1 Samweli 29

Akishi Amrudisha Daudi Huko Siklagi

1 Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.

2 Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi.

3 Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?”

Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lo lote kwake.”

4 Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe?

5 Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema:

“ ‘Sauli amewaua elfu zake,

naye Daudi makumi elfu yake’?”

6 Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Kama vileBwanaaishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lo lote kwako, lakini hao watawala hawakukubali.

7 Rudi na uende kwa amani; usifanye cho chote cha kuwakasirisha watawala wa Kifilisti.”

8 Daudi akauliza, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”

9 Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’

10 Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.”

11 Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1SA/29-dfc7a89459f785f2bd397fd9fea38ec9.mp3?version_id=1627—

1 Samweli 30

Daudi Aangamiza Waamaleki

1 Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto,

2 nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakuua ye yote, bali waliwachukua wakaenda zao.

3 Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao na binti zao wamechukuliwa mateka.

4 Hivyo Daudi na watu wake wakapiga yowe mpaka wakaishiwa na nguvu za kulia.

5 Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa, yaani Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.

6 Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana juu ya kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe na binti zake. Lakini Daudi akajitia nguvu katikaBwana, Mungu wake.

7 Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari, mwana wa Ahimeleki, “Niletee kile kisibau.” Abiathari akamletea,

8 naye Daudi akamwulizaBwana, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?”

Bwanaakajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”

9 Daudi pamoja na watu wake 600 wakafika kwenye Bonde la Besori, mahali ambapo wengine waliachwa nyuma,

10 kwa kuwa watu 200 walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu 400 wakaendelea kufuatia.

11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula,

12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula cho chote wala kunywa maji kwa siku tatu mchana na usiku.

13 Daudi akamwuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?”

Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita.

14 Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”

15 Daudi akamwuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?”

Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”

16 Akamwongoza Daudi mpaka mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka katika nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda.

17 Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna ye yote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana wanaume 400 waliopanda ngamia na kutoroka.

18 Daudi akarudisha kila kitu Waamaleki walichokuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili.

19 Hakuna cho chote kilichopotea kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine cho chote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu.

20 Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya wanyama wengine wa kufugwa, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”

21 Kisha Daudi akafika kwa wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu.

22 Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakwenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”

23 Daudi akajibu, “La hasha, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambachoBwanaametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu.

24 Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyekwenda vitani. Wote watashiriki sawa.”

25 Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.

26 Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka katika nyara za adui zaBwana.”

27 Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri;

28 kwa wale walioko Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa

29 na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni;

30 na kwa wale walioko Horma, Bori-Ashani, Athaki,

31 na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1SA/30-70ddc46f23f590e3c943c4e8f1909cba.mp3?version_id=1627—

1 Samweli 31

Sauli Ajiua

1 Basi Wafilisti wakapigana dhidi ya Israeli. Waisraeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, na wengi wakauawa kwenye Mlima wa Gilboa.

2 Wafilisti wakawasonga Sauli na wanawe kwa nguvu, na kuwaua wanawe Yonathani, Abinadabu na Malki-Shua.

3 Mapigano yakawa makali sana kumzunguka Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya.

4 Sauli akamwambia mchukua silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa jamaa wasiotahiriwa watakuja kunichoma na kunitendea vibaya.”

Lakini mchukua silaha wake aliogopa na hakuweza kufanya hivyo, basi Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia.

5 Mchukua silaha wake alipoona Sauli amekufa, naye pia akaangukia upanga wake akafa pamoja naye.

6 Basi Sauli, wanawe watatu, mchukua silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile.

7 Waisraeli waliokuwa kandokando ya bonde na wale waliokuwa ng’ambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaja na kumiliki humo.

8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, wakamkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka kwenye Mlima Gilboa.

9 Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao.

10 Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani.

11 Watu wa Yabeshi-Gileadi waliposikia kile Wafilisti walichomfanyia Sauli,

12 mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka kwenye ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, mahali ambapo waliiteketeza kwa moto.

13 Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1SA/31-5a13f618e2a33b51f5e785f2c130dd9c.mp3?version_id=1627—

Ruthu 1

Naomi Na Ruthu

1 Wakati Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi, akaondoka mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu.

2 Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu wakaishi huko.

3 Elimeleki mumewe Naomi akafa, Naomi akabaki na wanawe wawili.

4 Nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya miaka kumi,

5 Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili.

6 Aliposikia akiwa huko Moabu kwambaBwanaamewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakweze wakajiandaa kurudi nyumbani.

7 Yeye na wakweze wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda.

8 Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe zake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani kwa mama yake.Bwanana awatendee fadhili kama mlivyowatendea hao waliofariki pamoja na mimi.

9 Bwanana amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani kwa mume mwingine.”

Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa,

10 wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe nyumbani kwa watu wako.”

11 Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine, ambao wataweza kuwaoa ninyi?

12 Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana,

13 je, mngesubiri mpaka wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono waBwanaumekuwa kinyume nami!”

14 Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.

15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”

16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.

17 Pale utakapofia nami nitafia hapo na papo hapo nitazikwa.Bwanana aniadhibu vikali, kama kitu kingine cho chote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.”

18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.

19 Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”

20 Akawaambia, “Msiniite tena Naomi, niiteni Mara, kwa sababu Mwenyeziamenitendea mambo machungu sana.

21 Mimi niliondoka hali nimejaa, lakiniBwanaamenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi?Bwanaamenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”

22 Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabi mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/RUT/1-264bf0d79511b6af012519e44726e9f6.mp3?version_id=1627—

Ruthu 2

Ruthu Akutana Na Boazi

1 Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka katika ukoo wa Elimeleki, jina lake aliitwa Boazi.

2 Ruthu, Mmoabi, akamwambia Naomi, “Nitakwenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.”

Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.”

3 Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta anafanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alitoka kwenye ukoo wa Elimeleki.

4 Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “Bwanaawe nanyi!”

Nao wakamjibu, “Bwanaakubariki.”

5 Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, huyo mwanamwali ni wa nani?”

6 Msimamizi akamjibu, “Yeye ni yule Mmoabi aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi.

7 Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.”

8 Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa watumishi wangu wa kike.

9 Angalia shamba wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru hao wanaume wasikuguse. Wakati wo wote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka hao wanaume.”

10 Kwa ajili ya hili, akasujudu mpaka nchi, akamwambia, “Ni jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?”

11 Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wake alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu.

12 Bwanana akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi naBwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mbawani mwake.”

13 Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa watumishi wako wa kike.”

14 Wakati wa chakula Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya divai.”

Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza.

15 Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie.

16 Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwacheni ayaokote na msimkemee.”

17 Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja.

18 Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa.

19 Basi mkwewe akamwuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.”

Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake juu ya yule ambaye yeye alikuwa amefanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.”

20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, “Bwanaambariki! Hakuacha kuonyesha fadhili zake kwa walio hai na kwa hao waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kukomboa.”

21 Kisha Ruthu, Mmoabi, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu mpaka watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’ ”

22 Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wasichana wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.”

23 Kwa hivyo Ruthu akafuatana na watumishi wasichana wa Boazi kuokota mpaka mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/RUT/2-17e022638d26c6117275bc42e594aa6f.mp3?version_id=1627—

Ruthu 3

Ruthu Na Boazi Kwenye Sakafu Ya Kupuria

1 Kisha Naomi akamwambia mkwewe, “Binti yangu, je, nisingelikutafutia pumziko ambako utatunzika vyema?

2 Je, Boazi, ambaye umekuwa pamoja na watumishi wake wasichana, si jamaa yetu wa karibu? Usiku wa leo atakuwa anapepeta ngano kwenye sakafu ya kupuria.

3 Basi oga na ukajipake marashi, ujivalie nguo zako nzuri. Kisha uende kwenye sakafu ya kupuria, lakini angalia asijue kwamba upo pale mpaka atakapomaliza kula na kunywa.

4 Atakapokwenda kulala, angalia mahali atakapolala. Kisha uende ufunue miguu yake, ulale. Naye atakuambia utakalofanya.”

5 Ruthu akajibu, “Lo lote usemalo nitatenda.”

6 Basi akashuka mpaka kwenye sakafu ya kupuria, akafanya kila kitu mama mkwe wake alichomwambia kufanya.

7 Wakati Boazi alipomaliza kula na kunywa, naye alikuwa amejawa na furaha, alikwenda kulala mwisho wa lundo la nafaka. Ruthu akakaribia kimya kimya, akafunua miguu yake, akalala.

8 Usiku wa manane kitu kilimshtua Boazi, akajigeuza, akagundua yupo mwanamke amelala miguuni pake.

9 Akauliza, “Wewe ni nani?”

Akajibu, “Ni mimi Ruthu, mjakazi wako. Uitande nguo yako juu yangu, kwa sababu wewe ndiwe jamaa wa karibu wa kukomboa.”

10 Akamwambia, “Binti yangu, ubarikiwe naBwana. Wema huu wa sasa ni mkuu kushinda hata ule ulioonyesha mwanzoni. Hukuwakimbilia vijana, wakiwa matajiri au maskini.

11 Sasa, binti yangu, usiogope. Nitakufanyia yote uliyoomba. Kwa maana mji wote wa watu wangu wanakujua ya kwamba wewe ni mwanamke mwenye tabia nzuri.

12 Ingawa ni kweli kwamba mimi ndiye jamaa aliye karibu, lakini kuna mtu mwingine wa jamaa aliye karibu zaidi wa kukomboa kuliko mimi.

13 Wewe kaa hapa usiku huu, kisha asubuhi kama akikubali kukomboa, vyema na akomboe. La sivyo kama hayuko tayari, hakika kamaBwanaaishivyo nitafanya hivyo. Lala hapa mpaka asubuhi.”

14 Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake mpaka asubuhi, akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenzake, maana Boazi alisema, “Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika kwenye sakafu ya kupuria.”

15 Pia akamwambia, “Leta shela yako uliyoivaa, uitandaze.” Naye alipoitandaza, akamimina vipimo sita vya shayiri, akamtwika. Kisha Ruthu akarudi zake mjini.

16 Basi Ruthu alipofika kwa mama mkwe wake Naomi, akamwuliza, “Je, binti yangu, ilikuwaje huko?”

Ndipo akamwelezea kila kitu Boazi alichomfanyia.

17 Akaendelea kusema, “Amenipa shayiri vipimo sitaakisema, ‘Usiende kwa mama mkwe wako mikono mitupu.’ ”

18 Kisha Naomi akasema, “Subiri binti yangu, mpaka utakapojua kwamba hili jambo limekwendaje. Kwa sababu mtu huyu hatatulia mpaka akamilishe jambo hili leo.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/RUT/3-b9c23e28a75c7a73ab58630ff93fce42.mp3?version_id=1627—

Ruthu 4

Boazi Amwoa Ruthu

1 Boazi akakwea mpaka kwenye lango la mji, akaketi pale. Kisha muda si mrefu yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa rafiki yangu, karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi.

2 Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi.

3 Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki.

4 Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.”

Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”

5 Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua shamba kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabi, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”

6 Kuhusu hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kukomboa kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe komboa mwenyewe. Mimi sitaweza.”

7 (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.)

8 Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe nunua mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake.

9 Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni.

10 Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabi, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”

11 Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi.Bwanana amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao kwa pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrathi na uwe mashuhuri katika Bethlehemu.

12 Kupitia kwa watoto ambaoBwanaatakupa kutokana na huyu mwanamke kijana, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”

Wazao Wa Boazi

13 Basi Boazi akamwoa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake,Bwanaakamjalia Ruthu naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume.

14 Wanawake wakamwambia Naomi: “AhimidiweBwana, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote!

15 Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye aliyemzaa.”

16 Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake.

17 Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina lake Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.

18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi:

Peresi alimzaa Hesroni,

19 Hesroni akamzaa Ramu,

Ramu akamzaa Aminadabu,

20 Aminadabu akamzaa Nashoni,

Nashoni akamzaa Salmoni,

21 Salmoni akamzaa Boazi,

Boazi akamzaa Obedi,

22 Obedi akamzaa Yese,

na Yese akamzaa Daudi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/RUT/4-10184bfd1ceafc54f4e7046e3ecbeaab.mp3?version_id=1627—

Waamuzi 1

Israeli Wapigana Na Wakanaani Waliobaki

1 Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli wakamwulizaBwana, “Ni nani atakayetangulia kupanda mbele yetu kwa ajili ya kupigana na Wakanaani?”

2 Bwanaakajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia; nimewapa hiyo nchi mikononi mwao.”

3 Ndipo watu wa Yuda wakawaambia Wasimeoni ndugu zao, “Pandeni pamoja nasi katika nchi tuliyopewa, ili tupate kupigana na Wakanaani. Sisi pia tutakwenda pamoja nanyi katika sehemu yenu mliyopewa.” Basi Wasimeoni wakaenda pamoja nao.

4 Yuda aliposhambulia,Bwanaakawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, nao wakawaua watu 10,000 huko Bezeki.

5 Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafanya Wakanaani na Waperizi wakimbie.

6 Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuatia na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu.

7 Ndipo Adoni-Bezeki akasema, “Nimewatendea wafalme sabini kama nilivyotendewa na kuwalisha makombo ya chakula chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya, kama yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.

8 Watu wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto.

9 Baada ya hayo, watu wa Yuda wakatelemka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, yaani, Negebu na nchi chini ya vilima vya magharibi.

10 Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (ambayo hapo kwanza iliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.

11 Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (ambayo hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi.)

12 Kalebu akasema, “Mtu atakayewashinda Kiriath-Seferi nitamtoa binti yangu Aksa awe mkewe.”

13 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda, kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa akaolewa naye.

14 Aksa alipokuja kwa Othnieli, akamsisitiza amwombe Kalebu baba yake shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamwuliza, “Je, nikufanyie nini?”

15 Akajibu, “Naomba unifanyie upendeleo maalum. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo akampa chemchemi za juu na za chini.

16 Wazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Mose, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende, wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa Nyika ya Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi.

17 Basi watu wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao kushambulia Wakanaani waishio Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma.

18 Watu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka.

19 Bwanaalikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya chuma.

20 Kama vile Mose alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki.

21 Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wanaishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.

22 Basi nyumba ya Yosefu wakashambulia Betheli, nayeBwanaalikuwa pamoja nao.

23 Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo kwanza uliitwa Luzu),

24 wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuonyeshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.”

25 Hivyo akawaonyesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote.

26 Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambao ndio jina lake hadi leo.

27 Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na vijiji vyake, au watu wa Taanaki na vijiji vyake, au watu wa Dori na vijiji vyake, au watu wa Ibleamu na vijiji vyake, au watu wa Megido na vijiji vyake, lakini Wakanaani waliazimu kuishi katika nchi ile.

28 Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa.

29 Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi humo miongoni mwao.

30 Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, wala walioishi Nahaloli, ambao walibaki miongoni mwao; bali waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.

31 Wala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Ahlabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu

32 na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wale wenyeji wa nchi.

33 Wala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa.

34 Waamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, kwa maana hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare.

35 Waamori pia wakaendelea kukaa katika Mlima Heresi, katika Aiyaloni na Shaalbimu, lakini mkono wa nyumba ya Yosefu ukawalemea, nao wakashindwa hata wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa.

36 Mpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JDG/1-22c681990a665b316a7d299bf06d47a5.mp3?version_id=1627—

Waamuzi 2

Malaika Wa Bwana Huko Bokimu

1 Malaika waBwanaakakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja Agano langu nanyi.

2 Nanyi msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtazibomoa madhabahu zao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili?

3 Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke katikati yenu ila watakuwa miiba kwenu, nao miungu yao itakuwa tanzi kwenu.”

4 Malaika waBwanaalipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu.

5 Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtoleaBwanasadaka.

Kifo Cha Yoshua

6 Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao.

7 Watu wakamtumikiaBwanasiku zote za maisha za Yoshua na za wazee walioishi kuliko Yoshua, ambao walikuwa wameona mambo makuu ambayoBwanaalikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli.

8 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi waBwana, akafa akiwa na umri wa miaka 110.

9 Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresikatika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima Gaashi.

10 Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjuaBwana, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli.

11 Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni paBwanana kuwatumikia Mabaali.

12 WakamwachaBwana, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yanayowazunguka. WakamkasirishaBwana,

13 kwa sababu walimwacha yeye na kutumikia Baali na Maashtorethi.

14 Hivyo hasira yaBwanaikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao.

15 Po pote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono waBwanaulikuwa kinyume nao ili kuwashinda, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa.

16 NdipoBwanaakawainua waamuzi, ambao waliwaokoa katika mikono ya hao watu waliowashambulia.

17 Lakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka mara na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani, njia ya kutii amri zaBwana.

18 Kila maraBwanaalipowainulia mwamuzi,Bwanaalikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwaBwanaaliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha.

19 Lakini kila mara mwamuzi alipokufa, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu zaidi kuliko baba zao, wakiifuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi.

20 Kwa hiyoBwanaakawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja Agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza,

21 mimi nami sitafukuza taifa lo lote ambalo Yoshua aliliacha alipokufa.

22 Nitayatumia ili nipate kuwapima Israeli na kuona kama wataishika njia yaBwanana kuenenda katika hiyo kama baba zao walivyofanya.”

23 Bwanaalikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JDG/2-2c8fb430d3a9cedf1d755d1cac3f4efe.mp3?version_id=1627—

Waamuzi 3

Mataifa Yaliyobaki Katika Ile Nchi

1 Haya ndiyo mataifaBwanaaliyoyaacha ili kuwajaribu Waisraeli wote ambao hawakujua vita yo yote ya Kanaani

2 (alifanya hivi ili tu kuwafundisha wazao wa Waisraeli ambao hawakuwa wamejua vita hapo awali):

3 wafalme watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni, Wahivi waishio katika milima ya Lebanoni kuanzia Mlima wa Baal-Hermoni hadi Lebo-Hamathi.

4 Waliachwa ili kuwajaribu Waisraeli kuona kama wangetii amri zaBwana, alizokuwa amewapa baba zao kwa mkono wa Mose.

5 Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

6 Wakawaoa binti zao, nao wakawatoa binti zao waolewe na wana wa hayo mataifa, na kuitumikia miungu yao.

Othnieli

7 Waisraeli wakafanya maovu machoni paBwana, wakamsahauBwanaMungu wao na kutumikia Mabaali na Maashera.

8 Hasira yaBwanaikawaka dhidi ya Israeli, hivyo akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu-Naharaimuambaye Israeli walikuwa chini yake wakimtumikia kwa muda wa miaka minane.

9 WalipomliliaBwana, yeye akawainulia mwokozi, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, ambaye aliwaokoa.

10 Roho waBwanaakaja juu yake, hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, akaenda vitani.Bwanaakamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda.

11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arobaini, mpaka Othnieli mwana wa Kenazi alipokufa.

Ehudi

12 Waisraeli wakafanya yaliyo maovu mbele zaBwanatena, kwa kuwa walifanya maovu hayoBwanaakamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu dhidi ya Israeli.

13 Egloni akawataka Waamoni na Waamaleki waungane naye, akaja kuishambulia Israeli, nao wakatwaa Mji wa Mitende.

14 Waisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na minane.

15 Waisraeli wakamlilia tenaBwana, naye akawapa mwokozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera, Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi.

16 Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga wenye makali kuwili, urefu wake ni kama dhiraa moja, akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake kwenye paja lake la mkono wa kuume.

17 Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, ambaye alikuwa mtu mnene sana.

18 Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru aliwaruhusu waende zao.

19 Yeye mwenyewe akafuatana nao hadi kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwa ajili yako.”

Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.

20 Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kwenye kiti chake,

21 Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia na kuuchomeka tumboni mwa Mfalme Egloni kwa nguvu.

22 Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya panga.

23 Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu na kuifunga kwa funguo.

24 Baada ya kuondoka, watumishi wakaja na kukuta milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka amejipumzisha kwenye chumba cha ndani cha nyumba yake ya majira ya kiangazi.”

25 Wakangoja hata wakawa na fadhaa, basi alipokuwa hakufungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.

26 Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira.

27 Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakatelemka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.

28 Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwaBwanaamewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakatelemka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakuacha mtu ye yote kuvuka.

29 Wakati huo wakawaua Wamoabu watu waume wapatao 10,000 ambao wote walikuwa wenye nguvu na mashujaa; hakuna mtu ye yote aliyetoroka.

30 Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.

Shamgari

31 Baada ya Ehudi akaja Shamgari mwana wa Anathi, aliyewapiga Wafilisti 600 kwa fimbo iliyochongoka ya kuongozea ng’ombe. Naye pia akawaokoa Waisraeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JDG/3-c18a0782f94d8effb4cc5ff79b00e745.mp3?version_id=1627—