1 Yohana 2

Kristo Mwombezi Wetu

1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikieni haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu ye yote akitenda dhambi, tunaye mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo mwenye haki.

2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua kama tunazishika amri zake.

4 Mtu ye yote asemaye kuwa, “Ninamjua” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli.

5 Lakini kama mtu ye yote analitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake.

6 Ye yote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

Amri Mpya

7 Wapenzi, siwaandikii ninyi amri mpya bali ile ya zamani, ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni lile neno mlilosikia.

8 Lakini ninawaandikia amri mpya, yaani, lile neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu, kwa sababu giza linapita na ile nuru ya kweli tayari inang’aa.

9 Ye yote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani.

10 Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu cho chote ndani yake cha kumkwaza.

11 Lakini ye yote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakokwenda, kwa sababu giza limempofusha macho.

12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,

kwa sababu dhambi zenu

zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.

13 Nawaandikia ninyi, akina baba,

kwa sababu mmemjua

yeye aliye tangu mwanzo.

Nawaandikia ninyi vijana

kwa sababu mmemshinda yule mwovu.

Nawaandikia ninyi watoto wadogo,

kwa sababu mmemjua Baba.

14 Nawaandikia ninyi akina baba,

kwa sababu mmemjua

yeye aliye tangu mwanzo.

Nawaandikia ninyi vijana,

kwa sababu mna nguvu,

na neno la Mungu linakaa ndani yenu,

nanyi mmemshinda yule mwovu.

Msiupende Ulimwengu

15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyoko ulimwenguni. Kama mtu ye yote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake.

16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima: havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu.

17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.

Onyo Dhidi Ya Wapinga Kristo

18 Watoto wadogo, huu ni wakati wa mwisho! Kama mlivyosikia kwamba mpinga Kristo anakuja, hivyo basi wapinga Kristo wengi wamekwisha kuja. Kutokana na hili twajua kwamba huu ni wakati wa mwisho.

19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangelikuwa wa kwetu, wangelikaa pamoja nasi, lakini kutoka kwao kulionyesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu.

20 Lakini ninyi mmetiwa mafuta na yeye Aliye Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli.

21 Siwaandikii kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua, nanyi mnajua hakuna uongo utokao katika kweli.

22 Je, mwongo ni nani? Mwongo ni mtu yule asemaye kwamba Yesu si Kristo. Mtu wa namna hiyo ndiye mpinga Kristo, yaani, yeye humkana Baba na Mwana.

23 Hakuna ye yote amkanaye Mwana aliye na Baba. Ye yote anayemkubali Mwana anaye na Baba pia.

24 Hakikisheni kwamba lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu. Kama lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba.

25 Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani, uzima wa milele.

26 Ninawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha.

27 Kwa habari yenu ninyi, upako ule mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu ye yote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.

Watoto Wa Mungu

28 Sasa basi, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake wakati wa kuja kwake.

29 Kama mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa na yeye.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1JN/2-67c78abc9ba567e2ce6d22d40f617620.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twelve − 10 =