1 Petro 3

Mafundisho Kwa Wake Na Waume

1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama wako wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno,

2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu.

3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi.

4 Badala yake kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa ndani, kwa uzuri usioharibika, wa roho ya upole na utulivu, ambako ni kwa thamani sana machoni pa Mungu.

5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao,

6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema na bila kuogopa jambo lo lote.

7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha thamani cha uzima, ili kusiwepo na cho chote cha kuzuia maombi yenu.

Kuteseka Kwa Kutenda Mema

8 Hatimaye, ninyi nyote iweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, wasikitivu na wanyenyekevu.

9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.

10 Kwa maana,

“Ye yote apendaye uzima

na kuona siku njema,

basi auzuie ulimi wake usinene mabaya

na midomo yake isiseme hila.

11 Mtu huyo lazima aache ubaya, akatende mema;

atafute amani na kuifuatilia sana.

12 Kwa maana macho ya Bwana

huwaelekea wenye haki,

na masikio yake

husikiliza maombi yao,

bali uso wa Bwana ni dhidi yao

watendao maovu.”

Kuvumilia Mateso

13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye bidii katika kutenda mema?

14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao wala msiwe na wasiwasi.”

15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu ye yote atakayewauliza kuhusu tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima,

16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo, waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.

18 Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho,

19 ambayo kwa hiyo alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni.

20 Roho hizo ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Noa, wakati wa kujenga safina, ambako watu wachache tu, yaani, watu wanane waliokolewa wasiangamie kwa gharika.

21 Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia, si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo,

22 ambaye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu: pamoja na malaika, mamlaka na nguvu zote vikiwa vimetiishwa chini yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/3-98b8757cacb1561b46c7e02a2255272a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

17 − three =