1 Mambo ya Nyakati 14

Nyumba Ya Daudi Na Jamaa Yake

1 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akapeleka wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mierezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme.

2 Naye Daudi akatambua kwambaBwanaamemthibitisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya watu wake Israeli.

3 Huko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana na binti wengi.

4 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko; Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni,

5 Ibhari, Elishua, Elpeleti,

6 Noga, Nefegi, Yafia,

7 Elishama, Beeliada na Elifeleti.

Daudi Awashinda Wafilisti

8 Wakati Wafilisti waliposikia kwamba Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme katika Israeli yote, wakaondoka na jeshi lao lote ili kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao.

9 Basi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai,

10 Hivyo Daudi akamwuliza Mungu: “Je, niende na kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

Bwanaakamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.”

11 Hivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea mpaka Baal-Perasimu, akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yafurikayo, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu.

12 Wafilisti walikuwa wameacha miungu yao huko, Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto.

13 Kwa mara nyingine tena Wafilisti wakavamia lile bonde,

14 hivyo Daudi akamwuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwapandie moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi.

15 Mara usikiapo sauti ya kwenda juu ya hiyo miti ya miforosadi, hapo ndipo utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonyesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.”

16 Kwa hiyo Daudi akafanya sawasawa na alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri.

17 Hivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, nayeBwanaakayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CH/14-dc122d5963e0c4dd89dc7fe55c35c6c2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

18 − nine =