Esta 8

Amri Ya Mfalme Kuhusu Wayahudi

1 Siku ile ile Mfalme Ahusuero akampa Malkia Esta shamba la Hamani, adui wa Wayahudi. Naye Mordekai akaja mbele ya mfalme, kwa kuwa Esta alikuwa amesema jinsi anavyohusiana naye.

2 Mfalme akaivua pete yake ya muhuri, ambayo alikuwa amemnyang’anya Hamani, akampa Mordekai naye Esta akamweka Mordekai juu ya shamba la Hamani.

3 Esta alimsihi tena mfalme, akianguka miguuni pake na kulia. Akamwomba akomeshe mpango mwovu wa Hamani, Mwagagi, ambao alikuwa ameupanga dhidi ya Wayahudi.

4 Kisha mfalme alimnyoshea Esta fimbo yake ya utawala ya dhahabu naye aliinuka na kusimama mbele yake.

5 Esta akasema, “Kama ikimpendeza mfalme, nami kama nikipata kibali naye akiona ni jambo lililo sawa kunitendea na kama akipendezwa nami, basi iandikwe amri ya kuzitangua barua zile Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuandika kuangamiza Wayahudi katika majimbo yote ya mfalme.

6 Kwa maana nitawezaje kuvumilia kuona maafa yakiwapata watu wangu? Nitawezaje kuvumilia kuona maangamizi ya jamaa yangu?”

7 Mfalme Ahusuero akamjibu Malkia Esta na Mordekai Myahudi, kusema, “Kwa sababu Hamani aliwashambulia Wayahudi, nimetoa shamba la Hamani kwa Esta, naye ameangikwa kwenye mti wa kunyongea.

8 Basi andika amri nyingine kwa jina la mfalme kwa ajili ya Wayahudi kama unavyoona vyema, kisha uifunge kwa kutia muhuri kwa pete ya mfalme kwa kuwa hakuna andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme linaloweza kutanguliwa.”

9 Mara moja waandishi wa mfalme wakaitwa kwenye siku ya ishirini na tatu, mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani. Wakaandika yote Mordekai aliyoamuru kwa Wayahudi, kwa majemadari, watawala na wakuu wa majimbo 127 kuanzia Bara Hindi mpaka Kushi. Maagizo haya yaliandikwa kwa maandishi ya kila jimbo na kwa lugha ya kila mtu pia kwa Wayahudi kwa maandishi yao wenyewe na lugha yao.

10 Mordekai aliandika nyaraka kwa jina la Mfalme Ahusuero, akazitia muhuri kwa pete ya mfalme na kuzipeleka kwa njia ya matarishi, ambao waliendesha farasi waendao kasi waliozalishwa maalum kwa ajili ya mfalme.

11 Waraka wa mfalme uliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kuwa na haki ya kukusanyika na kujilinda wenyewe; kuharibu, kuua na kuangamiza jeshi lo lote, taifa lo lote au jimbo lile litakalowashambulia wao, wake zao, watoto wao na kuteka mali za adui zao.

12 Siku ambayo iliwekwa kwa Wayahudi kufanya hili katika majimbo yote ya Mfalme Ahusuero ilikuwa siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari.

13 Nakala ya tangazo ilikuwa itolewe kama sheria katika kila jimbo na iweze kujulikana kwa watu wa kila taifa, ili kwamba Wayahudi wawe tayari siku hiyo kulipiza kisasi kwa adui zao.

14 Matarishi wakiwa wamepanda farasi wa kifalme walitoka mbio wakichochewa na agizo la mfalme. Tangazo lilitolewa pia katika ngome ya mji wa Shushani.

15 Mordekai akaondoka mbele ya mfalme akiwa amevaa mavazi ya kifalme ya buluu na nyeupe, taji kubwa la dhahabu na joho la zambarau la kitani safi. Na mji wa Shushani ukasherekea kwa furaha.

16 Kwa maana kwa Wayahudi ulikuwa wakati wa raha na furaha, shangwe na heshima.

17 Katika kila jimbo na katika kila jiji, popote waraka wa mfalme ulipofika, kulikuwepo furaha na shangwe miongoni mwa Wayahudi, pamoja na karamu na kushangilia. Na watu wengi wa mataifa mengine wakajifanya Wayahudi kwa sababu ya kuwahofu Wayahudi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EST/8-48c9197f5672eafeecd5c0ad51ec725c.mp3?version_id=1627—

Esta 9

Ushindi Wa Wayahudi

1 Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia.

2 Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahusuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna ye yote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa.

3 Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai.

4 Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi.

5 Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia.

6 Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume 500.

7 Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha,

8 Poratha, Adalia, Ardatha,

9 Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha,

10 wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara.

11 Mfalme aliarifiwa siku iyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani.

12 Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume 500 na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utafanyiwa.”

13 Esta akajibu, “Ikimpendeza mfalme, uwape ruhusa Wayahudi walioko Shushani warudie amri ya leo kesho pia, na wana wa Hamani kumi wanyongwe mahali pa kunyongea watu.”

14 Basi mfalme akaamuru kwamba hili litendeke. Amri ilitolewa huko Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani.

15 Wayahudi huko Shushani wakakusanyika pamoja siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, nao wakawaua wanaume 300 huko Shushani, lakini hawakuchukua nyara zao.

16 Wakati ule ule, Wayahudi wengine waliokuwa kwenye majimbo ya mfalme, wakakusanyika kujilinda nao wakapata nafuu kutokana na adui zao. Waliua adui zao wapatao 75,000 lakini hawakugusa nyara zao.

17 Hili lilitendeka siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari na siku ya kumi na nne walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.

Kusherehekea Purimu

18 Wayahudi huko Shushani, hata hivyo, walikuwa wamekusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, pia siku ya kumi na tano walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.

19 Ndiyo sababu Wayahudi wanaokaa vijijini na katika miji midogo, huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kama siku ya furaha na karamu, siku ambayo hupeana zawadi.

20 Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walioko katika majimbo ya Mfalme Ahusuero, majimbo yaliyo mbali na karibu,

21 aliwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari

22 kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini.

23 Hivyo Wayahudi walikubali kuendeleza sherehe walizokuwa wamezianza, wakifanya lile Mordekai alilokuwa amewaandikia.

24 Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amepanga hila dhidi ya Wayahudi, kuwaangamiza na alikuwa amepigapuri(yaani kura) kwa ajili ya maangamizi na uharibifu wao.

25 Lakini wakati shauri hilo baya lilipoarifiwa kwa mfalme, alitoa amri iliyoandikwa kwamba mipango mibaya ambayo Hamani ameipanga dhidi ya Wayahudi inapasa imrudie juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe waangikwe mahali pa kunyongea watu.

26 (Kwa hiyo siku hizi ziliitwa Purimu, kutokana na neno puri.) Kwa sababu ya kila kitu kilichoandikwa kwenye barua hii na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowatokea,

27 Wayahudi wakachukua na kuifanya desturi kwamba wao na wazao wao na wote ambao walijiunga nao wangefanya bila kuacha kushika siku hizi mbili kila mwaka, kwa njia ilivyoelekezwa na kwa wakati wake.

28 Siku hizi zinapasa zikumbukwe na kuadhimishwa katika kila kizazi, kila jamaa na katika kila jimbo na kila jiji. Nazo siku hizi za purimu kamwe zisikome kusherehekewa na wayahudi, wala kumbukumbu zake zisipotee miongoni mwa wazao wake.

29 Basi Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai, Myahudi, waliandika kwa mamlaka yote kuthibitisha barua hii ya pili kuhusu Purimu.

30 Naye Mordekai akatuma barua kwa Wayahudi wote katika majimbo 127 ya ufalme wa Ahusuero barua zenye maneno ya amani na matumaini.

31 Kuimarisha siku hizi za Purimu katika majira yake yaliyowekwa, kama Mordekai, Myahudi na Malkia Esta alivyowaamuru na walivyojiimarisha wenyewe na wazao wao kuhusu nyakati za kufunga na kuomboleza.

32 Amri ya Esta ilithibitisha taratibu hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kumbukumbu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EST/9-fccce3a4d61d0591d78cbee60d99c667.mp3?version_id=1627—

Esta 10

Ukuu Wa Mordekai

1 Mfalme Ahusuero alitoza ushuru katika ufalme wake wote hadi kwenye miambao yake ya mbali.

2 Matendo yake yote ya nguvu na uwezo, pamoja na habari zote za ukuu wa Mordekai ambao mfalme alikuwa amemkuza, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Umedi na Uajemi?

3 Mordekai Myahudi alikuwa wa pili kwa cheo kutoka Mfalme Ahusuero, naye alikuwa bora kabisa miongoni mwa Wayahudi, alipandishwa katika heshima ya juu na ndugu zake Wayahudi kwa sababu aliwatendea mema watu wake na alizungumza kwa ajili ya ustawi wa Wayahudi wote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EST/10-442bb7374f3ef79323e7f678cee6414b.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 1

Maombi Ya Nehemia

1 Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia:

# Katika mwezi wa Kisleukatika mwaka wa ishirini, wakati nikiwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani,

2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu.

3 Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni nao wamerudi kwenye lile jimbo wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.”

4 Niliposikia mambo haya, niliketi na kulia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni.

5 Kisha nikasema:

“EeBwana, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika Agano lake la upendo na wale wampendao na kutii amri zake,

6 masikio yako na yawe masikivu na macho yako yafunguke ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako mchana na usiku kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako.

7 Tumetenda kwa uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo wala sheria ulizompa Mose mtumishi wako.

8 “Kumbuka agizo ulilompa Mose mtumishi wako, ukisema, ‘Kama mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa,

9 lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni wako mbali sana katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali ambapo nimepachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’

10 “Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu.

11 Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Umpe leo mtumishi wako mafanikio kwa kumpa kibali mbele ya mtu huyu.”

Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/1-16ec27541f7ee4ac63cf57bd66e158bd.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 2

Artashasta Amtuma Nehemia Yerusalemu

1 Katika mwezi wa Nisanimwaka wa ishirini wa kutawala kwake Mfalme Artashasta, wakati divai ilipoletwa kwa ajili yake, niliichukua na kumpa mfalme. Sikuwahi kuonekana mwenye huzuni mbele yake kabla ya hapo.

2 Basi mfalme akaniuliza, “Kwa nini uso wako unaonekana una huzuni wakati wewe si mgonjwa? Jambo hili si kitu kingine bali ni huzuni ya moyo.”

Niliogopa sana,

3 lakini nikamwambia mfalme, “Mfalme na aishi milele! Kwa nini uso wangu usiwe na huzuni wakati mji walipozikwa baba zangu umebaki magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto?”

4 Mfalme akaniambia, “Je, haja yako ni nini?”

Ndipo nikaomba kwa Mungu wa mbinguni,

5 nikamjibu mfalme, “Kama ikimpendeza mfalme na kama mtumishi wako amepata kibali machoni pake na anitume Yuda kwenye mji mahali baba zangu walipozikwa ili niweze kuujenga upya.”

6 Kisha mfalme, pamoja na malkia akiwa ameketi karibu naye, akaniuliza, “Safari yako itachukua muda gani, nawe utarudi lini?” Ilimpendeza mfalme kunituma kwa hiyo nikapanga muda.

7 Pia nikamwambia, “Kama ikimpendeza mfalme, naomba nipewe barua kwa watawala wa Ng’ambo ya Eufrati, ili wanipe ulinzi mpaka nifike Yuda.

8 Naomba nipewe barua nipeleke kwa Asafu, mtunzaji wa msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengeneza boriti kwa ajili ya malango ya ngome ya Hekalu, kwa ajili ya ukuta wa mji na makao yangu nitakapoishi.” Kwa kuwa mkono wenye neema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu, mfalme akanijalia ombi langu.

9 Basi nilikwenda kwa watawala wa Ng’ambo ya Eufrati na kuwapa barua za mfalme. Pia mfalme alikuwa ametuma maafisa wa jeshi na askari wapanda farasi pamoja nami.

10 Sanbalati Mhoroni na Tobia afisa Mwamoni waliposikia juu ya jambo hili, waliudhika sana kwamba amekuja mtu kuinua ustawi wa Waisraeli.

Nehemia Akagua Kuta Za Yerusalemu

11 Nilikwenda Yerusalemu, nami baada ya kukaa huko siku tatu

12 nikaondoka wakati wa usiku pamoja na watu wachache. Sikuwa nimemwambia mtu ye yote kile ambacho Mungu wangu alikuwa ameweka moyoni mwangu kufanya kwa ajili ya Yerusalemu. Hapakuwepo na mnyama ye yote pamoja nami isipokuwa yule niliyekuwa nimempanda.

13 Nikatoka nje usiku kupitia Lango la Bondeni, kuelekea Kisima cha Joka na Lango la Samadi, nikikagua kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomolewa na malango yake yaliyokuwa yameteketezwa kwa moto.

14 Kisha nikaelekea mpaka Lango la Chemchemi na Bwawa la Mfalme, lakini hapakuwepo nafasi ya kutosha kwa ajili ya mnyama wangu kupita,

15 kwa hiyo nikapandia bondeni usiku, nikikagua ukuta. Mwishoni, nikarudi na kuingia tena kupitia Lango la Bondeni.

16 Maafisa hawakujua nilikokwenda wala nilichokuwa nikifanya, kwa sababu mpaka sasa nilikuwa bado sijasema lo lote kwa Wayahudi wala makuhani wala wakuu wala maafisa wala mtu ye yote ambaye angefanya kazi.

17 Ndipo nilipowaambia, “Mnaona taabu tuliyonayo: Yerusalemu imebaki magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Njoni tujenge upya ukuta wa Yerusalemu, nasi hatutakuwa tena kwenye aibu hii.”

18 Pia niliwaambia kuhusu mkono wenye neema wa Mungu wangu uliokuwa juu yangu na kile mfalme alichokuwa ameniambia.

Wakajibu, “Haya na tuanze kujenga tena.” Kwa hiyo wakaanza kazi hii njema.

19 Lakini Sanbalati Mhoroni, Tobia afisa Mwamoni na Geshemu Mwarabu waliposikia kuhusu jambo hili, walitudhihaki na kutucheka. Wakauliza, “Ni nini hiki mnachokifanya? Je, mnaasi dhidi ya mfalme?”

20 Nikawajibu kwa kusema, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha. Sisi watumishi wake tutaanza kujenga upya, lakini kwenu ninyi, hamna sehemu wala dai lo lote wala kumbukumbu la haki katika Yerusalemu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/2-30878fbb6f4a237ff318c3108f320fac.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 3

Wajenzi Wa Ukuta

1 Eliyashibu Kuhani Mkuu na makuhani wenzake walikwenda kufanya kazi na kulijenga upya Lango la Kondoo. Waliliweka wakfu na kuweka milango mahali pake, wakajenga hadi kufikia Mnara wa Mia Moja, ambao waliuweka wakfu hadi Mnara wa Hananeli.

2 Watu wa Yeriko wakajenga sehemu zilizopakana nao, Zahuri mwana wa Imri aliendelea kujenga karibu nao.

3 Lango la Samaki lilijengwa upya na wana wa Hasena. Wakaweka boriti zake, wakaweka milango yake na makomeo na nondo.

4 Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu iliyofuatia. Aliyemfuatia ni Meshulamu mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli, alifanya ukarabati na aliyemfuatia ni Zadoki mwana wa Baana.

5 Sehemu iliyofuatia ilikarabatiwa na watu kutoka Tekoa, lakini wakuu wao walikataa kufanya kazi chini ya wasimamizi wao.

6 Lango la Yeshana lilikarabatiwa na Yoyada mwana wa Pasea na Meshulamu mwana wa Besodeya. Wakaziweka boriti zake, milango, makomeo na nondo.

7 Karibu nao ukarabati ulifanywa na watu kutoka Gibeoni na Mispa, Melati ya Gibeoni na Yadoni ya Meronothi, sehemu hizi zilikuwa chini ya mamlaka ya mtawala wa Ng’ambo ya Eufrati.

8 Uzieli mwana wa Harhaya, mmoja wa masonara, walikarabati sehemu iliyofuatia na Hanania mmoja wa watengenezaji marashi, alikarabati sehemu iliyofuatia. Walitengeneza Yerusalemu mpaka kufikia Ukuta Mpana.

9 Refaya mwana wa Huri, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia.

10 Kupakana na sehemu hii, Yedaya mwana wa Harumafu alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba yake, naye Hatushi mwana wa Hashabnea alifanya ukarabati sehemu iliyofuatia.

11 Malkiya mwana wa Harimu na Hashubu mwana wa Pahath-Moabu walikarabati sehemu nyingine pamoja na Mnara wa Matanuru.

12 Shalumu mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia akisaidiana na binti zake.

13 Lango la Bondeni lilikarabatiwa na Hanuni na wakazi wa Zanoa. Walilijenga kwa upya na kuweka milango yake na makomeo na nondo mahali pake. Pia walikarabati ukuta wenye urefu wa mita 450 hadi Lango la Samadi.

14 Lango la Samadi lilikarabatiwa na Malkiya mwana wa Rekabu, mtawala wa wilaya ya Beth-Hakeremu. Alijenga kwa upya na kuweka milango yake makomeo na nondo.

15 Lango la Chemchemi lilikarabatiwa na Shalumu mwana wa Kolhoze, mtawala wa wilaya ya Mispa. Alilijenga kwa upya, akaliezeka na kuweka milango yake, makomeo yake na nondo mahali pake. Pia alikarabati ukuta wa Bwawa la Siloamu karibu na Bustani ya Mfalme hadi kwenye ngazi zinazoshuka kutoka Mji wa Daudi.

16 Sehemu iliyofuatia, Nehemia mwana wa Azbuki, mtawala wa nusu ya wilaya ya Beth-Zuri, alikarabati kufikia mkabala na makaburi ya Daudi, mpaka kwenye bwawa lililotengenezwa na kufikia Nyumba ya Mashujaa.

17 Sehemu iliofuatia, ukarabati ulifanywa na Walawi chini ya uongozi wa Rehumu mwana wa Bani. Aliyefuatia ni Hashabia, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila. Aliendeleza ukarabati katika sehemu inayohusu wilaya yake.

18 Sehemu iliofuatia, ukarabati ulifanywa na ndugu zao chini ya usimamizi wa Binui, mwana wa Henadadi, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila.

19 Sehemu iliofuatia, Ezeri mwana wa Yeshua, mtawala wa Mispa, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia ile sehemu inayotazamana na mwinuko wa kuelekea kwenye ghala la kuhifadhia silaha, mpaka kwenye pembe ya ukuta.

20 Sehemu iliofuatia, Baruki mwana wa Zabai alikarabati kwa bidii sehemu nyingine kuanzia ile pembe mpaka kwenye lango la nyumba ya Eliyashibu Kuhani Mkuu.

21 Sehemu iliofuatia, Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia penye lango la nyumba ya Eliyashibu mpaka mwisho wake.

22 Sehemu iliofuatia, ukarabati ulifanywa na makuhani kuanzia eneo lililouzunguka mji.

23 Baada yao Benyamini na Hashubu walikarabati mbele ya nyumba zao, baada yao Azaria mwana wa Maaseya, mwana wa Anania alifanya ukarabati kando ya nyumba yake.

24 Sehemu iliofuatia, Binui mwana wa Henadadi alikarabati sehemu nyingine, kuanzia kwenye nyumba ya Azaria mpaka kwenye pembe ya ukuta.

25 Naye Palali, mwana wa Uzai alijenga sehemu iliyokuwa mkabala na pembe ya ukuta mpaka kwenye mnara wa juu ambao unajitokeza kuanzia kwenye jumba la kifalme kando ya ua wa walinzi. Sehemu iliofuatia, Pedaya mwana wa Paroshi,

26 na watumishi wa Hekalu waishio juu ya kilima cha Ofeli walikarabati hadi kufikia mkabala na Lango la Maji, kuelekea mashariki pamoja na ule mnara uliojitokeza.

27 Sehemu iliofuatia, watu wa Tekoa walikarabati sehemu nyingine, kuanzia mnara mkubwa utokezao hadi ukuta wa Ofeli.

28 Makuhani walifanya ukarabati juu ya Lango la Farasi, kila mmoja mbele ya nyumba yake.

29 Baada yao, Sadoki mwana wa Imeri alifanya ukarabati mkabala na nyumba yake. Sehemu iliofuatia, Shemaya mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki, alifanya ukarabati.

30 Sehemu iliofuatia, Hanania mwana wa Shelemia na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, alikarabati sehemu nyingine. Baada yao, Meshulamu mwana wa Berekia alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba zake za kuishi.

31 Sehemu iliofuatia, Malkiya, mmoja wa masonara, alifanya ukarabati mpaka kwenye nyumba za Wanethinina wafanyabiashara, mkabala na Lango la Ukaguzi, hadi kufikia chumba kilicho juu ya pembe.

32 Masonara na wafanya biashara walifanya ukarabati kati ya chumba kilichoko juu ya pembe ya Lango la Kondoo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/3-c90da1fa759d50072b52abd4d1b07c2f.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 4

Upinzani Wakati Wa Ujenzi

1 Sanbalati aliposikia kwamba tulikuwa tunajenga upya ukuta, alikasirika na akawa na uchungu sana. Aliwadhihaki Wayahudi,

2 mbele ya rafiki zake na jeshi la Samaria, akisema, “Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, wataweza kuurudishia ukuta wao? Je, watatoa dhabihu? Je, wataweza kumaliza kuujenga kwa siku moja? Je, wataweza kufufua mawe kutoka katika malundo ya vifusi yaliyoungua hivyo?”

3 Tobia Mwamoni, aliyekuwa upande wake akasema, “Wanachokijenga, hata kama mbweha angepanda juu yake, huo ukuta wao wa mawe angelibomoa!”

4 Ee Mungu wetu, utusikie, kwa kuwa tumedharauliwa. Warudishie matukano yao kwenye vichwa vyao wenyewe. Uwatoe ili wawe nyara katika nchi ya waliowateka.

5 Usiusitiri uovu wao wala usifute dhambi zao mbele zako, kwa kuwa wamewatukana wajenzi mbele ya macho yao.

6 Basi tuliujenga upya ukuta mpaka wote ukafikia nusu ya kimo chake, kwa kuwa watu walifanya kazi kwa moyo wote.

7 Lakini wakati Sanbalati, Tobia, Waarabu, Waamoni na watu wa Ashdodi waliposikia kuwa ukarabati wa kuta za Yerusalemu ulikuwa umeendelea na mianya ilikuwa inazibwa, walikasirika sana.

8 Wote walifanya shauri pamoja kuja kupigana dhidi ya Yerusalemu na kuchochea machafuko dhidi yake.

9 Lakini tulimwomba Mungu wetu na kuweka ulinzi mchana na usiku kupambana na tishio hili.

10 Wakati ule ule, watu wa Yuda wakasema, “Nguvu za wafanya kazi zinapungua, nacho kifusi ni kingi mno kiasi kwamba hatuwezi kuujenga upya ukuta.”

11 Pia adui zetu walisema, “Kabla hawajajua au kutuona, tutakuwa pale pale katikati yao na tutawaua na kuikomesha hiyo kazi.”

12 Kisha Wayahudi ambao waliishi karibu nao walikuja zaidi ya mara kumi na kutuambia, “Po pote mtakapoelekea, watatushambulia.”

13 Kwa hiyo nikaweka baadhi ya watu nyuma ya sehemu za chini za ukuta kwenye sehemu zilizo wazi, nikawaweka kufuatana na jamaa zao, wakiwa na panga zao, mikuki na pindi zao.

14 Baada ya kuona hali ilivyo, nikasimama na kuwaambia wakuu, maafisa na wengine wote, “Msiwaogope. Mkumbukeni Bwana, ambaye ni mkuu mwenye kuogofya. Piganeni kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu na binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.”

15 Adui zetu waliposikia kwamba tumetambua hila yao na kwamba Mungu amevuruga shauri lao, sote tulirudi kwenye ukuta, kila mmoja kwenye kazi yake.

16 Kuanzia siku ile na kuendelea, nusu ya watu wangu walifanya kazi ya ujenzi na nusu nyingine wakashika mikuki, ngao, pindi na kinga ya kifuani. Maafisa walijipanga nyuma ya watu wote wa Yuda

17 waliokuwa wakijenga ukuta. Wale waliobeba vifaa vya ujenzi walifanya kazi yao kwa mkono mmoja na kushika silaha kwa mkono mwingine,

18 kila mjenzi alijifunga upanga wake upande mmoja akiwa anafanya kazi. Lakini mtu wa kupiga baragumu alikaa pamoja nami.

19 Kisha nikawaambia wakuu, maafisa na watu wengine wote, “Kazi hii ni kubwa na imeenea sehemu kubwa, nasi tumetawanyika kila mmoja yuko mbali na mwenzake juu ya ukuta.

20 Po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, jiungeni nasi huko. Mungu wetu atatupigania!”

21 Basi tuliendelea na kazi, nusu ya watu wakishikilia mikuki, kuanzia maawio ya jua hadi nyota zilipoonekana.

22 Wakati huo pia niliwaambia watu, “Kila mtu na msaidizi wake wakae ndani ya Yerusalemu wakati wa usiku, ili waweze kutumika kama walinzi wakati wa usiku na kufanya kazi wakati wa mchana.”

23 Mimi, wala ndugu zangu, wala watu wangu, wala walinzi waliokuwa pamoja nami hatukuvua nguo zetu. Kila mmoja alikuwa na silaha yake, hata alipokwenda kuchota maji.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/4-7476571ae9dda5724d64d4fd62d031e3.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 5

Nehemia Anawasaidia Maskini

1 Wakati huu watu na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi.

2 Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu na binti zetu tu wengi, ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.”

3 Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”

4 Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu.

5 Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu na binti zetu kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya wengine.”

6 Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana.

7 Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaitisha mkutano mkubwa ili kuwashughulikia

8 na kusema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa Mataifa. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Walinyamaza kimya, kwa sababu hawakupata cho chote cha kusema.

9 Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu Mataifa?

10 Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome!

11 Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”

12 Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu cho chote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.”

Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi.

13 Pia nikakung’uta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkung’ute hivi kutoka katika nyumba yake na katika mali zake. Basi mtu wa jinsi hiyo na akung’utiwe nje na aachwe bila kitu!”

Katika hili mkutano wote ukasema, “Amen” wakamtukuzaBwana. Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.

14 Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, mpaka mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na miwili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala.

15 Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedhapamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walipata nafasi ya kufaidi watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo.

16 Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi kwenye ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi, hatukujipatia shamba lo lote.

17 Zaidi ya hayo, Wayahudi 150 na maafisa walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani.

18 Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri na kuku na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.

19 Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/5-2f6f42cbb00a68d11cc7cb243d8ff7c6.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 6

Upinzani Zaidi Wakati Wa Ujenzi

1 Habari zilipofika kwa Sanbalati, Tobia, Geshemu Mwarabu na adui zetu wengine kwamba nimejenga tena ukuta na hakuna nafasi iliyobakia ndani mwake, ingawa mpaka wakati huo sikuwa nimeweka milango kwenye malango,

2 Sanbalati na Geshemu wakanipelekea ujumbe huu: “Njoo, tukutane katika mojawapo ya vijiji katika nchi tambarare ya Ono.”

Lakini walikuwa wakikusudia kunidhuru,

3 kwa hiyo niliwatuma wajumbe kwao na majibu haya: “Kazi ninayoifanya ni kubwa sana siwezi kuja. Kwa nini niiache kazi isimame nije kwenu?”

4 Mara nne walinitumia ujumbe wa namna iyo hiyo na kila mara niliwapa jibu lile lile.

5 Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe wa aina ile ile, naye alikuwa amechukuwa mkononi mwake barua isiyofungwa,

6 iliyokuwa imeandikwa:

“Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnafanya hila ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kwa kufuatana na taarifa hizi karibu utakuwa mfalme wao

7 na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu wewe huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme; basi njoo, tufanye shauri pamoja.”

8 Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika; unalitunga tu kwenye kichwa chako.”

9 Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri kuwa, “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.”

Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”

10 Siku moja nilikwenda nyumbani kwa Shemaya mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, ambaye alikuwa amefungwa ndani ya nyumba yake. Akasema, “Tukutane katika nyumba ya Mungu, ndani ya Hekalu na tufunge milango ya Hekalu, kwa sababu watu wanakuja kukuua. Naam, usiku wanakuja kukuua.”

11 Lakini nikasema, “Je, mtu kama mimi akimbie? Au mtu kama mimi aende Hekaluni kuokoa maisha yake? Sitakwenda!”

12 Nilitambua kwamba Mungu hakumtuma, bali alitabiri dhidi yangu kwa sababu Tobia na Sanbalati walikuwa wamemwajiri.

13 Alikuwa ameajiriwa kunitisha ili kwa kufanya jambo hili nitende dhambi, kisha waweze kuniharibia jina langu na kuniaibisha.

14 Ee Mungu wangu, wakumbuke Tobia na Sanbalati kwa sababu ya yale waliyotenda, pia kumbuka nabii mke Noadia na manabii wengine ambao wamekuwa wakijaribu kunitisha.

Kukamilika Kwa Ukuta

15 Basi ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano mwezi wa Eluli, kazi ambayo ilichukua siku hamsini na mbili.

16 Adui zetu wote waliposikia kuhusu hili, mataifa yote yaliyotuzunguka yakaogopa na kupoteza ujasiri, kwa sababu yalitambua kuwa kazi hii imefanyika kwa msaada wa Mungu wetu.

17 Pia, katika siku hizo wakuu wa Yuda walikuwa wakituma barua nyingi kwa Tobia, nayo majibu yaliyotoka kwa Tobia yaliendelea kuwajia.

18 Kwa kuwa watu wengi katika Yuda walikuwa wamemwapia Tobia, kwani alikuwa mkwewe Shekania mwana wa Ara, naye ni mwanawe Yehohanani aliyekuwa amemwoa binti wa Meshulamu mwana wa Berekia.

19 Zaidi ya hayo walikuwa wakiniarifu jinsi Tobia alivyo mtu mwema, nao walimwambia kila kitu nilichosema. Naye Tobia alituma barua za kunitisha.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/6-55f7691920dd40664504bd07c4fee116.mp3?version_id=1627—

Nehemiah 7

1 Baada ya ukuta kukamilika kujengwa upya na kuweka milango, waliteuliwa mabawabu wa lango, waimbaji na Walawi.

2 Nikamweka Hanani ndugu yangu kuwa kiongozi wa Yerusalemu, pamoja na Hanania jemadari wa ngome, kwa kuwa alikuwa mtu mwadilifu na mwenye kumcha Mungu kuliko watu wengine.

3 Nikawaambia, “Malango ya Yerusalemu yasifunguliwe mpaka jua litakapokuwa limepanda. Wakati walinzi wa malango wakiwa kwenye zamu, wafunge milango na waweke makomeo. Pia wateueni wenyeji wa Yerusalemu wawe walinzi, kila mmoja kwenye lindo lake na wengine karibu na nyumba zao wenyewe.”

Orodha Ya Waliorudi Toka Uhamishoni

4 Mji ulikuwa mkubwa tena wenye nafasi nyingi, lakini walikuwepo watu wachache ndani yake, nazo nyumba zilikuwa bado ni magofu.

5 Hivyo Mungu wangu akaweka moyoni mwangu kuwakusanya wakuu, maafisa na watu wa kawaida kwa ajili ya kuorodheshwa kulingana na jamaa zao. Nilikuta orodha ya vizazi iliyoandikwa ya wale waliokuwa wa kwanza kurudi toka utumwani. Haya ndiyo niliyokuta yameandikwa humo:

6 Hawa ndio watu wa jimbo waliorudi kutoka utumwani uhamishoni walikokuwa wamepelekwa na Mfalme Nebukadneza wa Babeli (walirudi Yerusalemu na Yuda, kila mmoja kwenye mji wake,

7 wakiwa wamefuatana na Zerubabeli, Yeshua, Nehemia, Azaria, Raamia, Nahamani, Mordekai, Bilshani, Mispereti, Bigwai, Nehumu na Baana):

Orodha ya watu wa Israeli:

8 wazao wa Paroshi 2,172
9 wazao wa Shefatia 372
10 wazao wa Ara 652
11 wazao wa Pahath-Moabu (kupitia ukoo wa Yeshua na Yoabu) 2,818
12 wazao wa Elamu 1,254
13 wazao wa Zatu 845
14 wazao wa Zakai 760
15 wazao wa Binui 648
16 wazao wa Bebai 628
17 wazao wa Azgadi 2,322
18 wazao wa Adonikamu 667
19 wazao wa Bigwai 2,067
20 wazao wa Adini 655
21 wazao wa Ateri (kupitia Hezekia) 98
22 wazao wa Hashumu 328
23 wazao wa Besai 324
24 wazao wa Harifu 112
25 wazao wa Gibeoni 95
26 watu wa Bethlehemu na Netofa 188
27 watu wa Anathothi 128
28 watu wa Beth-Azmawethi 42
29 watu wa Kiriath-Yearimu, Kefira na Beerothi 743
30 watu wa Rama na Geba 621
31 watu wa Mikmashi 122
32 watu wa Betheli na Ai 123
33 watu wa Nebo 52
34 watu wa Elamu 1,254
35 watu wa Harimu 320
36 watu wa Yeriko 345
37 watu wa Lodi, Hadidi na Ono 721
38 watu wa Senaa 3,930

39 Makuhani:

wazao wa Yedaya (kupitia familia ya Yeshua) 973
40 wazao wa Imeri 1,052
41 wazao wa Pashuri 1,247
42 wazao wa Harimu 1,017

43 Walawi:

wazao wa Yeshua (kupitia Kadmieli kupitia ukoo wa Hodavia) 74

44 Waimbaji:

wazao wa Asafu 148

45 Mabawabu wa malango:

wazao waShalumu, Ateri, Talmoni,Akubu, Hatita na Shobai 138

46 Wanethiniwa Hekaluni:

wazao wa

Siha, Hasufa, Tabaothi,

47 Kerosi, Sia, Padoni,

48 Lebana, Hagaba, Shalmai,

49 Hanani, Gideli, Gahari,

50 Reaya, Resini, Nekoda,

51 Gazamu, Uza, Pasea,

52 Besai, Meunimu, Nefusimu,

53 Bakbuki, Hakufa, Harhuri,

54 Basluthi, Mehida, Harsha,

55 Barkosi, Sisera, Tema,

56 Nesia na Hatifa.

57 Wazao wa watumishi wa Solomoni:

wazao wa

Sotai, Soferethi, Perida,

58 Yaala, Darkoni, Gideli,

59 Shefatia, Hatili,

Pokereth-Hazebaimu na Amoni.

60 Wanethini wote na wazao wa watumishi wa Solomoni 392

61 Wafuatao ni watu waliorudi kutoka miji ya Tel-Mela, Tel-Harsha, Kerubu, Adoni na Imeri, lakini hawakuweza kuthibitisha kwamba jamii zao zilitokana na Israeli:

62 wazao waDelaya, Tobia na Nekoda 642

63 Na kutoka miongoni mwa makuhani:

wazao wa

Hobaya, Hakosi na Barzilai (mtu aliyekuwa amemwoa binti wa Barzilai, Mgileadi, naye akaitwa kwa jina hilo.)

64 Hawa walitafuta katika orodha ya jamii zao, lakini hawakuonekana kwa hiyo waliondolewa katika ukuhani kama watu najisi.

65 Kwa hiyo, Tirshathaaliagiza kuwa wasile cho chote miongoni mwa vyakula vitakatifu mpaka atakapopatikana kuhani ahudumuye kwa Urimu na Thumimu.

66 Jumla ya watu wote waliorudi kutoka utumwani uhamishoni walikuwa 42,360;

67 tena zaidi ya hao walikuwepo watumishi wa kiume na wa kike 7,337; pia walikuwemo waimbaji wanaume na wanawake 245.

68 Walikuwako farasi 736, nyumbu 245

69 ngamia 435 na punda 6,720.

70 Baadhi ya wakuu wa mbari walichangia kazi ya ujenzi. Tirshatha alikabidhi kwenye hazina darkoni 1,000za dhahabu, mabakuli 50 na mavazi 530 kwa ajili ya makuhani.

71 Baadhi ya wakuu wa mbari walikabidhi kwenye hazina kwa ajili ya kazi darkoni 20,000 za dhahabuna mane 2,200za fedha.

72 Jumla ya matoleo ya watu wengine yalikuwa ni darkoni 20,000 za dhahabu, mane 2,000 za fedha na mavazi sitini na saba ya makuhani.

73 Makuhani, Walawi, mabawabu wa malango, waimbaji na Wanethini, pamoja na baadhi ya watu wengine na Waisraeli wengine wote, waliishi katika miji yao wenyewe.

Ezara Asoma Sheria

Ilipotimia miezi saba, nao Waisraeli wakiwa tayari wanaishi katika miji yao,

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/7-4584123c74f1e3ac9b4d583f95216276.mp3?version_id=1627—