Luka 15

Mfano Wa Kondoo Aliyepotea

1 Basi watoza ushuru na wenye dhambi wote walikuwa wanakusanyika ili wapate kumsikiliza Yesu.

2 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria wakanung’unika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.”

3 Ndipo Yesu akawaambia mfano huu:

4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate?

5 Naye akiisha kumpata, kwa furaha humbeba mabegani mwake

6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, nimempata kondoo wangu aliyepotea.’

7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

Mfano Wa Sarafu Iliyopotea

8 “Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate?

9 Naye akisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’

10 Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

Mfano Wa Mwana Mpotevu

11 Yesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili.

12 Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.

13 “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa.

14 Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana cho chote.

15 Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.

16 Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa cho chote.

17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa!

18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako.

19 Sistahili tena kuitwa mwanao, nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’

20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

21 “Yule mtoto akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake.

23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi.

24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena, alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

25 “Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza.

26 Akamwita mmoja wa watumishi na kumwuliza, ‘Kuna nini?’

27 Akamwambia, ‘Mdogo wako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’

28 “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumbembeleza.

29 Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu.

30 Lakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’

31 “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako.

32 Lakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu mdogo wako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/15-e579d12e34698ff550faf587dc0db4c8.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

9 − 2 =