Ayubu 10

Ayubu: Nayachukia Maisha Yangu

1 “Nayachukia sana haya maisha yangu;

kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia,

nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.

2 Nitamwambia Mungu: Usinihukumu,

bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.

3 Je, inakupendeza wewe kunionea,

kuikataa kwa dharau kazi ya mikono yako,

huku wewe ukitabasamu juu ya mipango ya waovu?

4 Je, wewe una macho ya kimwili?

Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?

5 Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu

au miaka yako ni kama ile ya mtu,

6 ili kwamba utafute makosa yangu

na kuichunguza dhambi yangu,

7 ingawa wajua kuwa mimi sina hatia

na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?

8 “Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya.

Je, sasa utageuka na kuniangamiza?

9 Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi.

Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?

10 Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa

na kunigandisha kama jibini,

11 ukanivika ngozi na nyama

na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?

12 Umenipa uhai na kunitendea wema,

katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.

13 “Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako,

nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:

14 Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona,

wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.

15 Kama nina hatia, ole wangu!

Hata kama ningekuwa sina hatia,

siwezi kukiinua kichwa changu,

kwa kuwa nimejawa na aibu

na kuzama katika mateso yangu.

16 Kama nikiinua kichwa changu juu, unaninyatia kama simba

na kuonyesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.

17 Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu

na kuzidisha hasira yako juu yangu;

nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.

18 “Kwa nini basi ulinitoa tumboni?

Ninatamani ningekufa kabla jicho lo lote halijaniona.

19 Laiti nisingekuwako kamwe,

au ningekuwa nimechukuliwa moja kwa moja

kutoka tumboni kwenda kaburini!

20 Je, siku zangu chache si zimekaribia kuisha?

Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi

21 kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena,

katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,

22 nchi ya giza kuu sana,

yenye uvuli wa giza na machafuko,

mahali ambapo hata nuru ni giza.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/10-caa0a02a1bea04be51fd6a62f5adaf51.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 × five =