Yoshua 10

Jua Linasimama

1 Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, tena ya kwamba walikuwa wakiishi karibu yao.

2 Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmojawapo ya miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, nao watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita.

3 Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni.

4 Akawaambia, “Njoni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mapatano ya amani na Yoshua pamoja na Waisraeli.”

5 Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia.

6 Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwaache watumishi wako. Panda haraka uje kwetu kutuokoa! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao kwenye nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.”

7 Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo watu wote mashujaa wa vita.

8 Bwanaakamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna ye yote atakayeweza kushindana nawe.”

9 Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, Yoshua akawashambulia kwa ghafula.

10 Bwanaakawatia hofu ya ghafula na kuwafadhaisha mbele ya Waisraeli, nao wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Israeli wakawafukuza kuelekea njia iendayo Beth-Horoni wakiwaua mpaka kufikia njia iendayo Azeka hadi Makeda.

11 Walipokuwa wakikimbia mbele ya Israeli kwenye barabara itelemkayo kutoka Beth-Horoni hadi Azeka,Bwanaakawavumishia mawe makubwa ya mvua kutoka mbinguni, nao wengi wao wakauawa na hayo mawe kuliko wale waliouawa kwa upanga wa Waisraeli.

12 Katika siku ile ambayoBwanaaliwatia Waamori mikononi mwa Israeli, Yoshua akasema naBwanambele ya Waisraeli:

“Wewe jua, simama kimya juu ya Gibeoni,

wewe mwezi, simama

katika Bonde la Aiyaloni.”

13 Hivyo jua likasimama kimya,

nao mwezi ukatulia,

hadi Waisraeli walipokwisha

kujipatilizia kwa adui zao,

kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari.

Jua likasimama katikati ya mbingu kimya, likachelewa kuzama muda wa siku moja nzima.

14 Haijakuwepo siku nyingine mfano wa hiyo kabla au baada, siku ambayoBwanaalimsikiliza mwanadamu. HakikaBwanaalikuwa akiwapigania Israeli.

15 Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote.

Wafalme Watano Wa Waamori Wauawa

16 Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda.

17 Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda,

18 akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mdomo wa hilo pango, tena wekeni walinzi wa kulilinda.

19 Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni walio nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwaBwanaMungu wenu amewatia mikononi mwenu.”

20 Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza kabisa karibu wote, lakini wachache waliosalia ndio waliofika kwenye miji yao yenye maboma.

21 Jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda, hakuna ye yote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.

22 Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.”

23 Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni.

24 Baada ya kuwaleta kwa Yoshua, akawaita watu wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita waliokwenda pamoja naye, “Njoni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakawakanyaga shingoni.

25 Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Iweni hodari na wenye moyo mkuu. Hili ndiloBwanaatakalowatendea adui zenu wote mnaokwenda kupigana nao.”

26 Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wananing’inia juu ya ile miti hadi jioni.

27 Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru wawashushe kutoka kwenye ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Kwenye mdomo wa lile pango wakaweka mawe makubwa, ambayo yapo hadi leo.

28 Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamwua mfalme na kumwangamiza kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza mtu ye yote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.

Israeli Yaangamiza Miji Ya Kusini

29 Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli wote mpaka mji wa Libna na kuushambulia.

30 Bwanapia akautia mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu ye yote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.

31 Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli wote, wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.

32 Bwanaakautia Lakishi mikononi mwa Israeli, Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilicho ndani yake kwa upanga, kama vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna.

33 Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda yeye pamoja na jeshi lake, hadi alipowaangamiza wote.

34 Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli wote, wakajipanga dhidi yake na kuushambulia.

35 Wakauteka mji siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.

36 Kisha Yoshua akapanda kutoka Egloni kwenda Hebroni akiwa pamoja na Israeli wote na kuushambulia.

37 Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza huko mtu ye yote kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.

38 Ndipo Yoshua na Israeli wote wakageuka na kuushambulia Debiri.

39 Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza huko mtu ye yote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao.

40 Hivyo Yoshua akashinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, Negebu, sehemu ya magharibi chini ya vilima, matelemko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza humo mtu ye yote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vileBwana, Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru.

41 Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni.

42 Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababuBwana, Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli.

43 Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli wote kwenye kambi huko Gilgali.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOS/10-68bdea27562199370265f495a92a890d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × 1 =