Yoshua 17

Mgawo Wa Nusu Nyingine Ya Manase Upande Wa Magharibi

1 Huu ndio mgawo wa kabila la Manase kama mzaliwa wa kwanza wa Yosefu, yaani kwa ajili ya Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase. Makiri alikuwa baba wa Wagileadi, ambao walipokea Gileadi na Bashani kwa sababu Wamakiri walikuwa askari wakuu.

2 Kwa hiyo mgawo huu ulikuwa kwa ajili ya watu wa Manase waliokuwa wamebaki, ambao ni koo za Abiezeri, Heleki, Asrieli, Shekemu, Heferi na Shemida. Hawa ndio wanaume wengine wa uzao wa Manase mwana wa Yosefu kwa koo zao.

3 Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila binti tu, ambao majina yao ni Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.

4 Wakawaendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Bwanaalimwagiza Mose atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo laBwana.

5 Fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani,

6 kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa ndugu zao. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wale wazao wengine wa Manase waliobaki.

7 Nchi ya Manase ilienea kuanzia Asheri hadi Mikmeta mashariki mwa Shekemu. Mpaka ulielekea upande wa kusini kutoka pale ukajumuisha watu wanaoishi En-Tapua.

8 (Nchi ya Tapua ilikuwa mali ya Manase, lakini Tapua yenyewe iliyo mpakani mwa nchi ya Manase ilikuwa ya Waefraimu.)

9 Kisha mpaka uliendelea kuelekea kusini hadi Kijito cha Kana. Kulikuwepo miji ya Efraimu iliyokuwa miongoni mwa miji ya Manase, lakini mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa kile kijito na kuishia kwenye baharia.

10 Nchi ya kusini mwa kile kijito ilikuwa ya Efraimu, na ile iliyokuwa upande wa kaskazini mwa kile kijito ilikuwa ya Manase. Nchi ya Manase ilienea hadi baharini na ikapakana na Asheri upande wa kaskazini, na kupakana na nchi ya Isakari upande wa mashariki.

11 Miji ifuatayo katika nchi ya Isakari na Asheri ilipewa Manase: Beth-Shani, Ibleamu na watu wa Dori, Endori, Taanaki na Megido, pamoja na vijiji vyote vinavyohusika na miji hiyo.

12 Lakini Wamanase hawakuweza kuimiliki miji hii, kwa kuwa Wakanaani waliendelea kuishi katika maeneo hayo.

13 Hata hivyo, Waisraeli walivyoendelea kupata nguvu waliwatumikisha Wakanaani na kuwatia katika kazi ngumu za kulazimisha, lakini hawakuwafukuza kutoka katika ile nchi.

Kabila La Yosefu Lakataa

14 Kabila la Yosefu wakamwambia Yoshua, “Kwa nini umetupa sisi mgawo mmoja tu na sehemu moja tu kuwa urithi? Sisi tu watu wengi sana, nayeBwanaametubariki kwa wingi.”

15 Yoshua akajibu, “Kama ninyi ni wengi sana, na kama nchi ya vilima ya Efraimu ni ndogo sana kwenu, pandeni msituni mkafyeke eneo kwa ajili yenu huko kwenye nchi ya Waperizi na Warefai.”

16 Kabila la Yosefu wakajibu, “Hiyo nchi ya vilima haitutoshi, nao Wakanaani wote wanaoishi katika tambarare wanayo magari ya chuma, wote wa Beth-Shani na miji yake, na wale walio katika Bonde la Yezreeli.”

17 Lakini Yoshua akanena na nyumba ya Yosefu, yaani Efraimu na Manase: “Ninyi ni wengi sana na wenye nguvu sana. Hamtakuwa na mgawo mmoja tu,

18 bali pia nchi hii ya kilima yenye msitu. Ifyekeni, nayo mipaka yake itakuwa yenu umbali mtakaoweza kufika. Ingawa Wakanaani wana magari ya chuma, nao wana nguvu, mwaweza kuwafukuza humo.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOS/17-08fd184471b7bfdaf688e5db5159549f.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty + thirteen =