2 Timotheo 1

1 Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima uliomo ndani ya Kristo Yesu.

2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa:

Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Shukrani Na Kutiwa Moyo

3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu.

4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha.

5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo mimi ninasadiki sasa wewe pia unayo.

6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu.

7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,

9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu kabla ya kuwako kwa ulimwengu.

10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili.

11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii.

12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.

13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu.

14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.

15 Unajua ya kuwa watu wote katika Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene.

16 Bwana akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara wala hakuionea aibu minyororo yangu.

17 Badala yake, alipokuwa Rumi, alinitafuta kwa bidii mpaka akanipata.

18 Bwana na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TI/1-ec4901cdc1fc953af51c13f643df0866.mp3?version_id=1627—

2 Timotheo 2

Askari Mwema Wa Kristo Yesu

1 Basi, wewe mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu.

2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vile vile.

3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu.

4 Hakuna askari ye yote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari.

5 Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano.

6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno.

7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Mungu atakupa ufahamu katika mambo hayo yote.

8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu,

9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi.

10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

11 Hili ni neno la kuaminiwa:

Kwa maana kama tumekufa pamoja naye,

tutaishi pia pamoja naye.

12 Kama tukistahimili,

pia tutatawala pamoja naye.

Kama tukimkana yeye,

naye atatukana sisi.

13 Kama tusipoamini,

yeye hudumu kuwa mwaminifu,

kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

Mfanyakazi Aliyekubaliwa Na Mungu

14 Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yo yote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia.

15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtenda kazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.

16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu.

17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto

18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako na kupotosha baadhi ya watu.

19 Lakini msingi wa Mungu ulio madhubuti umesimama ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake” tena, “Kila alitajaye jina la Bwana auache uovu.”

20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo, vingine kwa matumizi maalum na vingine kwa matumizi ya kawaida.

21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.

22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi.

24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu.

25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli,

26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TI/2-f743a3b49b28b62e6c3be3269b9f94cf.mp3?version_id=1627—

2 Timotheo 3

Hatari Za Siku Za Mwisho

1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari.

2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu,

3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema,

4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu.

5 Wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo.

6 Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya.

7 Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli.

8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani.

9 Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili.

Paulo Amwagiza Timotheo

10 Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu,

11 mateso na taabu, yaani, yale mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote.

12 Naam, ye yote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa.

13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.

14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani

15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.

16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwafundisha katika haki

17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, ili apate kutenda kila kazi njema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TI/3-ce0abd464658ffcfdc67abde5aeb638c.mp3?version_id=1627—

2 Timotheo 4

Maagizo Ya Mwisho

1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake kwamba:

2 Uhubiri Neno, uwe tayari wakati ufaao na wakati usiofaa, karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.

3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima, badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia.

4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.

5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.

6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.

7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda.

8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile, wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

Maelekezo Ya Binafsi

9 Jitahidi kuja kwangu upesi

10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na amekwenda Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia na Tito amekwenda Dalmatia.

11 Ni Luka peke yake ndiye aliye hapa pamoja nami. Mtafute Marko uje naye kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu.

12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso.

13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.

14 Aleksanda, yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Mungu atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda.

15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu.

16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.

17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kwa kupitia mimi lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka katika kinywa cha simba.

18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen.

Salamu Za Mwisho

19 Wasalimu Prisilana Akila, na wote wa nyumbani kwa Onesiforo.

20 Erasto alibaki Korintho. Nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa.

21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.

22 Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TI/4-1888fb73fa92f723aeccf484ba9d66dd.mp3?version_id=1627—

1 Timotheo 1

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na ya Kristo Yesu tumaini letu.

2 Kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani:

Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Maonyo Dhidi Ya Walimu Wa Uongo

3 Kama nilivyokusihi kuendelea kubaki Efeso, wakati nilipokwenda Makedonia, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo

4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha zisizo na mwisho za majina ya vizazi ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Kimungu utokanao na imani.

5 Kusudi la maagizo haya ni upendo, utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli.

6 Watu wengine wamepotoka kutoka katika haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa,

7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa.

9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru, kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji,

10 kwa wazinzi na wahanithi, wauza watu na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa cho chote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli,

11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi Paulo nimewekea amana.

Neema Ya Mungu Kwa Paulo

12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake.

13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri. Lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutokujua na kutokuamini kwangu.

14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote.

16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili kwamba katika mimi niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini wapate uzima wa milele.

17 Basi, Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vile vita vizuri,

19 ukiishikilia imani na dhamiri njema ambayo wengine wamevikataa na hivyo, wakaangamia kwa habari ya imani yao.

20 Miongoni mwao wako Himenayo na Aleksanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TI/1-409b6376652847daea82368653bf1b12.mp3?version_id=1627—

1 Timotheo 2

Maagizo Kuhusu Kuabudu

1 Awali ya yote, nasihi, kwanza kabisa, naagiza kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote:

2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu.

3 Jambo hili ni jema tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu

4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli.

5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani, mwanadamu Kristo Yesu,

6 aliyejitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake.

7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu Mataifa katika imani na kweli.

8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.

9 Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,

10 bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.

11 Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utii wote.

12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya.

13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva.

14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji.

15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TI/2-c6d36e0052ed47debe344c3ce3fddcba.mp3?version_id=1627—

1 Timotheo 3

Sifa Za Waangalizi

1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri.

2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha,

3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.

4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia.

5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)

6 Asiwe mtu aliyeongoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya Shetani.

7 Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

Sifa Za Mashemasi

8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.

9 Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi.

10 Ni lazima wapimwe kwanza, kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.

11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasiozungumza maneno ya kuwadhuru wengine, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.

12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.

13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.

14 Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba,

15 kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.

16 Bila shaka yo yote, siri ya utauwa ni kubwa:

Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu,

akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,

akaonekana na malaika,

akahubiriwa miongoni mwa mataifa,

akaaminiwa ulimwenguni,

akachukuliwa juu katika utukufu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TI/3-c6237f1099bd9ead7ce85c3ff80fef55.mp3?version_id=1627—

1 Timotheo 4

Maagizo Kwa Timotheo

1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.

2 Mafundisho kama hayo huja kwa kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto.

3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli.

4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu cho chote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani,

5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

Mtumishi Mwema Wa Yesu Kristo

6 Kama ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata.

7 Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee, badala yake, jizoeze kuwa mtauwa.

8 Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.

9 Hili ni neno la kuaminiwa tena lastahili kukubaliwa kabisa,

10 (nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi), kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.

11 Mambo haya yaagize na kuyafundisha.

12 Mtu ye yote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waaminio katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.

13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja.

14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walipokuwekea mikono.

15 Uwe na bidii katika mambo haya, jitolee kwa ajili ya mambo hayo kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako.

16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TI/4-ab3daa3e74806105fc1d4551fc41c28b.mp3?version_id=1627—

1 Timotheo 5

Maagizo Kuhusu Wajane, Wazee Na Watumwa

1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umuonye kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako,

2 wanawake wazee uwatendee kama mama zako na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.

3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli.

4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo, kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe ili wawarudishie wema ule wazazi wao waliowatendea, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu.

5 Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie.

6 Lakini mjane aishiye kwa anasa, amekufa, ingawa anaishi.

7 Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo ye yote wa kulaumiwa.

8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

9 Mjane ye yote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja,

10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.

11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena.

12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza.

13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema.

14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu.

15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.

16 Lakini kama mwanamke ye yote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.

Wazee Wa Kanisa

17 Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha.

18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”

19 Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu.

20 Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa.

21 Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo.

22 Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.

23 Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.

24 Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao.

25 Vivyo hivyo, matendo mema yako dhahiri, na hata yale ambayo si mema hayawezi kufichika.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TI/5-964d1cc4c8192ccd44e575d926556537.mp3?version_id=1627—

1 Timotheo 6

Watumwa

1 Wale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.

2 Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu, badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao.

Mafundisho Ya Uongo Na Utajiri Wa Kweli

3 Ikiwa mtu ye yote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, huyo amejivuna wala hajui kitu cho chote.

4 Yeye ni mgonjwa aliyejaa tamaa ya mabishano na ugomvi ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya

5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa.

7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu cho chote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu.

8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo.

9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka haraka huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu, zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi.

10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

Vitu Vizuri Vya Imani

11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi.

13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri,

14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo,

15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe, yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.

16 Yeye peke yake hapatikani na mauti, ambaye anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie.

18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine.

19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

Maelekezo Ya Binafsi Na Maombi Ya Baraka

20 Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu,

21 ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.

Neema iwe nanyi. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TI/6-dcb4942357e748a02afbf31adbcf6280.mp3?version_id=1627—