Miji Ya Makimbilio
1 NdipoBwanaakamwambia Yoshua,
2 “Waambie Waisraeli, watenge miji ya kukimbilia, kama nilivyokuamuru kupitia Mose,
3 ili mtu ye yote atakayemwua mtu kwa bahati mbaya na pasipokukusudia aweze kukimbilia huko na kujiepusha na mlipiza kisasi cha damu.
4 “Anapokimbilia mojawapo ya miji hii, atasimama kwenye maingilio ya lango la mji na kueleza wazee wa mji kuhusu shauri lake. Kisha watampokea katika mji wao na kumpa mahali pa kuishi nao.
5 Kama mlipiza kisasi cha damu akimfuatilia, wazee wa mji kamwe wasimkabidhi yule mshtakiwa, kwa sababu alimwua jirani yake bila kukusudia, na bila kuwa na nia ya kudhuru.
6 Huyu aliyeua atakaa kwenye mji huo mpaka awe amesimama kukabili mashtaka yake mbele ya kusanyiko na mpaka Kuhani Mkuu anayehudumu kwa wakati huo atakapokufa. Ndipo atakapoweza kurudi nyumbani kwake katika mji ambao aliukimbia.”
7 Basi wakatenga Kedeshi katika Galilaya kwenye nchi ya vilima ya Naftali, Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-Arba (yaani Hebroni) kwenye nchi ya vilima ya Yuda.
8 Katika upande wa mashariki ya Yordani ya Yeriko wakatenga Bezeri katika jangwa katika uwanda wa juu katika kabila la Reubeni, Ramoth katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani huko Bashani katika kabila la Manase.
9 Mwisraeli ye yote au mgeni ye yote aishiye miongoni mwao aliyemwua mtu kwa bahati mbaya, angeweza kukimbilia katika miji hiyo iliyotengwa na asiuawe na mwenye kulipiza kisasi cha damu kabla hajasimama kukabili mashtaka mbele ya kusanyiko.
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOS/20-c7cceb20f5e46f9c32b9499b2e677e89.mp3?version_id=1627—