2 Wathesalonike 1

1 Paulo, Silvanona Timotheo:

Kwa kanisa la Wathesalonike mlio katika Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo:

2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

Shukrani Na Maombi

3 Ndugu, imetubidi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, kama ulivyo wajibu wetu, kwa sababu imani yenu inakua zaidi na zaidi na upendo wa kila mmoja wenu alio nao kwa mwenzake unazidi kuongezeka.

4 Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili Ufalme wa Mungu, ambao ninyi mnateswa kwa ajili yake.

6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi

7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu.

8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu.

9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake,

10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

11 Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili kwamba Mungu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu.

12 Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TH/1-0820fd132b2c68a2a847b81ffc04d4ff.mp3?version_id=1627—

2 Wathesalonike 2

Yule Mtu Wa Kuasi

1 Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi,

2 msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho wala neno au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, isemayo kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwako.

3 Mtu ye yote na asiwadanganye kwa namna yo yote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa.

4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.

5 Je, hamkumbuki ya kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya?

6 Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili kwamba apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia.

7 Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo mpaka atakapoondolewa.

8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake.

9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo

10 na kila aina ya udanganyifu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa.

11 Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo

12 na hivyo wote wahukumiwe ambao hawakuamini ule ukweli bali wamefurahia uovu.

Simameni Imara

13 Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli.

14 Kwa kusudi hili Mungu aliwaita kwa njia ya kuhubiri kwetu Injili, ili kwamba mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana Yesu Kristo.

15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.

16 Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema,

17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TH/2-353c646b730e695a504f56d93075ec80.mp3?version_id=1627—

2 Wathesalonike 3

Ombi La Kuhitaji Maombi

1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili kwamba Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwa upande wenu.

2 Ombeni pia ili kwamba tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si kila mmoja ana imani.

3 Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu.

4 Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza.

5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.

Onyo Dhidi Ya Uvivu

6 Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.

7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi,

8 wala hatukula chakula cha mtu ye yote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu ye yote miongoni mwenu.

9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, lakini ili kusudi tujifanye sisi wenyewe kuwa kielelezo.

10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri ili kwamba: “Mtu ye yote asiyetaka kufanya kazi, wala asile.”

11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine.

12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwaonya katika Jina la Bwana Yesu Kristo wafanye kazi kwa utulivu na kujipatia mahitaji ya maisha yao wao wenyewe.

13 Kwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.

14 Ikiwa mtu ye yote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili kwamba apate kuona aibu.

15 Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

Salamu Za Mwisho

16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

17 Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.

18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2TH/3-ff6d0d373cb935040c7ee8129426f3e7.mp3?version_id=1627—

1 Wathesalonike 1

Salamu

1 Paulo, Silvanona Timotheo:

Kwa kanisa la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu Baba yetu na ndani ya Bwana Yesu Kristo:

Neema iwe kwenu na amani, itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani Kwa Ajili Ya Imani Ya Wathesalonike

2 Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima.

3 Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo.

4 Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua,

5 kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda katikati yenu kwa ajili yenu.

6 Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu.

7 Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya.

8 Kwa maana kutoka kwenu Neno la Mungu limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali kiasi kwamba hatuna haja ya kusema lo lote kwa habari yake.

9 Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli

10 na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani, Yesu, yeye aliyetuokoa kutoka katika ghadhabu inayokuja.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/1-82635613553dd47423aab2aac573faa2.mp3?version_id=1627—

1 Wathesalonike 2

Huduma Ya Paulo Huko Thesalonike

1 Ndugu zangu, kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ya kwamba kuja kwetu kwenu hakukuwa bure,

2 kama vile mjuavyo, tulikuwa tumeteswa na kutukanwa huko Filipi, lakini hata hivyo, kwa msaada wa Mungu wetu, tulikuwa na ujasiri wa kuwaambia Injili ya Mungu ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa.

3 Kwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu.

4 Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu.

5 Kama mjuavyo na Mungu akiwa shahidi yetu hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli kwa ajili ya kuficha tamaa mbaya.

6 Wala hatukuwa tunatafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine awaye yote.

Kama mitume wa Kristo tungaliweza kuwa mzigo kwenu,

7 lakini tulikuwa wapole katikati yenu kama mama anayewatunza watoto wake wadogo.

8 Tuliwapenda sana kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu.

9 Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee mtu ye yote wa kwenu wakati tulipokuwa tunawahubiria Injili ya Mungu.

10 Ninyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini.

11 Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba awatendeavyo watoto wake mwenyewe.

12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yampendezayo Mungu, anayewaita katika Ufalme na utukufu wake.

13 Nasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, litendalo kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.

14 Kwa maana ninyi ndugu zetu, mlifanyika wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyoko ndani ya Kristo Yesu katika Uyahudi. Mlipata mateso yale yale kutoka kwa watu wenu wenyewe kama vile makanisa hayo yalivyoteswa na Wayahudi,

15 wale waliomwua Bwana Yesu na manabii, nasi wakatufukuza pia. Watu hao walimchukiza Mungu na tena ni adui wa watu wote,

16 wakijitahidi kutuzuia tusizungumze na watu wa Mataifa ili kwamba wapate kuokolewa. Kwa njia hii wanazidi kujilundikia dhambi zao ili kufikia upeo. Lakini hatimaye ghadhabu ya Mungu imewafikia.

Paulo Atamani Kuwaona Wathesalonike

17 Lakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa kitambo kidogo (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso.

18 Maana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia.

19 Kwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu au taji yetu ya kujisifia mbele za Bwana Yesu Kristo wakati wa kuja kwake? Je, si ninyi?

20 Naam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/2-67aafa193dde759379eb0b5214b9fd71.mp3?version_id=1627—

1 Wathesalonike 3

Timotheo Atumwa Kwenda Thesalonike

1 Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu,

2 tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Kristo, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu,

3 ili mtu ye yote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso.

4 Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mjuavyo.

5 Kwa sababu hii nilipokuwa siwezi kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure.

Taarifa Ya Timotheo Ya Kutia Moyo

6 Lakini sasa Timotheo ndiyo tu amerejea kwetu kutoka kwenu na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi.

7 Kwa hiyo, ndugu zetu, katika dhiki na mateso yetu yote tumefarijika kwa sababu ya imani yenu.

8 Kwa maana sasa kwa hakika tunaishi kwa kuwa ninyi mmesimama imara katika Bwana.

9 Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu?

10 Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaliza kile kilichopungua katika imani yenu.

11 Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Yesu atengeneze njia ya sisi kuja kwenu.

12 Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati ya ninyi kwa ninyi na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu.

13 Tunamwomba Mungu awaimarishe mioyo yenu katika utakatifu ili msiwe na lawama mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana Yesu pamoja na watakatifu wote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/3-a0d28d54a96602861b5e3340562f91c2.mp3?version_id=1627—

1 Wathesalonike 4

Maisha Yanayompendeza Mungu

1 Hatimaye, ndugu, tuliwaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu kwamba, kama mlivyojifunza kutoka kwetu jinsi iwapasavyo kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi, imewapasa mzidi sana kufanya hivyo.

2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

3 Kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu ninyi mwe watakatifu, ili kwamba mjiepushe na uasherati,

4 ili kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima,

5 si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu.

6 Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali.

7 Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu.

8 Kwa hiyo, mtu ye yote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

9 Sasa kuhusu upendano wa ndugu hamna haja mtu ye yote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.

10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza,

12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu ye yote.

Kuja Kwake Bwana

13 Lakini ndugu, hatutaki msijue kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.

14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, hata hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mauti katika yeye.

15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe tunawaambia kwamba, sisi ambao bado tuko hai, tutakaobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wale waliolala mauti.

16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu pamoja na sauti ya malaika mkuu na sauti ya tarumbeta ya Mungu, nao wale waliolala mauti wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza.

17 Baada ya hilo sisi tulio hai bado, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/4-d9f2fc62eb99b12a94f50e9a4d4ced21.mp3?version_id=1627—

1 Wathesalonike 5

Iweni Tayari Kwa Siku Ya Bwana

1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia,

2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwivi ajapo usiku.

3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba wala hawatatoroka.

4 Bali ninyi, ndugu, hamko gizani hata kwamba siku ile iwakute ghafula kama mwivi.

5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku.

6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi.

7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku.

8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.

9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili kwamba kama tuko macho au tukiwa tumelala tupate kuishi pamoja naye.

11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

Maagizo Ya Mwisho, Salamu Na Kuwatakia Heri

12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya.

13 Mkawajali sana katika upendo kwa ajili ya kazi yao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni wale wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na iweni na uvumilivu na kila mtu.

15 Angalieni kuwa mtu asilipe ovu kwa ovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

16 Furahini siku zote;

17 ombeni pasipo kukoma;

18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

19 Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu;

20 msiyadharau maneno ya unabii.

21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema.

22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.

23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo.

24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

25 Ndugu, tuombeeni.

26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.

27 Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.

28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/5-9e5b0ece028ec883a54dc818e52749aa.mp3?version_id=1627—

Wakolosai 1

Salamu

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu k wa mapenzi ya Mungu na Timotheo ndugu yetu:

2 Kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Kristo, waishio Kolosai:

Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu.

Shukrani Na Maombi

3 Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapowaombea ninyi,

4 kwa sababu tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote,

5 imani na upendo ule utokao katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani,

6 ile Injili iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote.

7 Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, yeye aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu,

8 ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho.

9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatukukoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu.

10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana na mpate kumpendeza kwa kila namna: Mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikuwa katika kumjua Bwana.

11 Mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu, nanyi kwa furaha

12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru.

13 Kwa maana ametuokoa kutoka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa,

14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi kwa njia ya damu yake.

Ukuu Wa Kristo

15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

16 Kwa yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa, vile vitu vinavyoonekana na vile visivyoonekana, kama ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala, vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake.

17 Yeye alikuwapo kabla ya vitu vyote na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.

18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani, Kanisa, naye ni wa mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote.

19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba ukamilifu wake wote wa Kiungu uwe ndani yake

20 na kwa njia ya Mwanawe aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, ikiwa ni vitu vilivyoko duniani au vilivyoko mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake iliyomwagika msalabani.

21 Hapo kwanza ninyi mlikuwa mmetengana na Mungu na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mwenendo wenu mbaya.

22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kwa kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama,

23 mradi tu kwamba mnaendelea kuwa waaminifu, mkiwa mmefanywa imara na thabiti katika imani, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa na Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu na ambayo mimi Paulo, nimekuwa mtumwa wake.

Taabu Ya Paulo Kwa Ajili Ya Kanisa

24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni Kanisa.

25 Mimi nimekuwa mtumishi wa Kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu.

26 Siri hii ilikuwa imefichika kwa karne nyingi na vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu.

27 Kwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.

28 Yeye Kristo ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo.

29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zile ambazo kwa uweza mwingi hutenda kazi ndani yangu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/COL/1-5e7586a32e83046f918bf14979237821.mp3?version_id=1627—

Wakolosai 2

1 Kwa kuwa nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia na kwa ajili ya wote wale ambao hawajapata kuniona mimi binafsi.

2 Kusudi langu ni kuwa watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu kikamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe,

3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa.

4 Nawaambia mambo haya ili mtu ye yote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi.

5 Kwa maana ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi gani uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.

Ukamilifu Wa Maisha Katika Kristo

6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake,

7 mwe na mizizi, mkiwa mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa na kufurika kwa wingi wa shukrani.

8 Angalieni mtu ye yote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu ambayo siyo ya Kristo.

9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu,

10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye yeye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka.

11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo,

12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu.

13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote,

14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili pamoja na amri zake, aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake.

15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba wa Kristo.

16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au Siku ya Sabato.

17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo.

18 Mtu ye yote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kumnyenyekea yeye na kuabudu malaika, akidumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu,

19 wala hakishiki kwa uthabiti kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, ambao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

Maonyo Dhidi Ya Walimu Wa Uongo

20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama vile ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri:

21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”?

22 Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu huo msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu.

23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/COL/2-984a4793f812cb1e7c5e7330e2a37cc8.mp3?version_id=1627—