2 Samweli 5

Daudi Awa Mfalme Juu Ya Israeli

1 Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu nyama yako na damu yako hasa.

2 Zamani, wakati Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ulikuwa ndiye uliyeongoza Israeli vitani. NayeBwanaakakuambia, ‘Utawachunga watu wangu Israeli, nawe utakuwa kiongozi wao.’ ”

3 Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele zaBwana, nao wakamtia Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.

4 Daudi alikuwa na miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli miaka arobaini.

5 Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na mitatu.

Daudi Anashinda Yerusalemu

6 Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi huko. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Hutaingia hapa ndani, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.”

7 Hata hivyo, Daudi akateka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.

8 Siku ile, Daudi akasema, “Ye yote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”

9 Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milokuelekea ndani.

10 Daudi akazidi kuwa na mamlaka zaidi na zaidi, kwa sababuBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.

11 Basi Hiramu mfalme wa Tiro akatuma wajumbe kwa Daudi, pamoja na magogo ya mierezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi.

12 Naye Daudi akafahamu kuwaBwanaamemwimarisha kama mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli watu wake.

13 Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana na binti wengi walizaliwa kwake.

14 Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni,

15 Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia,

16 Elishama, Eliada na Elifeleti.

Daudi Awashinda Wafilisti

17 Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda kwa nguvu zote kumtafuta, lakini Daudi akasikia kuhusu jambo hili akatelemka kwenye ngome.

18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Refaimu,

19 kwa hiyo Daudi akamwulizaBwana, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

Bwanaakamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”

20 Ndipo Daudi akaenda mpaka Baal-Perasimu na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yafurikavyo,Bwanaamewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu.

21 Wafilisti wakatelekeza vinyago vyao huko, naye Daudi na watu wake wakavichukua.

22 Wafilisti walikwea kwa mara nyingine tena na kusambaa katika Bonde la Refaimu.

23 Kwa hiyo Daudi akamwulizaBwana, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi.

24 Mara utakaposikia sauti ya kutembea kutoka kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwaBwanaametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.”

25 Basi Daudi akafanya kamaBwanaalivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Gebbahadi Gezeri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/5-3c5e80434167e682813875dc847580bc.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

18 + fourteen =