Ayubu 14

1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke

siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.

2 Huchanua kama ua kisha hunyauka,

huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.

3 Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo?

Je, utamleta mbele yako katika hukumu?

4 Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka katika kitu najisi?

Hakuna awezaye!

5 Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka,

umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake

na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.

6 Hivyo angalia mbali umwache,

hadi awe amekamilisha muda wake

kama mtu aliyeajiriwa.

7 “Kwa maana lipo tumaini kwa mti,

kama ukikatwa utachipuka tena,

nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.

8 Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini

na kisiki chake kufa udongoni,

9 lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua

na kutoa machipukizi kama mche.

10 Lakini mwanadamu hufa na huo ndio mwisho wake,

hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!

11 Kama vile maji yatowekavyo katika bahari,

au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,

12 ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke,

hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena;

wanadamu hawataamka au kuamshwa

kutoka kwenye usingizi wao.

13 “Laiti kama ungenificha kaburini

na kunisitiri hadi hasira yako ipite!

Laiti ungeniwekea wakati

na kisha ukanikumbuka!

14 Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena?

Siku zote za kazi zangu ngumu

nitangojea kufanywa upya kwangu.

15 Utaniita nami nitakuitika;

utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.

16 Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu,

lakini hutazifuatia dhambi zangu.

17 Makosa yangu yatafungiwa kwa lakiri kwenye mfuko,

nawe utazifunika dhambi zangu.

18 “Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika

na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,

19 kama maji yamalizavyo mawe

na mafuriko yachukuavyo udongo,

ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.

20 Humshinda mara moja kwa daima,

naye hutoweka, waibadilisha sura yake na kumwondoa.

21 Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu;

kama wakidharauliwa, yeye haoni.

22 Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe,

naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/14-f497accccff8d70b94db306801bbf2f5.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

5 × four =