Yoshua 8

Mji Wa Ai Waangamizwa

1 NdipoBwanaakamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo, chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako huyo mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake.

2 Utafanya Ai na mfalme wake kama ulivyofanya kwa mji wa Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kuchukua mateka yake na mifugo yake, kwa ajili yenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”

3 Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua watu mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku,

4 akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote iweni macho.

5 Mimi na watu walio pamoja nami, tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutawakimbia.

6 Watatufuatilia mpaka tutakapokuwa tumewavuta waende mbali na mji, kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia,

7 ninyi inawapasa mwinuke mtoke huko mafichoni na kuuteka mji.BwanaMungu wenu atautia mkononi mwenu.

8 Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vileBwanaalivyoamuru. Angalieni, nimewaagiza.”

9 Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.

10 Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku ya pili, akawakutanisha watu wake, yeye na viongozi wa Israeli wakawa mbele ya watu kwenda Ai.

11 Watu wote wa vita waliokuwa pamoja naye walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini ya Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji.

12 Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka mafichoni kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji.

13 Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wamejificha wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.

14 Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na watu wote wa mji wakatoka nje kwa haraka asubuhi na mapema, ili kukutana na Israeli katika vita mahali fulani panapotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji.

15 Yoshua na Israeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, wakakimbia kuelekea jangwani.

16 Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji.

17 Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.

18 NdipoBwanaakamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai.

19 Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mafichoni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbilia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.

20 Watu wa Ai wakaangalia nyuma wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani, lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wo wote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wanawakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili hao waliokuwa wakiwafuatia.

21 Basi Yoshua na Israeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kutoka kwenye mji, wakawageukia watu wa Ai na kuwashambulia.

22 Wale waviziaji nao wakatoka nje ya mji dhidi yao kuwashambulia kwa nyuma, hivyo watu wa Ai wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia ye yote aliyenusurika wala aliyetoroka.

23 Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.

24 Waisraeli walipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini.

25 Watu kumi na mbili elfu, waume kwa wake, waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai.

26 Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa ameinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi huko Ai.

27 Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vileBwanaalivyokuwa amemwagiza Yoshua.

28 Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa rundo la kudumu la magofu, mahali pa ukiwa hadi leo.

29 Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo mpaka jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakarundika mawe makubwa mengi juu yake, ambayo yamesalia huko mpaka leo.

Agano Linafanywa Upya Katika Mlima Ebali

30 Kisha Yoshua akajenga madhabahu yaBwana, Mungu wa Israeli, katika Mlima wa Ebali,

31 kama Mose mtumishi waBwanaalivyokuwa amewaamuru Waisraeli. Akaijenga sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Mose: madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna chombo cha chuma kilichotumika. Hapo juu yake wakamtoleaBwanasadaka za kuteketezwa na kutoa sadaka za amani.

32 Huko, mbele ya Waisraeli wote, Yoshua akanakili juu ya hayo mawe sheria ya Mose, aliyokuwa ameiandika.

33 Israeli wote, wageni na wazawa sawasawa, wazee wao, maafisa wao na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za hilo Sanduku la Agano laBwana, wakiwaelekea wale waliokuwa wamelichukua, yaani makuhani, ambao ni Walawi. Nusu ya watu walisimama mbele ya mlima wa Gerizimu na nusu yao walisimama mbele ya mlima wa Ebali, kama vile Mose mtumishi waBwanaalivyokuwa amewaagiza hapo mwanzo alipowapa maagizo ili kuwabariki watu wa Israeli.

34 Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati.

35 Hakuna neno lo lote katika yale yote ambayo Mose alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakulisomea kusanyiko lote la Israeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOS/8-888fc29b36b2726d2a6d12efa3c361db.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 + three =