2 Samweli 3

1 Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi.

2 Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni:

Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli;

3 mzaliwa wake wa pili alikuwa Danielimwana wa Abigaili mjane wa Nabali wa Karmeli;

wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka binti Talmai mfalme wa Geshuri;

4 wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi;

wa tano, Shefatia mwana wa Abitali;

5 wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi.

Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni.

Abneri Anamwendea Daudi

6 Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli.

7 Basi Sauli alikuwa amekuwa na suria, jina lake Rispa binti wa Aia. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?”

8 Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke!

9 Mungu na amshughulikie Abneri, tena kwa ukali, ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kileBwanaalichomwahidi kwa kiapo,

10 na kuuhamisha ufalme kutoka kwenye nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba.”

11 Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.

12 Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.”

13 Daudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu mpaka umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.”

14 Kisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi 100 ya Wafilisti.”

15 Kwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi.

16 Hata hivyo, mumewe alikwenda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi.

17 Abneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu.

18 Sasa fanyeni hivyo! Kwa maanaBwanaalimwahidi Daudi akisema, ‘Kwa kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’ ”

19 Pia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya.

20 Wakati Abneri aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake.

21 Ndipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili kwamba uweze kutawala juu ya yote yale ambayo moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamwaga Abneri, naye akaenda kwa amani.

Yoabu Amuua Abneri

22 Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kwenye kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani.

23 Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme na kwamba mfalme alikwishamruhusu aende zake, na kwamba alikwisha ondoka kwa amani.

24 Basi Yoabu alikwenda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikujia. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa amekwenda!

25 Wajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza nyendo zako na kupata kila kitu unachokifanya.”

26 Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili.

27 Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Pale pale kwa kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni, naye akafa.

28 Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele zaBwanakuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri.

29 Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane ye yote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha, au ukoma au mwenye kuegemea fimbo au aangukaye kwa upanga au kupungukiwa na chakula.”

30 (Yoabu na Abishai ndugu yake walimwua Abneri kwa sababu alikuwa amemwua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)

31 Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae nguo za gunia na mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza.

32 Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia.

33 Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri:

“Je, ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu?

34 Mikono yako haikufungwa,

miguu yako haikufungwa pingu.

Ulianguka kama yeye aangukaye

mbele ya watu waovu.”

Nao watu wote wakamlilia tena.

35 Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale cho chote kulipokuwa kungali bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama nikionja mkate au kitu kingine cho chote kabla ya jua kutua!”

36 Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza.

37 Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri.

38 Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mkuu na mtu mashuhuri ameanguka katika Israeli leo?

39 Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu.Bwanana amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/3-f8bba0ddcb4ab4165fc943314c0a994a.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 4

Ish-Boshethi Anauawa

1 Ish-Boshethi mwana wa Sauli aliposikia kwamba Abneri amekufa huko Hebroni, akakosa ujasiri, nayo Israeli yote wakatiwa hofu kuu.

2 Basi mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili ambao walikuwa viongozi wa vikundi vya uvamizi. Mmoja aliitwa Baana na mwingine Rekabu, waliokuwa wana wa Rimoni, Mbeerothi, kutoka kabila la Benyamini. Beerothi alihesabiwa kuwa sehemu ya Benyamini,

3 kwa sababu watu wa Beerothi walikimbilia huko Gitaimu na wameishi huko kama wageni mpaka siku hii ya leo.

4 (Yonathani mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa mlemavu miguu yote miwili. Alikuwa na miaka mitano wakati habari kuhusu Sauli na Yonathani zilipofika kutoka Yezreeli. Yaya wake akambeba ili kukimbia, lakini yaya alipokuwa anaharakisha kuondoka, mtoto alianguka akawa kiwete. Jina lake aliitwa Mefiboshethi.)

5 Basi Rekabu na Baana, wana wa Rimoni Mbeerothi wakaenda nyumbani kwa Ish-Boshethi, nao walifika huko wakati alipokuwa kwenye mapumziko yake ya mchana.

6 Wakaingia kwenye chumba cha ndani kana kwamba wanachukua ngano, wakamchoma Ish-Boshethi mkuki wa tumboni. Ndipo Rekabu na Baana nduguye wakatoroka.

7 Walikuwa wameingia ndani ya nyumba wakati alipokuwa amelala kitandani chumbani kwake. Baada ya kumchoma mkuki na kumwua, walikata kichwa chake. Wakiwa wamekichukua, walitembea usiku kucha kwa njia ya Araba.

8 Wakamletea Daudi kichwa cha Ish-Boshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, “Hiki hapa kichwa cha Ish-Boshethi mwana wa Sauli, adui yako, aliyejaribu kuondoa uhai wako. Siku hii ya leoBwanaamemlipia kisasi mfalme bwana wangu dhidi ya Sauli na mzao wake.”

9 Daudi akawajibu Rekabu na Baana nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akasema, “Hakika kamaBwanaaishivyo, ambaye ameniokoa kutoka katika taabu zote,

10 yule mtu aliponiambia, ‘Sauli amekufa,’ akadhani ananiletea habari njema, nilimkamata, nikamwua huko Siklagi. Hiyo ndiyo zawadi niliyompa kwa ajili ya taarifa yake!

11 Je, ni mara ngapi zaidi wakati watu waovu wamemwua mtu asiye na hatia akiwa ndani ya nyumba yake mwenyewe na kwenye kitanda chake mwenyewe? Je, sasa nisidai damu yake mikononi mwenu na kuwaondoa duniani?”

12 Kwa hiyo Daudi akawaamuru watu wake, wakawaua. Wakakata mikono yao na miguu, na kutundika viwiliwili vyao kando ya dimbwi huko Hebroni. Lakini wakakichukua kichwa cha Ish-Boshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/4-9677b2f9d68b46dc1459029a6e670fac.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 5

Daudi Awa Mfalme Juu Ya Israeli

1 Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu nyama yako na damu yako hasa.

2 Zamani, wakati Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ulikuwa ndiye uliyeongoza Israeli vitani. NayeBwanaakakuambia, ‘Utawachunga watu wangu Israeli, nawe utakuwa kiongozi wao.’ ”

3 Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele zaBwana, nao wakamtia Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.

4 Daudi alikuwa na miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli miaka arobaini.

5 Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na mitatu.

Daudi Anashinda Yerusalemu

6 Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi huko. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Hutaingia hapa ndani, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.”

7 Hata hivyo, Daudi akateka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.

8 Siku ile, Daudi akasema, “Ye yote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”

9 Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milokuelekea ndani.

10 Daudi akazidi kuwa na mamlaka zaidi na zaidi, kwa sababuBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.

11 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akatuma wajumbe kwa Daudi, pamoja na magogo ya mierezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi.

12 Naye Daudi akafahamu kuwaBwanaamemwimarisha kama mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli watu wake.

13 Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana na binti wengi walizaliwa kwake.

14 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni,

15 Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia,

16 Elishama, Eliada na Elifeleti.

Daudi Awashinda Wafilisti

17 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda kwa nguvu zote kumtafuta, lakini Daudi akasikia kuhusu jambo hili akatelemka kwenye ngome.

18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Refaimu,

19 kwa hiyo Daudi akamwulizaBwana, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

Bwanaakamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”

20 Ndipo Daudi akaenda mpaka Baal-Perasimu na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yafurikavyo,Bwanaamewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu.

21 Wafilisti wakatelekeza vinyago vyao huko, naye Daudi na watu wake wakavichukua.

22 Wafilisti walikwea kwa mara nyingine tena na kusambaa katika Bonde la Refaimu.

23 Kwa hiyo Daudi akamwulizaBwana, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi.

24 Mara utakaposikia sauti ya kutembea kutoka kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwaBwanaametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.”

25 Basi Daudi akafanya kamaBwanaalivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Gebbahadi Gezeri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/5-3c5e80434167e682813875dc847580bc.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 6

Sanduku La Mungu Laletwa Yerusalemu

1 Daudi akakusanya tena watu 30,000 wa Israeli waliochaguliwa.

2 Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yudakuleta kutoka huko Sanduku la Mungu, linaloitwa kwa Jina, naam, jina laBwanaMwenye Nguvu Zote, ambaye ameketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi walioko juu ya hilo Sanduku.

3 Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka katika nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa

4 likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake.

5 Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele zaBwanakwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi.

6 Walipofika kwenye sakafu ya kupuria ya Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa.

7 Hasira yaBwanaikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.

8 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu yaBwanailifurika juu ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza.

9 Daudi akamwogopaBwanasiku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku laBwanalitakavyoweza kunijia?”

10 Hakuwa radhi kulichukua Sanduku laBwanakwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti.

11 Sanduku laBwanalikabaki katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, nayeBwanaakambariki pamoja na nyumba yake yote.

12 Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Bwanaameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akatelemka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Obed-Edomu mpaka Mji wa Daudi kwa furaha.

13 Wale waliokuwa wamebeba Sanduku laBwanawalipokuwa wametembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenona.

14 Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele zaBwanakwa nguvu zake zote,

15 wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku laBwanakwa shangwe na sauti za tarumbeta.

16 Ikawa Sanduku laBwanalilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia kutoka dirishani. Naye alipoona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele zaBwana, akamdharau moyoni mwake.

17 Wakaleta Sanduku laBwanana kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimika kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani mbele zaBwana.

18 Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akawabariki watu katika jina laBwanaMwenye Nguvu Zote.

19 Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani kwao.

20 Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo machoni pa vijakazi wa watumishi wake, kama vile ambavyo mtu asiye na adabu angelifanya!”

21 Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele zaBwanaambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine ye yote kutoka katika nyumba yake wakati aliponiweka niwe mtawala juu ya Israeli, watu waBwana. Kwa hiyo nitacheza mbele zaBwana.

22 Nitakuwa asiye na heshima zaidi kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.”

23 Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto mpaka siku ya kufa kwake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/6-f38c8537422cae9c9c090d479a3d5222.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 7

Ahadi Ya Mungu Kwa Daudi

1 Baada ya mfalme kukaa katika jumba lake la kifalme kwa utulivu, nayeBwanaakiwa amemstarehesha pande zote mbali na adui zake,

2 akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa, ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.”

3 Nathani akamjibu mfalme, “Lo lote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maanaBwanayu pamoja nawe.”

4 Usiku ule neno laBwanalikamjia Nathani, kusema:

5 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndiloBwanaasemalo: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake?

6 Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu.

7 Po pote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao ye yote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?” ’

8 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli.

9 Nimekuwa pamoja nawe po pote ulipokwenda, nami nimekatilia mbali adui zako wote mbele ya uso wako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya walio wakuu sana wa dunia.

10 Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili kwamba wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni,

11 na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa raha mbele ya adui zenu wote.

“ ‘Bwanaakuambia kwambaBwanamwenyewe atakujengea nyumba.

12 Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake.

13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitaimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele.

14 Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu.

15 Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako.

16 Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha enzi kitafanywa imara milele.’ ”

17 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

Maombi Ya Daudi

18 Basi Daudi akaingia ndani, akaketi mbele zaBwana, akasema:

“EeBwanaMwenyezi, mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo?

19 Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, EeBwanaMwenyezi, wewe umenena pia habari za wakati ujao kuhusu nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, EeBwanaMwenyezi?

20 “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, EeBwanaMwenyezi.

21 Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako.

22 “Tazama jinsi ulivyo mkuu, EeBwanaMwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe,

23 Ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kuwa taifa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina mwenyewe na kufanya mambo makuu na maajabu ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao kutoka mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri?

24 Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, EeBwana, umekuwa Mungu wao.

25 “Basi sasa,Bwana, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Ukafanye kama ulivyoahidi,

26 ili kwamba jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘BwanaMwenye Nguvu Zote ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako.

27 “EeBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hii.

28 EeBwanaMwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umeahidi mambo haya mazuri kwa mtumishi wako.

29 Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili iweze kudumu mbele zako milele, kwa maana wewe, EeBwanaMwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/7-2fb9917aedfeeded850deec183f33ab5.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 8

Ushindi Wa Daudi

1 Ikawa baada ya jambo hili, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, akateka Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.

2 Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili hilo kundi waliuawa na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea kodi.

3 Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Eufrati.

4 Daudi akateka magari yake ya vita 1,000, askari wapanda farasi 7,000 na askari 20,000 watembeao kwa miguu. Daudi akawakata wale farasi wote wakokotao magari mishipa ya miguu, isipokuwa farasi 100 hakuwakata.

5 Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawaua 22,000 miongoni mwao.

6 Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa chini yake na kumlipa kodi.Bwanaakampa Daudi ushindi ko kote alikokwenda.

7 Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa mali ya maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu.

8 Kutoka miji ya Betana Berothai, ambayo alitawala Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.

9 Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amemshinda jeshi lote la Hadadezeri,

10 akamtuma Yoramu mwanawe kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ajili ya ushindi wake katika vita juu ya Hadadezeri, kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.

11 Mfalme Daudi akaviweka vyombo hivi wakfu kwaBwana, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda:

12 yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.

13 Naye Daudi akajulikana baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

14 Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi.Bwanaalimpatia Daudi ushindi ko kote alikokwenda.

Maafisa Wa Daudi

15 Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.

16 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;

17 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi;

18 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa kiongozi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa kifalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/8-7f72f1394b5279ed8acb38483db6d98c.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 9

Daudi Na Mefiboshethi

1 Daudi akauliza, “Je, hakuna mtu hata mmoja wa nyumba ya Sauli aliyebaki ambaye naweza kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani?”

2 Basi palikuwepo mtumishi wa nyumba ya Sauli aliyeitwa Siba. Wakamwita aje mbele ya Daudi, naye mfalme akamwambia, “Wewe ndiwe Siba?”

Akamjibu, “Naam, mimi ndiye mtumishi wako.”

3 Mfalme akauliza, “Je, hakuna ye yote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonyesha wema wa Mungu?”

Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani, yeye ni kiwete miguu yote.”

4 Mfalme akauliza, “Yuko wapi?”

Siba akajibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.”

5 Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli.

6 Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima.

Daudi akamwita, “Mefiboshethi!”

Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.”

7 Daudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.”

8 Mefiboshethi akasujudu akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?”

9 Ndipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake.

10 Wewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili kwamba mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini.)

11 Ndipo Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya cho chote bwana wangu mfalme atakachoagiza mtumishi wake kufanya.” Basi Mefiboshethi akala chakula mezani pa Daudi kama mmoja wa wana wa mfalme.

12 Mefiboshethi alikuwa na mwanawe mdogo aliyeitwa Mika, nao watu wote wa nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi.

13 Naye Mefiboshethi akaishi huko Yerusalemu, kwa sababu daima alikula mezani pa mfalme, naye alikuwa kiwete miguu yote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/9-68bbda1fc8c2665607e53ba28743d212.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 10

Daudi Awashinda Waamoni

1 Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akaingia mahali pake.

2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma ujumbe kuonyesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake.

Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni,

3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonyesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?”

4 Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaacha waende zao.

5 Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu zikishakuwa ndipo mje.”

6 Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa harufu mbaya kwenye pua za Daudi, wakaajiri askari wa miguu 20,000 wa Kiaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka pamoja na watu 1,000, na vile vile watu 12,000 kutoka Tobu.

7 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.

8 Waamoni wakatoka wakajipanga kwenye vita penye ingilio la lango la mji wao, wakati Waaramu wa Soba, wa Rehobu, watu wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi.

9 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; hivyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu.

10 Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni.

11 Yoabu akasema, “Ikiwa Waaramu wana nguvu kunizidi, basi itawabidi mje kuniokoa, lakini ikiwa Waamoni wana nguvu kuwazidi ninyi, basi nitakuja kuwaokoa.

12 Iweni hodari na tupigane kishujaa kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu.Bwanaatafanya lile lililo jema machoni pake.”

13 Basi Yoabu na vikosi vyake wakatangulia mbele kupigana na Waaramu, nao wakakimbia mbele yake.

14 Waamoni walipoona kwamba Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.

15 Baada ya Waaramu kuona wamekimbizwa na Israeli, wakajikusanya tena.

16 Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ng’ambo ya Mto Eufrati, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza.

17 Daudi alipoambiwa jambo hili, akakusanya Israeli yote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi.

18 Lakini wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akaua watu wao mia saba wapanda magari yao ya vita na askari wao wa miguu 40,000. Vile vile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko.

19 Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao.

Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/10-0b7a779cafb37ba3b50e9aac03bdf730.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 11

Daudi Na Bathsheba

1 Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme watokapo kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzunguka kwa jeshi mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.

2 Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Kutokea kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura,

3 naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Elamu, naye ni mke wa Uria, Mhiti?”

4 Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani kwake.

5 Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”

6 Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria, Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.

7 Uria alipofika, Daudi akamwuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje.

8 Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akaondoka kutoka kwenye jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme.

9 Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakutelemka kwenda nyumbani kwake.

10 Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakwenda nyumbani,” Daudi akamwuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukwenda nyumbani?”

11 Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani kwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo la namna hiyo!”

12 Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata.

13 Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakwenda nyumbani.

14 Asubuhi yake Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka.

15 Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele mahali ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.”

16 Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali ambapo alijua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana.

17 Wakati watu wa mjini walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa, zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, akafa.

18 Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita.

19 Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita,

20 hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani?

21 Ni nani aliyemwua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Ikiwa atakuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa.’ ”

22 Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema.

23 Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma mpaka kwenye ingilio la mji.

24 Ndipo wapiga upindi walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, mtumishi wako amekufa.”

25 Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”

26 Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea.

27 Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akamtaka aletwe nyumbani kwake, naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilokuwa amefanya Daudi lilimchukizaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/11-550dcfb2d5206b4650fa12bf5277d466.mp3?version_id=1627—

2 Samweli 12

Nathani Amkemea Daudi

1 Bwanaakamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwapo na watu wawili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini.

2 Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ng’ombe,

3 lakini yule maskini hakuwa na cho chote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.

4 “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri akaacha kuchukua mmoja wa kondoo au ng’ombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”

5 Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kamaBwanaaishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa!

6 Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”

7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyoBwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli.

8 Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba ya Israeli na Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi.

9 Kwa nini ulilidharau neno laBwanakwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimwua Uria, Mhiti kwa upanga na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimwua kwa upanga wa Waamoni.

10 Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria, Mhiti kuwa mkeo.’

11 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Kutoka katika nyumba yako mwenyewe nitaondokesha maafa juu yako, mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako wazi.

12 Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu wazi mbele ya Israeli yote.’ ”

13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi yaBwana.”

Nathani akamjibu, “Bwanaamekuondolea dhambi yako. Hutakufa.

14 Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui zaBwanakuonyesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”

15 Baada ya Nathani kurudi nyumbani kwake,Bwanaakampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua.

16 Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha.

17 Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula cho chote pamoja nao.

18 Kunako siku ya saba yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Wakati mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”

19 Daudi akaona kuwa watumishi wake wananong’onezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?”

Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”

20 Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Mungu akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani kwake kwa kutaka kwake, wakamwandalia chakula, naye akala.

21 Watumishi wake wakamwuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”

22 Akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa bado yungali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye?Bwanaaweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’

23 Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”

24 Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina lake Solomoni.Bwanaalimpenda Solomoni.

25 Kwa kuwaBwanaalimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidiakwa ajili yaBwana.

26 Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome ya kifalme.

27 Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji.

28 Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.”

29 Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka.

30 Akatwaa taji kutoka kwenye kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta ya dhahabu, nayo ilikuwa imewekewa vito vya thamani, nayo ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini,

31 akawatoa humo watu waliokuwa ndani yake akawaweka wafanye kazi wakitumia misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na Jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/12-8b167e4daffdc21a8b66d8a68f1b5333.mp3?version_id=1627—