2 Samweli 1

Daudi Afahamishwa Kifo Cha Sauli

1 Baada ya kifo cha Sauli, Daudi alipokuwa amerudi kutoka kuwashinda Waamaleki, Daudi alikaa siku mbili huko Siklagi.

2 Siku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kwenye kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima.

3 Daudi akamwuliza, “Wewe umetoka wapi?”

Akamjibu, “Nimetoroka kutoka katika kambi ya Waisraeli.”

4 Daudi akamwuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.”

Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.”

5 Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana mwanaume aliyemletea taarifa, “Je, umefahamuje kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”

6 Yule kijana mwanaume akasema, “Ilitokea nikawa juu ya Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwako huko akiwa ameegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana.

7 Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’

8 “Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’

“Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’

9 “Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’

10 “Kwa hiyo nikamkaribia nikamwua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”

11 Ndipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua.

12 Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi laBwanana nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.

13 Daudi akamwambia yule mwanaume kijana aliyemletea taarifa, “Wewe ni mwenyeji wa wapi?”

Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.”

14 Daudi akamwuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta waBwana?”

15 Kisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamwue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa.

16 Kwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimwua mpakwa mafuta waBwana.’ ”

Ombolezo La Daudi Kwa Ajili Ya Sauli Na Yonathani

17 Daudi akafanya maombolezo haya kuhusu Sauli na Yonathani mwanawe,

18 naye akaagiza kwamba watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hili la upindi (ambalo limeandikwa katika Kitabu cha Yashari):

19 “Walio fahari yako, Ee Israeli, wameuawa juu ya mahali pako palipoinuka.

Jinsi wenye nguvu walivyoanguka!

20 “Msilisimulie hili katika Gathi,

msilitangaze hili katika

barabara za Ashkeloni,

binti za Wafilisti wasije wakafurahia,

binti za hao wasiotahiriwa

wasije wakashangilia.

21 “Enyi milima ya Gilboa,

msipate umande wala mvua,

wala mashamba yazaayo sadaka ya nafaka.

Kwa maana huko ndiko ngao ya mwenye nguvu iliponajisiwa,

ngao ya Sauli haitapakwa tena mafuta.

22 Kutokana na damu ya waliouawa,

kutokana na miili ya wenye nguvu,

ule upindi wa Yonathani haukugeuka nyuma.

Upanga wa Sauli haukurudi bure.

23 “Sauli na Yonathani,

maishani walipendwa na kuneemeka,

na katika kifo hawakutengana.

Walikuwa wepesi kuliko tai,

walikuwa na nguvu kuliko simba.

24 “Enyi binti za Israeli,

lieni kwa ajili ya Sauli,

ambaye aliwavika nguo

nyekundu na maridadi,

ambaye aliremba mavazi yenu

kwa mapambo ya dhahabu.

25 “Tazama jinsi mashujaa

walivyoanguka vitani!

Yonathani ameuawa

mahali pako palipoinuka.

26 Nahuzunika kwa ajili yako,

Yonathani ndugu yangu,

kwangu ulikuwa mpendwa sana.

Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu,

wa ajabu zaidi kuliko ule wa wanawake.

27 “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka!

Silaha za vita zimeangamia!”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/1-38adc8e82f3885fc096407d8cee04f58.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

6 − 2 =