Zaburi 60

Kuomba Kuokolewa

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Shushani Eduthi. Utenzi Wa Daudi Wa Kufundisha Wakati Alipopigana Na Waaramu Kutoka Aramu-Naharaimu Na Aramu-Soba, Yoabu Aliporudi Nyuma Na Kuwaua Waedomu 12,000 Katika Bonde La Chumvi)

1 Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu,

umekasirika, sasa uturejeshe upya!

2 Umetetemesha nchi na kuipasua;

uiponye na kutengeneza mavunjiko yake,

kwa maana inatetemeka.

3 Umewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa;

umetunywesha mvinyo unaotufanya tupepesuke.

4 Kwa wale wanaokucha wewe,

umewainulia bendera,

ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.

5 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,

ili wale uwapendao waweze kuokolewa.

6 Mungu amenena kutoka mahali patakatifu pake:

“Kwa furaha kuu nitaigawa Shekemu

na kupima Bonde la Sukothi.

7 Gileadi ni yangu na Manase ni yangu,

Efraimu ni kofia yangu ya chuma,

na Yuda ni fimbo yangu ya utawala.

8 Moabu ni sinia langu la kunawia,

juu ya Edomu natupa kiatu changu;

nami nitashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”

9 Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wenye maboma?

Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?

10 Ee Mungu, si wewe, wewe uliyetukataa sisi

na hutoki tena na majeshi yetu?

11 Tupe msaada dhidi ya adui,

kwa maana msaada wa mwanadamu haufai.

12 Mungu akiwa pamoja nasi tutajipatia ushindi,

naye atawakanyaga chini adui zetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/60-1f5cd29a55f6c20cc05ab78c548a317c.mp3?version_id=1627—

Zaburi 61

Kuomba Ulinzi

(Kwa Mwimbishaji: Kwa Ala Za Nyuzi Za Uimbaji. Zaburi Ya Daudi)

1 Ee Mungu, sikia kilio changu,

usikilize maombi yangu.

2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

uniongoze kwenye mwamba

ule ulio juu kuliko mimi.

3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,

ngome imara dhidi ya adui.

4 Natamani kukaa hemani mwako milele

na kupata kimbilio chini ya uvuli wa mbawa zako.

5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu,

umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.

6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake,

miaka yake kwa vizazi vingi.

7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi

mbele za Mungu milele;

amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.

8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako

na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/61-3ac274c7c3493b29ad55324abf7cd5cb.mp3?version_id=1627—

Zaburi 62

Mungu Kimbilio La Pekee

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Yeduthuni. Zaburi Ya Daudi)

1 Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko;

wokovu wangu watoka kwake.

2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu

na wokovu wangu;

yeye ni ngome yangu,

sitatikisika kamwe.

3 Mtamshambulia mtu hata lini?

Je, ninyi nyote mtamtupa chini,

ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika?

4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha

toka mahali pake pa fahari;

wanafurahia uongo.

Kwa vinywa vyao hubariki,

lakini ndani ya mioyo yao hulaani.

5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,

tumaini langu latoka kwake.

6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu

na wokovu wangu;

ndiye ngome yangu, sitatikisika.

7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

ndiye mwamba wangu wenye nguvu

na kimbilio langu.

8 Enyi watu, mtumainini yeye, wakati wote,

mmiminieni yeye mioyo yenu,

kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

9 Binadamu wa ngazi ya chini ni kama pumzi,

wa ngazi ya juu ni uongo;

wakipimwa kwenye mizani,

si cho chote;

wote kwa pamoja ni pumzi tu.

10 Usitumainie vya udhalimu wala

usijivune kwa ajili ya vitu vya wizi,

ingawa utajiri wako utaongezeka,

usiviwekee moyo wako.

11 Jambo moja Mungu amelisema,

mambo mawili nimeyasikia:

Kwamba, Ee Mungu, wewe una nguvu,

12 na kwamba, EeBwana,

wewe ni mwenye upendo.

Hakika utampa kila mtu thawabu

kwa kadiri ya alivyotenda.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/62-a950032ccaebbb5077ac681c630c0766.mp3?version_id=1627—

Zaburi 63

Shauku Kwa Ajili Ya Uwepo Wa Mungu

(Zaburi Ya Daudi Wakati Alipokuwa Katika Jangwa La Yuda)

1 Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu,

nakutafuta kwa moyo wote;

nafsi yangu inakuonea kiu,

mwili wangu unakuonea wewe shauku,

katika nchi kame na iliyochoka

mahali ambapo hapana maji.

2 Nimekuona katika mahali patakatifu

na kuuona uwezo wako na utukufu wako.

3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai,

midomo yangu itakuadhimisha.

4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu,

na kwa jina lako nitainua mikono yangu.

5 Nafsi yangu itatoshelezwa

kama kwa wingi wa vyakula;

kwa midomo iimbayo

kinywa changu kitakusifu wewe.

6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe,

ninawaza juu yako makesha yote ya usiku.

7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu,

chini ya uvuli wa mbawa zako naimba.

8 Nafsi yangu inaambatana nawe,

mkono wako wa kuume hunishika.

9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa,

watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia.

10 Watatolewa wafe kwa upanga,

nao watakuwa chakula cha mbweha.

11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu,

wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu,

bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/63-bb48ec067525b38ebabf85dc1e30c3ea.mp3?version_id=1627—

Zaburi 64

Kuomba Ulinzi Dhidi Ya Maadui

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)

1 Ee Mungu, unisikie, ninapoeleza lalamiko langu,

uyahifadhi maisha yangu kutokana

na vitisho vya adui.

2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu,

kutokana na zile kelele

za kundi la watenda mabaya.

3 Wanaonoa ndimi zao kama panga

na kuelekeza maneno yao

kama mishale ya kufisha.

4 Hutupa mishale kutoka kwenye mavizio

kwa mtu asiye na hatia,

humrushia ghafula bila woga.

5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake

katika mipango mibaya;

huzungumza juu ya kuficha mitego yao,

nao husema, “Ni nani ataiona?”

6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema,

“Tumebuni mpango mkamilifu!”

Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.

7 Bali Mungu atawapiga wao kwa mshale,

nao utawapata ghafula na kuanguka.

8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao

na kuwaleta kwenye maangamizi;

wote wawaonao watatikisa vichwa vyao

kwa dharau.

9 Wanadamu wote wataogopa,

watatangaza kazi za Mungu

na kutafakari yale aliyoyatenda.

10 Wenye haki na wafurahi katikaBwana,

na wakimbilie kwake;

wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/64-0954e5e1243e91350d7b817e5d554bc1.mp3?version_id=1627—

Zaburi 65

Kusifu Na Kushukuru

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi. Wimbo)

1 Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni;

kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.

2 Ee wewe usikiaye maombi,

kwako wewe watu wote watakuja.

3 Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi,

wewe ulisamehe makosa yetu.

4 Heri wale uliowachagua

na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako!

Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako,

mema ya Hekalu lako takatifu.

5 Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki,

Ee Mungu Mwokozi wetu,

tumaini la miisho yote ya duniani

na la bahari zilizo mbali sana,

6 uliyeumba milima kwa uwezo wako,

ukiwa umejivika nguvu,

7 uliyenyamazisha dhoruba za bahari,

ngurumo za mawimbi yake,

na ghasia za mataifa.

8 Wale wanaoishi mbali sana

wanaogopa maajabu yako,

kule asubuhi ipambazukiapo

na kule jioni inakofifilia

umeziita nyimbo za furaha.

9 Waitunza nchi na kuinyeshea,

waitajirisha kwa wingi.

Vijito vya Mungu vimejaa maji

ili kuwapa watu nafaka,

kwa maana wewe umeviamuru.

10 Umeilowesha mifereji yake

na kusawazisha kingo zake;

umeilainisha kwa manyunyu

na kuibariki mimea yake.

11 Umeuvika mwaka taji ya baraka,

magari yako yanafurika kwa wingi.

12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha;

vilima vimevikwa furaha.

13 Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama,

na mabonde yamepambwa kwa mavuno;

vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/65-f12412d24536665e5d22b9fcfae35ba2.mp3?version_id=1627—

Zaburi 66

Kusifu Mungu Kwa Ajili Ya Wema Wake

(Kwa Mwimbishaji: Wimbo. Zaburi)

1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!

2 Imbeni utukufu wa jina lake;

mpeni sifa zake kwa utukufu!

3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!

Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba

adui wananyenyekea mbele zako.

4 Dunia yote yakusujudia,

wanakuimbia wewe sifa,

wanaliimbia sifa jina lako.”

5 Njoni mwone yale Mungu aliyoyatenda,

mambo ya kutisha aliyoyatenda

miongoni mwa wanadamu!

6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu,

wakapita kati ya maji kwa miguu,

njoni, tumshangilie.

7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,

macho yake huangalia mataifa yote,

waasi na wasithubutu kujiinua dhidi yake.

8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,

sauti ya sifa yake na isikike,

9 ameyahifadhi maisha yetu

na kuizuia miguu yetu kuteleza.

10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu,

ukatusafisha kama fedha.

11 Umetuingiza kwenye nyavu

na umetubebesha mizigo mizito

migongoni mwetu.

12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani,

tulipita kwenye moto na kwenye maji,

lakini ulituleta kwenye nchi

iliyojaa utajiri tele.

13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa

na kukutimizia nadhiri zangu:

14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi

na nilizotamka kwa kinywa changu

nilipokuwa katika shida.

15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono

na sadaka za kondoo waume,

nitakutolea mafahali na mbuzi.

16 Njoni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu,

nami niwaambie aliyonitendea.

17 Nilimlilia kwa kinywa changu,

sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.

18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu,

Bwana asingekuwa amenisikiliza;

19 lakini hakika Mungu amenisikiliza

na amesikia sauti yangu katika maombi.

20 Sifa apewe Mungu,

ambaye hakulikataa ombi langu

wala kunizuilia upendo wake!

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/66-70ae261997c556379da49c61557244d9.mp3?version_id=1627—

Zaburi 67

Mataifa Yahimizwa Kumsifu Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Na Ala Za Nyuzi Za Muziki. Zaburi. Wimbo)

1 Mungu uturehemu na kutubariki,

na kutuangazia nuru za uso wako,

2 ili njia zako zijulikane duniani,

wokovu wako katikati ya mataifa yote.

3 Ee Mungu, mataifa na wakusifu,

mataifa yote na wakusifu.

4 Mataifa yote na wafurahi na kuimba kwa shangwe,

kwa kuwa unatawala watu kwa haki

na kuongoza mataifa ya dunia.

5 Ee Mungu, mataifa na wakusifu,

mataifa yote na wakusifu.

6 Ndipo nchi itatoa mazao yake,

naye Mungu, Mungu wetu, atatubariki.

7 Mungu atatubariki

na miisho yote ya dunia itamcha yeye.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/67-2c582af6264c83c4cba031743f9b97c6.mp3?version_id=1627—

Zaburi 68

Wimbo Wa Taifa Wa Shangwe Kwa Ushindi

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi ya Daudi. Wimbo)

1 Mungu na ainuke, watesi wake na watawanyike,

adui zake na wakimbie mbele zake.

2 Kama vile moshi upeperushwavyo na upepo,

vivyo hivyo uwapeperushe mbali,

kama vile nta iyeyukavyo kwenye moto,

vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu.

3 Bali wenye haki na wafurahi,

washangilie mbele za Mungu,

na wafurahi na kushangilia.

4 Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake,

mwinueni juu yeye aendeshwaye juu ya mawingu,

jina lake niBwana,

furahini mbele zake.

5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,

ni Mungu katika makao yake matakatifu.

6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa,

huwaongoza wafungwa wakiimba,

bali waasi huishi katika nchi kame.

7 Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako,

ulipopita nyikani,

8 dunia ilitikisika,

mbingu zikanyesha mvua,

mbele za Mungu, Mungu wa Mlima Sinai,

mbele za Mungu, Mungu wa Israeli.

9 Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi

na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka.

10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko,

kwa wingi wa utajiri wako

uliwapa maskini mahitaji yao.

11 Bwana alitangaza neno,

waliolitangaza neno hilo walikuwa kundi kubwa:

12 “Wafalme na majeshi walikimbia upesi,

watu waliobaki kambini waligawana nyara.

13 Hata ulalapo katikati ya mioto ya kambini,

mabawa ya njiwa wangu, yamefunikwa kwa fedha,

manyoya yake kwa dhahabu ing’aayo.”

14 Wakati Mwenyezialipowatawanya wafalme katika nchi,

ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Salmoni.

15 Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka,

milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka.

16 Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka,

kwa nini mnakazia macho kwa wivu,

katika mlima Mungu anaochagua kutawala,

ambakoBwanamwenyewe ataishi milele?

17 Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu,

na maelfu ya maelfu;

Bwana amekuja kutoka Sinai

kuja katika patakatifu pake.

18 Ulipopanda juu, uliteka mateka,

ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu,

hata kutoka kwa wale walioasi,

ili wewe, EeBwana, upate kuishi huko.

19 Sifa apewe Bwana, Mungu Mwokozi wetu,

ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu.

20 Mungu wetu ni Mungu aokoaye,

BwanaMwenyezi hutuokoa na kifo.

21 Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake,

vichwa vya hao waendao katika njia za dhambi.

22 Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani;

nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,

23 ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako,

huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.”

24 Ee Mungu, maandamano yako yameonekana,

maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu,

yakielekea katika mahali patakatifu pake.

25 Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda,

pamoja nao wako wanawali wakipiga matari.

26 Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa,

msifuniBwanakatika kusanyiko la Israeli.

27 Kuna kabila dogo la Benyamini, likiwaongoza,

wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda,

hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali.

28 Ee Mungu, amuru uwezo wako,

Ee Mungu tuonyeshe nguvu zako,

kama ulivyofanya hapo awali.

29 Kwa sababu ya Hekalu lako la Yerusalemu

wafalme watakuletea zawadi.

30 Mkemee mnyama aliyeko kwenye manyasi,

kundi la mafahali katikati ya ndama za mataifa.

Wakiwa wamenyenyekea na walete minara ya madini ya fedha.

Tawanya mataifa yapendayo vita.

31 Wajumbe watakuja kutoka Misri,

# Kushiatajisalimisha kwa Mungu.

32 Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia,

mwimbieni Bwana sifa,

33 mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu,

yeye angurumaye kwa sauti kuu.

34 Tangazeni uwezo wa Mungu,

ambaye fahari yake iko juu ya Israeli,

ambaye uwezo wake uko katika anga.

35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako,

Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu.

Mungu Asifiwe!

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/68-d8dfb1c4c99c05a6b89a1af668daac70.mp3?version_id=1627—

Zaburi 69

Kilio Cha Kuomba Msaada Wakati Wa Dhiki

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Daudi)

1 Ee Mungu, uniokoe, kwa maana maji

yamenifika shingoni.

2 Ninazama kwenye vilindi vya matope,

pasipo mahali pa kukanyaga;

nimefika kwenye maji makuu,

mafuriko yamenigharikisha.

3 Nimechoka kwa kuomba msaada,

koo langu limekauka.

Macho yangu yanafifia,

nikimtafuta Mungu wangu.

4 Wale wanaonichukia bila sababu

ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;

wengi ni adui bila sababu,

wale wanaotafuta kuniangamiza.

Ninalazimishwa kurudisha

kitu ambacho sikuiba.

5 Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu,

wala maovu yangu hayakufichika kwako.

6 Ee Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

wakutumainio wasiaibishwe

kwa ajili yangu;

wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu,

Ee Mungu wa Israeli.

7 Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,

aibu imefunika uso wangu.

8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,

mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe,

9 kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,

matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.

10 Ninapolia na kufunga,

wao hunitukana kwa kufanya hivyo.

11 Nilipovaa nguo ya gunia,

nilikuwa kitu cha kudharauliwa na watu.

12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga,

nimekuwa wimbo wa walevi.

13 Lakini EeBwana, ninakuomba,

kwa wakati ukupendezao,

katika upendo wako mkuu;

Ee Mungu, unijibu

kwa wokovu wako wa hakika.

14 Uniokoe katika matope,

usiniache nizame;

niokoe na hao wanichukiao,

kutoka kwenye vilindi vya maji.

15 Usiache mafuriko yanigharikishe

au vilindi vinimeze,

au shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.

16 EeBwana, unijibu, kwa wema wa upendo wako;

kwa huruma zako nyingi unigeukie.

17 Usimfiche mtumishi wako uso wako,

uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.

18 Njoo karibu na uniokoe,

nikomboe kwa sababu ya adui zangu.

19 Unajua jinsi ninavyodharauliwa,

kufedheheshwa na kuaibishwa,

adui zangu wote unawajua.

20 Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa,

nimetafuta wa kunihurumia,

lakini sikumpata ye yote,

wa kunituliza, lakini sikumpata ye yote.

21 Waliweka nyongo katika chakula changu

na walinipa siki nilipokuwa na kiu.

22 Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego,

nayo iwe upatilizo na tanzi.

23 Macho yao yatiwe giza ili wasione,

migongo yao na ipinde milele.

24 Uwamwagie ghadhabu yako,

hasira yako kali na iwapate.

25 Mahali pao na pawe mahame,

asiwepo ye yote atakayeishi katika mahema yao.

26 Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi,

na kuzungumza juu ya maumivu

ya wale uliowaumiza.

27 Walipize uovu juu ya uovu,

usiwaache washiriki katika wokovu wako.

28 Wafutwe kutoka kitabu cha uzima

na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.

29 Mimi niko katika maumivu na dhiki;

Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.

30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,

nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.

31 Hili litampendezaBwanakuliko ng’ombe dume,

zaidi ya fahali akiwa

na pembe na kwato zake.

32 Maskini wataona na kufurahi,

ninyi mnaomtafuta Mungu,

mioyo yenu na iishi!

33 Bwanahuwasikia wahitaji

na wala hadharau watu wake waliotekwa.

34 Mbingu na dunia na vimsifu,

bahari na vyote viendavyo ndani yake,

35 kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni

na kuijenga tena miji ya Yuda.

Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki.

36 Watoto wa watumishi wake watairithi

na wale wote walipendao jina lake

wataishi humo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/69-14c7d602a9ec7a028a4fa2d12acf7a7d.mp3?version_id=1627—