Ayubu 6

Ayubu Anajibu: Malalamiko Yangu Ni Ya Haki

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa,

nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!

3 Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote,

kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.

4 Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu,

roho yangu inakunywa sumu yake,

vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.

5 Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani,

au ng’ombe dume hulia akiwa na chakula?

6 Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi,

au upo utamu katika ute mweupe wa yai?

7 Ninakataa kuvigusa,

vyakula vya aina hii hunichukiza.

8 “Laiti ningepata haja yangu,

kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,

9 kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda,

kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!

10 Ndipo bado ningekuwa na hii faraja,

bado ningekuwa na furaha katika maumivu makali:

kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.

11 “Ninazo nguvu gani, hata niendelee kutumaini?

Matazamio yangu ya mbele ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu?

12 Je, mimi nina nguvu za jiwe?

Je, mwili wangu ni shaba?

13 Je, ninao uwezo wo wote wa kujisaidia mimi mwenyewe,

wakati ambapo mafanikio yamefukuziwa mbali nami?

14 “Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,

hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.

15 Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa,

ni kama vijito vya msimu,

ni kama vijito ambavyo hufurika

16 wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo

ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,

17 lakini hukauka majira ya ukame,

na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.

18 Misafara hugeuka kutoka katika njia zake,

hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.

19 Misafara ya Tema inatafuta maji,

wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri

hutazama kwa matarajio.

20 Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini,

walipofika huko, wakahuzunika

kwa kukosa walichotarajia.

21 Sasa nanyi mmethibitika kwamba hamna msaada wo wote,

mnaona jambo la kutisha nanyi mnaogopa.

22 Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu,

au mnilipie fidia kutoka katika mali zenu,

23 au niokoeni mikononi mwa adui,

au nikomboeni kutoka kwenye makucha

ya wasio na huruma’?

24 “Nifundisheni, nami nitanyamaza kimya,

nionyesheni nilikokosea.

25 Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli!

Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?

26 Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema,

na kuyafanya maneno ya mtu

anayekata tamaa kama upepo?

27 Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima

na kubadilishana rafiki yenu na mali.

28 “Lakini sasa iweni na huruma mkaniangalie mimi.

Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?

29 Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu;

# angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu.

30 Je, pana uovu wo wote midomoni mwangu?

Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/6-a917806091f902715f12b0b700f6fcc5.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twelve − six =