2 Mambo ya nyakati 12

Shishaki Ashambulia Yerusalemu

1 Baada ya nafasi ya Rehoboamu kuimarika na kuwa na nguvu, yeye na Israeli yote waliiacha sheria yaBwanaMungu.

2 Kwa sababu hawakuwa waaminifu kwaBwana, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa kutawala kwa Mfalme Rehoboamu.

3 Akiwa na magari ya vita 1,200 na wapanda farasi 60,000 na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibya, Wasukii na Wakushiyaliyokuja pamoja naye kutoka Misri.

4 Akateka miji ya Yuda yenye ngome akaendelea mpaka Yerusalemu.

5 Ndipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyoBwana, ‘Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.’ ”

6 Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “BwanaMungu ni mwenye haki.”

7 BwanaMungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili laBwanalikamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kwa kupitia Shishaki.

8 Hata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”

9 Shishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu laBwanana hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza.

10 Hivyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la kifalme.

11 Kila mara mfalme alipokwenda katika Hekalu laBwanawalinzi walikwenda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

12 Kwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira yaBwanaikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.

13 Mfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambaoBwanaalikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, alikuwa Mwaamoni.

14 Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafutaBwanaMungu.

15 Kwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, tangu mwanzo mpaka mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwako na vita mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

16 Rehoboamu akalala pamoja na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Abiya mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/12-6397e3bacd988c897ddc40a1b72719ba.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

14 − thirteen =