Marko 13

Dalili Za Siku Za Mwisho

1 Wakati Yesu alipokuwa akitoka Hekaluni, mmojawapo wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa na majengo haya yalivyo mazuri!”

2 Ndipo Yesu akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, yote yatabomolewa.”

3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamwuliza faraghani,

4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo ni nini ishara ya wakati hayo yote yanapokaribia kutimia?”

5 Yesu akawaambia: “Jihadharini mtu ye yote asiwadanganye.

6 Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi.

7 Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.

8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na matetemeko sehemu mbalimbali na njaa. Huu ndio mwanzo wa utungu.

Mateso Yatabiriwa

9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka mahakamani na kuwapiga mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao.

10 Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia.

11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke kuhusu mtakalosema. Semeni tu lo lote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi msemao bali ni Roho Mtakatifu.

12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, baba atamsaliti mwanawe. Watoto watawaasi wazazi wao na kusababisha wauawe.

13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu, lakini atakayevumilia hata mwisho ataokoka.

Chukizo La Uharibifu

14 “Mtakapoona chukizo la uharibifu limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi na wakimbilie milimani.

15 Yeye aliyeko juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua kitu cho chote.

16 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.

17 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!

18 Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi.

19 Kwa maana siku hizo itakuwako dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa uumbaji, hapo Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo na wala haitakuwako tena kamwe.

20 Kama Bwana asingelifupiza siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu ye yote, lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupiza siku hizo.

21 Wakati huo mtu ye yote akiwaambia, ‘Tazama, Kristohuyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msiamini.

22 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana hata wale wateule.

23 Hivyo jihadharini, nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.

Kuja Kwa Mwana Wa Adamu

24 “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki,

“ ‘jua litatiwa giza

na mwezi hautatoa nuru yake;

25 nyota zitaanguka kutoka angani,

nazo nguvu za anga zitatikisika.’

26 “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.

27 Naye atawatuma malaika zake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.

Somo Kuhusu Mtini

28 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Mara mwonapo matawi yake yakichipua na kutoa majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

29 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, tambueni kwamba Kristo yu karibu malangoni.

30 Amin, amin nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yametukia.

31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa

32 “Lakini kwa habari ya siku ile na saa hakuna ye yote ajuaye, hata malaika walioko mbinguni wala Mwana hajui, ila Baba peke yake.

33 Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia.

34 Ni kama mtu anayesafiri akiiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwambia yule bawabu aliye mlangoni akeshe.

35 “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi, iwapo ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au wakati wa mapambazuko.

36 Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala.

37 Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/13-50067f3d3b3fd092b326b47433d9b7f4.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × four =