2 Wafalme 5

Naamani Aponywa Ukoma

1 Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kwa kupitia yeye,Bwanaalikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari shujaa, lakini alikuwa na ukoma.

2 Panapo siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimekwenda na vikawa vimemchukua mateka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani.

3 Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angelimwona nabii aliyeko Samaria! Angemponya ukoma wake.”

4 Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli.

5 Mfalme wa Aramuakamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumiza fedha, shekeli 6,000 za dhahabuna mivao kumi ya mavazi.

6 Barua aliyokuwa ameichukua ili aipeleke kwa mfalme wa Israeli ilisomeka hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu Naamani kwako ili uweze kumponya ukoma wake.”

7 Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua majoho yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!”

8 Elisha mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua majoho yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.”

9 Kwa hiyo Naamani akaenda akiwa na farasi wake na magari yake na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Elisha.

10 Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda ukaoge katika Mto Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona nawe utatakasika.”

11 Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika na kusema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje asimame na kuliitia jina laBwanaMungu wake na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa aniponye ukoma wangu.

12 Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yo yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu.

13 Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingefanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ”

14 Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Mto Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

15 Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.”

16 Nabii akajibu, “Hakika kamaBwanaaishivyo, ambaye ninamtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa.

17 Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwaBwana.

18 LakiniBwanana amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Wakati bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni,Bwanana amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.”

19 Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.”

Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani,

20 Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kamaBwanaaishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.”

21 Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka kwenye gari lake na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?”

22 Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya kilima cha Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedhana mivao miwili ya mavazi.’ ”

23 Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mivao miwili ya mavazi. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi.

24 Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha mbali ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka.

25 Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Elisha bwana wake.

Elisha akamwuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?”

Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakwenda po pote.”

26 Lakini Elisha akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka kwenye gari lake ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ng’ombe au watumishi wa kiume na wa kike?

27 Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Elisha, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/5-527fd40dda209d7a8e4fd8094397674d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × five =