Maombolezo 4

1 Jinsi dhahabu ilivyopoteza mng’ao wake,

dhahabu iliyo safi imekuwa haing’ai!

Vito vya thamani vimetawanywa

kwenye mwanzo wa kila barabara.

2 Jinsi wana wa Sayuni wenye thamani,

ambao mwanzo uzito wa thamani yao

ulikuwa wa dhahabu,

sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,

kazi ya mikono ya mfinyanzi!

3 Hata mbweha hutoa matiti yao

kunyonyesha watoto wao,

lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma

kama mbuni katika jangwa.

4 Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga

umegandamana na kaakaa la kinywa chake,

watoto huomba mkate,

lakini hakuna ye yote awapaye.

5 Wale waliokula vyakula vya kifahari

ni maskini barabarani.

Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau

sasa wanalala kwenye malundo ya majivu.

6 Adhabu ya watu wangu

ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,

ambayo ilipinduliwa ghafula

bila kuwepo mkono wa kumsaidia.

7 Wakuu wao walikuwa wameng’aa kuliko theluji

na weupe kuliko maziwa,

miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,

kuonekana kwao kama yakuti samawi.

8 Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;

hawatambulikani barabarani.

Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,

imekuwa mikavu kama fimbo.

9 Wale waliouawa kwa upanga ni bora

kuliko wale waliokufa kwa njaa;

waliteseka kwa njaa, walitokomea

kwa ajili ya kukosa chakula

kutoka shambani.

10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma

walipika watoto wao wenyewe,

ambao walikuwa chakula chao

wakati watu wangu walipoangamizwa.

11 Bwanaametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;

ameimwaga hasira yake kali.

Amewasha moto katika Sayuni

ambao umeteketeza misingi yake.

12 Wafalme wa dunia hawakuamini,

wala hapakuwepo mtu ye yote wa duniani,

kwamba adui na watesi wangeweza kuingia

kwenye malango ya Yerusalemu.

13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,

na maovu ya makuhani wake,

ambao walimwaga pamoja naye

damu ya wenye haki.

14 Sasa wanapapasa papasa barabarani

kama watu ambao ni vipofu.

Wamenajisiwa kabisa kwa damu

kwamba hakuna ye yote

anayethubutu kugusa mavazi yao.

15 Watu waliwapigia kelele wakisema, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!

Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”

Walipokimbia na kutangatanga huko na huko,

watu miongoni mwa mataifa walisema,

“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”

16 Bwanamwenyewe amewatawanya;

hawaangalii tena.

Makuhani hawaonyeshwi heshima,

wazee hawakubaliki.

17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,

kwa kutazamia bure msaada;

tuliangalia kutoka minara yetu

kwa taifa lile lisiloweza kutuokoa.

18 Watu walitunyemelea katika kila hatua

kwa hiyo hatukuweza kutembea

katika barabara zetu.

Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,

kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.

19 Waliotufuatia walikuwa wepesi

kuliko tai katika anga;

walitusaka juu milimani

na kutuvizia jangwani.

20 Mpakwa mafuta waBwana, pumzi ya uhai wetu hasa,

alinaswa katika mitego yao.

Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake

tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.

21 Shangilia na ufurahi, Ee Binti Edomu,

wewe ambaye unaishi katika nchi ya Usi.

Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,

Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.

22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,

hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.

Lakini, Ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako

na atafunua uovu wako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LAM/4-933953c0cd481067c2446f7585721e18.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

nineteen − fourteen =