Kutoka 12

Pasaka

1 Bwanaakamwambia Mose na Aroni katika nchi ya Misri,

2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu.

3 Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba.

4 Ikiwa nyumba yo yote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu.

5 Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasio kuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi.

6 Tunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni.

7 Ndipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao.

8 Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu.

9 Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani.

10 Msibakize nyama yo yote mpaka asubuhi; nazo kama zitabakia mpaka asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto.

11 Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka yaBwana.

12 “Usiku uo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumwua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimiBwana.

13 Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.

14 “Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu; mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwaBwana, katika vizazi vyenu vyote: mtaishika kuwa amri ya kudumu.

15 Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana ye yote atakayekula cho chote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka katika Israeli.

16 Katika siku ya kwanza mwe na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.

17 “Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa amri ya kudumu.

18 Katika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja.

19 Kwa muda wa siku saba isionekane chachu yo yote katika nyumba zenu. Ye yote alaye cho chote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka katika jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa.

20 Msile cho chote kilichotiwa chachu. Po pote muishipo, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”

21 Ndipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.

22 Chukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu ye yote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi.

23 Bwanaapitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.

24 “Shikeni maagizo haya kuwa kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu.

25 Mtakapoingia katika nchiBwanaatakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii.

26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’

27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwaBwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu.

28 Waisraeli wakafanya kama vileBwanaalivyomwagiza Mose na Aroni.

29 Ilipofika usiku wa manane,Bwanaakawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia.

30 Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.

Kutoka

31 Wakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni katika watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabuduBwanakama mlivyoomba.

32 Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ng’ombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”

33 Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!”

34 Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika vitambaa na kuyabeba mabegani mwao.

35 Waisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo.

36 BasiBwanaalikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.

37 Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi. Walikuwepo wanaume wapatao 600,000 waendao kwa miguu bila kuhesabu wanawake na watoto.

38 Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo wakiwemo kondoo, mbuzi na ng’ombe.

39 Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao.

40 Waisraeli walikuwa wameishi Misri kwa muda wa miaka 430.

41 Ilikuwa ni siku ya mwisho ya hiyo miaka 430, vikosi vyote vyaBwanavilipokuwa vimeondoka Misri.

42 Kwa sababuBwanaaliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, katika usiku huu Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimuBwanakatika vizazi vijavyo.

Masharti Kwa Ajili Ya Pasaka

43 Bwanaakamwambia Mose na Aroni, “Haya ndiyo masharti kwa ajili ya Pasaka:

“Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka.

44 Mtumwa ye yote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri,

45 lakini kibarua ye yote au msafiri haruhusiwi kula.

46 “Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yo yote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wo wote.

47 Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.

48 “Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka yaBwanani lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume ye yote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila.

49 Sheria iyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”

50 Waisraeli wote walifanya kama vileBwanaalivyomwagiza Mose na Aroni.

51 Siku ile ileBwanaakawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/12-461c48e88df7e68ba51136f2ea0fa276.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × 1 =