Ezra 5

Barua Ya Tatenai Kwa Dario

1 Ndipo nabii Hagai na nabii Zekaria mzao wa Ido, wakawatolea unabii Wayahudi waliokuwa Yuda na Yerusalemu kwa jina la Mungu wa Israeli, aliyekuwa pamoja nao.

2 Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli na Yeshua mwana wa Yosadaki wakaanza kujenga tena nyumba ya Mungu huko Yerusalemu. Nao manabii wa Mungu walikuwa pamoja nao, wakiwasaidia.

3 Wakati ule Tatenai mtawala wa ng’ambo ya mto Eufrati na Shethar-Bozenai na wenzao waliwaendea, wakawauliza, “Ni nani aliyewapa ruhusa ya kujenga tena Hekalu hili na kurudishia upya kama lilivyokuwa?”

4 Pia waliwauliza, “Je, majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?”

5 Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa likiwaangalia wazee wa Wayahudi, nao hawakuzuiliwa kujenga mpaka taarifa ikaandikwa kwa Dario na majibu yake kupokelewa.

6 Hii ni nakala ya barua ile Tatenai, mtawala wa ng’ambo ya mto Eufrati na Shethar-Bozenai na wenzao maafisa wa ng’ambo ya mto Eufrati waliyompelekea Mfalme Dario.

7 Taarifa waliyompelekea ilisomeka kama ifuatavyo:

Kwa Mfalme Dario:

Salamu kwa moyo mkunjufu.

8 Inampasa Mfalme ajue kwamba tulikwenda katika eneo la Yuda, kwenye Hekalu la Mungu mkuu. Watu wanalijenga kwa mawe makubwa na kuweka mbao kwenye kuta. Kazi inafanyika kwa bidii na inaendelea kwa haraka chini ya uongozi wao.

9 Tuliwauliza viongozi, “Ni nani aliyewapa ruhusa kujenga upya Hekalu hili na kurejesha hali ya jengo kama lilivyokuwa?”

10 Pia tuliwauliza majina yao, ili tukuandikie kukujulisha majina ya viongozi wao.

11 Hili ndilo jibu walilotupa:

“Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunalijenga upya Hekalu ambalo lilijengwa miaka mingi iliyopita, lile ambalo mfalme mkuu wa Israeli alilijenga na kulikamilisha.

12 Lakini kwa sababu baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbinguni, basi aliwatia mkononi mwa Nebukadneza, Mkaldayo, mfalme wa Babeli, ambaye aliliharibu Hekalu hili na kuwaondoa watu na kuwapeleka uhamishoni huko Babeli.

13 “Pamoja na hayo, katika mwaka wa kwanza wa kutawala Koreshi mfalme wa Babeli, Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujengwa upya nyumba hii ya Mungu.

14 Yeye hata aliviondoa vyombo vya dhahabu na fedha vya nyumba ya Mungu, kutoka Hekalu la Babeli ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka ndani ya Hekalu huko Yerusalemu na kuvileta katika Hekalu la Babeli.

“Vyombo hivyo Mfalme Koreshi alimkabidhi mtu aliyeitwa Sheshbaza, ambaye Koreshi alikuwa amemteua awe mtawala,

15 naye akamwambia, ‘Chukua vyombo hivi uende ukaviweke ndani ya Hekalu huko Yerusalemu. Nawe uijenge upya nyumba ya Mungu mahali pake.’

16 Hivyo huyu Sheshbaza alikuja na kuweka misingi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu. Tangu siku hiyo hadi sasa imekuwa ikiendelea kujengwa lakini bado haijamalizika.”

17 Sasa kama ikimpendeza mfalme, uchunguzi na ufanyike katika kumbukumbu ya maandishi ya kifalme mjini Babeli kuona kama kweli Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Kisha tunaomba mfalme na atutumie uamuzi wake kuhusu jambo hili.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZR/5-1098516aa3db9ccd8c29ac16cb9983e5.mp3?version_id=1627—

Ezra 6

Amri Ya Dario

1 Kisha Mfalme Dario alitoa amri, nao wakafanya uchunguzi katika kumbukumbu zilizohifadhiwa katika hazina huko Babeli.

2 Karatasi moja ndefu ya maandishi ilipatikana huko Ekbatana katika jimbo la Umedi. Haya ndiyo yaliyokuwa yameandikwa humo:

Kumbukumbu:

3 Katika mwaka wa kwanza wa kutawala Mfalme Koreshi, mfalme alitoa amri kuhusu Hekalu la Mungu katika Yerusalemu:

# Hekalu na lijengwe tena mahali pale pale Wayahudi walipokuwa wakitoa dhabihu, kwenye msingi ule ule. Iwe na kimo cha mikono sitini, upana wa mikono sitini,

4 kuta zijengwe kwa safu tatu za mawe makubwa kisha ifuate safu moja ya mbao. Gharama zitalipwa kutoka katika hazina ya mfalme.

5 Pia, vyombo vya dhahabu na vya fedha vya nyumba ya Mungu, ambavyo Nebukadneza alivichukua kutoka kwenye Hekalu huko Yerusalemu akavileta Babeli, yapasa virudishwe mahali pake ndani ya Hekalu huko Yerusalemu, yapasa viwekwe ndani ya nyumba ya Mungu.

6 Sasa basi, Tatenai, mtawala wa Ng’ambo ya Mto Eufrati na Shethar-Bozenai pamoja na ninyi, maafisa wenzao wa jimbo hilo kaeni mbali na mahali hapo.

7 Msiingilie kazi ya Hekalu hili la Mungu. Mwacheni mtawala wa Wayahudi na viongozi Wayahudi wajenge upya nyumba hii ya Mungu mahali pake.

8 Zaidi ya hayo, hapa natoa amri kuhusu mtakalofanya kwa ajili ya wazee wa Wayahudi katika ujenzi wa nyumba hii ya Mungu:

Gharama za watu hawa zitalipwa kikamilifu kutoka katika hazina ya mfalme, kutoka kwenye mapato ya Ng’ambo ya Mto Eufrati, ili ujenzi usisimame.

9 Cho chote kinachohitajika kama mafahali wachanga, kondoo waume, wana-kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, ngano, chumvi, divai na mafuta kama vitakavyohitajika na makuhani huko Yerusalemu, lazima wapewe kila siku pasipo kukosa,

10 ili waweze kutoa dhabihu inayompendeza Mungu wa mbinguni na kumwombea mfalme na wanawe hali njema.

11 Zaidi ya hayo, ninaamuru kwamba mtu ye yote atakayebadilisha amri hii, boriti itang’olewa kutoka katika nyumba yake, ichongwe upande mmoja na atumbuliwe nayo. Kwa ajili ya kosa hili nyumba yake ifanywe lundo la taka.

12 Naye Mungu, aliyeliweka Jina lake huko, amwangushe mfalme ye yote au watu watakaoinua mikono kubadili amri hii au kuharibu Hekalu hili lililoko Yerusalemu.

Mimi Dario nimetoa amri hii. Nayo itekelezwe kwa bidii na kwa makini.

Jengo Linakamilika Na Kuwekwa Wakfu

13 Kwa sababu ya amri aliyotoa Mfalme Dario, Tatenai mtawala wa Ng’ambo ya Mto Eufrati na Shethar-Bozenai na wenzao wakaitekeleza kwa bidii na kwa makini.

14 Hivyo wazee wa Wayahudi waliendelea kujenga na kustawi kutokana na mahubiri ya manabii Hagai na Zekaria, mwana wa Ido. Wakakamilisha ujenzi wa Hekalu kulingana na agizo la Mungu wa Israeli na amri ya Koreshi, Dario na Artashasta wafalme wa Uajemi.

15 Hekalu lilikamilika siku ya kumi na mbili ya mwezi wa Adari, ndio mwezi wa tatu, katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Dario.

16 Kisha watu wa Israeli: makuhani, Walawi na wengine wote waliohamishwa, wakaadhimisha kule kuwekwa wakfu nyumba ya Mungu kwa shangwe.

17 Kwa ajili ya kuwekwa wakfu nyumba hii ya Mungu walitoa mafahali mia moja, kondoo waume mia mbili, wana-kondoo mia nne, sadaka kwa ajili ya dhambi ya Israeli yote walitoa mbuzi waume kumi na wawili, mmoja kwa ajili ya kila kabila la Israeli.

18 Wakawaweka makuhani katika nafasi zao na Walawi wakawekwa katika makundi yao ya huduma kwa Mungu huko Yerusalemu, kulingana na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mose.

Pasaka

19 Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, waliorudi kutoka uhamishoni wakaadhimisha Pasaka.

20 Makuhani na Walawi walikuwa wamekwisha kujitakasa nao wamekuwa safi kwa kufuata kawaida za ibada. Walawi wakachinja kondoo wa Pasaka kwa ajili ya wana wa waliorudi kutoka utumwani uhamishoni, kwa ajili ya ndugu zao makuhani na wao wenyewe.

21 Hivyo Waisraeli waliokuwa wamerudi kutoka utumwani uhamishoni wakaila Pasaka, pamoja na wale waliokuwa wamejitenga na matendo ya unajisi wa Mataifa ya jirani ili kumtafutaBwana, Mungu wa Israeli.

22 Kwa muda wa siku saba waliiadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa furaha, kwa sababu alikuwa amewajaza furaha kwa kubadilisha nia ya mfalme wa Ashuru kwamba awasaidie ujenzi wa nyumba ya Mungu, Mungu wa Israeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZR/6-479a7b30be556bcd6c358da28f229db0.mp3?version_id=1627—

Ezra 7

Ezra Awasili Yerusalemu

1 Baada ya mambo haya, wakati wa utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Ezra mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia,

2 mwana wa Shalumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu,

3 mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayothi,

4 mwana wa Zerahia, mwana wa Uzi, mwana wa Buki,

5 mwana wa Abishua, mwana wa Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Kuhani Mkuu Aroni.

6 Huyu Ezra alipanda kutoka Babeli. Alikuwa mwalimu mwenye ujuzi mzuri katika sheria ya Mose, ambayoBwana, Mungu wa Israeli, alikuwa ametoa. Mfalme alikuwa amempa Ezra kila kitu alichoomba, kwa maanaBwanaMungu wake alikuwa pamoja naye.

7 Pia baadhi ya Waisraeli, wakiwemo makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu na Wanethini, nao walikuja Yerusalemu mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta.

8 Ezra aliwasili Yerusalemu mwezi wa tano wa mwaka wa saba wa utawala wa Mfalme Artashasta.

9 Ezra alianza safari yake kutoka Babeli tangu siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akawasili Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kwa maana mkono wa neema wa Mungu wake ulikuwa juu yake.

10 Kwa maana Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza na kushika sheria yaBwanana kuwafundisha watu wa Israeli amri na sheria zake.

Barua Ya Ezra Kutoka Kwa Mfalme Artashasta

11 Hii ni nakala ya barua ambayo Mfalme Artashasta alikuwa amempa Ezra aliyekuwa kuhani na mwalimu, mtu aliyeelimika katika mambo yahusuyo maagizo na amri zaBwanakwa Israeli.

12 Artashasta, mfalme wa wafalme,

Kwa Ezra kuhani, mwalimu wa Sheria ya Mungu wa mbinguni:

Salaam.

13 Sasa naamuru kwamba mtu ye yote Mwisraeli katika ufalme wangu, pamoja na makuhani na Walawi, ambaye anataka kwenda Yerusalemu pamoja nawe aweza kwenda.

14 Unatumwa na mfalme na washauri wake saba kuchunguza kuhusu Yuda na Yerusalemu kulingana na Sheria ya Mungu wako, iliyoko mkononi mwako.

15 Zaidi ya hayo, uchukue pamoja nawe fedha na dhahabu ambayo mfalme na washauri wake wamempa Mungu wa Israeli kwa hiari, Mungu ambaye maskani yake yako Yerusalemu,

16 pia fedha na dhahabu yote unayoweza kuipata kutoka jimbo la Babeli, pamoja na sadaka za hiari watakazotoa watu na makuhani kwa ajili ya Hekalu la Mungu wao katika Yerusalemu.

17 Hakikisha kwamba fedha hizi zimetumika kununua mafahali, kondoo waume na wana-kondoo pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, uvitoe dhabihu juu ya madhabahu ya Hekalu la Mungu wenu katika Yerusalemu.

18 Kisha wewe na Wayahudi ndugu zako mnaweza kufanya lo lote linaloonekana jema sana kwa fedha na dhahabu iliyosalia, kulingana na mapenzi ya Mungu wenu.

19 Uvitoe kwa Mungu wa Yerusalemu vyombo vyote ulivyokabidhiwa kwa ajili ya ibada katika Hekalu la Mungu wako.

20 Kitu kingine cho chote kinachohitajika kwa ajili ya Hekalu la Mungu wenu ambacho unatakiwa kukitoa, waweza kukitoa kutoka hazina ya mfalme.

21 Mimi, Mfalme Artashasta, sasa naagiza watunza hazina wote wa Ng’ambo ya Mto Eufrati kutoa kwa bidii cho chote kwa Ezra kuhani na mwalimu wa Sheria ya Mungu wa mbinguni atakachohitaji kwenu,

22 talanta 100za fedha, ngano kori 100, divai bathi 100, mafuta ya zeituni bathi 100 na chumvi kiasi cho chote.

23 Cho chote ambacho Mungu wa mbinguni ameagiza, kifanyike kwa ukamilifu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wa mbinguni. Kwa nini pawepo ghadhabu dhidi ya utawala wa mfalme na wanawe?

24 Pia ninyi fahamuni kuwa hamna mamlaka ya kuwatoza kodi, ushuru au ada makuhani, Walawi, waimbaji, mabawabu, Wanethini au wafanyakazi wengine kwenye nyumba ya Mungu.

25 Nawe Ezra, kufuatana na hekima ya Mungu wenu uliyo nayo, weka mahakimu na waamuzi wote wanaozifahamu Sheria za Mungu wenu ili watoe haki kwa watu wote wa Ng’ambo ya Mto Eufrati. Nawe inakupasa umfundishe ye yote ambaye hazifahamu.

26 Ye yote ambaye hataitii sheria ya Mungu wenu pia sheria ya mfalme, hakika lazima aadhibiwe kwa kuuawa, kuhamishwa, kunyang’anywa mali au kufungwa gerezani.

27 Sifa ziwe kwaBwana, Mungu wa baba zetu, Mungu ambaye kwa njia hii ameweka ndani ya moyo wa mfalme kuipa heshima nyumba yaBwanailiyoko Yerusalemu, kwa namna hii

28 ambaye ameniongezea kibali chake mbele ya mfalme, washauri wake na maafisa wote wa mfalme wenye uwezo. Kwa kuwa mkono waBwanaMungu wangu ulikuwa pamoja nami, nilijipa moyo nikakusanya watu walio viongozi kutoka Israeli wakwee pamoja nami.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZR/7-acb80b7d2e1dfe85f1faac2e05d62550.mp3?version_id=1627—

Ezra 8

Orodha Ya Viongozi Wa Jamaa Waliorudi Na Ezra

1 Hawa ndio viongozi wa jamaa pamoja na wale walioandikwa ambao walikuja pamoja nami kutoka Babeli wakati wa utawala wa Mfalme Artashasta:

2 wa wazao wa Finehasi, alikuwa Gershoni;

wa wazao wa Ithamari, alikuwa Danieli;

wa wazao wa Daudi, alikuwa Hatushi

3 wa wazao wa Shekania;

wa wazao wa Paroshi, alikuwa Zekaria, na watu 150 walioandikishwa pamoja naye;

4 wa wazao wa Pahath-Moabu, alikuwa Eliehoenai mwana wa Zerahia na wanaume 200 pamoja naye;

5 wa wazao wa Zatu, alikuwa Shekania mwana wa Yahazieli na wanaume 300 pamoja naye;

6 wa wazao wa Adini, alikuwa Ebedi mwana wa Yonathani na wanaume 50 pamoja naye;

7 wa wazao wa Elamu, alikuwa Yeshaya mwana wa Athalia, na wanaume 70 pamoja naye;

8 wa wazao wa Shefatia, alikuwa Zebadia mwana wa Mikaeli na wanaume 80 pamoja naye;

9 wa wazao wa Yoabu, alikuwa Obadia mwana wa Yehieli na wanaume 218 pamoja naye;

10 wa wazao wa Bani, alikuwa Shelomithi mwana wa Yosifia na wanaume 160 pamoja naye;

11 wa wazao wa Bebai, alikuwa Zekaria mwana wa Bebai na wanaume 28 pamoja naye;

12 wa wazao wa Azgadi, alikuwa Yohana mwana wa Hakatani na wanaume 110 pamoja naye;

13 wa wazao wa Adonikamu, hawa walikuwa wa mwisho ambao majina yao ni Elifeleti, Yeueli, Shemaya na wanaume 60 pamoja nao;

14 wa wazao wa Bigwai, walikuwa Uthai na Zakuri na wanaume 70 pamoja nao.

Kurudi Yerusalemu

15 Niliwakusanya kwenye mto utiririkao kuelekea Ahava, nasi tukapiga kambi pale siku tatu. Wakati nilipokagua kati ya watu na makuhani, sikuwapata Walawi.

16 Basi niliwaita Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu ambao walikuwa viongozi na Yoyaribu na Elnathani ambao walikuwa wasomi,

17 nikawatuma kwa Ido kiongozi huko Kasifia. Niliwaambia watakayomwambia Ido na ndugu zake, Wanethinihuko Kasifia, ili kwamba waweze kutuletea wahudumu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.

18 Kwa sababu mkono wa neema wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, walituletea Sherebia, mtu mwenye uwezo kutoka wazao wa Mahli mwana wa Lawi, mwana wa Israeli, na wana wa Sherebia pamoja na ndugu zao wanaume kumi na wanane.

19 Naye Hashabia, pamoja na Yeshaya kutoka wazao wa Merari na ndugu zake na wapwa wake wanaume ishirini.

20 Vile vile walileta Wanethini 220, kikundi ambacho Daudi na maafisa walikuwa wamekiweka kusaidia Walawi. Wote walikuwa wameorodheshwa kwa majina.

21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeshe mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali zetu zote.

22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.”

23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.

24 Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi,

25 nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Israeli wote waliokuwapo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu.

26 Niliwapimia talanta 650za fedha, vifaa vingine vya fedha talanta 100, talanta 100 za dhahabu,

27 mabakuli ishirini ya dhahabu thamani yake darkoni 1,000na vyombo viwili vilivyonakshiwa kwa shaba, thamani yake sawa na dhahabu.

28 Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwaBwana. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwaBwana, Mungu wa baba zenu.

29 Vilindeni kwa uangalifu mpaka mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba yaBwanakatika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.”

30 Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu.

31 Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu kwenye siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyang’anyi.

32 Kwa hiyo tuliwasili Yerusalemu ambapo tulipumzika kwa siku tatu.

33 Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eliyazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, pia walikuwako Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua na Noadia mwana wa Binui.

34 Kila kitu kilihesabiwa kwa idadi na kupimwa kwa uzito, nao uzito wote uliandikwa wakati ule.

35 Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo waume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba na mbuzi waume kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwaBwana.

36 Pia walikabidhi manaibu wa kifalme na watawala wa Ng’ambo ya Mto Eufrati maagizo ya mfalme, ambao baadaye walitoa msaada kwa watu na kwa nyumba ya Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZR/8-6d71cad26dccde72a943b85ecaa817e8.mp3?version_id=1627—

Ezra 9

Maombi Ya Ezra Kuhusu Kuoa Wake Wa Kigeni

1 Baada ya mambo haya kutendeka, viongozi walinijia na kusema, “Watu wa Israeli, wakiwemo makuhani na Walawi, hawakujitenga na majirani zao katika kufanya machukizo, kama yale ya Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabi, Wamisri na Waamori.

2 Wamewaoa baadhi ya binti zao kuwa wake zao na wake za wana wao, nao wamechanganya taifa takatifu na watu waliowazunguka. Nao viongozi na maafisa wamekuwa mstari wa mbele katika njia hii potovu.”

3 Niliposikia jambo hili nilirarua koti langu na joho langu, nikazing’oa nywele za kichwa changu na ndevu zangu na kuketi nikishangaa.

4 Kisha kila mmoja aliyetetemeshwa na maneno ya Mungu wa Israeli alikusanyika kunizunguka kwa sababu ya upotovu huu wa hao watu waliorudi kutoka utumwani. Nami niliketi pale nikishangaa mpaka wakati wa dhabihu ya jioni.

5 Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka katika kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwaBwanaMungu wangu.

6 Nami nikaomba:

“Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni.

7 Tokea siku za babu zetu mpaka sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo.

8 “Lakini sasa, kwa muda mfupi,BwanaMungu wetu amekuwa na neema kwa kutuachia mabaki na kutupa mahali imara katika mahali pake patakatifu, hivyo Mungu wetu atupa mwanga machoni petu na unafuu katika utumwa wetu.

9 Ingawa tu watumwa, Mungu wetu hajatuacha katika kufungwa kwetu. Ametuonyesha huruma mbele ya wafalme wa Uajemi: Ametujalia maisha mapya kwa kujenga upya nyumba ya Mungu wetu na kukarabati magofu yake, naye ametupa ukuta wa ulinzi katika Yuda na Yerusalemu.

10 “Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo

11 uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.

12 Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wo wote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’

13 “Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupa mabaki kama haya.

14 Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika?

15 EeBwana, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZR/9-7cddfbd2fe26240e50c28e2ea255ce42.mp3?version_id=1627—

Ezra 10

Toba Ya Watu

1 Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama, huku akilia na kujitupa chini mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa Waisraeli, wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kumzunguka. Nao pia wakalia sana.

2 Kisha Shekania mwana wa Yehieli, mmoja wa wazao wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni kutoka mataifa yanayotuzunguka. Lakini pamoja na hili, bado liko tumaini kwa ajili ya Israeli.

3 Sasa na tufanye agano mbele za Mungu wetu kuwafukuza hawa wanawake wote pamoja na watoto wao, kulingana na maonyo ya bwana wangu pamoja na wale ambao wanaogopa amri za Mungu wetu. Hili na lifanyike sawasawa na hii Sheria.

4 Inuka, suala hili lipo mikononi mwako. Sisi tutaungana nawe, uwe na ujasiri ukatende hili.”

5 Basi Ezra akainuka na kuwaapisha makuhani viongozi, Walawi na Israeli yote kufanya lile lililokuwa limependekezwa. Nao wakaapa.

6 Ndipo Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu akaenda kwenye chumba cha Yehohanani mwana wa Eliashibu. Wakati alipokuwa hapo, hakula chakula wala hakunywa maji, kwa sababu aliendelea kuomboleza kuhusu kukosa uaminifu kwa watu wa uhamishoni.

7 Ndipo lilipotolewa tangazo Yuda yote na Yerusalemu kwa watu wote waliokuwa uhamishoni kukusanyika Yerusalemu.

8 Ye yote ambaye hangejitokeza kwa muda wa siku tatu angepoteza mali yake yote, kulingana na uamuzi wa maafisa na wazee, naye mtu huyo angefukuzwa kutoka kusanyiko la watu waliokuwa uhamishoni.

9 Katika muda wa siku tatu, watu wote wa Yuda na Benyamini wakawa wamekusanyika huko Yerusalemu. Kwenye siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walikuwa wameketi ndani ya uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakiwa na majonzi mno kwa tukio hilo na kwa sababu ya mvua kubwa.

10 Ndipo Kuhani Ezra aliposimama akawaambia, “Mmekosa uaminifu, mmeoa wanawake wa kigeni, mkaongezea hatia ya Israeli.

11 Sasa tubuni kwaBwana, Mungu wa baba zenu mkafanye mapenzi yake. Jitengeni na mataifa wanaowazunguka na wake zenu wa kigeni.”

12 Kusanyiko lote likajibu kwa sauti kubwa: “Uko sawa kabisa! Ni lazima tufanye kama unavyosema.

13 Lakini hapa pana watu wengi na ni wakati wa mvua, hivyo hatuwezi kusimama nje. Hata hivyo, shauri hili haliwezi kumalizika kwa siku moja au mbili, kwa sababu tumefanya dhambi kubwa katika jambo hili.

14 Maafisa wetu na wafanye kwa niaba ya kusanyiko lote. Kisha kila mmoja katika miji yetu ambaye ameoa mwanamke wa kigeni aje kwa wakati uliopangwa, akiwa pamoja na wazee na waamuzi wa kila mji, hadi hasira kali ya Mungu wetu katika shauri hili itakapoondolewa kwetu.”

15 Yonathani mwana wa Asaheli na Yazeya mwana wa Tikwa peke yao, wakiungwa mkono na Meshulamu na Shabethai Mlawi, ndio waliopinga jambo hili.

16 Basi watu wa uhamishoni wakafanya kama ilivyokuwa imependekezwa. Kuhani Ezra akachagua wanaume waliokuwa viongozi wa jamaa, mmoja kutoka kila mgawanyo wa jamaa, nao wote wakachaguliwa kwa majina. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kumi waliketi kuchunguza mashauri hayo.

17 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wakawa wamemaliza kushughulikia wanaume wote ambao walikuwa wameoa wanawake wa kigeni.

Wenye Hatia Ya Kuoa Wake Wa Kigeni

18 Miongoni mwa wazao wa makuhani, wafuatao walikuwa wameoa wanawake wa kigeni:

Kutoka wazao wa Yeshua mwana wa Yozadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia.

19 (Wote walitoa nadhiri kwa kuandika kwa mikono yao kuwafukuza wake zao, kwa hatia yao, kila mmoja akatoa kondoo dume kutoka kundini mwake kama sadaka ya hatia.)

20 Kutoka wazao wa Imeri:

Hanani na Zebadia.

21 Kutoka wazao wa Harimu:

Maaseya, Eliya, Shemaya, Yehieli na Uzia.

22 Kutoka wazao wa Pashuri:

Elioenai, Maaseya, Ishmaeli, Nethaneli, Yozabadi na Elasa.

23 Miongoni mwa Walawi:

Yozabadi, Shimei, Kelaya (ndiye Kelita), Pethahia, Yuda na Eliezeri.

24 Kutoka waimbaji:

Eliyashibu.

Kutoka mabawabu:

Shalumu, Telemu na Uri.

25 Miongoni mwa Waisraeli wengine:

Kutoka wazao wa Paroshi:

Ramia, Izia, Malkiya, Miyamini, Eleazari, Malkiya na Benaya.

26 Kutoka wazao wa Elamu:

Matania, Zekaria, Yehieli, Abdi, Yeremothi na Eliya.

27 Kutoka wazao wa Zatu:

Elioenai, Eliyashibu, Matania, Yeremothi, Zabadi na Aziza.

28 Kutoka uzao wa Bebai:

Yehohanani, Hanania, Zabai na Athlai.

29 Kutoka wazao wa Bani:

Meshulamu, Maluki, Adaia, Yashubu, Sheali na Yeremothi.

30 Kutoka wazao wa Pahath-Moabu:

Adna, Kelali, Benaya, Maaseya, Matania, Bezaleli, Binui na Manase.

31 Kutoka wazao wa Harimu:

Eliezeri, Ishiya, Malkiya, Shemaya, Shimeoni,

32 Benyamini, Maluki, na Shemaria.

33 Kutoka wazao wa Hashumu:

Matenai, Matata, Zabadi, Elifeleti, Yeremai, Manase na Shimei.

34 Kutoka wazao wa Bani:

Maadai, Amramu, Ueli,

35 Benaya, Bedeya, Keluhi,

36 Vania, Meremothi, Eliyashibu,

37 Matania, Matenai na Yaasu.

38 Kutoka wazao wa Binui:

Shimei,

39 Shelamia, Nathani, Adaya,

40 Maknadebai, Shashai, Sharai,

41 Azareli, Shelemia, Shemaria,

42 Shalumu, Amaria na Yosefu.

43 Kutoka wazao wa Nebo:

Yeieli, Matithia, Zabadi, Zebina, Yadai, Yoeli na Benaya.

44 Hawa wote walikuwa wameoa wanawake wa kigeni, na baadhi yao walikuwa wamezaa nao watoto.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZR/10-6edb30447d3a77c8b1f7d5ac8359812e.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 1

Solomoni Aomba Hekima

1 Solomoni mwana wa Daudi alijiimarisha kwenye milango yote! Katika ufalme wake, kwa kuwaBwanaMungu wake alikuwa pamoja naye, naye akamfanya mkuu mno.

2 Ndipo Solomoni akasema na Israeli wote, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, waamuzi na viongozi wote katika Israeli, pamoja na wakuu wa jamaa.

3 Naye Solomoni na kusanyiko lote wakakwea mpaka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kwa kuwa huko ndiko hema la Mungu la Mkutano lilipokuwa, ambalo Mose mtumishi waBwanaalikuwa amelitengeneza huko jangwani.

4 Basi Daudi alikuwa amelipandisha Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu mpaka mahali alipokuwa amepatengeneza kwa ajili yake, kwa sababu alikuwa amesimamisha hema kwa ajili ya hilo Sanduku huko Yerusalemu.

5 Lakini ile madhabahu ya shaba ambayo Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, alikuwa ametengeneza ilikuwa huko Gibeoni mbele ya Maskani yaBwanaMungu, hivyo Solomoni na kusanyiko lote walimtafuta Mungu huko.

6 Solomoni akapanda huko ilikokuwa madhabahu ya shaba mbele zaBwanakatika Hema la Kukutania na kutoa dhabihu 1,000 za sadaka za kuteketezwa juu yake.

7 Usiku ule Mungu akamtokea Solomoni na kumwambia, “Omba lo lote unalotaka nami nitakupa.”

8 Solomoni akamjibu Mungu, “Umemwonyesha baba yangu Daudi fadhili nyingi nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake.

9 Sasa,BwanaMungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi.

10 Nakuomba unipe mimi hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?”

11 Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao,

12 kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima ambayo hakuna mfalme ye yote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo na hakuna ye yote baada yako atakayekuwa navyo.”

13 Ndipo Solomoni akaenda mpaka Yerusalemu kutoka mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni, kutoka mbele ya Hema la Kukutania. Naye akatawala juu ya Israeli.

14 Solomoni akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari ya vita 1,400 na farasi 12,000, ambayo aliyaweka katika miji ya magari ya vita na mengine akawanayo huko Yerusalemu.

15 Mfalme akaongeza fedha na dhahabu vikawa vitu vya kawaida kama vile mawe huko Yerusalemu, nayo mierezi ikawa mingi kama miti ya mikuyu chini ya vilima.

16 Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanya biashara wa kifalme waliwanunua kutoka Kue.

17 Walileta magari ya vita kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600za fedha kwa kila moja, na kwa kila farasi shekeli 150. Pia wakawapeleka ili kuwauzia wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/1-5ef19118ea4007a9ea50e0c041c1639a.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 2

Maandalizi Ya Kujenga Hekalu

1 Solomoni akatoa amri kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina laBwanana jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe.

2 Akaandika watu 70,000 kuwa wachukuzi wa mizigo, na watu 80,000 kuwa wachonga mawe vilimani, na watu 3,600 kuwa wasimamizi wao.

3 Solomoni akapeleka ujumbe huu kwa Mfalme Hiramu wa Tiro:

“Unitumie magogo ya mierezi kama ulivyomfanyia baba yangu Daudi wakati ulipompelekea mierezi ya kujenga jumba lake la kifalme la kuishi.

4 Sasa ninakaribia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina laBwanaMungu wangu na kuliweka wakfu kwake kwa ajili yakufukizia uvumba wenye harufu nzuri mbele zake, mahali pa kuweka mikate Mitakatifu kwa kufuata utaratibu na kwa ajili ya mahali pa kutolea sadaka za kuteketezwa kila siku asubuhi na jioni, siku za Sabato na Mwezi Mwandamo pia katika sikukuu zilizoamuriwa zaBwanaMungu wetu. Hili ni agizo la kudumu kwa ajili ya Waisraeli.

5 “Hekalu nitakalolijenga litakuwa kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu kuliko miungu mingine yote.

6 Lakini ni nani awezaye kumjengea Hekalu, maadamu mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, hazimtoshi? Mimi ni nani basi hata nijenge Hekalu kwa ajili yake, isipokuwa liwe tu kama mahali pa kutolea dhabihu za kuteketezwa mbele zake?

7 “Hivyo basi nitumie mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi ya kutengeneza dhahabu na fedha, shaba na chuma, nyuzi za rangi ya zambarau, nyekundu na buluu, mwenye uzoefu wa kutia nakshi, ili afanye kazi Yuda na Yerusalemu pamoja na mafundi wangu wenye ustadi, ambao baba yangu Daudi aliwaweka.

8 “Pia nitumie magogo ya mierezi, miberoshi na misanduku kutoka Lebanoni kwa maana najua kwamba watu wako wanao ujuzi wa kupasua mbao huko. Watu wangu watafanya kazi pamoja na watu wako

9 ili wanipatie mbao kwa wingi kwa sababu Hekalu nitakalojenga lazima liwe kubwa na zuri kabisa.

10 Nitawapa watumishi wako, yaani, maseremala wakatao mbao, kori 20,000za unga wa ngano, kori 20,000 za shayiri, bathi 20,000za mvinyo, na bathi 20,000 za mafuta ya zeituni.”

11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akamjibu Solomoni kwa barua:

“Kwa sababuBwanaanawapenda watu wake, amekufanya wewe kuwa mfalme wao.”

12 Naye Hiramu akaongeza kusema:

“AhimidiweBwana, Mungu wa Israeli aliyezifanya mbingu na nchi! Amempa Mfalme Daudi mwana mwenye hekima, aliyejaliwa maarifa na ufahamu, ambaye atajenga Hekalu kwa ajili yaBwana, na jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe.

13 “Mimi nitamtuma kwako Huramu-Abi, mtu mwenye ustadi mwingi,

14 ambaye mama yake alitoka Dani na baba yake alitoka Tiro. Yeye ni stadi wa kutengeneza vitu, kufanya kazi zote za dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe na mbao pamoja na kufuma. Ni stadi katika kutia rangi ya zambarau, buluu, nyekundu na nguo za kitani safi. Yeye ana ujuzi katika aina zote za kutia nakshi na anaweza kufuatiliza mchoro wo wote wa kazi anayopewa. Atafanya kazi na mafundi wako na wale wa bwana wangu, Daudi baba yako.

15 “Sasa basi bwana wangu na awapelekee watumishi wake ngano, shayiri, mafuta ya zeituni na mvinyo kama alivyoahidi,

16 nasi tutakata magogo yote yale unayohitaji kutoka Lebanoni nasi tutayafunga pamoja na kuyaweka yaelee baharini mpaka Yafa. Kisha utaweza kuyachukua mpaka Yerusalemu.”

17 Ndipo Solomoni akaamuru ifanyike hesabu ya wageni wote waliokuwa katika Israeli, baada ya ile hesabu iliyofanywa na Daudi; wakapatikana watu 153,600.

18 Akawaweka watu 70,000 miongoni mwao kuwa wachukuzi wa mizigo, na 80,000 kuwa wachonga mawe vilimani, na 3,600 wakiwa wasimamizi juu yao ili wawahimize watu kufanya kazi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/2-3b02c501231c34d5184877de66f2c8bf.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 3

Solomoni Ajenga Hekalu

1 Ndipo Solomoni akaanza kujenga Hekalu laBwanakatika Yerusalemu juu ya Mlima Moria, pale ambapoBwanaalikuwa amemtokea Daudi baba yake. Ilikuwa katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi, mahali palipotolewa na Daudi.

2 Alianza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa kutawala kwake.

3 Msingi aliouweka Solomoni kwa ajili ya kulijenga Hekalu la Mungu ulikuwa urefu wa dhiraa sitinina upana dhiraa ishirini.

4 Ukumbi wa mbele wa Hekalu ulikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, yaani, kuanzia upande mmoja hadi upande mwingine wa upana wa nyumba hiyo na kimo chake dhiraa thelathini.

Akaufunika ndani kwa dhahabu safi.

5 Akaufunika ukumbi mkuu kwa mbao za miberoshi na kufunikwa kwa dhahabu safi na kuupamba kwa miti ya mitende na kuifanyizia kwa minyororo.

6 Alilipamba Hekalu kwa mawe ya thamani. Hiyo dhahabu aliyotumia ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.

7 Akazifunika boriti za dari, miimo na vizingiti vya milango, kuta na milango ya Hekalu kwa dhahabu, naye akatia nakshi ya makerubi kwenye kuta.

8 Akajenga Patakatifu pa Patakatifu, urefu na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini, sawasawa na upana wa Hekalu. Alifunika ndani kwa talanta 120za dhahabu safi.

9 Misumari ya dhahabu ilikuwa na uzito wa shekeli hamsini. Alivifunika pia vyumba vya juu kwa dhahabu.

10 Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akafanyiza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu.

11 Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano, nalo liligusa ukuta wa Hekalu, bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi lingine.

12 Vivyo hivyo bawa moja la kerubi wa pili lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na liligusa ukuta mwingine wa pili wa Hekalu na bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano nalo liligusa bawa la kerubi wa kwanza.

13 Mabawa ya makerubi hawa yalitanda dhiraa ishirini. Walisimama kwa miguu yao, nyuso zao zikielekea ukumbi mkubwa.

14 Akatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na za kitani safi na kutarizi makerubi juu yake.

15 Mbele ya Hekalu Solomoni akatengeneza nguzo mbili, ambazo kwa pamoja zilikuwa na dhiraa thelathini na tano kwenda juu kwake na urefu wa kila moja ilikuwa na taji juu yake yenye dhiraa tano.

16 Akatengeneza minyororo iliyosokotwa na kuiweka juu ya zile nguzo. Pia akatengeneza makomamanga 100 na kuyashikamanisha kwenye minyororo.

17 Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya Hekalu, moja upande wa kusini na nyingine upande wa kaskazini. Ile moja ya upande wa kusini akaiita Yakinina ya upande wa kaskazini akaiita Boazi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/3-afa104b48820ef241793df3f1842922d.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 4

Vifaa Vya Hekalu

1 Mfalme Solomoni akatengeneza madhabahu ya shaba yenye urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini na kimo chake dhiraa kumi.

2 Akatengeneza Bahari ya kusubu, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kina chake kilikuwa dhiraa tano. Kamba ya urefu wa dhiraa thelathiniingeweza kuizunguka.

3 Chini ya huo ukingo, kulikuwa na mafahali kuizunguka, yaani mafahali kumi katika kila dhiraa moja. Hayo mafahali waliyasubu katika safu mbili yakiwa ya kitu kimoja na hiyo Bahari.

4 Bahari hiyo ilikaa juu ya mafahali kumi na mawili, mafahali matatu yalielekeza nyuso zao kaskazini, matatu magharibi, matatu kusini na matatu mashariki. Bahari hiyo ilikaa juu ya hao mafahali, nazo sehemu zao za nyuma zilielekea katikati.

5 Unene wake ulikuwa nyanda nne, ambao ulikuwa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi li lililochanua. Bahari hii iliweza kuchukua kiasi cha bathi 3,000.

6 Kisha akatengeneza masinia kumi kwa ajili ya kuoshea vifaa, naye akayaweka matano upande wa kusini na matano upande wa kaskazini. Ndani yake ndimo vilimooshewa vifaa vya kutumika katika sadaka za kuteketezwa, lakini ile Bahari ilikuwa ni kwa ajili ya makuhani kunawia.

7 Akatengeneza vinara vya taa kumi vya dhahabu kama ilivyoainishwa kwao na kuviweka hekaluni, vinara vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini.

8 Akatengeneza meza kumi na kuziweka hekaluni, tano upande wa kusini na tano upande wa kaskazini. Pia akatengeneza mabakuli 100 ya dhahabu ya kunyunyizia.

9 Akatengeneza ukumbi wa makuhani na ukumbi mwingine mkubwa na milango yake, naye akaifunika hiyo milango kwa shaba.

10 Akaweka ile Bahari upande wa kusini, kwenye pembe ya kusini mashariki ya nyumba.

11 Pia akatengeneza masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.

Kwa hiyo Huramu akamaliza kazi aliyokuwa amefanya kwa ajili ya Mfalme Solomoni katika Hekalu la Mungu:

12 zile nguzo mbili;

yale mataji mawili yaliyokuwa juu ya hizo nguzo,

zile nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli yaliyowekwa juu ya zile nguzo;

13 yale makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu yakipamba hizo nyavu mbili zilizowekwa juu ya zile nguzo);

14 vishikio pamoja na masinia yake;

15 hiyo Bahari na hao mafahali kumi na wawili chini yake;

16 pia hayo masufuria, masepetu, nyuma za nyama na vyombo vingine vyote vilivyohusiana.

Vitu vyote ambavyo Huramu-Abi alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu laBwanavilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.

17 Mfalme aliagiza wavisubu vitu hivi kwenye kalibu za udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani kati ya Sukothi na Seredatha.

18 Vitu hivi vyote Mfalme Solomoni alivyotengeneza vilikuwa vingi sana kwamba uzito wa shaba haukuweza kuonyeshwa.

19 Solomoni pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu:

madhabahu ya dhahabu;

meza za kuweka mikate Mitakatifu;

20 vinara vya taa vya dhahabu safi pamoja na taa zake ili ziwake mbele ya mahali pa ndani pa mahali Patakatifu kama ilivyoelekezwa;

21 maua ya dhahabu yaliyofanyizwa, taa na makoleo (vilikuwa vya dhahabu bora kabisa);

22 mikasi ya dhahabu safi, mabakuli ya kunyunyizia, masinia na vyetezo; milango ya dhahabu ya Hekalu: yaani milango ya ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, na milango ya ukumbi mkuu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/4-1ec53461b6822a89bcf07cbc99b022b3.mp3?version_id=1627—