Hesabu 6

Mnadhiri

1 Bwanaakamwambia Mose,

2 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili yaBwanakama Mnadhiri,

3 ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine cho chote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu.

4 Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula cho chote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.

5 “ ‘Kwa muda wote wa nadhiri yake ya kujitenga kwa ajili yaBwana, wembe hautapita kichwani mwake. Ni lazima awe mtakatifu mpaka kipindi cha kujitenga kwake kwa ajili yaBwanakiishe; ni lazima aache nywele za kichwa chake zirefuke.

6 Kwa kipindi cho chote cha kujitenga kwa ajili yaBwanahatakaribia maiti.

7 Hata kama baba yake mwenyewe au mama au kaka au dada akifa, hatajinajisi mwenyewe kwa taratibu za ibada kwa ajili yao, kwa sababu ishara ya kujiweka wakfu kwake kwa Mungu ipo katika kichwa chake.

8 Kwa kipindi chote cha kujitenga kwake yeye ni wakfu kwaBwana.

9 “ ‘Kama mtu ye yote akifa ghafula karibu naye, atakuwa ametiwa unajisi nywele zake alizoziweka wakfu, hivyo ni lazima anyoe nywele zake siku ya utakaso wake, yaani siku ya saba.

10 Kisha siku ya nane ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani katika mlango wa Hema la Kukutania.

11 Kuhani atatoa mmoja kama sadaka ya dhambi, na mwingine kama sadaka ya kuteketezwa ili kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa sababu ametenda dhambi kwa kuwepo mbele ya maiti. Siku iyo hiyo atakiweka wakfu kichwa chake.

12 Ni lazima ajitoe kabisa kwaBwanakwa kipindi cha kujitenga kwake, na ni lazima atoe mwana-kondoo wa mwaka mmoja kama sadaka ya hatia. Siku zilizopita hazitahesabiwa kwa sababu alijitia unajisi katika siku zake za kujitenga.

13 “ ‘Basi hii ndiyo sheria kwa ajili ya Mnadhiri baada ya kipindi chake cha kujitenga kupita. Ataletwa kwenye ingilio la Hema la Kukutania.

14 Hapo atatoa sadaka zake kwaBwana: yaani, mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kondoo mke wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya amani,

15 pamoja na sadaka zake za nafaka na za vinywaji, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, yaani maandazi yaliyotengenezwa kwa unga laini uliochanganywa na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta.

16 “ ‘Kuhani atavileta vitu hivyo mbele zaBwanana kufanya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa.

17 Ataleta pia kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, na atatoa dhabihu kondoo dume kama sadaka ya amani kwaBwana, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka ya kinywaji.

18 “ ‘Kisha kwenye ingilio la Hema la Kukutania, Mnadhiri ni lazima anyoe nywele zake ambazo alikuwa ameziweka wakfu. Atazichukua hizo nywele na kuziweka ndani ya moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka ya amani.

19 “ ‘Baada ya Mnadhiri kunyoa hizo nywele zake za kujitenga kwake, kuhani atampa mikononi mwake bega la kondoo dume lililochemshwa, na pia andazi na mkate mwembamba kutoka kwenye kikapu, vyote vikiwa vimetengenezwa bila kuwekwa chachu.

20 Kisha kuhani atavipunga mbele zaBwanakama sadaka ya kupunga; ni vitakatifu na ni mali ya kuhani, pamoja na kile kidari kilichopungwa na lile paja lililotolewa. Baada ya hayo, Mnadhiri anaweza kunywa divai.

21 “ ‘Hii ndiyo sheria ya Mnadhiri ambaye anaweka nadhiri kwa matoleo yake kwaBwanakufuatana na kujitenga kwake, zaidi ya cho chote kile anachoweza kupata. Ni lazima atimize nadhiri aliyoiweka kufuatana na sheria ya Mnadhiri.’ ”

Baraka Ya Kikuhani

22 Bwanaakamwambia Mose,

23 “Mwambie Aroni na wanawe, ‘Hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli. Waambieni:

24 “ ‘ “Bwanaakubariki

na kukulinda;

25 Bwanaakuangazie nuru ya uso wake

na kukufadhili;

26 Bwanaakugeuzie uso wake

na kukupa amani.” ’

27 “Hivyo wataliweka Jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/6-9851c137e30f5a4ecb9302071f22f373.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

18 − five =