Esta 3

Hila Ya Hamani Kuwaangamiza Wayahudi

1 Baada ya matukio haya, Mfalme Ahusuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote.

2 Maafisa wote wa kifalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu.

3 Kisha maafisa wa kifalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?”

4 Siku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi.

5 Wakati Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima alighadhibika.

6 Hata hivyo baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumwua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani, Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahusuero.

7 Katika mwaka wa kumi na mbili wa kutawala Mfalme Ahusuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.

8 Kisha Hamani alimwambia Mfalme Ahusuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa.

9 Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta 10,000za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.”

10 Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kwenye kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui wa Wayahudi.

11 Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”

12 Kisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahusuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe.

13 Barua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo kwa siku moja. Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, walipaswa pia kuteka nyara vitu vyao.

14 Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile.

15 Kwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walikwenda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EST/3-23ed20a0f6d821ef9f1d8123c27b17f1.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × 4 =