Ayubu 20

Sofari Anasema: Uovu Hupokea Malipo Ya Haki

1 Ndipo Sofari, Mnaamathi akajibu na kusema:

2 “Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu,

kwa sababu nimehangaika sana.

3 Ninasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima,

nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu.

4 “Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani,

tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani,

5 macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi,

nayo furaha ya wasiomcha Mungu

hudumu kwa kitambo tu.

6 Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni

na kichwa chake hugusa mawingu,

7 ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe,

wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’

8 Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena,

amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.

9 Jicho lililomwona halitamwona tena,

mahali pake hapatamwona tena.

10 Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini,

nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyang’anya watu.

11 Nguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake,

zitalala naye mavumbini.

12 “Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake

naye huuficha chini ya ulimi wake,

13 ingawa hawezi kukubali kuuachia uende,

lakini huuweka kinywani mwake,

14 hata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake,

nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake.

15 Atatema mali alizozimeza,

Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika.

16 Atanyonya sumu za majoka,

meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamwua.

17 Hatafurahia vijito,

mito inayotiririsha asali na siagi.

18 Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila,

hatafurahia faida itokanayo na biashara yake.

19 Kwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu,

amenyang’anya kwa nguvu nyumba asizozijenga.

20 “Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana,

hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake.

21 Hakuna cho chote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale,

kufanikiwa kwake hakutadumu.

22 Katikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata,

taabu itamjia kwa nguvu zote.

23 Wakati atakapokuwa amelijaza tumbo lake,

Mungu ataionyesha ghadhabu kali dhidi yake

na kumnyeshea mapigo yake juu yake.

24 Ijapokuwa aikimbia silaha ya chuma,

mshale wa shaba utamchoma.

25 Atauchomoa katika mgongo wake,

ncha ing’aayo kutoka katika ini lake.

Vitisho vitakuja juu yake,

26 giza nene linavizia hazina zake.

Moto usiopepewa na mtu utamteketeza

na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake.

27 Mbingu zitaweka wazi hatia yake,

nayo nchi itainuka kinyume chake.

28 Mafuriko yataichukua nyumba yake,

mali za nyumbani mwake zitachukuliwa na maji yaendayo kasi

katika siku ya ghadhabu ya Mungu.

29 Hili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu,

urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/20-ac760fc64b5b2d89b62f0d88b39c61c4.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ten − 7 =