2 Samweli 8

Ushindi Wa Daudi

1 Ikawa baada ya jambo hili, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, akateka Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.

2 Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili hilo kundi waliuawa na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea kodi.

3 Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Eufrati.

4 Daudi akateka magari yake ya vita 1,000, askari wapanda farasi 7,000 na askari 20,000 watembeao kwa miguu. Daudi akawakata wale farasi wote wakokotao magari mishipa ya miguu, isipokuwa farasi 100 hakuwakata.

5 Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawaua 22,000 miongoni mwao.

6 Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa chini yake na kumlipa kodi.Bwanaakampa Daudi ushindi ko kote alikokwenda.

7 Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa mali ya maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu.

8 Kutoka miji ya Betana Berothai, ambayo alitawala Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.

9 Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amemshinda jeshi lote la Hadadezeri,

10 akamtuma Yoramu mwanawe kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ajili ya ushindi wake katika vita juu ya Hadadezeri, kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.

11 Mfalme Daudi akaviweka vyombo hivi wakfu kwaBwana, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda:

12 yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.

13 Naye Daudi akajulikana baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

14 Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi.Bwanaalimpatia Daudi ushindi ko kote alikokwenda.

Maafisa Wa Daudi

15 Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.

16 Yoabu mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;

17 Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi;

18 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa kiongozi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa kifalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2SA/8-7f72f1394b5279ed8acb38483db6d98c.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 − 14 =