1 Wafalme 2

Maagizo Ya Daudi Kwa Solomoni

1 Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.

2 Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume,

3 shika lileBwanaMungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na po pote uendako,

4 ili kwambaBwanaaweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’

5 “Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake.

6 Shughulika naye kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani.

7 “Lakini uwaonyeshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu.

8 “Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, ambaye alinilaani kwa laana kali siku niliyokwenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwaBwana: ‘Sitakuua kwa upanga!’

9 Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.”

10 Kisha Daudi akapumzika pamoja na baba zake naye akazikwa katika Mji wa Daudi.

11 Alikuwa ametawala juu ya Israeli miaka arobaini, miaka saba huko Hebroni na miaka thelathini na mitatu katika Yerusalemu.

12 Kwa hiyo Solomoni akaketi katika kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana.

Kiti Cha Ufalme Cha Solomoni Chaimarishwa

13 Basi Adonia, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamwuliza, “Je, umekuja kwa amani?”

Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.”

14 Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.”

Akajibu, “Waweza kulisema.”

15 Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, ufalme umekwenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwaBwana.

16 Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.”

Bathsheba akasema, “Waweza kuliomba.”

17 Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Solomoni, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.”

18 Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.”

19 Bathsheba alipokwenda kwa Mfalme Solomoni kuzungumza naye kwa ajili ya Adonia, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akaketi mkono wake wa kuume.

20 Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.”

Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.”

21 Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adonia.”

22 Mfalme Solomoni akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi, Mshunami, kwa ajili ya Adonia? Ungeweza pia kuomba ufalme kwa ajili yake, hata hivyo, yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, pia kuhani Abiathari na Yoabu mwana wa Seruya wapo upande wake!”

23 Mfalme Solomoni akaapa kwaBwana, akasema: “Mungu na aniulie mbali, tena bila huruma, ikiwa Adonia hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili!

24 Basi sasa, hakika kamaBwanaaishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu naye amenipatia ukoo wa kifalme kama alivyoahidi, Adonia atauawa leo!”

25 Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adonia akafa.

26 Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku laBwanaMwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.”

27 Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani waBwana, akilitimiza neno laBwanaalilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.

28 Habari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adonia, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema laBwanana kushika pembe za madhabahu.

29 Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema laBwananaye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamwue!”

30 Ndipo Benaya akaingia kwenye hema laBwanana kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ”

Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.”

Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”

31 Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Mwue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga.

32 Bwanaatamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye.

33 Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani yaBwanamilele.”

34 Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumwua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa.

35 Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.

36 Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine po pote.

37 Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”

38 Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.

39 Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.”

40 Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.

41 Solomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi,

42 mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwaBwanana kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine po pote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’

43 Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwaBwanana kutii amri niliyokupa?”

44 Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. SasaBwanaatakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda.

45 Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele zaBwanamilele.”

46 Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumwua.

Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/2-04b04cb74127ecd57d457455875f8458.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one × one =