Kutoka 39

Mavazi Ya Kikuhani

1 Kutokana na nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu akatengeneza mavazi yaliyofumwa kwa ajili ya kuhudumu katika mahali patakatifu. Pia akamshonea Aroni mavazi matakatifu, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Kisibau

2 Akatengeneza kisibau kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, ya buluu, ya zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.

3 Akafua kwa nyundo vipande vyembamba vya dhahabu na kutengeneza nyuzi nyembamba ili kufuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi, kazi ya fundi stadi.

4 Akatengeneza vile vipande vya begani kwa ajili ya kisibau, vilivyokuwa vimeshikizwa kwenye pembe zake mbili, ili kiweze kufungwa.

5 Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi ulifanana nacho, ulikuwa kitu kimoja na hicho kisibau, nao ulitengenezwa kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, ya buluu, ya zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

6 Akatengeneza vito vya shohamu, vilivyowekwa katika vijalizo vya dhahabu, navyo vilichorwa kama muhuri vikiwa na majina ya wana wa Israeli.

7 Kisha akavifungia kwenye vipande vya begani vya kisibau kuwa mawe ya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Kifuko Cha Kifuani

8 Akatengeneza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kisibau: kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, ya buluu, ya zambarau, nyekundu na za kitani iliyosokotwa vizuri.

9 Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri mojana upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili.

10 Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, yakuti manjano na zabarajadi;

11 safu ya pili ilikuwa ya almasi, yakuti samawi na zumaridi;

12 safu ya tatu ilikuwa ya yakintho, akiki nyekundu na amethisto;

13 katika safu ya nne ilikuwa ya krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo viliwekwa kwenye vijalizo vya dhahabu.

14 Palikuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kikiwa na jina mojawapo la wana wa Israeli; kila kito kilichorwa kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.

15 Kwa kile kifuko cha kifuani akakitengenezea mikufu ya dhahabu safi, mfano wa kamba.

16 Akaitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.

17 Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,

18 zile ncha nyingine za mikufu kwenye vile vijalizo viwili, akazishikamanisha na vile vipande vya begani vya kile kisibau kwa mbele.

19 Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzishikamanisha kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani kwenye ukingo wa ndani karibu na kisibau.

20 Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzishikamanisha upande wa chini wa vipande vya begani mbele ya kile kisibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kisibau.

21 Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kisibau kwa kamba ya buluu, wakiiunganisha na mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisije kikasogea kutoka kwenye kile kisibau, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Mavazi Mengine Ya Kikuhani

22 Akatengeneza joho la kisibau lote la rangi ya buluu, kazi ya mfumaji.

23 Joho hilo lilikuwa na nafasi ya shingo yenye ukosi na utepe ulishonewa kwa kuizunguka nafasi hiyo ili lisichanike.

24 Akatengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na ya kitani iliyosokotwa vizuri kuzunguka pindo la hilo joho.

25 Kisha akatengeneza njuga za dhahabu safi na kuzishikamanisha kuzunguka pindo kati ya makomamanga.

26 Njuga hizo na makomamanga vilipitana kwa kuzunguka upindo wa joho ili livaliwe kwa kuhudumu, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

27 Pia akamtengenezea Aroni na wanawe makoti ya kitani safi, kazi ya mfumaji,

28 kilemba cha kitani safi, tepe za kichwani za kitani na nguo za ndani za kitani zilizosokotwa vizuri.

29 Mshipi ulikuwa wa kitani iliyosokotwa vizuri ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, kazi ya mtarizi, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

30 Kisha akatengeneza bamba, taji takatifu, kwa dhahabu safi na kuchora juu yake kama mchoro juu ya muhuri: MTAKATIFU KWABwana.

31 Kisha wakalifunga kwa kamba ya rangi ya buluu ili kulishikamanisha na kile kilemba kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Mose Akagua Maskani Ya Mungu

32 Kwa hiyo kazi yote ya maskani, Hema la Kukutania ikakamilika. Waisraeli wakafanya kila kitu sawasawa kama vileBwanaalivyomwagiza Mose.

33 Ndipo wakaleta maskani kwa Mose: hema pamoja na vifaa vyake vyote, vibanio vyake, mihimili yake, mataruma yake, nguzo na vitako vyake;

34 kifuniko cha ngozi za kondoo waume kilichotiwa rangi nyekundu, kifuniko cha ngozi laini za wanyama, pazia la kufunikia;

35 Sanduku la Ushuhuda pamoja na mipiko yake na kiti cha rehema,

36 meza pamoja na vyombo vyake vyote na mikate ya Wonyesho;

37 kinara cha taa cha dhahabu safi, safu zake za taa pamoja na vifaa vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa;

38 madhabahu ya dhahabu, mafuta ya upako, uvumba wenye harufu nzuri na pazia la ingilio la hema;

39 madhabahu ya shaba, pamoja na wavu wa shaba, nguzo zake na vyombo vyake vyote, sinia, na kishikilio chake;

40 mapazia ya ua pamoja na nguzo na vitako vyake, pia na mapazia kwa ajili ya ingilio la kwenye ua; kamba zake na vigingi vya hema kwa ajili ya ua; vyombo vyote vilivyohitajiwa kwa ajili ya maskani, Hema la Kukutania;

41 na mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa kwa kuhudumia mahali patakatifu, mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanapohudumu katika kazi ya ukuhani.

42 Waisraeli walikuwa wamefanya kazi yote sawasawa na vileBwanaalivyokuwa amemwagiza Mose.

43 Mose akakagua kazi na kuona kuwa walikuwa wameifanya sawasawa kama vileBwanaalivyokuwa ameagiza. Kwa hiyo Mose akawabariki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/39-9b32e7b9076812dcc57e7df68337f72f.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

thirteen − two =