Ufunuo 1

Utangulizi Na Salamu

1 Ufunuo wa Yesu Kristo aliopewa na Mungu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake,

2 ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichoona, yaani, Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo.

3 Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na pia wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.

Salamu Kwa Makanisa Saba

4 Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia:

Neema na amani iwe kwenu kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja na kutoka kwa wale Roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi

5 na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni shahidi mwaminifu, aliye mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ambaye yeye ndiye mtawala wa wafalme wa dunia.

Kwake yeye anayetupenda na ambaye ametuweka huru kutoka katika dhambi zetu kwa damu yake,

6 akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba yake. Utukufu na uwezo vina yeye milele na milele! Amen.

7 Tazama! Anakuja na mawingu

na kila jicho litamwona,

hata wale waliomchoma mkuki;

na mataifa yote ulimwenguni

yataomboleza kwa sababu yake.

Naam, ndivyo itakavyokuwa! Amen.

8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

Maono Ya Kristo

9 Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Yesu na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu.

10 Nilikuwa katika Roho siku ya Bwana, nikasikia sauti kubwa kama ya tarumbeta nyuma yangu

11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makanisa saba, yaani: Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”

12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu,

13 katikati ya vile vinara vya taa, nikaona mtu kama Mwana wa Adamu, amevaa joho refu na mkanda wa dhahabu umefungwa kifuani mwake.

14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto.

15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba iliyosuguliwa sana, kama vile imesafishwa katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi.

16 Katika mkono wake wa kuume alishikilia nyota saba na kinywani mwake ulitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake kama jua kali linalong’aa kwa nguvu zake zote.

17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akaweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ni wa Kwanza na wa Mwisho.

18 Mimi ni yeye aliye hai, niliyekuwa nimekufa na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya.

20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/1-1b3e8e306581865c9d3e066dfca8cc01.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × two =