2 Wafalme 23

Yosia Analifanya Upya Agano

1 Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.

2 Akapanda mpaka kwenye Hekalu laBwanapamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote kuanzia aliye mdogo hadi aliye mkubwa kabisa. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu laBwana.

3 Mfalme akasimama karibu na nguzo na kulifanya upya lile Agano mbele zaBwana: yaani kumfuataBwanana kuzishika amri zake, maagizo na hukumu zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, hivyo kuyathibitisha maneno ya hilo Agano yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika Agano.

4 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani wanaomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka kwenye Hekalu laBwanavyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni na kuyachukua hayo majivu mpaka Betheli.

5 Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile inayozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani.

6 Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka kwenye Hekalu laBwanana kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu na kuiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wabaya ambao waliitolea kafara.

7 Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada za miungu, zilizokuwa ndani ya Hekalu laBwanana mahali wanawake walipofuma kwa ajili ya Ashera.

8 Yosia akawaleta makuhani wote waBwanakutoka miji yote ya Yuda na kupafanya mahali pa juu pa kuabudia miungu pasifae tena kufanyia hizo ibada, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji.

9 Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu hawakuhudumu katika madhabahu yaBwanakatika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu miongoni mwa ndugu zao.

10 Kisha mfalme akapafanya Tofethi pasifae tena kufanyiwa hizo ibada za miungu, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu ye yote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe au binti yake katika moto kwa mungu Moleki.

11 Akaondoa kutoka kwenye ingilio la Hekalu laBwanawale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya mungu jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathani-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa mungu jua.

12 Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu laBwana. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni.

13 Mfalme pia akapaharibu mahali pa juu pa kuabudia miungu palipokuwa mashariki ya Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, pale ambapo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amejenga kwa ajili ya Ashtorethi mungu mke aliye chukizo la Wasidoni, kwa ajili ya Kemoshi yule mungu chukizo la Wamoabu, na kwa ajili ya Moleki mungu aliye chukizo la watu wa Amoni, pasifae tena kufanyia hizo ibada.

14 Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.

15 Hata madhabahu iliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia miungu palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, hata hiyo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia miungu alipabomoa. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia miungu na kupasaga hadi pakawa vumbi na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia.

16 Kisha Yosia akatazamatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa huko kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu hiyo ya Betheli ili kupafanya pasifae tena kufanyia hizo ibada za miungu. Hili lilitokea sawasawa na neno laBwanalililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya.

17 Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?”

Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya hii madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.”

18 Akasema, “Liacheni msiliguse. Msimruhusu mtu ye yote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii ambaye alikuwa amekuja kutoka Samaria.

19 Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa na kuharibu kabisa mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu ambapo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria ambayo ilikuwa imemghadhibishaBwana, pasifae tena kwa ibada.

20 Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika madhabahu zao wenyewe na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu.

Yosia Aadhimisha Pasaka

21 Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwaBwanaMungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.”

22 Hapakuwahi kuwapo na adhimisho jingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za Waamuzi walioongoza Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda.

23 Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwaBwanahuko Yerusalemu.

24 Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa wapunga pepo, wanaoabudu mizimu, sanamu za kuagulia, sanamu za kuabudiwa na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana katika Yuda na Yerusalemu. Haya aliyafanya ili kutimiza itakiwavyo kulingana na sheria iliyoandikwa ndani ya kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikikuta ndani ya Hekalu laBwana.

25 Kabla wala baada ya Mfalme Yosia hapakuwepo na mfalme mwingine ye yote ambaye alimpendaBwanakwa moyo wake wote, kwa roho yake yote na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria yote ya Mose.

26 Hata hivyo,Bwanahakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya ili kumghadhibisha.

27 HivyoBwanaakasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Humo Jina langu litakaa.’ ”

28 Matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

29 Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda mpaka Mto Eufrati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumwua huko Megido.

30 Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake ndani ya gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu na kumzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake.

Yehoahazi Mfalme Wa Yuda

31 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, akatawala katika Yerusalemu kwa miezi mitatu. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna.

32 Akafanya maovu machoni mwaBwana, kama baba zake walivyofanya.

33 Farao Neko akamfunga katika minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili kwamba asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akaamuru kodi ya talanta 100za fedha na talanta ya dhahabukatika Yuda.

34 Farao Neko akamfanya Eliyakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliyakimu kuwa Yehoiakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko.

35 Yehoiakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoiakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadrio ya mapato yao.

Yehoiakimu Mfalme Wa Yuda

36 Yehoiakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma.

37 Naye akafanya maovu machoni mwaBwana, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/23-51087db5fe9fa4ddeda8323be0d0a6cd.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 + seventeen =