Ayubu 12

Ayubu Anajibu: Mimi Ni Mtu Wa Kuchekwa

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Bila shaka ninyi ndio watu,

nayo hekima itakoma mtakapokufa!

3 Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi,

Mimi si duni kwenu.

Ni nani asiyejua mambo haya yote?

4 “Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu,

ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu,

mimi ni mtu wa kuchekwa tu,

ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!

5 Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau

kwa wale wenye msiba

kana kwamba ndiyo haki yao

wale ambao miguu yao inateleza.

6 Hema za wanyang’anyi hazisumbuliwi,

wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama,

wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.

7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,

au ndege wa angani, nao watawaambia,

8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,

au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.

9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua

kwamba mkono waBwanandio uliofanya hili?

10 Mkononi mwake uko uhai wa kila kiumbe

na pumzi ya wanadamu wote.

11 Je, sikio haliyajaribu maneno

kama vile ulimi uonjavyo chakula?

12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee?

Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?

13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu,

shauri na ufahamu ni vyake yeye.

14 Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena,

mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.

15 Akizuia maji, huwa pana ukame,

akiyaachia maji, huharibu nchi.

16 Kwake kuna nguvu na ushindi,

adanganywaye na adanganyaye,

wote wawili ni wake.

17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara,

naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.

18 Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme

na kuwafunga mishipi ya kiunoni.

19 Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara

na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.

20 Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika

na kuondoa busara ya wazee.

21 Huwamwagia dharau wale wanaoheshimika

na kuwavua silaha wenye nguvu.

22 Hufunua mambo ya ndani ya gizani

na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.

23 Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza,

hufanya mataifa kuwa makubwa,

naye huyatawanya.

24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao;

huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.

25 Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga,

huwafanya wapepesuke kama walevi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/12-1a7d2e9f5e33539ac126e3c024589272.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

20 − 12 =