Ufunuo 4

Kiti Cha Enzi Kilichoko Mbinguni

1 Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango ulio wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo kwanza ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo panda huku nami nitakuonyesha yale ambayo hayana budi kutokea baada ya haya.”

2 Ghafula nilikuwa katika Roho, hapo mbele yangu kilikuwapo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu mmoja.

3 Yeye aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi.

4 Pia kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti ishirini na vinne na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne, waliovaa majoho meupe, wakiwa na taji za dhahabu vichwani mwao.

5 Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya hicho kiti cha enzi, palikuwa na taa saba zilizokuwa zinawaka. Hizi ndizo Roho sabaza Mungu.

6 Pia mbele ya hicho kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama jiwe lisilo na rangi yo yote ling’aalo sana.

Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma.

7 Huyo kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ng’ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.

8 Kila mmoja wa hawa viumbe wenye uhai wanne, alikuwa na mabawa sita na kujawa na macho pande zote, hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kusema:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

ni BWANA Mungu Mwenyezi,

aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

9 Kila mara viumbe hao wenye uhai wanne walipomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele,

10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Wao huziweka taji zao mbele ya hicho kiti cha enzi, wakisema:

11 “Bwana wetu na Mungu wetu,

wewe umestahili kupokea utukufu

na heshima na uweza,

kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,

na kwa mapenzi yako viliumbwa

na vimekuwako.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/4-937f7ca6d3e9708cbb1096b059c882bd.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × 2 =