Luka 23

Yesu Apelekwa Kwa Pilato

1 Kisha umati wote wa watu wakainuka na kumpeleka Yesu kwa Pilato.

2 Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Kristo, mfalme.”

3 Basi Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Wewe wasema.”

4 Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwapo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!”

5 Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”

Yesu Apelekwa Kwa Herode

6 Pilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?”

7 Alipofahamu kwamba Yesu alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.

8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha.

9 Herode akamwuliza maswali mengi, lakini Yesu hakumjibu lo lote.

10 Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana.

11 Herode na maaskari wake wakamdhihaki Yesu na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato.

12 Siku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki, kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.

Yesu Ahukumiwa Kifo

13 Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu,

14 akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wo wote wa mashtaka yenu dhidi yake.

15 Wala Herode hakumwona na kosa lo lote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lo lote linalostahili kifo.

16 Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.”

17 (Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu).

18 Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!”

19 (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini na kwa ajili ya mauaji).

20 Pilato akitaka kumwachia Yesu, akasema nao tena.

21 Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulibishe! Msulibishe!”

22 Kwa mara ya tatu Pilato akawaambia, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yo yote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kisha nitamwachia.”

23 Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu wakidai kwamba Yesu asulibiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda.

24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe.

25 Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Yesu mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.

Kusulibiwa Kwa Yesu

26 Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anatoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu.

27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea.

28 Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu.

29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’

30 Ndipo

“ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni”

na vilima, “Tufunikeni!” ’

31 Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”

32 Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulibiwe.

33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulibisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto.

34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.”

36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki, wakamletea siki ili anywe.

37 Nao wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

38 Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha ya Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.

39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulibiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Kristo? Jiokoe ili utuokoe na sisi.”

40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu hiyo hiyo?

41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lo lote.”

42 Kisha akasema, “Bwana Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”

43 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”

Kifo Cha Yesu

44 Ilikuwa kama saa sita mchana, kukawa na giza katika nchi yote mpaka saa tisa,

45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.

46 Yesu akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.

47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”

48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao.

49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.

Maziko Ya Yesu

50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki jina lake Yosefu. Yeye alikuwa mjumbe wa Barazala Wayahudi,

51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa.

52 Yosefu alikwenda kwa Pilato akaomba apewe mwili wa Yesu.

53 Akaushusha kutoka msalabani, akauzungushia kitani safi na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo lilikuwa halijazikiwa mtu mwingine ye yote.

54 Ilikuwa siku ya maandalio, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.

55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Yesu wakimfuata kutoka Galilaya, wakamfuata Yosefu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa.

56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/23-503ccfcc7c852a47541324d3f78d4958.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty − five =