2 Samweli 10

Daudi Awashinda Waamoni

1 Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akaingia mahali pake.

2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma ujumbe kuonyesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake.

Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni,

3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonyesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?”

4 Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaacha waende zao.

5 Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu zikishakuwa ndipo mje.”

6 Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa harufu mbaya kwenye pua za Daudi, wakaajiri askari wa miguu 20,000 wa Kiaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka pamoja na watu 1,000, na vile vile watu 12,000 kutoka Tobu.

7 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.

8 Waamoni wakatoka wakajipanga kwenye vita penye ingilio la lango la mji wao, wakati Waaramu wa Soba, wa Rehobu, watu wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi.

9 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; hivyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu.

10 Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni.

11 Yoabu akasema, “Ikiwa Waaramu wana nguvu kunizidi, basi itawabidi mje kuniokoa, lakini ikiwa Waamoni wana nguvu kuwazidi ninyi, basi nitakuja kuwaokoa.

12 Iweni hodari na tupigane kishujaa kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu.Bwanaatafanya lile lililo jema machoni pake.”

13 Basi Yoabu na vikosi vyake wakatangulia mbele kupigana na Waaramu, nao wakakimbia mbele yake.

14 Waamoni walipoona kwamba Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.

15 Baada ya Waaramu kuona wamekimbizwa na Israeli, wakajikusanya tena.

16 Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ng’ambo ya Mto Eufrati, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza.

17 Daudi alipoambiwa jambo hili, akakusanya Israeli yote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi.

18 Lakini wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akaua watu wao mia saba wapanda magari yao ya vita na askari wao wa miguu 40,000. Vile vile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko.

19 Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao.

Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/10-0b7a779cafb37ba3b50e9aac03bdf730.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen + two =