Wakolosai 3

Kanuni Za Kuishi Maisha Matakatifu

1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.

2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani.

3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.

4 Wakati Kristo atakapotokea yeye aliye uzima wenu ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.

5 Kwa hiyo, ueni kabisa cho chote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: Yaani, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na kutamani, ambayo ndiyo ibada ya sanamu.

6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja.

7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo.

8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote, yaani: Hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu.

9 Msiambiane uongo kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake,

10 nanyi mmevaa utu mpya unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake.

11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote na ndani ya wote.

12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu, wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu.

13 Vumilianeni na kusameheana. Mtu akiwa na lalamiko lo lote dhidi ya mwenzake, sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi.

14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena iweni watu wa shukrani.

16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.

17 Lo lote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika Jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

Kanuni Katika Madaraka Ya Nyumbani

18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

21 Ninyi akina baba msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

22 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, bali mkimwogopa Mungu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao wakati wanapowaona.

23 Lo lote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana na si wanadamu.

24 Kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana kuwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia.

25 Ye yote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/COL/3-8cca7b89906432ece482487c00ec4398.mp3?version_id=1627—

Wakolosai 4

1 Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua ya kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.

Maagizo Zaidi

2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru.

3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa.

4 Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena.

5 Iweni na hekima jinsi mnavyoenenda mbele yao wale walio nje, mkiutumia vizuri wakati wenu.

6 Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu.

Salamu Za Mwisho

7 Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtenda kazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana.

8 Nimemtuma kwenu kwa madhumuni haya ili kwamba mpate kufahamu hali yetu na pia awatie moyo.

9 Anakuja pamoja na Onesmo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.

10 Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni).

11 Yesu, yeye aitwaye Yusto, pia anawasalimu. Hawa peke yao, ndio Wayahudi miongoni mwa watenda kazi wenzangu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.

12 Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu mkiwa wakamilifu na thabiti.

13 Ninashuhudia kwa ajili yake kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.

14 Rafiki yetu mpenzi Luka, yaani, yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.

15 Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia na pia Nimfa pamoja na kanisa linalokutana katika nyumba yake.

16 Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kanisa la Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.

17 Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana.”

18 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/COL/4-33abcd4fb0623743df664f1b62a3862c.mp3?version_id=1627—

Wafilipi 1

Salamu

1 Waraka wa Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu:

Kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu walioko Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi:

2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Shukrani Na Maombi

3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi.

4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha,

5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo,

6 nina hakika kwamba, yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.

7 Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu, ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami.

8 Mungu ni shahidi yangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu.

9 Haya ndiyo maombi yangu kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote,

10 ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo,

11 mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.

Kufungwa Kwa Paulo Kwaieneza Injili

12 Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili.

13 Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo.

14 Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.

15 Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema.

16 Hawa wa mwisho wanamhubiri Kristo kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili.

17 Hao wa kwanza wanamtangaza Kristo kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu.

18 Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi.

Naam, nami nitaendelea kufurahi,

19 kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu.

20 Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yo yote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wo wote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa.

21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida.

22 Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini sijui nichague lipi? Mimi sijui!

23 Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi.

24 Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili.

25 Kwa kuwa nina matumaini haya, ninajua kwamba nitaendelea kuwapo na kuwa pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani.

26 Ili kwamba furaha yenu iwe nyingi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu kwa kule kuja kwangu kwenu tena.

Kuenenda Ipasavyo Injili

27 Lakini lo lote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja,

28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa na hii ni kazi ya Mungu.

29 Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake,

30 kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PHP/1-b7aafafa48e28b75ebb7020107e60715.mp3?version_id=1627—

Wafilipi 2

Kuiga Unyenyekevu Wa Kristo

1 Kama kukiwa na jambo lo lote la kutia moyo, kukiwako faraja yo yote katika upendo, kukiwa na ushirika wo wote katika Roho, kukiwa na wema wo wote na huruma,

2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia kama hiyo, mkiwa na upendo huo huo, wenye roho moja na kusudi moja.

3 Msitende jambo lo lote kwa nia ya kujitukuza, bali kwa unyenyekevu, kila mtu akimhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

5 Iweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

hakuona kule kuwa sawa na Mungu

ni kitu cha kushikilia,

7 bali alijifanya si kitu,

akajifanya sawa hasa na mtumwa,

akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

naam, mauti ya msalaba!

9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana

na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

la vitu vya mbinguni, vya duniani

na vya chini ya nchi,

11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

YESU KRISTO NI BWANA,

kwa utukufu wa Mungu Baba.

Ng’aeni Kama Mianga Katika Ulimwengu

12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka,

13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

14 Fanyeni mambo yote bila kunung’unika wala kushindana,

15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnang’aa kama mianga ulimwenguni.

16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.

17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote.

18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.

Paulo Amsifu Timotheo

19 Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu.

20 Sina mtu mwingine kama yeye ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi.

21 Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo.

22 Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana amefanya kazi ya Injili pamoja nami kama vile mwana kwa baba yake.

23 Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa.

24 Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni.

Paulo Amsifu Epafrodito

25 Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtenda kazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu.

26 Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa.

27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni.

28 Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue.

29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa,

30 kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunipa msaada ambao ninyi hamkuweza kunipa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PHP/2-c4c4f604b469dca9baebdfea358fe437.mp3?version_id=1627—

Wafilipi 3

Hakuna Tumaini Katika Mwili

1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.

2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa.

3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,

4 ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili.

Kama mtu ye yote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi.

5 Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo,

6 kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia.

7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.

8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi ya kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo,

9 nami nionekane mbele zake nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani.

10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake,

11 ili kwa njia yo yote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

Kukaza Mwendo Ili Kufikia Lengo

12 Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu.

13 Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele.

14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.

15 Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo.

16 Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia.

17 Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea.

18 Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Kristo.

19 Mwisho wa watu hao ni uangamivu, Mungu wao ni tumbo na utukufu wao ni aibu na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia.

20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo,

21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PHP/3-945354f8780b4743617c17627c857b09.mp3?version_id=1627—

Wafilipi 4

1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

Mausia

2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana.

3 Naam, nawasihi ninyi pia, wenzi wangu waaminifu, wasaidieni hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watenda kazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini!

5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu.

6 Msijisumbue kwa jambo lo lote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.

7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itawalinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo na sifa njema, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote ya kupendeza, yo yote yenye staha, ukiwako uzuri wo wote, pakiwepo cho chote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.

9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

Shukrani Kwa Matoleo Yenu

10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo.

11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yo yote.

12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa.

13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu.

15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi.

16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja.

17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu.

18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi, nimetoshelezwa kabisa, sasa kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu.

19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

20 Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.

Salamu Za Mwisho

21 Msalimuni kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walioko pamoja nami wanawasalimu.

22 Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale watu wa nyumbani mwa Kaisari.

23 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PHP/4-14544951b0432ee787978db780199908.mp3?version_id=1627—

Waefeso 1

Salamu

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu:

Kwa watakatifu walioko Efeso, walio waaminifu katika Kristo Yesu:

2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Baraka Za Kiroho Katika Kristo Yesu

3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo.

4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake.

5 Kwa upendo alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe.

6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

7 Katika yeye tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake

8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote.

9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo,

10 ili yapate kutimizwa katika wakati mkalimifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukiisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake,

12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.

13 Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa,

14 yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.

Shukrani Na Maombi

15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote,

16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu.

17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi.

18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu

19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno

20 ambayo aliitumia alipomfufua Kristo kutoka kwa wafu, akamketisha mkono wake wa kuume katika mbingu,

21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali na katika ule ujao pia.

22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa,

23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EPH/1-a5456c701fa7166a4fa174ed32de3765.mp3?version_id=1627—

Waefeso 2

Tumefanywa Kuwa Hai Ndani Ya Kristo

1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu,

2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii.

3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine ye yote.

4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema,

5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema.

6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu,

7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu.

8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu,

9 si kwa matendo, ili mtu awaye yote asije akajisifu.

10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

Wamoja Katika Kristo

11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba ninyi ambao hapo awali mlikuwa watu Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu),

12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa hamna Kristo, mkiwa mmtengwa kutoka katika jumuiya ya watu wa Mungu, yaani, Israeli mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, mliishi duniani mkiwa hamna tumaini wala Mungu.

13 Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kwa njia ya damu ya Kristo.

14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu,

15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani,

16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kwa kupitia msalaba, ambao kwa huo aliangamiza uadui wao.

17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu.

18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu.

20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni.

21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana.

22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EPH/2-e23a39884fd17de61de72e94b73333b5.mp3?version_id=1627—

Waefeso 3

Huduma Ya Paulo Kwa Watu Mataifa

1 Kwa sababu hii, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi watu Mataifa,

2 Kwa hakika mmekwisha kusikia kuhusu ile huduma ya neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu,

3 yaani, ile siri iliodhihirishwa kwangu kwa njia ya ufunuo, kama nilivyotangulia kuandika kwa kifupi.

4 Kwa kusoma haya, basi mtaweza kuelewa ufahamu wangu katika siri ya Kristo.

5 Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu.

6 Siri hii ni kwamba, kwa njia ya Injili, watu Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu.

7 Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi.

8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii ili niwahubirie watu Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo na

9 kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa kwa nyakati zote katika Mungu aliyeumba vitu vyote.

10 Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho,

11 sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

12 Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri.

13 Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.

Maombi Ya Paulo Kwa Waefeso

14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti,

15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye.

16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake,

17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo,

18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo

19 na kujua upendo huu kwamba unapita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu,

21 yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EPH/3-864e88cbc9a15e6af5877450826f39f8.mp3?version_id=1627—

Waefeso 4

Umoja Katika Mwili Wa Kristo

1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa.

2 Iweni wanyenyekevu kabisa na wapole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo.

3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja.

5 Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja,

6 Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.

7 Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo.

8 Kwa hiyo husema:

# “Alipopaa juu zaidi,

aliteka mateka

akawapa wanadamu vipawa.”

9 (Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia?

10 Yeye aliyeshuka ndiye aliyepaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.)

11 Yeye ndiye aliyeweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu,

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa

13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu.

15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo.

16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

Maisha Ya Zamani Na Maisha Mapya

17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao.

18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao.

19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyomjifunza Kristo.

21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu.

22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu,

23 ili mfanywe upya roho na nia zenu,

24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

Kanuni Za Maisha Mapya

25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja.

26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika,

27 wala msimpe ibilisi nafasi.

28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.

30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwa huyo mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi.

31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu.

32 Iweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EPH/4-2263790e73751ef16d256801284c812f.mp3?version_id=1627—