3 Yohana 1

Salamu

1 Mzee:

Kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli.

Gayo Anasifiwa Kwa Ajili Ya Ukarimu Wake

2 Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo.

3 Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza juu ya uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli.

4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

5 Mpenzi, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako.

6 Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya kanisa. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu.

7 Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wo wote kutoka kwa watu wasioamini.

8 Kwa hiyo imetupasa sisi kuonyesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.

Deotrefe

9 Nililiandikia kanisa, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu.

10 Hivyo kama nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke kanisani.

Demetrio

11 Mpenzi, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Ye yote atendaye mema atoka kwa Mungu, atendaye mabaya hakumwona Mungu.

12 Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.

Salamu Za Mwisho

13 Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino.

14 Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.

Amani iwe kwako. Rafiki zetu walioko hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walioko huko, kila mmoja kwa jina lake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/3JN/1-4387cdc648dbd7fbbedcd1fbc89ff6c1.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × four =