Ufunuo 1

Utangulizi Na Salamu

1 Ufunuo wa Yesu Kristo aliopewa na Mungu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake,

2 ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichoona, yaani, Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo.

3 Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na pia wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.

Salamu Kwa Makanisa Saba

4 Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia:

Neema na amani iwe kwenu kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja na kutoka kwa wale Roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi

5 na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni shahidi mwaminifu, aliye mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ambaye yeye ndiye mtawala wa wafalme wa dunia.

Kwake yeye anayetupenda na ambaye ametuweka huru kutoka katika dhambi zetu kwa damu yake,

6 akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba yake. Utukufu na uwezo vina yeye milele na milele! Amen.

7 Tazama! Anakuja na mawingu

na kila jicho litamwona,

hata wale waliomchoma mkuki;

na mataifa yote ulimwenguni

yataomboleza kwa sababu yake.

Naam, ndivyo itakavyokuwa! Amen.

8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

Maono Ya Kristo

9 Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Yesu na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu.

10 Nilikuwa katika Roho siku ya Bwana, nikasikia sauti kubwa kama ya tarumbeta nyuma yangu

11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makanisa saba, yaani: Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”

12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu,

13 katikati ya vile vinara vya taa, nikaona mtu kama Mwana wa Adamu, amevaa joho refu na mkanda wa dhahabu umefungwa kifuani mwake.

14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto.

15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba iliyosuguliwa sana, kama vile imesafishwa katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi.

16 Katika mkono wake wa kuume alishikilia nyota saba na kinywani mwake ulitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake kama jua kali linalong’aa kwa nguvu zake zote.

17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akaweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ni wa Kwanza na wa Mwisho.

18 Mimi ni yeye aliye hai, niliyekuwa nimekufa na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya.

20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/1-1b3e8e306581865c9d3e066dfca8cc01.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 2

Kwa Kanisa Lililoko Efeso

1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:

“Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea katikati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu.

2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo.

3 Nami najua umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.

4 “Lakini nina neno juu yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza.

5 Kumbuka basi ni wapi ulikoanguka! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake.

6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami nayachukia.

7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye atakayeshinda, nitampa haki ya kula matunda ya mti wa uzima, ambao uko katika paradisoya Mungu.

Kwa Kanisa Lililoko Smirna

8 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka.

9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, wao ni sinagogi la Shetani.

10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia Shetani atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu, hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

11 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa na mauti ya pili.

Kwa Kanisa Lililoko Pergamo

12 “Kwa malaika wa Kanisa lililoko Pergamo andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na upanga wenye makali kuwili.

13 Ninajua unakoishi, ni kule ambako Shetani ana kiti chake cha enzi. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji wenu, ambako ndiko anakokaa Shetani.

14 “Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati.

15 Vivyo hivyo unao wale wayashikao mafundisho ya Wanikolai.

16 Basi tubuni! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.

17 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa yeye jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.

Kwa Kanisa Lililoko Thiatira

18 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika:

“Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana.

19 Nayajua matendo yako, upendo wako, imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.

20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu.

21 Nimempa muda ili atubie uasherati wake, lakini hataki.

22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, nami nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake.

23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia za watu na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.

24 Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo wengine wanayoyaita mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wo wote juu yenu):

25 Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja.

26 “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa:

27 “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma,

atawavunja vipande vipande

kama chombo cha udongo’:

kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu.

28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi.

29 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/2-3da260843ae4c59492025e2d9db423ce.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 3

Kwa Kanisa Lililoko Sardi

1 “Kwa malaika wa Kanisa lililoko Sardi andika:

# “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na zile Roho sabaza Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa.

2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu.

3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwivi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.

4 “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili.

5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao, nami sitafuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.

6 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

Kwa Kanisa Lililoko Filadelfia

7 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua.

8 Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu.

9 Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, waje wapige magoti miguuni pako, nao watatambua ya kwamba nimekupenda.

10 Kwa kuwa umelishika neno la saburi yangu nitakulinda hata utoke katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote ili kuwajaribu wote wakaao duniani.

11 “Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akaichukua taji yako.

12 Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika Hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya.

13 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.

Kwa Kanisa Lililoko Laodikia

14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa baridi au moto.

16 Hivyo kwa kuwa u uvuguvugu, kwamba wewe si baridi wala si moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu.

17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu cho chote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi.

18 Kwa hiyo nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri na mavazi meupe ili uyavae, upate kuficha aibu ya uchi wako na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.

19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.

20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu ye yote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.

21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/3-47298f51be8a257e39d9a63c209e5019.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 4

Kiti Cha Enzi Kilichoko Mbinguni

1 Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango ulio wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo kwanza ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo panda huku nami nitakuonyesha yale ambayo hayana budi kutokea baada ya haya.”

2 Ghafula nilikuwa katika Roho, hapo mbele yangu kilikuwapo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu mmoja.

3 Yeye aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi.

4 Pia kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti ishirini na vinne na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne, waliovaa majoho meupe, wakiwa na taji za dhahabu vichwani mwao.

5 Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya hicho kiti cha enzi, palikuwa na taa saba zilizokuwa zinawaka. Hizi ndizo Roho sabaza Mungu.

6 Pia mbele ya hicho kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama jiwe lisilo na rangi yo yote ling’aalo sana.

Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma.

7 Huyo kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ng’ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.

8 Kila mmoja wa hawa viumbe wenye uhai wanne, alikuwa na mabawa sita na kujawa na macho pande zote, hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kusema:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

ni BWANA Mungu Mwenyezi,

aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

9 Kila mara viumbe hao wenye uhai wanne walipomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele,

10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Wao huziweka taji zao mbele ya hicho kiti cha enzi, wakisema:

11 “Bwana wetu na Mungu wetu,

wewe umestahili kupokea utukufu

na heshima na uweza,

kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,

na kwa mapenzi yako viliumbwa

na vimekuwako.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/4-937f7ca6d3e9708cbb1096b059c882bd.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 5

Kitabu Na Mwana-Kondoo

1 Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na upande wa nyuma kikiwa kimefungwa kwa lakiri saba.

2 Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua hicho kitabu?”

3 Lakini hapakuwa na ye yote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu wala hata kutazama ndani yake.

4 Nikalia sana sana kwa sababu hakuonekana ye yote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake.

5 Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja hizo lakiri zake saba.”

6 Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho sabaza Mungu zilizotumwa duniani pote.

7 Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi.

8 Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.

9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

“Wewe unastahili kukitwaa kitabu

na kuzivunja lakiri zake,

kwa sababu ulichinjwa

na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu

kutoka katika kila kabila, kila lugha,

kila jamaa na kila taifa.

10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani

wa kumtumikia Mungu wetu,

nao watatawala duniani.”

11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne, idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu.

12 Nao wakiimba kwa sauti kuu, wakisema:

“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,

kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu

na heshima na utukufu na sifa!”

13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:

“Sifa na heshima na utukufu na uweza

ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi

na kwa Mwana-Kondoo,

milele na milele!”

14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/5-959fdf8919d949a4dcb65436c8dcb771.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 6

Mwana-Kondoo Avunja Lakiri Saba

1 Kisha nikaangalia wakati Mwana-Kondoo akivunja ile lakiri ya kwanza miongoni mwa zile saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wenye uhai wanne akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!”

2 Nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akishinda, tena apate kushinda.

3 Alipoivunja ile lakiri ya pili, nikamsikia yule kiumbe mwenye uhai wa pili akisema, “Njoo!”

4 Ndipo akatokea farasi mwingine wa rangi nyekundu. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.

5 Alipoivunja ile lakiri ya tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama na mbele yangu alikuwepo farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake.

6 Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimojacha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja. Vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua wa siku moja. Lakini usiharibu mafuta ya zeituni wala divai!”

7 Alipovunja ile lakiri ya nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!”

8 Nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda huyo farasi aliitwa Mauti, naye Kuzimualikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu, nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.

9 Alipoivunja ile lakiri ya tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya Neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza.

10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, “Hata lini, Ee Bwana Mwenyezi, uliye Mtakatifu na Mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi juu ya watu waishio duniani kwa ajili ya damu yetu?”

11 Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, mpaka idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.

12 Nikaangalia, naye alipokuwa akiivunja ile lakiri ya sita, pakatokea tetemeko kuu la nchi na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, mwezi wote ukawa mwekundu kama damu.

13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali.

14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima.

16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo!

17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/6-f94a7c1e47564abb8380bde59e06230d.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 7

Waisraeli 144,000 Watiwa Muhuri

1 Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili kwamba pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wo wote.

2 Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka maawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema,

3 “Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye vipaji vya nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”

4 Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: yaani 144,000 kutoka katika makabila yote ya Israeli.

5 Kutoka kabila la Yuda 12,000,

kabila la Reubeni 12,000,

kabila la Gadi 12,000,

6 kabila la Asheri 12,000,

kabila la Naftali 12,000,

kabila la Manase 12,000,

7 kabila la Simeoni 12,000,

kabila la Lawi 12,000,

kabila la Isakari 12,000,

8 kabila la Zabuloni 12,000,

kabila la Yosefu 12,000,

na kabila la Benyamini 12,000.

Umati Mkubwa Wa Watu Kutoka Mataifa Yote

9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna ye yote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao.

10 Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema:

“Wokovu una Mungu wetu,

yeye aketiye kwenye kiti cha enzi

na Mwana-Kondoo!”

11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu,

12 wakisema:

“Amen!

Sifa na utukufu

na hekima na shukrani na heshima

na uweza na nguvu

viwe kwa Mungu wetu milele na milele.

Amen!”

13 Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

14 Nikamjibu, “Bwana, wewe wajua.”

Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.

15 Kwa hiyo,

“Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu

na kumtumikia usiku na mchana

katika Hekalu lake;

naye aketiye katika kile kiti cha enzi

atakaa pamoja nao na kuwalinda.

16 Kamwe hawataona njaa

wala kiu tena.

Jua halitawapiga

wala joto lo lote liunguzalo.

17 Kwa maana Mwana-Kondoo

aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi

atakuwa Mchungaji wao;

naye atawaongoza kwenda

kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.

Naye Mungu atafuta kila chozi

kutoka katika macho yao.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/7-8b7013eb05bcff29f19be4256b6999e8.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 8

Lakiri Ya Saba Na Chetezo Cha Dhahabu

1 Mwana-Kondoo alipoivunja ile lakiri ya saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.

2 Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.

3 Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya Watakatifu wote, juu ya ile madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele ya kile kiti cha enzi.

4 Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika.

5 Kisha yule malaika akachukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwenye ile madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi, ngurumo, umeme wa radi na tetemeko la nchi.

TARUMBETA SABA

Tarumbeta Ya Kwanza

6 Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.

7 Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea na majani yote mabichi yakateketea.

Tarumbeta Ya Pili

8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu,

9 theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa.

Tarumbeta Ya Tatu

10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji.

11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

Tarumbeta Ya Nne

12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota, zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.

13 Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/8-15812af24b0916e4120c5c42cd1394ab.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 9

Tarumbeta Ya Tano

1 Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo lisilo na mwisho.

2 Alipolifungua hilo Shimo lisilo na mwisho, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo shimo lisilokuwa na mwisho.

3 Ndipo katika ule moshi wakatoka nzige wakaenda juu ya nchi, nao wakapewa nguvu kama zile za nge wa duniani.

4 Wakaambiwa wasidhuru majani ya nchi, wala mmea wala mti wo wote, bali wawadhuru tu wale watu ambao hawana muhuri wa Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao.

5 Wakaruhusiwa kuwatesa kwa muda wa miezi mitano, lakini wasiwaue. Uchungu wa kuuma kwao ulikuwa kama ule wa mtu aumwapo na nge.

6 Katika siku hizo watu watatafuta kifo lakini hawatakiona, watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia.

7 Wale nzige walikuwa na umbo kama la farasi waliotayarishwa kwa ajili ya vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji za dhahabu na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.

8 Walikuwa na nywele kama za wanawake na meno yao yalikuwa kama ya simba.

9 Walikuwa na dirii kama za chuma na sauti za mabawa yao zilikuwa kama ngurumo za magari mengi ya farasi wanaokimbilia vitani.

10 Walikuwa na mikia yenye miiba ya kuumia kama nge. Nguvu yao ya kutesa watu kwa huo muda wa miezi mitano ilikuwa katika hiyo mikia yao.

11 Walikuwa na mfalme wao, ambaye ni malaika wa lile Shimo lisilo na mwisho, ambaye jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani ni Apolioni.

12 Ole ya kwanza imepita, bado nyingine mbili zinakuja.

Tarumbeta Ya Sita

13 Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele za Mungu.

14 Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Eufrati.”

15 Basi wale malaika wanne wakafunguliwa ambao walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo na siku hiyo na mwezi huo na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu.

16 Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa 200,000,000. Nilisikia idadi yao.

17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika maono yangu: Wapanda farasi walivaa dirii vifuani zenye rangi ya moto na yakuti samawi na kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vichwa vya simba. Moto, moshi na kiberiti vilitoka vinywani mwao.

18 Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa maafa hayo matatu, yaani, huo moto, moshi na kiberiti, vilivyotoka kwenye vinywa vya hao farasi.

19 Nguvu za hao farasi zilikuwa katika vinywa vyao na kwenye mikia yao, kwa sababu mikia yao ilikuwa kama nyoka, yenye vichwa ambayo waliitumia kudhuru.

20 Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea.

21 Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/9-53de142a7e350b6300b149724819fa7b.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 10

Malaika Mwenye Kitabu Kidogo

1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake uling’aa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.

2 Mkononi mwake alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu.

3 Naye akapiga kelele kwa sauti kuu kama simba anayenguruma. Alipopiga kelele, zile radi saba zikatoa ngurumo zake.

4 Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.”

5 Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni.

6 Naye akaapa kwa Jina la Mungu aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena!

7 Lakini katika siku zile ambazo huyo malaika wa saba atakapokaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”

8 Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”

9 Basi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.”

10 Hivyo nikakichukua kile kitabu kidogo kutoka mkononi mwa yule malaika nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu.

11 Kisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/10-78b78836d7a2b6fcffe1a2c3f63deed8.mp3?version_id=1627—