1 Wafalme 4

Maafisa Wa Solomoni Na Watawala

1 Basi Mfalme Solomoni akatawala Israeli yote.

2 Hawa ndio waliokuwa maafisa wake wakuu:

Kuhani: Azaria mwana wa Sadoki;

3 Elihorefu na Ahiya, wana wa Shisha: waandishi;

Yehoshafati mwana wa Ahiludi: karani;

4 Benaya mwana wa Yehoyada: jemadari mkuu wa jeshi;

Sadoki na Abiathari: makuhani;

5 Azaria mwana wa Nathani: kiongozi wa maafisa wa wilaya;

Zabudi mwana wa Nathani: kuhani na mshauri binafsi wa mfalme;

6 Ahishari: msimamizi wa jumba la kifalme;

Adoniramu mwana wa Abda: msimamizi wa kazi za kulazimisha.

7 Pia Solomoni alikuwa na watawala kumi na wawili wa wilaya katika Israeli yote, walioleta mahitaji kwa mfalme na kwa watu wa nyumbani kwa mfalme. Kila mmoja alitoa chakula kwa mwezi mmoja katika mwaka.

8 Majina yao ni haya:

Ben-Huri: katika nchi ya vilima ya Efraimu;

9 Ben-Dekeri: katika Makasi, Shaalbimu, Beth-Shemeshi na Elon-Bethhanani;

10 Ben-Hesedi: katika Arubothi (Soko na nchi yote ya Heferi zilikuwa zake);

11 Ben-Abinadabu: katika Nafoth-Dori (alimwoa Tafathi binti Solomoni);

12 Baana mwana wa Ahihudi: katika Taanaki na Megido, na katika Beth-Shani yote karibu na Zarethani chini ya Yezreeli, kuanzia Beth-Shani hadi Abel-Mehola kupita hadi Yokmeamu;

13 Ben-Geberi: katika Ramoth-Gileadi (makao ya Yairi mwana wa Manase katika Gileadi ilikuwa miji yake, pamoja na wilaya ya Argobu katika Bashani na miji yake mikubwa sitini yenye kuzungukwa na kuta zenye makomeo ya shaba);

14 Ahinadabu mwana wa Ido: katika Mahanaimu;

15 Ahimaasi: katika Naftali (alikuwa amemwoa Basemathi binti Solomoni);

16 Baana mwana wa Hushai: katika Asheri na katika Alothi;

17 Yehoshafati mwana wa Parua: katika Isakari;

18 Shimei mwana wa Ela: katika Benyamini;

19 Geberi mwana wa Uri: katika Gileadi (nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani). Naye alikuwa ndiye mtawala pekee katika eneo hilo.

Mahitaji Ya Solomoni Ya Kila Siku

20 Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi.

21 Mfalme Solomoni akatawala katika falme zote kuanzia Mto Eufrati hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Solomoni, siku zote za maisha yake.

22 Mahitaji ya Solomoni ya kila siku yalikuwa kori thelathiniza unga laini, kori sitiniza unga wa kawaida.

23 Ng’ombe kumi wa zizini, ng’ombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana.

24 Kwa kuwa Solomoni alitawala falme zote magharibi ya mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote.

25 Wakati wa maisha ya Solomoni Yuda na Israeli, kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba, wakaishi salama kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.

26 Solomoni alikuwa na mabanda 4,000ya magari ya vita, na farasi 12,000.

27 Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Solomoni na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna cho chote kilichopungua.

28 Pia walileta sehemu walizopangiwa za shayiri na majani kwa ajili ya farasi wavutao magari na farasi wengine mahali palipostahili.

Hekima Ya Solomoni

29 Mungu akampa Solomoni hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari.

30 Hekima ya Solomoni ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri.

31 Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi: kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka.

32 Akanena mithali 3,000 na nyimbo zake zilikuwa 1,005.

33 Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wenye damu baridi, wakiwemo samaki.

34 Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Solomoni, waliotumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia juu ya hekima yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/4-58b64b3ca7467ebf775e033f9e990b2a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ten − nine =