Marko 6

Nabii Hana Heshima Kwao

1 Yesu akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiwa amefuatana na wanafunzi wake.

2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi na wengi waliomsikia wakashangaa.

Wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!

3 Huyu si yule seremala, mwana wa Maria? Na ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa petu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake wakakataa kumwamini.

4 Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe na miongoni mwa jamaa na ndugu zake.”

5 Hakufanya miujiza yo yote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya.

6 Naye akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani.

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

Kisha Yesu akawa anakwenda huku na huko kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha.

7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

8 Akawaagiza akisema, “Msichukue cho chote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu,

9 bali mvae viatu, lakini msivae nguo ya ziada.”

10 Akawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yo yote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.

11 Kama mahali po pote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kung’uteni mavumbi yaliyoko miguuni mwenu, ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”

12 Kwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi.

13 Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.

Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa

14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana kila mahali. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu ndiyo maana uwezo wa kutenda miujiza unafanya kazi ndani yake!”

15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”

Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.”

16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuka!”

17 Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo ndugu yake, ambaye alikuwa amemwoa.

18 Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali wewe kumwoa mke wa ndugu yako.”

19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumwua. Lakini hakuweza,

20 kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, akawa anamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.

21 Mfalme Herode alifanya karamu kubwa, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta.

22 Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.

Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu cho chote utakacho, nami nitakupa.”

23 Tena akamwahidi kwa kiapo akamwambia, “Cho chote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”

24 Yule binti akatoka nje akaenda kumwuliza mama yake, “Niombe nini?”

Mama yake akajibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”

25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”

26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa mbele ya wageni wake hakutaka kumkatalia.

27 Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani,

28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake.

29 Wanafunzi wake walipopata habari hizi, wakaja kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Yesu Awalisha Watu 5,000

30 Wale wanafunzi wa Yesu wakamkusanyikia na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha.

31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”

32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao wakaenda mahali pa faragha pasipo na watu.

33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakawatangulia haraka kwa miguu kutoka katika miji yote, nao wakatangulia kufika.

34 Yesu alipofika nchi kavu na kuuona huo umati wa watu, aliwaonea huruma kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mahali hapa ni mbali na pasipo na watu, nazo saa zimekwenda sana.

36 Waage watu ili waweze kwenda sehemu za mashambani na vijiji vya jirani, wakajinunulie chakula.”

37 Lakini Yesu akawajibu, “Wapeni ninyi chakula.”

# Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200ili tuwape watu hawa wale?”

38 Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”

Walipokwisha kuona wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39 Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani,

40 nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini.

41 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili akatazama mbinguni, akashukuru, kisha akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili.

42 Watu wote wakala, wakashiba.

43 Wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.

44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

45 Mara Yesu akawataka wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye anauaga ule umati wa watu.

46 Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba.

47 Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu.

48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Karibu na mapambazuko, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akitembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita,

49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu, wakapiga yowe,

50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.

Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni Mimi, msiogope!”

51 Akapanda kwenye mashua yao na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa.

52 Kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate, mioyo yao ilikuwa migumu.

53 Walipokwisha kuvuka, wakafika Genesareti, wakatia nanga.

54 Mara waliposhuka kutoka katika mashua yao, watu wakamtambua Yesu,

55 wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali po pote waliposikia kuwa Yesu yupo.

56 Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini na mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni, wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa, waliponywa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/6-6c9770ed2bdb5cff6a5f180b2ee16308.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty − 7 =