1 Wafalme 5

Maandalio Ya Ujenzi Wa Hekalu

1 Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kuwa Solomoni ametiwa mafuta awe mfalme mahali pa Daudi baba yake, akatuma wajumbe kwa Solomoni, kwa sababu Hiramu siku zote alikuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na Daudi.

2 Solomoni akapeleka ujumbe huu kwa Hiramu:

3 “Unajua kwamba kwa sababu ya vita vilivyopiganwa dhidi ya baba yangu Daudi kutoka pande zote, hakuweza kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina laBwanaMungu wake, hadiBwanaalipowaweka adui zake chini ya miguu yake.

4 Lakini sasaBwanaMungu wangu amenipa utulivu kila upande hakuna adui wala maafa.

5 Kwa hiyo, ninakusudia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina laBwana, Mungu wangu, kamaBwanaalivyomwambia baba yangu Daudi, wakati aliposema, ‘Mwanao nitakayemweka kwenye kiti cha ufalme mahali pako, ndiye atajenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’

6 “Hivyo toa amri ili mierezi ya Lebanoni ikatwe kwa ajili yangu. Watu wangu watafanya kazi na watu wako, nami nitawalipa watu wako kwa ujira wo wote utakaoupanga. Unajua kwamba hatuna mtu ye yote mwenye ustadi katika kukata miti kama Wasidoni.”

7 Hiramu aliposikia ujumbe wa Solomoni, akafurahishwa sana akasema, “AhimidiweBwanaleo, kwa kuwa amempa Daudi mwana mwenye hekima kutawala juu ya taifa hili kubwa.”

8 Hiramu akatuma neno kwa Solomoni:

“Nimepokea ujumbe ulionipelekea na nitafanya yote unayohitaji katika kukupatia magogo ya mierezi na misunobari.

9 Watu wangu watayakokota kutoka Lebanoni hadi kwenye bahari, nami nitayafunga mafungu mafungu yaelee juu ya maji hadi utakapoelekeza. Huko nitayatenganisha, nawe utaweza kuyachukua. Wewe utakidhi haja yangu kwa kunipatia chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwangu.”

10 Kwa njia hii Hiramu akampa Solomoni miti yote ya mierezi na magogo ya misunobari kama alivyohitaji,

11 naye Solomoni akampa Hiramu kori 20,000za ngano kama chakula kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, pamoja na mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa bathi 20,000. Solomoni aliendelea kumfanyia Hiramu hivyo mwaka baada ya mwaka.

12 Bwanaakampa Solomoni hekima, kama alivyomwahidi. Palikuwepo na uhusiano wa amani kati ya Hiramu na Solomoni, na wote wawili wakafanya mkataba.

13 Mfalme Solomoni akakusanya wafanya kazi 30,000 kutoka Israeli yote.

14 Akawapeleka Lebanoni kwa zamu za watu 10,000 kwa mwezi, hivyo walikaa Lebanoni kwa mwezi mmoja na miezi miwili nyumbani. Adoniramu ndiye aliyekuwa kiongozi wa shokoa.

15 Solomoni alikuwa na wachukuzi wa mizigo 70,000 na wachonga mawe 80,000 huko vilimani,

16 pamoja na wasimamizi 3,300 ambao walisimamia kazi hiyo na kuwaongoza wafanyakazi.

17 Kwa amri ya mfalme walitoa kwenye machimbo ya mawe, mawe makubwa, yaliyo bora kwa kujengea msingi wa nyumba yaliyochongwa kwa ajili ya Hekalu.

18 Mafundi wa Solomoni, wa Hiramu na watu wa Gebaliwalikata na kuandaa mbao na mawe kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/5-b5b0b6feca32220192b5c7736d52f4c4.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 6

Solomoni Ajenga Hekalu

1 Katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka katika nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwa Solomoni katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, ambao ndio mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu laBwana.

2 Hekalu hilo Mfalme Solomoni alilojenga kwa ajili yaBwanalilikuwa na urefu wa dhiraa sitini, upana wa dhiraa ishirinina kimo cha dhiraa thelathinikwenda juu.

3 Baraza ya mbele ya Hekalu ilienea dhiraa ishirini kulingana na upana wa Hekalu na kujitokeza dhiraa kumi mbele ya Hekalu.

4 Akatengeneza madirisha membamba yenye vidirisha vidogo vya juu katika Hekalu.

5 Akafanyiza vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote vikishikamana na kuta za Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu.

6 Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano, ya kati ilikuwa dhiraa sita na ya tatu ilikuwa dhiraa saba. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.

7 Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine cho chote cha chuma kilichosikika sauti yake katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.

8 Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu, ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutokea hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu.

9 Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha, akilipaua kwa boriti na mbao za mierezi.

10 Mfalme Solomoni akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mierezi.

11 Neno laBwanalikamjia Solomoni kusema:

12 “Kwa habari ya Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, kwa kupitia wewe nitatimiza ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako.

13 Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”

14 Basi Solomoni akajenga Hekalu na kulikamilisha.

15 Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mierezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari.

16 Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mierezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu ya ndani ya patakatifu, yaani Patakatifu pa Patakatifu.

17 Ukumbi mkubwa uliokuwa mbele ya chumba hiki ndio ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini.

18 Ndani ya Hekalu kulikuwa na mierezi, ilionakishiwa mfano wa maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi, hakuna jiwe ambalo lilionekana.

19 Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa ndani, kwa ajili kuweka Sanduku la Agano laBwana.

20 Mahali Patakatifu pa Patakatifu palikuwa na upana, urefu na kimo cha dhiraa ishirini ndani kwa ndani. Akakifunika ndani kwa dhahabu safi, pia akaifunika madhabahu ya mierezi vivyo hivyo.

21 Solomoni akaifunika sehemu ya ndani ya Hekalu kwa dhahabu safi, naye akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande huu hadi upande mwingine, mbele ya Patakatifu pa Patakatifu ambako palifunikwa kwa dhahabu.

22 Basi akafunika sehemu yote ya ndani kwa dhahabu. Pia akafunika madhabahu ile iliyokuwa ndani ya Patakatifu pa Patakatifu kwa dhahabu.

23 Katika mahali Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumikwenda juu.

24 Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi.

25 Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, hivyo makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo.

26 Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi.

27 Aliwaweka makerubi hao ndani ya Patakatifu pa Patakatifu pa Hekalu, mabawa yake yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba.

28 Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.

29 Juu ya kuta zote zilizozunguka Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi zilizokatwa za makerubi, miti ya mitende na maua yaliyochanua.

30 Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu.

31 Kwa ingilio la mahali Patakatifu pa Patakatifu akapatengeneza milango ya mbao za mzeituni, zikiwa na miimo na vizingiti vyenye umbo la pembe tano.

32 Juu ya milango miwili ya mbao za mzeituni alinakshi makerubi, miti ya mitende pamoja na maua yaliyochanua na kufunika makerubi na miti ya mitende kwa dhahabu iliyofuliwa.

33 Kwa njia iyo hiyo akatengeneza miimo yenye pande nne ya miti ya mizeituni, kwa ajili ya ingilio la ukumbi mkubwa.

34 Kulikuwa na milango miwili iliyoweza kukunjuka iliyotengenezwa kwa mbao za msunobari na kila mmoja ulikuwa na bawaba ambazo zingeuwezesha kujikunja kila kipande juu ya kingine.

35 Akanakshi makerubi, miti ya mitende na maua yaliyochanua juu yake na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro.

36 Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa na safu moja ya boriti za mierezi zilizorembwa.

37 Msingi wa Hekalu laBwanauliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa tano.

38 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Solomoni. Alilijenga kwa miaka saba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/6-1108a929c25bfbc2db4aefeb4e511871.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 7

Solomoni Ajenga Jumba Lake La Kifalme

1 Ilimchukua Solomoni miaka kumi na mitatu kukamilisha ujenzi wa Jumba lake la kifalme.

2 Alijenga Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni, urefu wake ulikuwa dhiraa 100, upana wake dhiraa hamsini na kimo chake dhiraa thelathini, likiwa na safu nne za nguzo za mierezi zikishikilia boriti za mierezi zilizorembwa.

3 Ilipauliwa kwa mierezi juu ya boriti zile zilizolala juu ya nguzo arobaini na tano, kumi na tano kwa kila safu.

4 Madirisha yake yaliwekwa juu kwa safu tatu, yakielekeana.

5 Milango yote ilikuwa na miimo ya mstatili, ilikuwa upande wa mbele katika safu tatu, ikielekeana.

6 Akajenga ukumbi wa nguzo, ambao urefu wake ulikuwa dhiraa hamsinina upana wake dhiraa thelathini. Mbele ya jengo hilo kulikuwepo baraza. Mbele ya baraza kulikuwapo na nguzo na paa lililoning’inia.

7 Akajenga ukumbi wa kiti cha enzi, Ukumbi wa Hukumu, mahali ambapo angelitolea hukumu, akaufunika kwa mierezi kutoka sakafuni hadi darini.

8 Kwenye jumba la kifalme ambamo angeliishi, aliiweka nyuma zaidi, ikiwa na mjengo wa aina moja na hiyo nyingine. Pia Solomoni akajenga jumba la kifalme linalofanana na huo ukumbi mkubwa kwa ajili ya binti Farao, aliyekuwa amemwoa.

9 Ujenzi huu wote, kuanzia nje mpaka kwenye ua mkuu na kuanzia kwenye msingi hadi upenuni, ulifanywa kwa mawe ya ubora wa hali ya juu yaliyokuwa yamechongwa kwa vipimo na kusawazishwa kwa msumeno nyuso zake za ndani na za nje.

10 Misingi iliwekwa kwa mawe makubwa yaliyo bora, yenye urefu wa dhiraa kumina mengine yenye urefu wa dhiraa nane.

11 Sehemu za juu kulikuwepo na mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo na boriti za mierezi.

12 Ule ua mkuu ulizungukwa na ukuta wa safu tatu za mawe yaliyochongwa na safu moja ya boriti za mierezi zilizorembwa, kama ulivyokuwa ua wa ndani wa Hekalu laBwanana baraza yake.

Samani Za Hekalu

13 Mfalme Solomoni akatuma watu Tiro kumleta Hiramu,

14 ambaye mama yake alikuwa mjane kutoka kabila la Naftali na baba yake alikuwa mtu wa Tiro tena fundi wa shaba. Hiramu alikuwa na ustadi wa hali ya juu na mzoefu katika aina zote za kazi ya shaba. Alikuja kwa Mfalme Solomoni na kufanya kazi zake zote alizopangiwa.

15 Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kila nguzo ikiwa na mzingo wa dhiraa kumi na mbilikwa mstari.

16 Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tanokwenda juu.

17 Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji.

18 Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo.

19 Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne.

20 Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga 200 katika safu kuzunguka pande zote.

21 Hiramu akasimamisha nguzo kwenye baraza ya Hekalu. Nguzo ya upande wa kusini akaiita Yakinina ile ya upande wa kaskazini Boazi.

22 Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika.

23 Hiramu akasubu Bahari ya chuma, yenye umbo la mviringo, vipimo vyake dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kimo cha dhiraa tano. Mzunguko wake ulikuwa dhiraa thelathini.

24 Chini ya ukingo, ilizungukwa na maboga, kumi kwenye kila dhiraa moja. Maboga yalikuwa yamesubiwa katika safu mbili ili kuwa kitu kimoja na hiyo bahari.

25 Bahari iliwekwa juu ya mafahali kumi na wawili, watatu wakielekea kaskazini, watatu wakielekea magharibi, watatu wakielekea kusini na watatu wakielekea mashariki. Bahari iliwekwa juu yao na sehemu zao za nyuma zilielekeana.

26 Ilikuwa na unene wa nyanda nnena ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi iliyochanua. Iliweza kuchukua bathi 2,000.

27 Pia akatengeneza vitako kumi vya shaba vinavyoweza kuhamishika, kila kimoja kilikuwa na urefu wa dhiraa nne, upana dhiraa nne na kimo chake dhiraa tatu.

28 Hivi ndivyo vile vitako vilivyotengenezwa: Vilikuwa na mbao za pembeni zilizoshikamanishwa na mihimili.

29 Juu ya mbao kati ya hiyo mihimili kulikuwa na simba, mafahali na makerubi, pia kwenye mihimili yake. Juu na chini ya simba na mafahali kulikuwa kumesokotewa taji za kufuliwa.

30 Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungusha hayo magurudumu na kila kimoja kilikuwa na sinia kwenye vishikizo vinne vya taji iliyosubiwa kila upande.

31 Ndani ya kitako kulikuwa na nafasi ya wazi iliyokuwa na umbile la mviringo lenye kina cha dhiraa moja. Nafasi hii ya wazi ilikuwa ya mviringo, pamoja na kitako chake ilikuwa dhiraa moja na nusu. Kuzunguka huo mdomo wake kulitiwa nakshi. Papi za vitako zilikuwa mraba na si za mviringo.

32 Magurudumu manne yalikuwa chini ya papi, na vyuma vya katikati vya kuzungushia magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa kwenye kitako. Kipenyo cha kila gurudumu kilikuwa dhiraa moja na nusu.

33 Magurudumu yalitengenezwa kama ya magari ya vita ya kukokotwa, vyuma vya katikati vya magurudumu, duara zake, matindi yake na vikombe vyake vyote vilikuwa vya kusubu.

34 Kila kitako kilikuwa na mikono minne, moja kwenye kila pembe, ukitokeza kutoka kwenye kitako.

35 Juu ya kitako kulikuwepo na utepe wa mviringo wenye kina cha nusu dhiraa. Vishikio na papi vilishikamana upande wa juu wa kitako.

36 Alitia nakshi za makerubi, simba na miti ya mitende juu ya uso wa vishikio na juu ya papi, katika kila nafasi iliyopatikana, pamoja na mataji yaliyosokotwa kuzunguka pande zote.

37 Hivi ndivyo Hiramu alivyotengeneza vile vitako kumi. Vyote vilikuwa vya kusubu kwenye kalibu za kufanana kwa vipimo na kwa umbo.

38 Kisha akatengeneza masinia kumi ya shaba, kila moja likiwa na ujazo wa bathi arobainiyakiwa na kipenyo cha dhiraa nne, kila sinia moja kwa kila kimoja ya vile vitako kumi.

39 Aliweka vitako vitano upande wa kusini wa Hekalu na vingine vitano upande wa kaskazini. Akaweka ile bahari upande wa kusini, katika pembe ya kusini ya Hekalu.

40 Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.

Hivyo hatimaye Hiramu akakamilisha kazi zote za Hekalu laBwanasawasawa na Mfalme Solomoni alivyomwagiza, yaani:

41 nguzo mbili;

mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;

nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo;

42 makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (zikiwa na safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, zikipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo);

43 vitako kumi pamoja na masinia yake kumi;

44 ile Bahari ya chuma na yale mafahali kumi na mawili chini yake;

45 masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.

Vyombo hivi vyote ambavyo Hiramu alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu laBwanavilikuwa vya shaba iliyong’arishwa.

46 Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani.

47 Solomoni akaviacha vitu hivi vyote bila kupima uzani wake, kwa sababu vilikuwa vingi sana, uzito wa shaba haukujulikana.

48 Pia Solomoni akatengeneza samani zote kwa ajili ya Hekalu laBwana:

madhabahu ya dhahabu;

meza ya dhahabu ambayo juu yake ndipo palipokuwa mikate Mitakatifu;

49 vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya Patakatifu pa Patakatifu);

kazi ya maua ya dhahabu na taa na makoleo;

50 masinia ya dhahabu safi, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo;

na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu.

51 Mfalme Solomoni alipomaliza kazi ya Hekalu laBwana, akavileta vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina ya Hekalu laBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/7-5dcf93f26953a88cd4fa959233cd95cd.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 8

Sanduku La Agano Laletwa Hekaluni

1 Kisha Mfalme Solomoni akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano laBwanakutoka Sayuni, Mji wa Daudi.

2 Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Solomoni wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.

3 Viongozi wote wa Israeli walipokwisha kufika, makuhani wakajitwika hilo Sanduku la Agano,

4 wakalipandisha Sanduku laBwana, Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba,

5 naye Mfalme Solomoni pamoja na kusanyiko lote la Israeli waliokusanyika kumzunguka walikuwa mbele ya hilo Sanduku, wakatoa dhabihu nyingi za kondoo na ng’ombe ambao idadi yao haikuwezekana kuandikwa au kuhesabiwa.

6 Ndipo makuhani wakalileta Sanduku la Agano laBwanamahali pake ndani ya Hekalu, katika Patakatifu pa Patakatifu na kuliweka chini ya mabawa ya yale makerubi.

7 Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea.

8 Mipiko hiyo ilikuwa mirefu kiasi kwamba ncha zake ziliweza kuonekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya mahali Patakatifu pa Patakatifu, lakini si kutoka nje ya Mahali Patakatifu, nayo iko huko hadi leo.

9 Hapakuwa na cho chote ndani ya Sanduku la Agano isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo ziliwekwa na Mose huko Horebu, mahali ambapoBwanaalifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.

10 Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likalijaza Hekalu laBwana.

11 Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu waBwanaulilijaza Hekalu lake.

12 Ndipo Solomoni akasema, “Bwanaalisema kwamba ataishi katika giza nene;

13 naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.”

Hotuba Ya Solomoni

14 Kusanyiko lote la Israeli lilipokuwa limesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki.

15 Kisha akasema:

“AhimidiweBwana, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi baba yangu Daudi kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema,

16 ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lo lote la Israeli Hekalu lijengwe kwa ajili ya Jina langu ili lipate kuwako huko, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’

17 “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina laBwana, Mungu wa Israeli.

18 LakiniBwanaakamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako.

19 Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni nyama yako na damu yako mwenyewe, ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’

20 “Bwanaametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vileBwanaalivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina laBwana, Mungu wa Israeli.

21 Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambamo ndani yake kuna Agano laBwanalile alilofanya na baba zetu wakati alipowatoa Misri.”

Maombi Ya Solomoni Ya Kuweka Hekalu Wakfu

22 Kisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu yaBwanamachoni pa kusanyiko lote la Israeli, akakunjua mikono yake kuelekea mbinguni

23 na kusema:

“EeBwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe mbinguni juu wala duniani chini, wewe unayetunza Agano lako la upendo pamoja na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.

24 Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.

25 “SasaBwana, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’

26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litokee sawasawa.

27 “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga!

28 Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, EeBwanaMungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo.

29 Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa.

30 Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe.

31 “Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili,

32 basi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie asiye na hatia kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kutokuwa na hatia kwake.

33 “Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili,

34 basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.

35 “Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka katika dhambi zao kwa sababu umewaadhibu,

36 basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.

37 “Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wo wote, maafa ya namna yo yote au ugonjwa wo wote unaoweza kuwajia,

38 wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akijua juu ya taabu ya moyo wake mwenyewe, akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili:

39 basi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote),

40 ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.

41 “Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako,

42 kwa maana watu watasikia juu ya Jina lako kuu na juu ya mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, wakati atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili,

43 basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lo lote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli na wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.

44 “Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, po pote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwaBwanakuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako,

45 basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao.

46 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu ye yote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao nakuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu;

47 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda kwa uovu’;

48 kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako;

49 basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na ukawatetee haki yao.

50 Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma;

51 kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka kwenye lile tanuru lakuyeyushia chuma.

52 “Macho yako na yafumbuke juu ya ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wo wote wanapokulilia.

53 Kwa maana uliwachagua wao kutoka mataifa yote ya ulimwengu kuwa urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Mose wakati wewe, EeBwanaMwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.”

54 Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwaBwana, akainuka kutoka mbele ya madhabahu yaBwana, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni.

55 Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa akisema:

56 “AhimidiweBwana, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose.

57 BwanaMungu wetu na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa.

58 Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kuzishika amri na maagizo na masharti aliyowapa baba zetu.

59 Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele zaBwana, yawe karibu naBwanaMungu wetu mchana na usiku, ili kwamba atetee shauri la mtumishi wake na la watu wake Israeli kulingana na hitaji lao la kila siku,

60 ili kwamba mataifa yote ya dunia wajue kwambaBwanandiye Mungu na kwamba hakuna mwingine.

61 Lakini ni lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwaBwanaMungu wetu, kuishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.”

Kuwekwa Wakfu Hekalu

62 Kisha mfalme na Israeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele zaBwana.

63 Solomoni akatoa dhabihu sadaka za amani kwaBwana: ng’ombe 22,000, kondoo pamoja na mbuzi 120,000. Hivyo mfalme pamoja na Waisraeli wote wakaliweka wakfu Hekalu laBwana.

64 Siku iyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya kati ya ua ulioko mbele ya Hekalu laBwanana hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele zaBwanailikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani.

65 Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Israeli wote pamoja naye: walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka ingilio la Hamathi hadi Korongo la Misri. Wakiadhimisha mbele zaBwanaMungu wetu kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani, jumla siku kumi na nne.

66 Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani, wakiwa na mashangilio na furaha rohoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayoBwanaametenda kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/8-04ab805c8b329ea2ca747a159e98325a.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 9

Bwana Anamtokea Solomoni

1 Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu laBwanapamoja na jumba la kifalme, alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya,

2 Bwanaakamtokea mara ya pili, kama alivyokuwa amemtokea huko Gibeoni.

3 Bwanaakamwambia:

“Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote.

4 “Kukuhusu wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria,

5 nitaimarisha kiti chako cha ufalme juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako nikisema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’

6 “Lakini kama ninyi au wana wenu wakigeukia mbali nami na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuwatumikia miungu mingine na kuiabudu,

7 basi nitakatilia mbali Israeli kutoka katika nchi niliyowapa na kulikataa Hekalu hili nililoliweka wakfu kwa Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha mzaha miongoni mwa watu wote.

8 Ingawa Hekalu hili linavutia sasa, wote watakaopita karibu yake watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa niniBwanaamefanya kitu cha namna hii katika nchi hii na kwenye Hekalu hili?’

9 Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwachaBwanaMungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakiiabudu na kuitumikia, ndiyo sababuBwanaameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”

Shughuli Nyingine Za Solomoni

10 Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu laBwanana jumba la kifalme,

11 Mfalme Solomoni akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi yote, misunobari na dhahabu yote aliyohitaji.

12 Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Solomoni alikuwa amempa, hakupendezwa nayo.

13 Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?”

# Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo.

14 Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta 120za dhahabu.

15 Haya ni maelezo kuhusu Mfalme Solomoni, jinsi alivyowafanyiza watu kazi za kulazimishwa ili kulijenga Hekalu laBwana, jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe, Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri.

16 (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameshambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Solomoni, kama zawadi ya arusi.

17 Solomoni akaujenga tena upya Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini,

18 akajenga pia Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake,

19 vile vile miji ya ghala na miji kwa ajili ya magari yake na farasi wake: cho chote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni na katika nchi yote iliyokuwa chini ya mamlaka yake.

20 Watu wote waliobaki kutoka kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (mataifa haya hayakuwa Waisraeli),

21 yaani, uzao wao uliobaki katika nchi, ambao Waisraeli wasingeweza kuwaangamiza, hawa Solomoni akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo.

22 Lakini Solomoni hakumfanya ye yote wa Waisraeli kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa wapiganaji wake, maafisa wake wa serikali, maafisa wake, wakuu wake, majemadari wa jeshi wa magari yake ya vita na wapanda farasi.

23 Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Solomoni: maafisa 550 waliowasimamia watu waliofanya kazi.

24 Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia katika jumba la kifalme Solomoni alilokuwa amemjengea, akajenga Milo.

25 Solomoni akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani mara tatu kwa mwaka, juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga kwa ajili yaBwana, akifukiza uvumba mbele zaBwanapamoja na dhabihu hizo, hivyo kutimiza kanuni za Hekalu.

26 Mfalme Solomoni akatengeneza pia meli huko Ezion-Geberi, ambayo iko karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu.

27 Naye Hiramu akatuma watu wake, mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Solomoni.

28 Wakasafiri kwenda Ofiri na kurudi na talanta 420za dhahabu, ambazo walimletea Mfalme Solomoni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/9-b98f8502b4f443b4ac84ba6596c45db7.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 10

Malkia Wa Sheba Amtembelea Solomoni

1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina laBwana, malkia alikuja kumjaribu kwa maswali magumu.

2 Alipofika Yerusalemu pamoja na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake.

3 Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lo lote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea.

4 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,

5 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu laBwana, alipatwa na mshangao.

6 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.

7 Lakini sikuamini mambo haya mpaka nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake, katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia.

8 Watu wako wanafurahi namna gani! Maafisa wako wanafurahi namna gani, wale ambao husimama mbele yako daima na kusikia hekima yako!

9 AhimidiweBwanaMungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wakeBwanawa milele kwa ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”

10 Naye akampa mfalme talanta 120za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezi na mawe ya thamani. Haikuwahi kamwe kutokea tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni.

11 (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na mawe ya thamani.

12 Mfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo kwa ajili ya Hekalu laBwanana kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha miti ya msandali hakijawahi kuingizwa nchini tangu siku ile.)

13 Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichohitaji na kukiomba, zaidi ya vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka akarudi pamoja na wafuasi wake kwenye nchi yake mwenyewe.

Fahari Ya Solomoni

14 Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666,

15 pasipo kuweka mapato kutoka wafanya biashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi.

16 Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600.

17 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatuza dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.

18 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.

19 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na egemeo la nyuma lilikuwa la mviringo kwa juu. Juu pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuwekea mikono, sanamu ya simba akisimama kila upande wake mahali pa kuwekea mikono.

20 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, wawili kwenye kila ngazi, yaani, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wo wote.

21 Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Solomoni.

22 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biasharabaharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wadogo na wakubwa.

23 Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.

24 Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameweka katika moyo wake.

25 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.

26 Solomoni akalimbikiza magari makubwa mazuri na farasi; alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000 ambayo aliyaweka katika miji ya magari pia pamoja naye huko Yerusalemu.

27 Mfalme akafanya fedha kuwa ya kawaida huko Yerusalemu kama mawe, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima.

28 Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue; wafanyabiashara wa kifalme waliwanunua kutoka Kue.

29 Waliingiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli za fedha 600na farasi kwa shekeli za fedha 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na Waaramu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/10-6409c8c690e73e8debb9d217df7b0f62.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 11

Wakeze Solomoni

1 Hata hivyo, Mfalme Solomoni akawapenda wanawake wengi wa kigeni zaidi, mbali na binti Farao: wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti.

2 Wakitoka katika mataifa ambayoBwanaaliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Solomoni akakaza kuwapenda.

3 Alikuwa na wake 700 wa uzao wa kifalme na masuria 300, nao hao wake zake wakampotosha.

4 Kadiri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakageuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukuwa mkamilifu kwaBwanaMungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake.

5 Akafuata Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, na Molekimungu aliyekuwa chukizo la Waamoni.

6 Kwa hiyo Solomoni akafanya uovu machoni paBwana; hakumfuataBwanakikamilifu kama alivyofanya Daudi baba yake.

7 Kwenye kilima mashariki mwa Yerusalemu, Solomoni akajenga mahali pa juu kwa ajili ya Kemoshi chukizo la Wamoabu, na kwa Moleki mungu chukizo la Waamoni.

8 Akafanya hivyo kwa wake zake wote wa kigeni, ambao walifukiza uvumba na kutoa dhabihu kwa miungu yao.

9 Bwanaakamkasirikia Solomoni kwa sababu moyo wake uligeuka mbali naBwana, Mungu wa Israeli, ambaye alikuwa amemtokea mara mbili.

10 Ingawa alikuwa amemkataza Solomoni kufuata miungu mingine, Solomoni hakutii amri yaBwana.

11 Kwa hiyoBwanaakamwambia Solomoni, “Kwa kuwa hii ndiyo hali yako na hukushika Agano langu na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme kutoka kwako na kumpa mmoja wa walio chini yako.

12 Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi baba yako, sitafanya jambo hili wakati wa uhai wako. Nitaurarua kutoka mikononi mwa mwanao.

13 Lakini pia sitaurarua ufalme wote kutoka kwake, bali nitampa kabila moja kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu na kwa ajili ya Yerusalemu, ambao nimeuchagua.”

Adui Za Solomoni

14 KishaBwanaakamwinua adui dhidi ya Solomoni, Hadadi, Mwedomu, kutoka ukoo wa kifalme wa Edomu.

15 Huko nyuma wakati Daudi alipokuwa akipigana na Edomu, Yoabu jemadari wa jeshi, aliyekuwa amekwenda kuzika waliouawa, alikuwa amewaua wanaume wote waliokuwako Edomu.

16 Yoabu na Waisraeli wote walikaa huko kwa miezi sita, mpaka walipomaliza kuwaangamiza wanaume wote huko Edomu.

17 Lakini Hadadi, akiwa bado mvulana mdogo, alikimbilia Misri akiwa na baadhi ya maafisa wa Kiedomu waliokuwa wakimhudumia baba yake.

18 Wakaondoka Midiani wakaenda Parani. Basi wakichukua pamoja nao wanaume kutoka Parani, wakaenda Misri, kwa Farao mfalme wa Misri, ambaye alimpa Hadadi nyumba, ardhi na akampatia chakula.

19 Farao akapendezwa sana na Hadadi hata akampa ndugu wa mkewe mwenyewe, Malkia Tapenesi, ili aolewe na Hadadi.

20 Huyo ndugu wa Tapenesi akamzalia mwana aliyeitwa Genubathi, ambaye alilelewa na Tapenesi katika jumba la kifalme. Huko Genubathi aliishi pamoja na watoto wa Farao mwenyewe.

21 Alipokuwa huko Misri, Hadadi alisikia kwamba Daudi amepumzika na baba zake na ya kwamba pia Yoabu aliyekuwa jemadari wa jeshi amekufa. Ndipo Hadadi akamwambia Farao, “Niruhusu niende ili niweze kurudi katika nchi yangu.”

22 Farao akauliza, “Umekosa nini hapa, kwamba unataka kurudi katika nchi yako?”

Hadadi akajibu, “Hakuna, lakini niruhusu niende!”

23 Mungu akamwinua adui mwingine dhidi ya Solomoni, Rezoni mwana wa Eliyada, ambaye alikuwa amemkimbia bwana wake Hadadezeri, mfalme wa Soba.

24 Akawakusanya watu, naye akawa kiongozi wa kundi la waasi, wakati Daudi alipoangamiza majeshi ya Soba; waasi walikwenda Dameski, mahali walipokaa na kumiliki.

25 Rezoni alikuwa adui wa Israeli kwa muda wote alioishi Solomoni, ukiongezea matatizo yaliyosababishwa na Hadadi. Kwa hiyo Rezoni akatawala katika Aramuna alikuwa mkatili kwa Israeli.

Yeroboamu Anaasi Dhidi Ya Solomoni

26 Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Solomoni, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua.

27 Haya ndiyo maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Solomoni alikuwa amejenga Milonaye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake.

28 Basi Yeroboamu alikuwa mtu shujaa na hodari, naye Solomoni alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yosefu.

29 Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani,

30 naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili.

31 Kisha akamwambia Yeroboamu, “Chukua vipande kumi kwa ajili yako, kwa kuwa hivi ndivyoBwana, Mungu wa Israeli asemavyo: ‘Tazama, ninakwenda kuuchana ufalme kutoka mikononi mwa Solomoni na kukupa wewe makabila kumi.

32 Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja.

33 Nitafanya hivi kwa sababu wameniacha mimi na kuabudu Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakwenda katika njia zangu ili kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Solomoni, alivyofanya.

34 “ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote kutoka mikononi mwa Solomoni, nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu.

35 Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi.

36 Nitampa mwanawe kabila moja ili kwamba Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu.

37 Hata hivyo, kukuhusu wewe Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala juu ya yote yale moyo wako unayotamani, utakuwa mfalme juu ya Israeli.

38 Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kuzishika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ukoo wa kifalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli.

39 Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya hili, lakini siyo milele.’ ”

40 Solomoni akajaribu kumwua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko mpaka Solomoni alipokufa.

Kifo Cha Solomoni

41 Kwa habari za matukio mengine ya utawala wa Solomoni, yote aliyoyafanya na hekima aliyoionyesha, je hayakuandikwa yote katika kitabu cha matendo cha Solomoni?

42 Solomoni alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu.

43 Kisha akalala pamoja na baba zake na akazikwa katika mji wa Daudi baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akatawala badala yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/11-ab621601f450bca3a133e73cfaac4bcb.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 12

Israeli Yaasi Dhidi Ya Rehoboamu

1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wamekwenda huko kumfanya yeye kuwa mfalme.

2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Solomoni), akarudi kutoka Misri.

3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu, yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia,

4 “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa ufanye nyepesi kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”

5 Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.

6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee ambao walimtumikia Solomoni baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri nini katika kuwajibu watu hawa?”

7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”

8 Lakini Rehoboamu akakataa shauri alilopewa na wazee na akataka ushauri kwa vijana wanaume rika lake waliokuwa wakimtumikia.

9 Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu?’ ”

10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Waambie watu hawa waliokuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ kuwa, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.

11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.’ ”

12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.”

13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Akikataa shauri alilopewa na wazee,

14 akafuata shauri la vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.”

15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwaBwana, ili kutimiza neno ambaloBwanaalikuwa amenena kwa Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia Ahiya Mshiloni.

16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:

“Tuna fungu gani kwa Daudi?

Sisi hatuna urithi kwa mwana wa Yese.

Nendeni kwenye mahema yenu, Ee Israeli!

Angalia nyumba yako mwenyewe, Ee Daudi!”

Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao.

17 Lakini kwa habari ya Waisraeli waliokuwa wakiishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.

18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli yote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake na kutorokea Yerusalemu.

19 Hivyo Israeli ameasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.

20 Waisraeli wote waliposikia kwamba Yeroboamu amerudi, wakatuma watu na kumwita kwenye kusanyiko na kumfanya mfalme juu ya Israeli yote. Ni kabila la Yuda peke yake lililobaki kuwa tiifu kwa nyumba ya Daudi.

21 Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda na kabila la Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.

22 Lakini neno hili la Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu:

23 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, nayo nyumba yote ya Yuda, ya Benyamini na watu wengine wote,

24 ‘Hili ndilo asemaloBwana: Usipande kupigana dhidi ya ndugu zako, Waisraeli. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili limetoka kwangu.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno laBwanana kurudi nyumbani, kamaBwanaalivyokuwa ameagiza.

Ndama Wa Dhahabu Huko Betheli Na Dani

25 Kisha Yeroboamu akajenga Shekemu akaizungushia ngome katika nchi ya vilima ya Efraimu na akaishi huko. Akatoka huko, akaenda akajenga Penueli.

26 Yeroboamu akawaza moyoni mwake, “Sasa inawezekana ufalme ukarudi katika nyumba ya Daudi.

27 Kama watu hawa watapanda kwenda kutoa dhabihu katika Hekalu laBwanahuko Yerusalemu, mioyo yao itamrudia bwana wao, Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua mimi na kurudi kwa Mfalme Rehoboamu.”

28 Baada ya kutafuta shauri, mfalme akatengeneza ndama wawili wa dhahabu. Akawaambia watu, “Ni gharama kubwa kwenu kukwea kwenda Yerusalemu. Hii hapa miungu yenu, Ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”

29 Ndama mmoja akamweka Betheli na mwingine Dani.

30 Nalo jambo hili likawa dhambi, watu wakawa wanaenda hadi Dani kumwabudu huyo aliyewekwa huko.

31 Yeroboamu akajenga madhabahu mahali pa juu pa kuabudia miungu na kuwateua makuhani kutoka watu wa aina zote, ijapokuwa hawakuwa Walawi.

32 Akaweka sikukuu katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, kama sikukuu iliyokuwa ikifanyika huko Yuda na akatoa dhabihu juu ya madhabahu. Akafanya hivyo huko Betheli akitoa dhabihu kwa ndama alizotengeneza. Huko Betheli, akawaweka makuhani pia katika sehemu za juu za kuabudia miungu alizotengeneza.

33 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouchagua mwenyewe, alitoa dhabihu juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga huko Betheli. Kwa hiyo akaweka sikukuu kwa ajili ya Waisraeli na akapanda madhabahuni kutoa sadaka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/12-97d7fb609fe4debedc65f4bdd611e9d4.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 13

Mtu Wa Mungu Kutoka Yuda

1 Kwa neno laBwana, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka.

2 Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno laBwana: “Ee madhabahu, madhabahu! Hivi ndivyo asemavyoBwana: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu wale ambao wanatoa sadaka hapa sasa, nayo mifupa ya wanadamu itachomwa juu yako.’ ”

3 Siku iyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo isharaBwanaaliyotangaza: Madhabahu hii itapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”

4 Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamate!” Lakini mkono aliokuwa ameunyoosha kumwelekea yule mtu ukasinyaa na kubaki hapo hapo, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha.

5 Pia, madhabahu ilipasuka na majivu yakamwagika sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno laBwana.

6 Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwaBwanaMungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwaBwana, nao mkono wa mfalme ukapona na kuwa kama ulivyokuwa hapo kwanza.

7 Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”

8 Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali zako, nisingekwenda pamoja na wewe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa.

9 Kwa kuwa niliagizwa kwa neno laBwana: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ”

10 Kwa hiyo akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia ile ambayo alikuwa ameijia Betheli.

11 Basi kulikuwepo na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme.

12 Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonyesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita.

13 Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda

14 na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na akamwuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?”

Akamjibu, “Mimi ndiye.”

15 Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi ule.”

16 Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa.

17 Nimeambiwa kwa neno laBwana: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”

18 Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno laBwana: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.)

19 Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.

20 Wakati walipokuwa wameketi mezani, neno laBwanalikamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu.

21 Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyoBwana: ‘Umeasi neno laBwanana hukushika amri uliyopewa naBwanaMungu wako,

22 bali ulirudi na ukala mkate na kunywa maji mahali ambapo alikuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”

23 Wakati huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake.

24 Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamwua na maiti yake ikabwagwa barabarani, yule punda wake na simba wakiwa wamesimama karibu yake.

25 Baadhi ya watu waliopita pale waliona maiti imebwagwa pale chini, simba akiwa amesimama kando ya maiti, wakaenda na kutoa habari katika mji ambao nabii mzee aliishi.

26 Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka katika safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu ambaye aliasi neno laBwana.Bwanaamemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumwua, sawasawa na neno laBwanalilivyokuwa limemwonya.”

27 Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo.

28 Kisha akatoka akaenda akakuta maiti imebwagwa chini barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda.

29 Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika.

30 Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”

31 Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Wakati nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.

32 Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno laBwanadhidi ya madhabahu huko Betheli na dhidi ya madhabahu yote katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Samaria, hakika yatatokea kweli.”

33 Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu kutoka watu wa aina zote. Ye yote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu.

34 Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/13-47acff3a56673090ff7bef2871722cc5.mp3?version_id=1627—

1 Wafalme 14

Unabii Wa Ahiya Dhidi Ya Yeroboamu

1 Wakati ule Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua,

2 naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya yuko huko, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme juu ya watu hawa.

3 Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.”

4 Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama alivyosema mumewe, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo.

Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake.

5 LakiniBwanaalikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.”

6 Hivyo Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini kujibadilisha? Nimetumwa kwako nikiwa na habari mbaya.

7 Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyoBwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya kiongozi juu ya watu wangu Israeli.

8 Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu.

9 Umefanya maovu mengi kuliko wote walio kutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunitupa nyuma yako.

10 “ ‘Kwa sababu ya hili, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu mpaka iteketee yote kama mtu achomaye kinyesi.

11 Mbwa watawala wale walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji na ndege wa angani watajilisha kwa wale watakaofia mashambani.Bwanaamesema!’

12 “Kukuhusu wewe, rudi nyumbani. Wakati utakapotia mguu katika mji wako, kijana atakufa.

13 Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Kwa sababu ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye peke yake ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambayeBwana, Mungu wa Israeli, ameona walau kitu cho chote chema kwake.

14 “Bwanaatajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku ndiyo hii! Nini? Naam, hata sasa hivi.

15 NayeBwanaataipiga Israeli, hata iwe kama unyasi unaosukwasukwa juu ya maji. Ataing’oa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ng’ambo ya Mto Eufrati, kwa sababu wamemghadhibishaBwanakwa kutengeneza nguzo za Ashera.

16 Naye atawaacha Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu aliyoyatenda na kusababisha Israeli kuyatenda.”

17 Kisha mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirza. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa.

18 Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kamaBwanaalivyokuwa amesema kupitia mtumishi wake, nabii Ahiya.

19 Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli.

20 Akawatawala kwa miaka ishirini na miwili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Rehoboamu Mfalme Wa Yuda

21 Rehoboamu mwana wa Solomoni alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambaoBwanaalikuwa ameuchagua kutoka makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni.

22 Yuda wakatenda maovu machoni paBwana. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu zaidi kuliko baba zao walivyofanya.

23 Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu, mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda.

24 Walikuwepo hata wanaume mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi; watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayoBwanaaliyafukuza mbele ya Waisraeli.

25 Katika mwaka wa tano wa kutawala kwake Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu.

26 Akachukua hazina yote ya Hekalu laBwanana hazina yote ya jumba la kifalme. Alichukua kila kitu, pamoja na ngao zote za dhahabu Solomoni alizotengeneza.

27 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba kuweka mahali pa zile za dhahabu, akawagawia wakuu wa ulinzi, waliokuwa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme.

28 Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu laBwana, walinzi walizichukua zile ngao, hatimaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

29 Kwa matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

30 Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

31 Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni. Naye Abiyamwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/14-6ca50177776e121608a55051c9924c50.mp3?version_id=1627—