,

ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.

3 Unapenda mabaya kuliko mema,

uongo kuliko kusema kweli.

4 Unapenda kila neno lenye kudhuru,

ewe ulimi wenye hila!

5 Hakika Mungu atakushusha chini

kwa maangamizi ya milele:

atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu

kutoka katika hema yako,

atakung’oa kutoka nchi ya walio hai.

6 Wenye haki wataona na kuogopa,

watamcheka, wakisema,

7 “Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,

bali alitumainia wingi wa utajiri wake

na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”

Neema Ya Mungu

8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni

unaostawi katika nyumba ya Mungu,

nautegemea upendo wa Mungu usiokoma

milele na milele.

9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,

nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.

Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/52-866b48522de5e9ba80791781fd94b645.mp3?version_id=1627—

Zaburi 53

Uovu Wa Wanadamu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Mahalathi. Utenzi Wa Daudi)

1 Mpumbavu anasema moyoni mwake,

“Hakuna Mungu.”

Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa,

hakuna hata mmoja atendaye mema.

2 Mungu huwachungulia wanadamu chini

kutoka mbinguni

aone kama wako wenye akili,

wo wote wanaomtafuta Mungu.

3 Kila mmoja amegeukia mbali,

wameharibika wote pamoja,

hakuna hata mmoja atendaye mema,

naam! Hata mmoja.

4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza,

wale ambao huwala watu wangu

kama watu walavyo mkate,

na ambao hawamwiti Mungu?

5 Hapo watatetemeka kwa hofu kuu,

ambapo hakuna cha kutetemesha.

Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia;

umewaaibisha, kwa sababu Mungu amewadharau.

6 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni!

Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake,

Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/53-b53885ea57ed4462561650e8e252af99.mp3?version_id=1627—

Zaburi 54

Kuomba Ulinzi Wa Mungu Kutokana Na Adui

(Kwa Mwimbishaji Na Ala Za Nyuzi Za Uimbaji. Utenzi Wa Daudi Wakati Mtu Mmoja Wa Zifu Alipomwendea Sauli Na Kumjulisha Kuwa Daudi Amejificha Kwao)

1 Ee Mungu uniokoe kwa jina lako,

unifanyie hukumu kwa uwezo wako.

2 Ee Mungu, sikia maombi yangu,

usikilize maneno ya kinywa changu.

3 Wageni wananishambulia,

watu wakatili wanayatafuta maisha yangu,

watu wasiomjali Mungu.

4 Hakika Mungu ni msaada wangu,

Bwana ndiye anayenitegemeza.

5 Mabaya na yawarudie wale wanaonisingizia,

kwa uaminifu wako uwaangamize.

6 Nitakutolea dhabihu za hiari;

EeBwana, nitalisifu jina lako

kwa kuwa ni vyema.

7 Kwa maana ameniokoa

kutoka katika shida zangu zote,

macho yangu yameona kwa furaha

ushindi dhidi ya adui zangu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/54-d49c4c9ba5831ca660230c77e7a26ee4.mp3?version_id=1627—

Zaburi 55

Maombi Ya Mtu Aliyesalitiwa Na Rafiki

(Kwa Mwimbishaji: Na Ala Za Uimbaji. Utenzi Wa Daudi)

1 Ee Mungu, sikiliza maombi yangu,

wala usidharau hoja yangu,

2 nisikie na unijibu.

Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa

3 kwa sauti ya adui,

kwa kukaziwa macho na waovu,

kwa sababu wananiletea mateso juu yangu

na kunitukana kwa hasira zao.

4 Moyo wangu umejaa uchungu,

hofu ya kifo imenishambulia.

5 Woga na kutetemeka vimenizunguka,

hofu kuu imenigharikisha.

6 Nilisema, “Laiti ningekuwa na mbawa za njiwa!

Ningeruka niende mbali kupumzika.

7 Ningalitorokea mbali sana

na kukaa jangwani,

8 ningaliharakisha kwenda mahali pa salama,

mbali na tufani kali na dhoruba.”

9 EeBwana, uwatahayarishe waovu

na uwafanye maadui wasielewane semi zao,

maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.

10 Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake,

uovu na dhuluma vimo ndani yake.

11 Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini,

vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.

12 Kama aliyenitukana ni adui yangu ningevumilia,

kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,

ningejificha asinione.

13 Kumbe ni wewe, mwenzangu,

mshiriki na rafiki yangu wa karibu,

14 ambaye wakati fulani tulifurahia ushirika mzuri

tulipokuwa tukienda katikati ya umati

hekaluni mwa Mungu.

15 Kifo na kiwajilie adui zangu ghafula,

na washuke kuzimu wangali hai,

kwa maana ubaya upo ndani yao.

16 Lakini ninamwita Mungu,

nayeBwanahuniokoa.

17 Jioni, asubuhi na adhuhuri

ninalia kwa huzuni,

naye husikia sauti yangu.

18 Huniokoa nikawa salama kutoka katika vita

vilivyopangwa dhidi yangu,

ingawa watu wengi hunipinga.

19 Mungu anayemiliki milele,

atawasikia na kuwaadhibu,

watu ambao hawabadilishi njia zao

na wala hawana hofu ya Mungu.

20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake,

naye huvunja agano lake.

21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi,

hata hivyo vita vimo moyoni mwake,

maneno yake mororo kuliko mafuta,

hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.

22 MtwikeBwanafadhaa zako,

naye atakutegemeza,

hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

23 Lakini wewe, Ee Mungu,

utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.

Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,

hawataishi nusu ya siku zao.

Lakini mimi, ninakutumaini wewe.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/55-3175e503e9a8a5521761076cc2711731.mp3?version_id=1627—

Zaburi 56

Kumtumaini Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Njiwa Mkimya Wa Mbali. Utenzi Wa Daudi Baada Ya Kukamatwa Na Wafilisti Huko Gathi)

1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;

mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.

2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,

wengi wananishambulia kwa kiburi chao.

3 Wakati ninapoogopa,

nitakutumaini wewe.

4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.

Mwanadamu apatikanaye na kufa,

atanitenda nini?

5 Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu,

siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.

6 Wanapatana kunifanyia ubaya na kujificha,

wanatazama hatua zangu,

wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.

7 Kwa vyo vyote wasiepuke,

Ee Mungu katika hasira yako yaangushe mataifa.

8 Andika maombolezo yangu,

orodhesha machozi yangu katika gombo lako:

je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?

9 Ndipo adui zangu hugeuzwa nyuma

ninapoita msaada.

Kwa hili nitajua kwamba Mungu

yuko upande wangu.

10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

katikaBwana, ambaye neno lake ninalisifu,

11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa.

Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako,

nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.

13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti

na miguu yangu kwenye kujikwaa,

ili kwamba niweze kuenenda mbele za Mungu

katika nuru ya uzima.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/56-f0003c24e12c7c001b28418bb94b4285.mp3?version_id=1627—

Zaburi 57

Kuomba Msaada

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Usiharibu! Utenzi Wa Daudi Baada Ya Kumponyoka Sauli Pangoni)

1 Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,

kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.

Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia

mpaka maafa yapite.

2 Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,

Mungu atimizaye makusudi yake kwangu.

3 Hutuma kutoka mbinguni na kuniokoa,

akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;

Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.

4 Niko katikati ya simba,

nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kuu,

watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,

ambao ndimi zao ni panga kali.

5 Ee Mungu, utukuzwe, juu mbinguni,

utukufu wako na uenee duniani kote.

6 Waliitegea miguu yangu nyavu,

nikainamishwa chini na dhiki.

Wamechimba shimo katika njia yangu,

lakini wametumbukia humo wao wenyewe.

7 Ee Mungu, moyo wangu uko imara,

naam moyo wangu uko imara,

nitaimba na kupiga vinanda.

8 Amka, nafsi yangu!

Amka, kinubi na zeze!

Nitayaamsha mapambazuko.

9 Nitakusifu wewe, EeBwana,

katikati ya mataifa,

nitaimba habari zako,

katikati ya jamaa za watu.

10 Kwa maana upendo wako,

waenea hadi mbinguni,

uaminifu wako unazifikia anga.

11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,

utukufu wako na uwe duniani pote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/57-1a616b85bc55b04c8c07c200ab7055be.mp3?version_id=1627—

Zaburi 58

Mungu Kuwaadhibu Waovu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Usiharibu! Utenzi Wa Daudi)

1 Enyi watawala, Je, kweli mwanena kwa haki?

Je, mnahukumu kwa unyofu

miongoni mwa watu?

2 La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu,

na mikono yenu hupima jeuri duniani.

3 Waovu ni wapotovu hata tangu kuzaliwa kwao,

toka tumboni mwa mama zao

ni wakaidi na husema uongo.

4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka,

kama ile ya nyoka mwenye sumu kali

ambaye ameziba masikio yake,

5 ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi,

hata kama mganga angeagua

kwa ustadi kiasi gani.

6 Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao;

EeBwana, vunja meno makali ya hao simba!

7 Wana na watoweke kama maji yatiririkayo kwa kasi,

wavutapo pinde zao,

mishale yao na iwe butu.

8 Kama konokono ayeyukavyo akitembea,

kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu,

na wasilione jua.

9 Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba,

zikiwa mbichi au kavu,

waovu watakuwa

wamefagiliwa mbali.

10 Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi,

wakati wakichovya nyayo zao

katika damu ya waovu.

11 Ndipo wanadamu watasema,

“Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu,

hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/58-08ae4a791ab7ffb065875e6c58cfcf43.mp3?version_id=1627—

Zaburi 59

Kuomba Ulinzi Wa Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Usiharibu. Utenzi Wa Daudi Wakati Sauli Alipotuma Wapelelezi Wamwue)

1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,

unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.

2 Uniponye na watu watendao mabaya,

uniokoe kutokana na wamwagao damu.

3 Tazama wanavyonivizia!

Watu wakali wanajiunga pamoja

kwa ubaya dhidi yangu,

EeBwana, mimi sijakosea

wala kutenda dhambi.

4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.

Inuka unisaidie,

uone hali yangu mbaya!

5 EeBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli!

Zinduka uyaadhibu mataifa yote,

usionyeshe huruma kwa wasaliti.

6 Hurudi wakati wa jioni,

wakibweka kama mbwa,

wakiuzungukazunguka mji.

7 Tazama yale wanayotema kutoka katika vinywa vyao,

hutema upanga kutoka katika midomo yao,

nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”

8 Lakini wewe,Bwana, uwacheke;

unayadharau mataifa hayo yote.

9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,

wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

10 Mungu wangu unipendaye.

Mungu atanitangulia,

naye atanifanya niwatazame kwa furaha

wale wanaonisingizia.

11 EeBwana, ngao yetu, usiwaue,

au sivyo watu wangu watasahau.

Katika uwezo wako wafanye watangetange

na uwashushe chini.

12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,

kwa ajili ya maneno ya midomo yao,

waache wanaswe katika kiburi chao.

Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,

13 wateketeze katika ghadhabu,

wateketeze hadi wasiwepo tena.

Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia

kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.

14 Hurudi jioni,

wakibweka kama mbwa,

wakiuzunguka zunguka mji.

15 Wanatangatanga wakitafuta chakula

wasipotosheka hubweka kama mbwa.

16 Lakini mimi nitaimba juu ya nguvu zako,

wakati wa asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;

kwa maana wewe ndiwe ngome yangu

na kimbilio langu wakati wa shida.

17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa,

wewe, Ee Mungu ndiwe ngome yangu,

Mungu unipendaye.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/59-00e3ed39a1437da771044d392663d592.mp3?version_id=1627—