Ezekieli 19

Maombolezo Kwa Ajili Ya Wakuu Wa Israeli

1 “Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli

2 na useme:

“ ‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike

miongoni mwa simba!

Alilala katikati ya wana simba

na kulisha watoto wake.

3 Alimlea mmoja wa watoto wake,

naye akawa simba mwenye nguvu.

Akajifunza kurarua mawindo

naye akala watu.

4 Mataifa wakasikia habari zake,

naye akanaswa katika shimo lao.

Wakamwongoza kwa ndoana

mpaka nchi ya Misri.

5 “ ‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki,

nayo matarajio yake yametoweka,

akamchukua mwanawe mwingine

na kumfanya simba mwenye nguvu.

6 Alizungukazunguka miongoni mwa simba,

kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu.

Akajifunza kurarua mawindo

naye akala watu.

7 Akabomoa ngome zao

na kuiharibu miji yao.

Nchi na wote waliokuwa ndani yake

wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake.

8 Kisha mataifa wakaja dhidi yake

kutoka sehemu zilizomzunguka.

Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake,

naye akanaswa katika shimo lao.

9 Kwa kutumia ndoana wakamvutia kwenye tundu

na kumleta mpaka kwa mfalme wa Babeli.

Wakamtia gerezani, hivyo kunguruma kwake

hakukusikika tena

katika milima ya Israeli.

10 “ ‘Mama yako alikuwa kama mzabibu

katika shamba lako la mizabibu

uliopandwa kando ya maji,

ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi

kwa sababu ya wingi wa maji.

11 Matawi yake yalikuwa na nguvu,

yaliyofaa kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.

Ulikuwa mrefu kupita miti mingine

katikati ya matawi manene;

ulionekana kwa urahisi

kwa ajili ya urefu wake

na wingi wa matawi yake.

12 Lakini uling’olewa kwa hasira kali

na kutupwa chini.

Upepo wa mashariki uliufanya usinyae,

matunda yake yakapukutika,

matawi yake yenye nguvu yakanyauka

na moto ukayateketeza.

13 Sasa umepandwa jangwani

katika nchi kame na ya kiu.

14 Moto ulienea kuanzia katika mmojawapo ya matawi yake makubwa

na kuteketeza matunda yake.

Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake

lifaalo kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.’

Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZK/19-89ac9b9aa938911dd35fc7da69f4da6e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

10 − nine =