2 Wafalme 25

1 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akaenda kupigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na jeshi lake lote. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka kwa jeshi kote.

2 Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa Mfalme Sedekia.

3 Kufikia siku ya tisa ya mwezi wa nne njaa ilizidi kuwa kali sana ndani ya mji, hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.

4 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, jeshi lote likakimbia usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba,

5 lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatilia mfalme na kumkuta katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakajitenga naye na kutawanyika,

6 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, mahali ambapo hukumu yake ilitangazwa.

7 Wakawaua wanawe Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayang’oa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.

8 Katika siku ya saba ya mwezi wa tano katika mwaka wa kumi na tisa wa kutawala kwake Mfalme Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa jeshi la walinzi wa mfalme na afisa wa mfalme wa Babeli, wakaja Yerusalemu.

9 Akachoma moto Hekalu laBwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Alichoma kila jengo muhimu.

10 Jeshi lote la Wakaldayo chini ya jemadari wa jeshi la walinzi wa mfalme, wakavunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu.

11 Nebuzaradani jemadari wa jeshi la walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na watu wengine waliokuwa wamebaki, na wale askari waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli.

12 Lakini yule jemadari wa jeshi akawaacha baadhi ya wale watu maskini mno wa nchi ili kutunza mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

13 Wakaldayo wakavunja zile nguzo za shaba, vishikilio vya shaba vinavyohamishika na ile Bahari ya shaba, vile vitu ambavyo vilikuwa katika Hekalu laBwana, nao wakaichukua hiyo shaba kwenda Babeli.

14 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia utambi, vile vyombo vya udongo na vile vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma hekaluni.

15 Yule jemadari wa jeshi la walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.

16 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu laBwana, ilikuwa nzito kiasi kwamba haikuweza kupimika.

17 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. Ile taji ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa dhiraa tatuna ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine, pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo.

18 Yule jemadari wa jeshi la walinzi akawachukua Seraya aliyekuwa kuhani mkuu, Sefania kuhani aliyekuwa msaidizi wake, pamoja na mabawabu watatu kama wafungwa.

19 Miongoni mwa wale ambao bado walikuwa katika mji, akamchukua afisa aliyesimamia mashujaa na washauri watano wa kifalme. Akamchukua pia mwandishi ambaye alikuwa afisa aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliokutwa ndani ya mji.

20 Nebuzaradani jemadari wa jeshi akawachukua hao wote akawaleta kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.

21 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme akaamuru wanyongwe.

Hivyo Yuda akaenda utumwani, mbali na nchi yake.

22 Nebukadneza mfalme wa Babeli akamteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, awe msimamizi wa watu aliowaacha Yuda.

23 Wakati maafisa wote wa jeshi na watu wao waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia kama mtawala, wakamjia Gedalia huko Mispa, nao ni Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofa, Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao.

24 Gedalia akaapa kuwahakikishia wao na watu wao. Akasema, “Msiwaogope maafisa wa Kikaldayo. Kaeni katika nchi na mtumikieni mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.”

25 Hata hivyo, katika mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, aliyekuwa wa damu ya kifalme, akaja na watu kumi na wakamwua Gedalia na watu wa Yuda, pamoja na Wakaldayo waliokuwa pamoja naye huko Mispa.

26 Katika hili, watu wote kuanzia aliye mdogo sana hadi aliye mkubwa kabisa, pamoja na maafisa wa jeshi, wakakimbilia Misri kwa kuwaogopa Wakaldayo.

Yehoyakini Anaachiwa

27 Katika mwaka wa thelathini na saba wa uhamisho wa Yehoyakini mfalme wa Yuda, katika mwaka ule ambao Evil-Merodakialikuwa mfalme wa Babeli, akamfungua Yehoyakini kutoka gerezani siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili.

28 Akazungumza naye kwa wema na akampa kiti cha heshima kilicho juu kuliko cha wale wafalme wengine waliokuwa naye huko Babeli.

29 Hivyo Yehoyakini akayavua yale mavazi yake ya kufungwa na kwa maisha yake yote, akawa anakula mezani mwa mfalme.

30 Pia siku kwa siku, mfalme akampa Yehoyakini mahitaji yake siku zote za maisha yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/25-c749dd03d84d04af0b36cf8d7ccba8b2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

5 × 4 =