2 Mambo ya nyakati 25

Amazia Mfalme Wa Yuda

1 Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani kutoka Yerusalemu.

2 Akatenda yaliyo mema machoni paBwana, lakini si kwa moyo wake wote.

3 Baada ya ufalme wote kuimarika katika milki yake, aliwaua maafisa waliomwua mfalme baba yake.

4 Hata hivyo hakuwaua watoto wao, lakini akafanya sawasawa na yaliyoandikwa kwenye Sheria, katika kitabu cha Mose, mahaliBwanaalipoamuru: “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya baba zao, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”

5 Amazia akawaita watu wa Yuda pamoja, akawaweka chini ya majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia kufuatana na jamaa zao katika Yuda yote na Benyamini. Kisha akawahesabu wale wenye umri wa miaka ishirini au zaidi na akakuta kwamba walikuwa wanaume 300,000 watu walio tayari kwa utumishi wa jeshi, walio na uwezo wa kutumia mkuki na ngao.

6 Akawaajiri pia watu 100,000 wapiganaji kutoka Israeli kwa talanta 100 za fedha.

7 Lakini mtu wa Mungu akamjia na kumwambia, “Ee mfalme, haya majeshi kutoka Israeli kamwe usiyaruhusu yaende pamoja na wewe kwa kuwaBwanahayuko pamoja na Israeli, wala hayupo pamoja na ye yote wa watu wa Efraimu.

8 Hata kama ukienda na kupigana kwa ujasiri katika vita, Mungu atakufanya ukimbie mbele ya adui, kwa kuwa Mungu anao uwezo wa kusaidia au wa kuangusha.”

9 Amazia akamwuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta 100 za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?”

Yule mtu wa Mungu akajibu, “Bwanaaweza kukupa zaidi sana ya hizo.”

10 Hivyo Amazia akayaondoa yale majeshi yaliyokuwa yamekuja kutoka Efraimu na kuyarudisha nyumbani. Waliwakasirikia sana Yuda, nao wakarudi nyumbani wakiwa na hasira kali.

11 Ndipo Amazia akajitia nguvu na kuliongoza jeshi lake kwenye Bonde la Chumvi, ambako aliua watu 10,000 wa Seiri.

12 Jeshi la Yuda pia likawateka watu 10,000 wakiwa hai, likawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini kwa nguvu hata wote wakavunjika vipande vipande.

13 Wakati huo yale majeshi Amazia aliyoyarudisha na ambayo hakuyaruhusu kushiriki katika vita, yalivamia miji ya Yuda kuanzia Samaria hata Beth-Horoni. Yakawaua watu 3,000 na kuchukua kiasi kikubwa sana cha mateka.

14 Amazia aliporudi kutoka kuwachinja Waedomu, alileta pia kutoka huko miungu ya watu wa Seiri. Akaisimamisha kama miungu yake mwenyewe, akaisujudia na kuitolea kafara za kuteketezwa.

15 Hasira yaBwanaikawaka dhidi ya Amazia, naye akamtuma nabii kwake, ambaye alisema: “Kwa nini unauliza kwa miungu ya hawa watu, ambayo haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mkononi mwako?”

16 Wakati nabii alipokuwa angali anazungumza, mfalme akamwambia, “Je, wewe tumekuchagua kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza, ya nini uuawe?”

Hivyo nabii akanyamaza lakini akasema, “Najua kuwa Mungu ameazimia kukuangamiza kwa sababu umefanya jambo hili na hukusikiliza shauri langu.”

17 Baada ya Amazia mfalme wa Yuda kushauriana na washauri wake akatuma ujumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli kusema: “Njoo tukabiliane uso kwa uso.”

18 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, “Mbaruti uliokuwa huko Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa huko Lebanoni kusema, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa huko Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti.

19 Wewe unasema moyoni mwako kwamba umemshinda Edomu, nawe sasa unajigamba na kujivuna. Lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini utafute matatizo na kusababisha anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”

20 Hata hivyo, Amazia hakutaka kusikia, kwa kuwa Mungu alifanya hivyo ili awatie mikononi mwa Yehoashi, kwa sababu waliitafuta miungu ya Edomu.

21 Hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea kuwashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakabiliana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.

22 Yuda akashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake.

23 Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akamleta Yerusalemu na akaubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu dhiraa 400,

24 akachukua dhahabu yote, fedha na vyombo vyote vilivyopatikana katika Hekalu la Mungu, ambavyo vilikuwa chini ya uangalizi wa Obed-Edomu, pamoja na hazina za jumba la mfalme na mateka, kisha akarudi Samaria.

25 Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli.

26 Kwa habari ya matukio mengine katika utawala wa Amazia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na wa Israeli?

27 Kuanzia wakati ule Amazia alipogeuka na kuacha kumfuataBwanawalifanya shauri baya dhidi yake huko Yerusalemu naye akakimbilia Lakishi, lakini wakatuma watu wamfuatilie huko Lakishi nao wakamwulia huko.

28 Akarudishwa kwa farasi nao wakamzika pamoja na baba zake katika Mji wa Yuda.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/25-547f3b03ba6927e321ab8b475e06010e.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 26

Uzia Mfalme Wa Yuda

1 Kisha watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake.

2 Yeye ndiye aliyejenga upya Elathi kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.

3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipokuwa mfalme, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na miwili. Mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.

4 Akafanya yaliyo mema machoni paBwanasawasawa na Amazia baba yake alivyokuwa amefanya.

5 Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafutaBwana, Mungu alimfanikisha.

6 Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi na mahali pengine katikati ya Wafilisti.

7 Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni.

8 Waamoni wakamletea Uzia ushuru, umaarufu wake ukaenea hadi kwenye mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa amekuwa na nguvu sana.

9 Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome.

10 Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilimani na kwenye nchi tambarare. Alikuwa na watu wanaofanya kazi katika mashamba yake na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.

11 Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmojawapo wa maafisa wa kifalme.

12 Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza hawa wapiganaji walikuwa 2,600.

13 Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la askari 307,500 watu waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake.

14 Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, deraya, pinde na mawe ya kombeo.

15 Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno mpaka akawa na nguvu sana.

16 Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwaBwanaMungu wake, naye akaingia hekaluni mwaBwanaili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba.

17 Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini waBwanawenye ujasiri wakamfuata huko ndani.

18 Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukiziaBwanauvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Aroni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa naBwana.”

19 Uzia, ambaye alikuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu laBwana, ukoma ukamtokea penye kipaji chake cha uso.

20 Azaria Kuhani Mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma penye kipaji chake cha uso wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alikuwa anatamani kuondoka kwa sababuBwanaalikuwa amempiga.

21 Mfalme Uzia alikuwa na ukoma mpaka siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu laBwana. Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la kifalme, pia akawaongoza watu wa nchi.

22 Matukio mengine ya utawala wa Uzia, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, yameandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi.

23 Uzia akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika shamba la kuzikia lililokuwa mali ya wafalme, kwa kuwa watu walisema, “Alikuwa na ukoma.” Yothamu mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/26-b06ac37742ec3f3aa81498860e7caa94.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 27

Yothamu Mfalme Wa Yuda

1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki.

2 Akafanya yaliyo mema machoni paBwanakama vile Uzia baba yake alivyokuwa amefanya, lakini tofauti na yeye, hakuingilia huduma za hekaluni mwaBwana. Lakini hata hivyo, watu wakaendelea na desturi zao mbaya.

3 Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu laBwanana kufanya kazi kubwa kwenye ukuta katika kilima cha Ofeli.

4 Akajenga miji katika vilima vya Yuda pamoja na ngome na minara mwituni.

5 Yothamu akafanya vita na mfalme wa Waamoni na kumshinda. Mwaka ule Waamoni wakamlipa talanta 100za fedha, kori 10,000za ngano na kori 10,000 za shayiri. Waamoni wakamletea kiasi hicho hicho mwaka wa pili na wa tatu.

6 Yothamu akaendelea kuwa na nguvu kwa sababu alienenda kwa ukamilifu mbele zaBwanaMungu wake.

7 Matukio mengine ya utawala wa Yothamu, pamoja na vita vyake vyote na vitu vingine alivyofanya, vimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.

8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita.

9 Yothamu akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/27-81cb9949e4867f496f9f9d2415eb423a.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 28

Ahazi Mfalme Wa Yuda

1 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala. Akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni paBwana.

2 Akaziendea njia za wafalme wa Israeli na pia akasubu sanamu kwa ajili ya kuabudu Mabaali.

3 Akatoa sadaka za kuteketezwa katika Bonde la Hinomu na kuwatoa wanawe kafara kwa kuwateketeza kwa moto, akifuata njia za machukizo za yale mataifaBwanaaliyoyafukuza humo mbele ya Waisraeli.

4 Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu, juu ya vilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi uliotanda.

5 Kwa hiyoBwanaMungu wake akamtia mikononi mwa mfalme wa Aramu. Waaramu wakamshinda, wakachukua watu wake wengi mateka na kuwaleta mpaka Dameski.

Tena alitiwa mikononi mwa mfalme wa Israeli, ambaye aliwaua watu wake wengi.

6 Kwa siku moja Peka mwana wa Remalia aliwaua askari 120,000 katika Yuda, kwa kuwa Yuda walikuwa wamemwachaBwana, Mungu wa baba zao.

7 Zikri, askari shujaa Mwefraimu, akamwua Maaseya mwana wa mfalme, Azrikamu mkuu wa jumba la kifalme na Elikana aliyekuwa wa pili kwa mfalme.

8 Waisraeli wakawachukuwa mateka kutoka ndugu zao, watu wapatao 200,000 hawa wakiwa ni wanawake, watoto wa kiume na wa kike. Wakachukua pia kiasi kikubwa cha nyara, ambazo walirudi nazo Samaria.

9 Lakini kulikuwako huko nabii waBwanaaliyeitwa Odedi, akaondoka ili kukutana na jeshi liliporejea Samaria. Akawaambia, “Kwa kuwaBwana, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, aliwatia mikononi mwenu. Lakini mmewachinja kwa hasira ambayo imefika hadi mbinguni.

10 Nanyi sasa mnakusudia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Lakini ninyi je, hamna pia hatia ya dhambi mliyotenda dhidi yaBwanaMungu wenu?

11 Basi nisikilizeni! Mkawarudishe mateka mliowachukua kutoka kwa ndugu zenu, kwa kuwa hasira kali yaBwanaiko juu yenu.”

12 Ndipo baadhi ya viongozi katika Efraimu, yaani, Azaria mwana wa Yehohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, wakakubaliana na huyo nabii, hivyo wakawapinga wale waliokuwa wanawasili kutoka vitani.

13 Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele zaBwana. Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali yaBwanaiko juu ya Israeli.”

14 Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote.

15 Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukuwa wale mateka na kutoka katika zile nyara, wakachukua mavazi wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao mpaka Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.

Waashuru Wakataa Kusaidia Yuda

16 Wakati ule, Mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada.

17 Waedomu walikuwa wamekuja tena na kuwashambulia Yuda na kuchukua mateka.

18 Pia Wafilisti walikuwa wameshambulia miji iliyokuwa chini ya vilima na katika miji ya Negebu ya Yuda. Nao wakawa wametwaa Beth-Shemeshi, Aiyaloni, Gederothi, Soko pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake, Gimzo pia pamoja na vijiji vyake na kuishi humo.

19 Bwanaaliishusha Yuda kwa sababu ya Ahazi mfalme wa Israeli, kwa kuwa alikuwa ameongeza uovu katika Yuda na kumkoseaBwanamno.

20 Hivyo Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru akaja kumtesa badala ya kumsaidia.

21 Ahazi akachukua baadhi ya vitu kutoka katika Hekalu laBwana, jumba la kifalme na kutoka kwa wakuu wake na kumpa mfalme wa Ashuru kama ushuru, lakini hilo halikumsaidia.

22 Katika wakati wake wa mateso Mfalme Ahazi akazidi kukosa uaminifu kwaBwana.

23 Akatoa kafara kwa miungu ya Dameski, ambao walikuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie na mimi.” Lakini haya ndiyo yaliyokuwa maangamizi yake na Israeli wote.

24 Ahazi akakusanya pamoja vyombo vya nyumba ya Mungu na kuvivunja vipande vipande. Akafunga milango ya Hekalu laBwanana kusimamisha madhabahu katika kila njia panda ya barabara za Yerusalemu.

25 Katika kila mji wa Yuda akajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ili kutolea miungu mingine kafara za kuteketezwa na kuchochea hasira yaBwana, Mungu wa baba zake.

26 Matukio mengine ya utawala wake na njia zake nyingine zote, tangu mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

27 Ahazi akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Yerusalemu, lakini hawakumleta kwenye makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/28-21c8411581c3b61dcbfdb963cd16c9fb.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 29

Hezekia Mfalme Wa Yuda

1 Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala. Akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria.

2 Akafanya yaliyo mema machoni paBwanasawasawa na alivyokuwa amefanya Daudi baba yake.

3 Katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa kutawala kwake alifungua milango ya Hekalu laBwana, na kuikarabati.

4 Akawaingiza makuhani na Walawi ndani na kuwakutanisha katika uwanja upande wa mashariki

5 na kusema: “Nisikilizeni mimi, enyi Walawi! Jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba yaBwana, Mungu wa baba zenu. Ondoeni uchafu wote kutoka katika mahali patakatifu.

6 Baba zetu hawakuwa waaminifu, walifanya maovu machoni paBwanaMungu wetu na wakamwacha yeye. Wakageuza nyuso zao mbali na Maskani yaBwanawakamgeuzia visogo vyao.

7 Pia walifunga milango ya ukumbi wa Hekalu na kuzima taa zake. Hawakufukiza uvumba wala kutoa sadaka yo yote ya kuteketezwa katika mahali patakatifu kwa Mungu wa Israeli.

8 Kwa hiyo, hasira yaBwanaikashuka juu ya Yuda na Yerusalemu, naye akawa amewafanya kitu cha kutisha, cha kushangaza na kitu cha kufanyia mzaha kama mnavyoona kwa macho yenu wenyewe.

9 Hii ndiyo sababu baba zetu wameanguka kwa upanga na ndiyo sababu wana wetu na binti zetu, pia wake zetu wamekuwa mateka.

10 Sasa ninadhamiria moyoni mwangu kuweka Agano naBwana, Mungu wa Israeli, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nasi.

11 Wanangu, basi msipuuze jambo hili sasa, kwa kuwaBwanaamewachagua ninyi msimame mbele zake na kumtumikia, mkawe watumishi wake na mkamfukizie uvumba.”

12 Ndipo Walawi wafuatao wakaanza kazi:

Kutoka kwa Wakohathi,

Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria;

kutoka kwa Wamerari,

Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yahaleleli;

kutoka kwa Wagerishoni,

Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;

13 kutoka kwa wana wa Elisafani,

Shimri na Yeieli;

kutoka kwa wana wa Asafu,

Zekaria na Matania;

14 kutoka kwa wana wa Hemani,

Yeieli na Shimei;

kutoka kwa wana wa Yeduthuni,

Shemaya na Uzieli.

15 Walipomaliza kuwakusanya ndugu zao na kujiweka wakfu, wakaingia ndani ili kutakasa Hekalu laBwana, kama vile mfalme alivyokuwa ameagiza, kwa kufuata neno laBwana.

16 Makuhani wakaingia patakatifu pa Hekalu laBwanaili kupatakasa. Wakatoa nje penye ua wa Hekalu la Mungu kila kitu kichafu walichokikuta kwenye Hekalu laBwana. Walawi wakavichukua na kuvipeleka nje katika Bonde la Kidroni.

17 Walianza kazi ya utakaso siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza na kufikia siku ya nane ya mwezi huo wakawa wamefikia kwenye ukumbi waBwana. Kwa siku zingine nane wakalitakasa Hekalu lenyewe laBwanawakakamilisha katika siku ya kumi na sita ya mwezi huo wa kwanza.

18 Kisha wakaingia ndani kwa Mfalme Hezekia kutoa habari na kusema: “Tumelitakasa Hekalu lote laBwana, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa pamoja na vyombo vyake vyote, meza ya kupanga mikate iliyowekwa wakfu, pamoja na vyombo vyake vyote.

19 Tumeviandaa na kuvitakasa vyombo vyote vile ambavyo Mfalme Ahazi, kwa kukosa uaminifu kwake, aliviondoa wakati alipokuwa mfalme. Sasa viko mbele ya madhabahu yaBwana.”

Kuabudu Hekaluni Kwarudishwa

20 Ndipo Mfalme Hezekia akainuka asubuhi na mapema, akakusanya pamoja maafisa wa mji wakakwea hekaluni mwaBwana.

21 Wakaleta mafahali saba, kondoo waume saba, wana-kondoo waume saba na mabeberu saba kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, kwa ajili ya mahali patakatifu na kwa ajili ya Yuda. Mfalme akawaamuru makuhani, wazao wa Aroni, kuvitoa vitu hivyo sadaka katika madhabahu yaBwana.

22 Hivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo waume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo waume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu.

23 Wale mabeberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao mabeberu.

24 Ndipo makuhani wakawachinja hao mabeberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli yote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli yote.

25 Akawaweka Walawi kwenye Hekalu laBwanawakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamuriwa naBwanakupitia manabii wake.

26 Hivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.

27 Hezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbiaBwanapamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli.

28 Kusanyiko lote wakaabudu kwa kusujudu, wakati waimbaji wakiwa wanaimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea mpaka walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.

29 Kutoa sadaka kulipomalizika, mfalme na kila mtu aliyekuwapo pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu.

30 Mfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifuBwanakwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.

31 Kisha Hezekia akasema, “Sasa mmejiweka wakfu kwaBwana. Njoni mlete dhabihu na sadaka za shukrani Hekaluni mwaBwana.” Hivyo kusanyiko likaleta dhabihu na sadaka za shukrani, nao wote waliokuwa na mioyo ya hiari wakaleta sadaka za kuteketezwa.

32 Idadi ya sadaka za kuteketezwa zilizoletwa na kusanyiko zilikuwa mafahali sabini, kondoo waume 100 na wana-kondoo waume 200. Wote hawa walikuwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwaBwana.

33 Wanyama waliowekwa wakfu kwa sadaka ya kuteketezwa walikuwa mafahali 600, pamoja na kondoo na mbuzi 3,000.

34 Lakini makuhani walikuwa wachache sana kuweza kuchuna wale wanyama wote wa sadaka za kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia mpaka kazi ile ikakamilika na mpaka makuhani wengine walipowekwa wakfu, kwa kuwa Walawi walikuwa makini kujiweka wakfu kuliko walivyokuwa makuhani.

35 Kulikuwa na sadaka nyingi za kuteketezwa, pamoja na mafuta ya wanyama ya sadaka za amani na sadaka za kinywaji ambazo ziliambatana na sadaka za kuteketezwa.

Kwa hiyo huduma ya Hekalu laBwanaikarudishwa kwa upya.

36 Hezekia pamoja na watu wote wakafurahi kwa sababu ya lile Mungu alilolifanya kwa ajili ya watu wake, kwa kuwa lilitendeka papo hapo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/29-17faaedf66f4b0ccef965f841978faa2.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 30

Hezekia Aadhimisha Pasaka

1 Hezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwaBwanahuko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwaBwana, Mungu wa Israeli.

2 Mfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili.

3 Kwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa idadi ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida.

4 Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote.

5 Wakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka yaBwana, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.

6 Kwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema:

“Watu wa Israeli, mrudieniBwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.

7 Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwaBwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona.

8 Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwaBwana. Njoni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. MtumikieniBwanaMungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi.

9 Kama mkimrudiaBwanandipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwaBwanaMungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”

10 Matarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika mpaka Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki.

11 Lakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu.

12 Pia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno laBwana.

13 Basi umati mkubwa wa watu ukakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili.

14 Wakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakaziondoa pia zile madhabahu za kufukizia uvumba kwa miungu na kuzitupa katika Bonde la Kidroni.

15 Kisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu laBwana.

16 Kisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi.

17 Kwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa safi, kwa kufuata taratibu za ibada ili kuwatakasa kwaBwana.

18 Ingawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Bwana, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja

19 ambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu,Bwana, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.”

20 NayeBwanaakamsikia Hezekia akawaponya watu.

21 Waisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba wakiwa na ala za uimbaji za kumsifuBwana.

22 Hezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionyesha ustadi katika kumtumikiaBwana. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa dhabihu za amani na kumshukuruBwana, Mungu wa baba zao.

23 Kisha kusanyiko lote likakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi, kwa hiyo kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha.

24 Hezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali 1,000, kondoo na mbuzi 7,000 kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali 1,000 pamoja na kondoo na mbuzi 10,000. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu.

25 Kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na lile kusanyiko lote lililotoka Israeli, pamoja na wale wageni waliotoka Israeli na wale walioishi katika Yuda wakafurahi.

26 Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Solomoni mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwapo jambo kama hili katika Yerusalemu.

27 Ndipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/30-4512b6283fea904d91e6d44d985efc40.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 31

Sehemu Za Ibada Za Kipagani Zaondolewa

1 Baada ya mambo haya yote kumalizika, Waisraeli ambao walikuwako huko wakaenda kwenye miji ya Yuda, wakayavunja yale mawe ya kuabudia na kuzikatakata zile nguzo za Ashera. Wakabomoa mahali pa juu pa kuabudia miungu pamoja na madhabahu zake kila mahali katika Yuda na Benyamini na katika Efraimu na Manase. Baada ya kuviharibu hivi vyote, Waisraeli wakarudi katika miji yao wenyewe na kwenye milki zao.

2 Hezekia akawapanga makuhani na Walawi katika migawanyo, kila mgawanyo kulingana na wajibu wao, kama ni makuhani au Walawi, ili kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, kuhudumu, kushukuru na kuimba sifa katika malango ya makao yaBwana.

3 Mfalme akatoa matoleo kutoka katika mali zake mwenyewe kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni na sadaka za kuteketezwa kwa siku za Sabato, kwa Sikukuu za Mwezi Mwandamo na kwa ajili ya sikukuu zilizoamuriwa kama ilivyoandikwa katika Sheria yaBwana.

4 Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria yaBwana.

5 Mara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu.

6 Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ng’ombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili yaBwanaMungu wao na kuvikusanya katika malundo.

7 Wakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba.

8 Wakati Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifuBwanana kuwabariki watu wake Israeli.

9 Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo,

10 naye Azaria aliyekuwa Kuhani Mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu laBwanatumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababuBwanaamewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”

Kutambuliwa Kwa Makuhani Na Walawi

11 Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu laBwananalo hili likafanyika.

12 Kisha kwa uaminifu wakaleta sadaka zao, mafungu yao ya kumi na vitu vilivyowekwa wakfu. Konania Mlawi, ndiye aliyekuwa msimamizi wa vitu hivi na Shimei ndugu yake ndiye aliyekuwa msaidizi wake.

13 Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yerimothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya walikuwa waangalizi chini ya Konania na Shimei ndugu yake, waliokuwa wamewekwa na Mfalme Hezekia na Azaria, afisa msimamizi wa Hekalu la Mungu.

14 Kore mwana wa Imna Mlawi, bawabu wa Lango la Mashariki, alikuwa msimamizi wa sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mungu, akiyagawanya hayo matoleo yaliyotolewa kwaBwanana pia zile sadaka zilizowekwa wakfu.

15 Edeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania walimsaidia kwa uaminifu katika miji ya makuhani, wakiwagawia makuhani wenzao kufuatana na migawanyo yao, wazee kwa vijana sawasawa.

16 Zaidi ya hao wakawagawia wanaume wenye umri wa miaka mitatu au zaidi ambao majina yao yalikuwa kwenye orodha ya vizazi, wale wote ambao wangeingia katika Hekalu laBwanaili kufanya kazi zao mbalimbali za kila siku kulingana na wajibu katika mgawanyo wao.

17 Kuandikishwa kwa makuhani kulikuwa kwa kufuata chimbuko la nyumba za baba zao na Walawi kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi ilikuwa kufuatana na huduma zao, kwa migawanyo yao.

18 Makuhani waliandikishwa pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, watoto wao wa kiume na wa kike, jamii yote iliandikishwa kwa kufuata orodha ya vizazi vyao. Kwa kuwa walikuwa waaminifu katika kujitakasa.

19 Kuhusu makuhani, wazao wa Aroni walioishi kwenye mashamba yaliyozunguka miji yao au katika miji mingine yo yote, watu walitajwa majina ili kumgawia kila mwanaume miongoni mwao na kwa wote ambao walikuwa katika orodha ya vizazi vya Walawi.

20 Hivi ndivyo Hezekia alivyofanya katika Yuda yote, akifanya lile lililo jema, sawa na la uaminifu mbele zaBwanaMungu wake.

21 Naye katika kila kitu alichofanya katika huduma kwenye Hekalu la Mungu na katika utii kwa sheria na amri, alimtafuta Mungu wake na kufanya kazi kwa moyo wake wote. Naye hivyo akafanikiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/31-6f1abf5d96df8bc19eb33de6ea17e378.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 32

Senakeribu Aitishia Yerusalemu

1 Baada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu, mfalme wa Ashuru akaja na kuivamia Yuda. Akaizunguka kwa jeshi miji yenye ngome, akifikiri kuiteka.

2 Hezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu,

3 akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia.

4 Umati mkubwa wa watu ukakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?”

5 Hezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwepo na kuimarisha milokatika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao.

6 Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya:

7 “Iweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye.

8 Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yukoBwanaMungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.

9 Hatimaye Senakeribu mfalme wa Ashuru na majeshi yake yote walipokuwa wameuzunguka Lakishi, akatuma maafisa wake kwenda Yerusalemu wakiwa na ujumbe huu kwa Hezekia mfalme wa Yuda na kwa watu wote wa Yuda waliokuwako humo kusema:

10 “Hili ndilo Senakeribu Mfalme wa Ashuru asemalo: Je, mmetumainia nini, kwamba mnaendelea kukaa hali mmezungukwa na jeshi katika Yerusalemu?

11 Hezekia asemapo, ‘BwanaMungu wetu atatuokoa kutokana na mkono wa mfalme wa Ashuru,’ anawapotosha ninyi, akiwaacha mfe kwa njaa na kiu.

12 Je, si Hezekia mwenyewe aliyeondoa mahali pa juu pakuabudia miungu pamoja na madhabahu zake, akiwaambia Yuda wa Yerusalemu, ‘Hamna budi kuabudu mbele ya madhabahu moja na kuteketeza dhabihu juu yake’?

13 “Je, hamjui kile mimi na baba zangu tulichokifanya kwa mataifa yote ya nchi nyingine? Je, miungu ya mataifa hayo iliweza kuokoa nchi zao kutoka mkononi mwangu?

14 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya mataifa haya ambayo baba zangu waliyaangamiza, iliyoweza kuwaokoa watu wake mkononi mwangu? Ni vipi basi Mungu wenu atakavyoweza kuwaokoa kutoka katika mkono wangu?

15 Sasa basi, msikubali Hezekia awadanganye nakuwapotosha namna hii. Msimwamini kwa kuwa hakuna mungu wa taifa lo lote wala wa ufalme wo wote aliyeweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu au mkononi mwa baba zangu. Sembuse huyo Mungu wenu atawaokoaje kutoka mkononi mwangu!”

16 Maafisa wa Senakeribu wakaendelea kunena dhidi yaBwanaaliye Mungu na dhidi ya mtumishi wake Hezekia.

17 Mfalme pia aliandika barua akimtukanaBwana, Mungu wa Israeli na kusema haya dhidi yake: “Kama vile miungu ya mataifa ya nchi nyingine ilivyoshindwa kuwaokoa watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu.”

18 Kisha wakawaita kwa Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa juu ya ukuta ili kuwatisha na kuwatia hofu ili waweze kuuteka mji.

19 Wakanena juu ya Mungu wa Yerusalemu kama vile walivyonena juu ya miungu ya mataifa mengine ya dunia ambayo ni kazi ya mikono ya wanadamu.

20 Mfalme Hezekia na nabii Isaya mwana wa Amozi wakalilia mbingu katika maombi kuhusu jambo hili.

21 NayeBwanaakamtuma malaika ambaye aliangamiza wanaume wote wenye kupigana na viongozi na maafisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Kwa hiyo, Mfalme wa Ashuru akarudi kwenye nchi yake mwenyewe kwa aibu. Naye alipokwenda katika hekalu la mungu wake, baadhi ya watoto wake walimkata na kumwua kwa upanga.

22 HivyoBwanaakamwokoa Hezekia na watu wa Yerusalemu kutoka mkononi mwa Senakeribu mfalme wa Ashuru na kutoka mikononi mwa wengine wote.Bwanaakawastarehesha kila upande.

23 Watu wengi wakaleta sadaka Yerusalemu kwa ajili yaBwanana zawadi za thamani kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda. Tangu hapo na kuendelea, Hezekia aliheshimiwa sana na mataifa yote.

Kiburi Cha Hezekia, Mafanikio Na Kifo

24 Katika siku zile, Hezekia akaugua naye akawa katika hatari ya kufa. AkamwombaBwanaambaye alimjibu na kumpa ishara.

25 Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonyesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu yaBwanaikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu.

26 Ndipo Hezekia akatubu kwa ajili ya kiburi cha moyo wake, kama walivyofanya watu wa Yerusalemu, kwa hiyo ghadhabu yaBwanahaikuja juu yao katika siku za Hezekia.

27 Hezekia alikuwa na utajiri mwingi sana na heshima, naye akajifanyia hazina kwa ajili ya fedha yake na dhahabu na kwa ajili ya vito vyake vya thamani, vikolezi, ngao na aina zote za vyombo vya thamani.

28 Akajenga pia maghala ya kuhifadhi mavuno ya nafaka, divai mpya na mafuta, akatengeneza mabanda kwa ajili ya aina mbalimbali za mifugo na mazizi kwa ajili ya kondoo na mbuzi.

29 Akajenga vijiji na kujipatia idadi kubwa ya kondoo na mbuzi, pamoja na ng’ombe kwa kuwa Mungu alikuwa amempa utajiri mwingi sana.

30 Ilikuwa ni Hezekia aliyeziba njia za kutolea maji za chemchemi za juu za Gihoni na kuyaelekeza maji kutiririkia upande wa magharibi wa Mji wa Daudi. Akafanikiwa katika kila kitu alichofanya.

31 Lakini wakati wajumbe walipotumwa na watawala wa Babeli kumwuliza juu ya ishara ambayo ilitokea katika nchi, Mungu alimwacha ili kumjaribu na kujua kila kitu kilichokuwa moyoni mwake.

32 Matukio mengine ya utawala wa Hezekia na matendo yake ya kujitoa kwa moyo yameandikwa katika maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi kwenye kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

33 Hezekia akalala na baba zake na akazikwa kwenye kilima mahali yalipo makaburi ya wazao wa Daudi. Yuda wote na watu wa Yerusalemu wakamheshimu alipokufa. Naye Manase mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/32-fbb162eb4f41bdc35c927fa04448a2b4.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 33

Manase Mfalme Wa Yuda

1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano.

2 Akafanya yaliyo maovu machoni paBwana, akafanya machukizo kama walivyofanya mataifaBwanaaliyoyafukuza mbele ya Waisraeli.

3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake, alikuwa amepabomoa, pia akasimamisha madhabahu za Mabaali na nguzo za Maashera. Akalisujudia jeshi lote la vitu vya angani na kuliabudu.

4 Akajenga madhabahu za Baali katika Hekalu laBwanaambamoBwanaalikuwa amesema, “Jina langu litakaa Yerusalemu milele.”

5 Katika nyua zote za Hekalu laBwanaakajengea madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la vitu vya angani.

6 Akawatoa wanawe kuwa kafara kwa kuwapitisha katika moto katika Bonde la Hinomu, akafanya ulozi, uaguzi na uchawi, akataka ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni paBwana, akaichochea hasira yake.

7 Akachukua ile sanamu aliyoichonga akaiweka katika Hekalu laBwanaambalo Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Solomoni, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu niliouchagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka Jina langu milele.

8 Sitaifanya miguu ya Waisraeli iondoke tena katika nchi niliyowapa baba zenu, kama watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru kuhusu sheria zote, maagizo na amri zilizotolewa kwa mkono wa Mose.”

9 Lakini Manase akawaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu katika upotovu, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kupita mataifa ambayoBwanaaliwaangamiza mbele ya Waisraeli.

10 Bwanaakasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali.

11 HivyoBwanaakaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.

12 Katika dhiki yake akamsihiBwanaMungu wake na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.

13 Naye alipomwomba,Bwanaakaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza kilio chake, kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwambaBwanandiye Mungu.

14 Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli, pia akaufanya kuwa mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.

15 Akaondolea mbali miungu ya kigeni na kuondoa sanamu kutoka katika Hekalu laBwanapamoja na madhabahu zote alizozijenga katika kile kilima kilichojengwa Hekalu na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.

16 Kisha akarudisha madhabahu yaBwanana kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikieBwana, Mungu wa Israeli.

17 Lakini hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia miungu, lakini wakimtoleaBwanaMungu wao peke yake.

18 Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina laBwana, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli.

19 Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa kwake uaminifu pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia miungu, kule kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake, yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji.

20 Manase akalala pamoja na baba zake akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Amoni Mfalme Wa Yuda

21 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili, alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili.

22 Akafanya maovu machoni paBwanakama alivyokuwa amefanya Manase baba yake. Amoni akaabudu na kutoa dhabihu kwa sanamu zote alizokuwa ametengeneza Manase.

23 Lakini tofauti na Manase baba yake, hakujinyenyekeza mbele zaBwana, badala yake Amoni aliongeza makosa zaidi na zaidi.

24 Maafisa wa Amoni wakafanya shauri pamoja wakamwua katika jumba lake la kifalme.

25 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme badala yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/33-9f18842abea748d3ac812d496a7bbd8c.mp3?version_id=1627—

2 Mambo ya nyakati 34

Yosia Afanya Matengenezo

1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka thelathini na mmoja.

2 Akafanya yaliyo mema machoni paBwanana kuenenda katika njia za Daudi baba yake, pasipo kugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.

3 Katika mwaka wa nane wa utawala wake, alipokuwa angali bado mdogo, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi baba yake. Katika mwaka wake wa kumi na mbili alianza kusafisha mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Yuda na Yerusalemu, akiondoa nguzo za Ashera, sanamu za kuchonga na vinyago vya kusubu.

4 Mbele ya macho yake, wakazibomoa madhabahu za Mabaali, wakazivunja madhabahu za kufukizia uvumba zilizokuwa zimesimama juu yake, wakazivunja nguzo za Ashera, sanamu na vinyago. Hivi alivivunja vipande vipande na kuvisambaza juu ya makaburi ya waliokuwa wamevitolea kafara.

5 Akachoma mifupa ya makuhani wao juu ya madhabahu zao na kwa njia hiyo akaitakasa Yuda na Yerusalemu.

6 Katika miji ya Manase, Efraimu na Simeoni, hadi Naftali na kwenye magofu yanayoizunguka,

7 akavunja madhabahu na nguzo za Ashera na kuzipondaponda hizo sanamu hadi zikawa unga na kukata vipande vipande madhabahu zote za kufukizia uvumba katika Israeli yote. Kisha akarudi Yerusalemu.

8 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yosia, ili kutakasa nchi na Hekalu, akawatuma Shafani, mwana wa Azalia na Maaseya mtawala wa mji, pamoja na Yoa mwana wa Yoahazi, mwandishi ili kukarabati Hekalu laBwanaMungu wake.

9 Wakamwendea Hilkia kuhani mkuu na kumpa fedha ambazo zilikuwa zimeletwa ndani ya Hekalu laBwanaambazo Walawi waliokuwa mabawabu walikuwa wamezikusanya kutoka kwa watu wa Manase, Efraimu na mabaki wote wa Israeli kutoka kwa watu wote wa Yuda na Benyamini na wakazi wa Yerusalemu.

10 Kisha wakazikabidhi hizo fedha kwa watu waliowekwa ili kusimamia kazi ya Hekalu laBwana. Hawa watu waliwalipa wafanyakazi waliokarabati na kutengeneza Hekalu lipate kurudi katika hali yake.

11 Wakawapa pia mafundi seremala na waashi fedha ili kununua mawe yaliyochongwa, mbao kwa ajili ya kufungia na boriti kwa ajili ya majengo ambayo wafalme wa Yuda walikuwa wameyaacha yakawa magofu.

12 Watu wakafanya kazi kwa uaminifu. Waliokuwa wamewekwa juu yao ili kuwaelekeza ni Yahathi na Obadia, Walawi wa uzao wa Merari, Zekaria na Meshulamu, waliotoka kwenye uzao wa Kohathi. Walawi wote waliokuwa na ufundi wa kupiga ala za uimbaji,

13 wakawa wasimamizi wa vibarua na kuwaongoza wale waliofanya kila aina ya kazi. Baadhi ya Walawi walikuwa, waandishi, maafisa na mabawabu.

Kitabu Cha Sheria Chapatikana

14 Wakati walipokuwa wakizitoa nje zile fedha zilizokuwa zimetolewa kwenye Hekalu laBwanakuhani Hilkia akakipata kile Kitabu cha Sheria yaBwanakilichokua kimetolewa kwa mkono wa Mose.

15 Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, “nimekiona Kitabu cha Sheria ndani ya Hekalu laBwana.” Akampatia Shafani kile Kitabu.

16 Ndipo Shafani akakipeleka kile Kitabu kwa mfalme na kumwambia, “Maafisa wako wanafanya kila kitu kama walivyokabidhiwa kufanya.

17 Wamelipa fedha zilizokuwa katika Hekalu laBwanana wamewakabidhi wasimamizi na wafanyakazi.”

18 Kisha Shafani mwandishi akamwarifu mfalme kuwa, “Kuhani Hilkia amenipatia Kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.

19 Mfalme aliposikia yale maneno ya Sheria, akayararua mavazi yake.

20 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme,

21 “Nendeni mkamwulizeBwanakwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki walioko Israeli na Yuda kuhusu haya yaliyoandikwa katika kitabu hiki ambacho kimeonekana hekaluni. Hasira yaBwanani kubwa mno ambayo imemwagwa juu yetu kwa sababu baba zetu hawakulishika neno laBwanawala hawakutenda sawasawa na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.”

22 Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa kabati la mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili.

23 Akawaambia, “Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli asemalo, mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu,

24 ‘Hili ndiloBwanaasemalo: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, laana zote zilizoandikwa ndani ya hicho kitabu ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda.

25 Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine ili waichochee hasira yangu kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa juu ya mahali hapa, wala haitatulizwa.

26 Mwambieni mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwulizaBwana, Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu maneno uliyoyasikia:

27 Kwa sababu moyo wako ulikuwa mwepesi kusikia, nawe ukajinyenyekeza mbele za Mungu wakati uliposikia kile alichokisema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu ukararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asemaBwana.

28 Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ”

Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake.

29 Ndipo mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.

30 Akapanda kwenda hekaluni mwaBwanapamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na Walawi, yaani watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi mkubwa kabisa. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu laBwana.

31 Mfalme akasimama karibu na nguzo yake na kufanya upya Agano mbele zaBwanaili kumfuataBwanana kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na ili kuyatii maneno ya Agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

32 Ndipo akamtaka kila mmoja katika Yerusalemu na Benyamini kuweka ahadi zao wenyewe kwa hilo Agano, watu wa Yerusalemu wakafanya hivyo kwa kufuata Agano laBwana, Mungu wa baba zao.

33 Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka katika nchi yote iliyokuwa mali ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuweko katika Israeli wamtumikieBwanaMungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuataBwana, Mungu wa baba zao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/34-c0109b8dbe62dca2feb91f1ab080952b.mp3?version_id=1627—